UHALISIA
WA TENDI ZA KISWAHILI KATIKA JAMII YA SASA ;MFANO KUTOKA UTENZI WA FUMO LIYONGO.
Dutwa
Dutwa
Makala hii imejikita katika
kuangalia uhalisia wa tendi za kiswahili katika jamii ya sasa ya maendeleo ya
sayansi na teknolojia. Dhana ya tendi imekua ikihusishwa sana na historia (yaani ekiolojia) ikihusisha mambo
ya kale yaani visa na matukio ambayo yalitendeka zamani. Dhana hii ya kuhusisha
tendi na mambo ya kale ndiyo inapelekea dhana hii kuonekana kuwa ni mambo ya
kale tu na kukosa uhalisia katika jamii ya sasa. Kwahiyo makala hii imejikita
katika kuangalia namna tendi za Kiswahili, mfano kutoka katika utendi wa Fumo
Lyongo jinsi ambavyo fani(lugha) na maudhui hayo yanavyosawiri uhalisia katika
jamii ya sasa. Hivyo itaonesha kama tendi za kiswahili zinasawiri maisha halisi
ya jamii ya sasa au la.
1.0 Utangulizi
Tendi
za Kiswahili zinahusishwa na historia za jamii mbalimbali kwa kuangazia visa na
matukio yaliyopata kutokea au yanaaminika na wanajamii kuwa yalipata kutokea katika
jamii husika. Jambo la kujiuliza ni kuwa je tendi za Kiswahili katika maudhui
yake zinabeba uhalisia wa jamii ya sasa au ni dhana ambayo inabaki kuwa ni
historia tu ambayo inaaminika kuwa ilitokea na siyo dhana inayoweza kurejelea
jamii za kisasa ambazo zimeendelea zaidi ya zile jamii za kale. Dhana hii ya ukale
au historia katika tendi zimeshadidiwa na wataalamu kama vile Chadwick’s (1932) ambaye alichunguza masimulizi ya kijadi, na kuona
kuwa mashujaa wanaakisi historia. Mtaaalamu mwingine anayeonyesha dhana ya historia
katika tendi ni Vansina (1965) ambaye
katika kuthibitisha historia katika utendi,alionyesha vitu viwili yaani ukweli
wa kihistoria na uhakika wa kihistoria. Anaeleza kuwa ukweli wa kihistoria ni
sharti uweze kukubaliwa na kuaminiwa na watu wengi katika jamii. Mashujaa wakuu
huakisi moja kwa moja historia.
huweza
kueleza ukweli wa kihistoria na si hakika ya kihistoria. Pia Mulokozi (2002)
anashadadia uwepo wa historia katika tendi wa kusema kuwa shujaa hawezi kuwa
nje ya historia. Vitu hivi vinakamilishana, ukijumuisha na ubunifu wa kisanaa.
Shujaa huakisi mfano halisi katika historia na vipindi vinavyozunguka matukio
ya kihistoria. Mara nyingi katika tendi, matukio na mashujaa
Hivyo
maelezo ya wataalamu hao yanathibitisha kuwa tendi hubeba historia za jamii
kuhusu visa na matukio yaliyopita . Hivyo kuacha swali je zinaendana na jamii
ya sasa kiuhalisia au zinabaki tu kuwa kama amali ya ukumbusho kwa kizazi cha
sasa?.
1.1
Mawanda ya utafiti wa makala hii
Makala hii, imejikita katika kuangalia uhalisia wa
tendi za Kiswahili kwa kuangalia uhalisia huo katika utendi wa Fumo Lyongo, uliotungwa
na Muhammad Abubakar Kijumwa (1913). Kuna tendi mbalimbali za Kiswahili zinazoweza
kuangazia mada ya utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii, lakini ulichaguliwa
utendi huu kuziwakilisha tendi nyingine zinazoweza kuangaziwa ili kuangalia uhalisia
wa tendi hizo katika jamii ya sasa ya watanzania na Waafrika kwa ujumla.
Mwandishi ameweza kueleza dhana ya jamii ya sasa kwa kurejelea jamii ya karne
ya na 20 na kuendelea ambayo imepiga hatua zaidi katika maendeleo ya sayansi na
teknolojia.
1.2 Kiunzi cha
nadharia
Makala hii imeabiri mambo mbalimbali kwa kuzingatia
nadharia ya uhalisia. Ntarangwi(2004) anasema kuwa nadharia hii katika upana
wake, humaanisha uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi. Mhalisia huamini
katika matokeo ya mambo na ukweli anaouzingatia ni ule unaoweza kuonekana na
kuthibitishwa kwa tajriba.
2.0 Dhana ya Tendi
Kwa mujibu wa Bowra (1952) tendi ni masimulizi
marefu ambayo yanahusu matukio yenye uzito na muhimu kwenye jamii.Mara nyingi
tendi zinahusu masuala ya vita.
Mulokozi (2002) Utendi ni ushairi wa
matendo na ni utungo mrefu wenye kuzungumzia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii,
kitaifa. Historia, visasili na Visakale.
TUKI (2013) tendi pia utenzi, hasa wenye kuhusu
matukio ya ushujaa. Hivyo fasili hii inasisitiza kuwa tendi huzungumzia zaidi kuhusu
matukio yaliyotendwa na mashujaa mbalimbali waliopata kutokea katika jamii.
2.1
Kuhusu mtunzi
Mulokozi (1999) anaeleza kuwa Muhamadi Abubakar
Kijumwa alikuwa mwenyeji wa Lamu nchini Kenya. Alikuwa msanii mashuhuri ambaye,
mbali na kutunga mashairi na tendi, vilevile alikuwa mjomi ( mchongaji wa
milango yenye nakshi), msanii-msanifu, msawidi
na mnukuzi wa miswada ya zamani. Habari za maisha yake hazijulikani
vizuri. Alianza kujitokeza katika utunzi kwenye miaka ya 1890, alipoanza
kuwasaidia watafiti wa kizungu waliotaka kufahamu habari za waswahili. Baadhi
ya watafiti mashuhuri aliowasaidia ni Alice Werner (miaka ya 1930) na Ernst Dammann
(miaka ya 1900-1940). Alifariki mwanzoni mwa miaka ya 1940 ( hatukufanikiwa
kupata tarehe halisi ya kifo chake). Mtoto wake wa kiume aitwaye Elewa aliishi
Lamu (hatuna hakika kama bado yu hai), na mjukuu wake, Esha Elewa anaishi Saudi
Arabia ambako ameolewa. Mbali na utendi wa Fumo Liyongo, kijumwa alitunga
mashairi mengine kadha ambayo si mashuhuri, ukiwemo Utendi wa Helewa( Siraji).
2.2 Muhtasari wa kisa cha Fumo
Liyongo
Kisa cha Liyongo kinahusu mgogoro kati ya Fumo
Liyongo na kaka yake, mfalme wa Pate, ambaye katika utendi huu hatajwi jina
lake, bali katika mapokezi mengine anaitwa Daudi Mringwari. Hadithi inaanza
Liyongo akiwa ni kijana amekwisha balehe, mwenye kusifiwa nchini kote kwa nguvu
na ushujaa wake. Anaishi nyumbani kwake Ungwana wa Mashaha ( eneo la Shaka,
jimbo la Ozi). Ujumbe wa Wagalla unafika Pate kumtembelea Sultani Daudi.
Sultani anamsifia Liyongo kwa Wagalla, lakini wao hawaamini maneno yake.
Anampelekea barua Liyongo ya kumwita na Liyongo anaitikia wito huo kwa kufika
barazani kwa Sultani. Wagalla wanakiri kweli Liyongo ni mtu mwenye nguvu.
Wanamwomba Sultani awaruhusu wachukue mbegu yake, sultani anakubali na Liyongo
anaozwa mke wa kigalla na kupata mtoto wa kiume . Mfalme anaingiwa na hofu ya
kupinduliwa na Liyongo, anaanza njama za
kumuua kisha Liyongo anagundua njama hizo na hatimaye anakimbilia mwituni
miongoni mwa Wasanye na Wadahalo na kufanya naye urafiki.Liyongo anakamatwa na
kufungwa gerezani lakini anafanikiwa kutoroka. Baada ya jaribio hilo kushindwa
mfalme anamtumia mwana wa Liyongo kumpeleleza na kujua siri ya namna ya kumuua
Fumo Liyongo. Anafanikiwa kuijua siri na hatimaye kumuua baba yake kwa kumchoma
sindano ya shaba kitovuni akiwa usingizini. Mwishoni mfalme anapata habari za
kifo cha Liyongo, hivyo anafurahi sana lakini anamsaliti mtoto wa Liyongo kwa
kumnyang`anya vitu alivyompa na hatimaye anaenda porini kwa Wagalla na kufia
huko.
Katika kutazama uhalisia wa tendi za kiswahili
katika jamii za sasa. Makala hii itajikita katika kutazama lugha inayotumiwa na
mtunzi wa utendi huu, pamoja na maudhui
yanayobebwa na utendi huu Utenzi wa
Fumo Liyongo, uliotungwa na Muhammadi Abubakar Kijumwa (1913) . Tunaangazia
vipengele vifuatavyo ili kubaini uhalisia
wa utendi huu katika jamii ya sasa:
3.0 Lugha iliyotumiwa
na mtunzi
Kwa mujibu wa Wamitila (2003), lugha hutumiwa kuelezea
mfumo wa sauti za nasibu zinazotumika na watu wa jamii fulani wenye utamaduni
unaofanana, kuwasiliana. Lugha ina nafasi kubwa sana katika fasihi kwa kuwa
fasihi yenyewe ni sanaa ya lugha. Lugha ndiyo nyenzo inayotofautisha fasihi na
sanaa nyingine kama uchoraji, ufinyanzi, udarizi n.k. Lugha ni uchunguzi wowote
wa kazi hizo hauna budi kuangalia suala la
kazi ya kifasihi, huyawasilisha maudhui yake. Dhamira yake na maana yake
kwa kutegemea lugha. Baadhi ya wahakiki wa fasihi huitumia lugha kwa namna maalumu.
Kipengele cha lugha ni muhimu sana katika
uwasilishaji wa kazi ya sanaa, kwani lugha ndiyo silaha ya mtunzi wa kazi ya
fasihi ikiwemo utendi. Katika utendi huo, lugha iliyotumika ni ile yenye lahaja
ya kiamu kwa kiasi kikubwa. Lahaja hii inakosa wazungumzaji wengi katika jamii
ya sasa ya watanzania na hivyo kupelekea ugumu wa kuweza kuusoma utenzi huu na
kuuelewa papo hapo bila ya kutatizwa na suala
la lugha iliyotumiwa na mwandishi (Muhammad Abubakar Kijumwa). Hali hii
inapelekea watu wengi kushindwa kuusoma utenzi huu na kuuelewa bila ya
kurejelea maana za maneno hayo ili waweze kupata maana kamili iliyokusudiwa na
mwandishi na hivyo kusababisha ugumu wa kuusoma na kuelewa ujumbe uliomo
ukilinganisha fani nyingine za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya. Katika
kuthibitisha suala la matumizi ya lugha isiyoeleweka na idadi kubwa ya
watanzania wa sasa hebu tutazame baadhi ya beti zinazotoka katika utenzi huu
15.
Mato
kikodoleya
Ghafula
utazimiya
Kufaa
kutakurubiya
Khufa
kuingiya
16.
Wagala
wakipulika
Kwa
dhihaka wakateka
Wakanena
“Twamtaka
Na
sisi kumwangaliya.
161.
Kamfanyiza
zakula
Za
ndiani ili kula
Uwe
mwana wa Kigala
Katoka
kashika ndiya
162.
Naye
chanenda ndiani
Una
khaufu mouoni
“nifanye
shauri gani
163.
Yakumu
ya matatizo
“
iye mimi kumpata
Kutokufa
ni matata
Taniumwa
Mara moya..”
Beti
hizo ni mfano tu wa beti zote zilizotumiwa na mtunzi katika kufikisha ujumbe
wake kwa hadhira. Lakini tukiangazia uhalisia wa lugha iliyotumika katika beti
hizo, tunatambua kuwa ni lugha ya Kiswahili kilichotumika ni kile
kilichosheheni matumizi makubwa ya lahaja ya Kiamu. Hivyo tukitazama uhalisia
wa lugha hiyo na Kiswahili sanifu ambacho ndiyo kinazungumzwa na watu wengi
katika jamii ya sasa ya watanzania utaona kuwa watu wengi wa hii leo
wanashindwa kutambua maana za maneno mengi yaliyotumiwa na mtunzi katika
kufikisha ujumbe wake kwa jamii husika katika kipindi hicho. Hivyo matumizi ya
lahaja ya kiamu imepelekea baadhi ya wasomaji kuona kuwa utendi ni kazi ya
fasihi inayotumia lugha ngumu katika kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira. Lugha
ya Kiswahili sanifu ni ile iliyosanifishwa kutoka katika lahaja ya kiunguja.
Katika jamii ya sasa ya Watanzania Kiswahili na wanaosoma tendi, Kiswahili
chenye lahaja ya kiamu hakina wigo mkubwa kimatumizi na hivyo hali hii
inapelekea ugumu wa kuelewa kile kinachowasilishwa na mtunzi wa utendi kwa
urahisi.
4.0 Maudhui
Kwa mujibu wa Wamitila (2003), maudhui ni jumla ya
mambo yote yanayozungumziwa katika kazi
ya fasihi. Maudhui hutumiwa kwa upana kujumlisha dhamira, falsafa, itikadi na
msimamo. Hivyo maudhui ni jumla ya mambo yote anayotoa fanani au msanii wa kazi
ya fasihi kupitia mbinu mbalimbali alizozitumia ili kufikisha ujumbe kwa
hadhira aliyoikusudia.Maudhui yaliyomo katika tendi za Kiswahili hususani Fumo Liyongo ni pamoja na:
4.1
Ushujaa katika utendi
Kwa
mujibu wa Wamitila (2003), shujaa ni mhusika mkuu katika kazi ya kifasihi
ambaye anaweza kuwa wa kike au wa kiume. Kimsingi neno hili haliashirii wema
tu, mhusika mkuu anaweza kuwa mbaya.
TUKI
(2013), shujaa ni mtu mwenye moyo thabiti anayeweza kukabili mambo, hata kama
ni ya hatari.
Kama
ilivyo maana ya utendi kuwa ni masimulizi marefu ya kinudhumu yenye kuelezea
matendo ya kishujaa. Hivyo tendi hutawaliwa na matendo yanayotendwa na shujaa
husika katika kuleta maudhui yenye ujumbe fulani kwa jamii. Hapa tutaangazia sifa
mbalimbali za shujaa wa Kiswahili, hususani Fumo
Liyongo ili kuona kama sifa za shujaa huyu zinasawiri au kwenda sambamba na
sifa za mashujaa wa kisasa na kama tofauti zozote baina yao. Sifa za Shujaa wa tendi
za Kiswahili. Kwa mijibu wa Mulokozi (1999 & 2002) ni
4.1.1
Anatoka tabaka lolote
Shujaa
wa Kiswahili katika tendi huweza kutoka tabaka lolote na hatimaye kuweza kutenda
matendo ya kishujaa ambayo yanadhihirisha ushujaa wake. Katika utenzi wa Fumo Liyongo, shujaa Lyongo, hatuelezwi
wazi na mwandishi kama anatoka katika tabaka lipi lakini inasemekana kuwa
alitoka tabaka la juu, kwani adui yake mfalme Daudi Mringwari anasemekana kuwa
alikua ndugu yake wa damu. Ambapo Liyongo alikimbia mji wa Pate ulikokuwa ukitawaliwa
na nduguye kwasababu ya visa vya nduguye.Pia hata katika utenzi wa Rasil Ighul,
shujaa mkuu Mtume Muhamamad (S.A.W) anatoka katika tabaka la chini lakini
anaibuka kuwa shujaa katika kuongoza vita dhidi ya wasiokuwa waumini wa
uislamu. Sifa hii ya shujaa inasawirika hadi katika jamii ya sasa, kwani
mashujaa wake wametoka katika matabaka tofauti tofauti. Mfano shujaa wa taifa
la Tanganyika Julius k Nyerere alitoka katika tabaka la juu kiuchumi kwani baba
yake alikuwa ni chifu.
4.1.2 Shujaa huwa jasiri
Kwa
mujibu wa TUKI (2013), Ujasiri ni hali ya kukabili jambo bila ya hofu. Hivyo
ujasiri huonyesha kuwa shujaa ni mtu anayejiamni katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali anazokutana nazo.
Katika
utendi huu shujaa Liyongo ni mtu jasiri anayeweza kupambana na kundi la watu na
kuwashinda, anafanikiwa kutoroka hata jela kwa kutumia tupa.Ujasiri wake ndiyo
unaomchochea kutenda matendo ya kishujaa, matendo yaliyomwogopesha Sultwani. Katika
kuonyesha dhana ya ujasiri kwa shujaa Liyongo, mtunzi anabainisha katika beti
zifuatazo
7.
Kimo
kawa mtukufu
Mpana
sana mrefu
Majimboni
yu maarufu
Watu
huya kwangaliya
12.
Mfalme
kawambiya
Wagala
kiwasifiya
Huwegemea
watu miya
Wasiweze
kukimbiya
13.
mwanamume
swahihi
Ni Kama simba unazihi
Usiku
na asubuhi
Kutembeya ni mamoya
Sifa hii ya ujasiri inadhihirika hata katika
mashujaa wa jamii ya sasa kwani huwezi kutenda matendo ya kishujaa katika jamii bila ya kuwa na ujasiri unaokuchochea
kutenda matendo hayo. Mfano shujaa wa taifa la Afrika kusini , Nelson Mandela
alikuwa na ujasiri wa kuwapinga makaburu walioogopwa na jamii ya watu wengi
lakini yeye alijitokeza hadharani katika kuwapinga. Kitendo hiko kinachoonyesha
ujasiri wa hali ya juu aliokuwa nao Nelson Mandela.
4.1.3 Uogofu
(aogopwe), shujaa wa Kiswahili anatakiwa
aogopwe kutokana na matendo ya kutisha au yasiyo ya kawaida yanayotendwa na
shujaa huyo. Katika utenzi wa Fumo Liyongo,
shujaa Liyongo anaonekana kuogopwa kutokana na matendo yake ya kishujaa
anayoweza kuyatenda kutokana na nguvu za ajabu alizokuwa nazo. Suala hili
linathibitika kupitia beti zifuatazo
12.
Mfalme
kawambiya
Wagala
kinasifiya
Huwegemea
watu miya
Wasiweze
kukimbiya.
14.
Ghafula
kikutokeya
Mkoyo
hukupoteya
Tapo
ukikumiliya
Ukatapa
na kuliya.
15.
Mato
kikodololeya
Ghafula
utazimiya
Kufaa
kutakurubiya
Kwa
khaufu kuingiya
16.
Wagala
wakipulika
Kwa
dhihaka wakateka
Wakanena
“ twamtaka
Na
sisi kumwangaliya”
Mfano
wa beti hizi ni baadhi tu ya zile zinazomwonyesha shujaa Liyongo ambaye
anamiminiwa sifa kedekede na mfalme wa Pate, kwa matendo yake na haiba yake.
Haiba yake inaonyeshwa kama mtu anayetisha ukikutana naye uso kwa uso kwani
akikukodolea macho yake unaweza kuzimia. Katika jamii ya sasa shujaa si lazima
atishe kwani mashujaa hutumia zaidi akili kuliko nguvu kama ilivyokuwa katika
jamii zamani. Shujaa wa kisasa hutumia maneno katika kuhamasisha na kuleta
mapinduzi au maendeleo chanya kwa jamii yake inayomzunguka. Mfano, Rais
Magufuli ni shujaa katika jamii ya watanzania wa leo lakini siyo mtu anayetisha
kimuonekano, lakini hutumua maneno tu katika kutoa maagizo na maelekezo kwa
viongozi wengine na hivyo kupelekea maendeleo katika nchi yetu.
4.1.4 Shujaa huwa rijali
Kama
ilivvyo kawaida katika tendi za Kiafrika, nguvu za kimwili za shujaa wa utendi
wa Kiswahili huambatana na urijali ambapo shujaa huwa na uwezo wa kufanya
mapenzi na mwanamke/ wanawake kwa muda mrefu bila ya kuchoka. Katika utendi huu
Wagalla wanavutiwa na umbo la Liyongo, wanataka wapate “mbegu yake na wanaipata
“ . Suala hili linaweza kuonekana katika beti zifuatazo
6.
Liyongo
kitamkali
Akabalighi
rijali
Akawa
mtu wa kweli
Na
haiba kaongeya
40.
Wagala
wakabaini
Kumwambia
sulutwani
Twamtaka
kwa thamani
Kijana
kutuweleya
41.
Twaitaka
mbeu yake
Nasi
kwetu tuipeke
Kwa
furaha tumuweke
Apate
kutuzaliya.
Sifa
hii ya urijali kwa shujaa katika jamii ya sasa haina mashiko kwani shujaa
hupaswa kufanya mambo yale chanya na muhimu kwa jamii yake na siyo kufanya
mapenzi, pia katika jamii ya sasa magonjwa ya zinaa ni mengi ukiwemo Upungufu
wa Kinga Mwilini (UKIMWI).
4.1.5 mashujaa
wake wakuu ni wanaume tu. Pia katika
tendi karibia zote alizozisoma mwandishi, Ilibainika kuwa katika tendi za Kiswahili mashujaa wote ni wanaume hivyo kuleta
dhana ya mfumo dume uliopo katika jamii kwa kuona kuwa wanaume tu ndo huweza
kutenda matendo ya kishujaa. Mfano, shujaa Nyakiiru na Kanyamaishwa katika Utendi wa Nyakiiru Kibi, Mtume Muhammad katika utendi wa Rasil Ighul. Katika utenzi wa
Fumo Liyongo, Tunaona kuwa shujaa
mkuu ni Liyongo ambaye anaonekana kama mwanaume mwenye nguvu.
Suala
hili ni tofauti au linakosa uhalisia katika jamii ya sasa ya watanzania na
ulimwengu mzima kwa ujumla kwani kuna
dhana ya ufeministi ambayo imetawala katika jamii. Unasisitizwa usawa, pia katika
jamii ya sasa kuna baadhi ya mashujaa wa kike. Kwa mfano Bibi titi Mohamed
ambaye alishiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika kutoka kwa wakoloni
akiwa sambamba na mwalimu Jukius k Nyerere.
Suala
la kuwachukulia wanaume kuwa ndiyo mashujaa linaonyeshwa kupitia shujaa wa Utenzi wa Fumo Liyongo yaani Lyongo
kupitia beti zifuatazo
13.
Ni
mwanamume swahihi
Kama
simba nazihi
Usiku
na asubuhi
Kutembeya
ni mamoya
15.
Mato
kikodoleya
Ghafula
utazimiya
Kufaa
utakiruibiya
Kwa
khaufa kuingiya
16.
Wagala
wakipulika
Kwa
dhihaka wakateka
Wakanena
“twamtaka
Na
sisi kumwanagliya.”
4.2 Usaliti,
katika tendi nyingi za Kiswahili hususani katika utendi huu, dhana ya usaliti
imejitokeza wazi kwa mtoto wa shujaa Liyongo kumsaliti baba yake kutokana na
uroho na uchu wa mali na madaraka. Usaliti huo ndiyo unapelekea anguko la
shujaa hadi kusababisha kifo chake kwa kuwa tu alimpeleleza baba yake na kupata
kutambua siri iliyo nyuma ya pazia kuhusu nguvu za baba yake baada ya kutumwa
na Sultwani kumpeleza na kisha amuue baba yake. Hivyo anamuua baba yake kwa
kutumia sindano ya shaba kwa kumchoma kitovun, alipokuwa usingizini. Mtunzi
anathibitisha hili katika beti zifuatazo
143.
Nisikiya
wangu baba
Liniuwalo
ni baba
Ni
msumari wa shaba
Kitovuni
nikitiya
144.
Jamaasilaha
ya
Haziniuwi
swabiya
Ila
nimezokwambiya
Ni
ya kweli yote piya
145.
Kijana
akisikiya
Shughuli
lalimngiya
Kataka
kusikiliya
Pate
akanene haya.
Jambo
hili la usaliti lipo hata katika jamii za sasa ambapo baadhi ya watu wamekua
wakiwasaliti jamaa zao kwa tamaa mbalimbali zikiwemo za mali. Viongozi
mbalimbali wa kisiasa wamekua wakisaliti wananchi wao kwa mataifa makubwa ya
kibeberu. Kwa kukubali masharti magumu ya misaada na mikopo bila ya
kuwashirikisha wananchi hao, hivyo huo ni usaliti kwani wananchi hao ndio
wanawajibika kulipa mikopo hiyo kuipitia kodi zao.
4.3 Mgogoro kati ya tabaka tawala na
tabaka tawaliwa
likiongozwa na shujaa (Liyongo). Katuka utendi huu Liyongo anaonekana kuwa
katika mgogoro na mfalme wa Pate, hali inayosababisha yeye kukimbia mji huo na
kwenda kuishi porini. Ndipo mfalme anamtumia mwana wa damu wa Liyongo kwa
kumlaghai kumpa sehemu nzuri ya kuishi akisaidiwa na wajakazi na kumuahidi
kumuoza mwana wa mfalme akiifanikisha zoezi la kumuua baba yake. Mfame au
sultan anafanya haya yote ili aweze kumuondoa Liyongo anayeishi katika tabaka
tawaliwa. Anaonekana kutishia utawala wake kwani angeweza kumpindua muda wowote.
Tuangazie beti zifuatazo
154.
Kamkirimu
kijana
Kwa
zitu kulla namna
Malalo mazuri sana
Winyi
kumtumikiya
156.
Kijana kafurahiya
tamaa zikamshika
“
na kuoa ni hakika
huwa
watanitendeya
158.
Kisa kumi kutimiya
Sulutwani kamwambiya
“ hii sindano pokeya
haya kwake sikiliya..”
Suala
la mgogoro kati ya tabaka tawala na lile tawaliwa bado lipo sana katika jamii
ya sasa. Mashujaa kutoka tabaka tawaliwa wanaojaribu kupambana na tabaka tawala
mara nyingi hupata madhila mengi ikiwamo kufa, kufungwa. Mfano Nelson Mandela
wa Afrika kusini, aliyefungwa kwa miaka takribani 27 kwa kwa kupigania haki na
maslahi ya watu weusi wa Afrika kusini waliokuwa wakikandamizwa na utawala wa
kikatili wa mabeberu.
4.4 Tamaa au kugombania utawala na
mali
Katika
kuangalia dhana hii ya tamaa au uchu wa utawala katika utendi huu, mtunzi
anamchora Liyongo kama muhanga wa tamaa
ya utawala ya Sultani na mtoto wake. Ni
mtu mwema anayeponzwa na wema na uwezo wake (Mulokozi 1999). Dhamira ya usaliti
inawasiwiriwa tunamwona mwana wa Liyongo akirubuniwa hadi kumsaliti baba yake
kwa tamaa ya mali na hadhi. Suala hili linaonyeshwa kupitia beti zifuatazo
178.
Kayuwa hana fahamu
Kijana aliazimu
Kwa ile yakwe hamuhamu
Mke kwenda kuzengeya
179.
Kamtiya kitovuni
Naye uleule kwa t`ani
Achamka hamuoni
Kiyana amekimbiya.
180.
Babake akishutuka
Chembe uta ukashika
Kwa haraka akatoka
Nde mui kayendeya
Suala la hili la kugombania utawala na mali,
linadhihirika wazi katika jamii ya sasa, kwani watu wamekua wakitumia hila na
nguvu nyingi katika kupigania utawala, mfano viongozi au wanasiasa wengi kutoka
bara la Afrika wamekuwa wakisababisha vita na migogoro mbalimbali kutokana na tamaa
zao za kushika madaraka. Mathalani; Wanasiasa au viongozi wa Sudani Kusini
Salva kiir na Riek Marshali wamekua wakisababisha vita na migogoro katika nchi
hiyo kutokana na uchu wao wa madaraka, pia migogoro inayotokea katika nchi kama
za Kongo D.R.C, Somalia chanzo kikubwa ni kupigania utawala.
5.0
Hitimisho
Makala
hii imegusia namna tendi za kiswahili zinavyosawirika katika jamii ya sasa kwa
kuangalia uhalisia licha ya ukale wake. Pia katika sehemu hii ya hitimisho
ninapendekeza kuwa lugha ya tendi mbalimbali za Kiswahili ni muhimu
ikarahisishwa ili kuleta uhalisia wa kiswahili kama kinavyotumika katika jamii
yetu ya kisasa. Pia zinaweza kuandikwa tendi juu ya matendo ya mashujaa wa
kisasa waliopo katika jamii za kisasa zilizoendelea katika nyanja za sayansi na
teknolojia, kuliko kubaki tu na tendi zinazoangazia matendo ya mashujaa
yaliyotendwa kataka jamii za zamani.
MAREJELEO
Bowra, C.M (1952). Heroic Poetry. London: Macmillan Publishers.
Mulokozi, M.M (1999). Tenzi Tatu Za Kale.Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili.
Mulokozi M.M (2002). The African Epic Controversy. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota.
Ntarangwi, M (2004). Uhakiki wa kazi za Fasihi.
Augustana College, Rock Island, IL 61201
Vansina, J (1965). Oral Tradition: A Study in Historical
Methodology. Chicago: Aldine Publishing.
Wamitila, K.W (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia.
Nairobi: Focus Publication Ltd.
|
JINA
|
NAMBA YA USAJILI
|
KOZI
|
SAHIHI
|
|
DUTWA DUTWA K
|
2016-04-02493
|
BAK
|
|
0 Comments