NA SAADA SALIM
YANGA wamecharuka, kwani baada ya kuona beki wao Vincent Bossou ameanza nyodo kwa kuwatajia dau kubwa ili aendelee kukipiga Jangwani, wameamua kumtwaa Yussuf Ndikumana ili kuziba nafasi ya Mtogo huyo.
Katika kuhakikisha wanampata kirahisi Ndikumana, Yanga wameanza mchakato wa kumtafutia nyumba jijini Dar es Salaam ili kumwezesha kuishi kwa raha zake na kuitumikia vilivyo timu hiyo.
Ndikumana ameonyesha kiwango kizuri katika kikosi cha Mbao msimu uliopita kiasi cha kuzivutia timu kadhaa za hapa nchini ikiwamo Simba.
Yanga imeamua kuachana na Bossou baada ya wakala wake Gibby Kibinge, kutaka dau kubwa ili mchezaji huyo aweze kubaki Jangwani.
Kibinge alisema mchezaji huyo anapaswa kulipwa Dola za Marekani 4, 200 (Sh milioni 9.2) kama mshahara wake kwa mwezi.
Mbali na fedha hizo, pia anahitaji dola 42,000 (Sh milioni 92.8) kama fedha za usajili wa mkataba mpya na pia Dola 500 (Sh milioni 1.1) kama bonasi iwapo timu hiyo itafanikiwa kutwaa ubingwa.
Kutokana na dau hilo, Kamati ya Usajili ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Hussein Nyika, imeamua kuachana na Mtogo huyo na kuhamia kwa Ndikumana.
Taarifa za kutoka kwa ndugu wa karibu wa mchezaji huyo, zinasema kuwa kuna mazungumzo yanaendelea kati ya Ndikumana na Yanga kwa ajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
“Kila kitu kinaenda vizuri kwani mazungumzo yanaendelea na muda wowote wataafikiana vizuri na katika makubaliano hayo walimwambia watampatia nyumba ya kuishi,” alisema.
Masshele blog ilimtafuta mchezaji huyo na kusema kwa sasa hawezi kuzungumza suala lolote juu ya Yanga, kwani tayari kuna ofa nyingi kutoka timu za ndani na nje ya Tanzania.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote vitu vikiwa tayari kila kitu kitawekwa wazi, kikubwa ni kwamba kuna ofa nyingi ndani na nje ya Tanzania ikiwamo Yanga,” alisema.
1 Comments
Acha comment
ReplyDelete