NGOMA, OKWI KUMALIZANA NA SIMBA KESHO
NA ZAITUNI KIBWANA,
HIKI wanachokifanya Simba kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara sasa ni sifa na Mungu anawaona.
Baada ya kupeleka kilio kwa mahasimu wao, Yanga kwa kumnasa kiungo Haruna Niyonzima, sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanataka kuzidisha machungu kwa mshambuliaji wa klabu hiyo ya Jangwani, Donald Ngoma.
Pamoja na Ngoma, ambaye wengi hawajui kama yuko hapa nchini, mshambuliaji mwingine wa zamani wa klabu hiyo ya Simba, Emanuel Okwi, naye atamalizana na klabu hiyo ya Msimbazi.
Mshambuliaji huyo wa Zimbabwe, Ngoma, mara kadhaa amekanusha mpango wa kuondoka Yanga, lakini uvumilivu umemshinda kutokana na dau alilowekewa na Simba linalokadiriwa kuwa Sh milioni 70 hadi 90, limeweza kumbadili mawazo yake.
Masshele Blog ame fuatilia na kugundua kwamba, mchezaji huyo, ambaye amekuwa akiishi kwa kujificha hapa nchini ili asijulikane, ameshafanya mazungumzo na Simba kwa muda mrefu na kesho atasaini mkataba wa miaka miwili.
“Tutamalizana na Donald Ngoma kesho kutwa (kesho) baada ya kufanya naye mazungumzo kwa muda mrefu sasa,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, amesema Okwi atatua Dar es Salaam Jumamosi hii (kesho) kwa ajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
“Okwi nimezungumza naye na tumefanya makubaliano na ataingia hapa Jumamosi (kesho) kuja kusaini mkataba wa miaka miwili,” alisema Hanspope.
Kiongozi huyo aliongeza: “Tunamtaka Okwi kwasababu ni mchezaji mzuri. Mchezaji ambaye amekuwa anatupatia matokeo mazuri na ni mchezaji mwenye uwezo wa kubadilisha matokeo ya mchezo ndani ya sekunde moja. Kwahiyo ni mchezaji ambaye tunamfahamu.”
Msimu huu Simba inaonekana kuwa na jeuri ya fedha kutoka kwa tajiri wao, Mohammed Dewji ‘Mo’, ambaye amewapa kiburi cha kusajili mchezaji yeyote wanayemtaka.
0 Comments