Header Ads Widget

Responsive Advertisement

FALSAFA NA MTAZAMO WA SHAABAAN ROBERT


Mwandishi
Sephania Kyungu
Simu: 0756719643
Gmail: Sephaniakyungu1996@gmail.com
Iks UDSM 2019
@masshele swahili.

IKISIRI
Katika makala hii itahabiri kazi mbalimbali za Shaaban Robert za kinathari na zile za kishairi, kwa kueleza kinagaubaga dhana ya falsafa na mtazamo kwa mujibu wa wataalam mbalimbali. Kiini cha makala hii kitahusu uchambuzi na upembuzi wa falsafa na mitazamo ya Shabaan Robert.
1.0 Utangulizi
Njogu na Chimerah (2017) wanaeleza kuwa neno falsafa limetoholewa kutoka neno la Kiingereza Philosophy ambapo kwa Kilatini Philo ikimaanisha "harakati" na Sophia ikimaanisha "busara". Wanaeleza zaidi kuwa falsafa ni busara iliyofikiwa baada ya mtu au watu kutafakari kwa kina kuhusu jambo lolote la kiulimwengu. Aidha, wanabainisha aina mbili za falsafa ambazo ni falsafa ya kiufundi na falsafa ya kijumla. Falsafa ya kiufundi ina istilahi maalumu na mbinu maalumu zinazoielekea katika utafiti pevu, ilihali falsafa ya kijumla ni mtazamo wowote madhubuti wa mtu au watu kuhusu kipengele chochote cha maisha. Kwahiyo, inapozungumzwa kuhusu falsafa ya mwandishi inarejelea falsafa ya kijumla.
Aidha, Barry (2002) anaeleza kuwa kwa kawaida hisia kwa kiasi kikubwa huathiriwa na mazingira anamoishi msanii kwa sababu akili na uzoefu wa mwandishi vinachunguzwa na kuathiriwa na mazingira yanayomzunguka, kama nadharia ya Umarx inavyoeleza. Naye, Vazquez (1973) anafafanua kuwa msanii huathiriwa na kuathiri jamii kwa namna mbalimbali. Hata hivyo, mazingira na makuzi havimzuii msanii kutunga ama kuandika mawazo mapya kabisa ambayo hayapo katika jamii inayomzunguka, kwa sababu msanii anahisia na akili yenye uwezo wa kuibua mawazo mapya yaliyo nje ya mazingira yanayomzunguka. (Finnegan, 1977 na Okpewho 1992).
Hivyo, falsafa ya mwandishi inaweza kutokana na athari mbalimbali za kimazingira yaliyomzunguka mwandishi na makuzi aliyokulia mwandishi ama falsafa mpya ambayo haijatokana na athari za kimazingira.
Vilevile, mtazamo kwa mujibu wa TUKI (2014 ) wanaeleza kuwa ni jinsi mtu anavyochukulia au kufikiria jambo au mawazo ya mtu juu ya jambo fulani.
Kwa ujumla, kama ilivyo falsafa, mtazamo wa mwandishi huathiriwa na jamii inayomzunguka sanjari na makuzi yake.
2.0 Kiini
Katika sehemu hii, falsafa mbalimbali zilizojitokeza katika kazi za kinathari na za kishairi za Shaaban Robert na mtazamo wake kuhusu suala la maisha zimefafanuliwa na kuchambuliwa.
2.1 Falsafa ya Utu/ Ubuntu
Samwel (2015) anaeleza kuwa falsafa ya utu ni falsafa ya Kiafrika inayosisitiza mahusiano na ushirikiano wa jamii kama msingi wa maisha bora na amani katika jamii. Anaeleza zaidi kuwa neno Ubuntu limetoka katika neno la Kizuru na Kixhosa. Falsafa ya utu ni miongoni mwa falsafa iliyojitokeza sana kwenye kazi za Shaaban Robert, kwa mfano katika kitabu chake cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini  anasema:
        "....Utu ulikuwa jambo la aushi lilohusu wanadamu wote na kanuni ilikuwa tabia ya milele, haikufa, haifi wala haitakufa...". (uk. 100).
Katika mfano huu, mwandishi Shaaban Robert anasisitiza kwamba utu ndiyo kiini cha binadamu na yeyote ambaye amekiukana nao si mtu bali ni mnyama.
Aidha, falsafa hii inajitokeza katika kitabu chake cha Adili na Nduguze ambapo mwandishi anasema:
         "...Adili alikuwa si mtu ovyo. Alikuwa ana moyo mwema usiokata tamaa; mvumilivu, mwenye huruma na aliyetayari kusamehe..". (uk.56).
Mwandishi anafafanua zaidi falsafa hii pale anapoeleza:
      "... kama nusu ya watu duniani wangekuwa na moyo kama Adili, nusu ya mashaka yao ungetoweka na bila shaka wangeishi maisha ya peponi hapa na katika ardhi... (uk.56).
Kuhusu falsafa hii Chuachua (2011) anaeleza kwamba Shaaban Robert alikusudia hasa kupafanya hapa duniani pawe mahali patulivu. Watu wote waheshimiane na kupendana. Aliutazama ulimwengu kwa maisha ya wakati uliopita, wakati wake na wakati uliombele yake. Anafafanua zaidi kuwa lengo la Shaaban Robert ni kuwataka watu waishi kwa amani, upendo na utulivu  na hiyo ifanyike kama misingi ya maisha.  Kwa ujumla falsafa hii ni kama kioo cha jamii kujiangalia ili kuona jamii iishivyo, itakavyoishi na jinsi inavyotakiwa kuishi ili dunia ibaki na amani, utulivu na upendo.
2.2 Falsafa Juu ya Mungu
Mbiti (1990) anaeleza kwamba kiontolojia Waafrika wanaamini kuwa Mungu ndiye muumbaji wa kila kitu. Yeye ni wa milele na mkuu kuliko chochote, anafafanua zaidi kuwa Mungu anayafahamu yote na yupo mahali pote. Falsafa hii inajidhihirisha katika kazi mbalimbali za Shaaban Robert ambaye ameathirika zaidi na imani ya Kiislamu kwani anaamini kuwa Mungu ndiye kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Katika riwaya ya Adili na Nduguze mwandishi anasema:
         "...Walionywa na Adili kuwa mwanadamu aliumbwa kwa heri na shari hasa heri...". (uk. 24)
Hii ina maana kuwa mwandishi anaamini mwanadamu hakutegemewa kufikiwa na kheri tupu katika maisha yake, wala asitegemee kufikwa na shari tupu. Anatakiwa aamini kwamba kila kheri na shari katika mzunguko wa maisha na kwamba kheri na shari hizo hutoka kwa Mungu.
Vilevile, falsafa hii inajidhihirisha katika kitabu chake cha "Utubora Mkulima" ambapo mwandishi anasema:
              "... na kama umeamua kujipatia riziki yako kwa kulima itakuwa kheri Insha- Allah..." (uk.45)
Hapa mwandishi ametumia neno insha- Allah akiwa na maana ya "Mwenyezi Mungu akipenda", hapa mwandishi anadokeza kuwa Mungu ndiye mwenye uwezo wote na pia mwanadamu hufanya na kutekeleza mipango yake, lakini mipango hiyo haitekelezeki wala haifanikiwi mpaka Mwenyezi Mungu apende.
Hivyo, katika falsafa hii, Mungu ndiye mwenye nguvu zote na mwandishi anamtaka mwanadamu awe mcha Mungu.
2.3 Falsafa ya Kifo
Temples (1945) anaeleza kuwa fikra za Mwafrika zimetawaliwa na mambo mawili ambayo ni uhai na kifo. Anaamini kuwa Waafrika wanaamini kuna maisha baada ya kifo, aidha baada ya maisha ya hapa duniani hatimaye ni kifo. Shaaban Robert hatofautiani sana na imani ya Waafrika iliyolezwa na Temples, anaamini kuwa kuna maisha baada ya kifo. Falsafa yake juu ya kifo imeathiriwa sana na muktadha wa imani ya Kiislamu ambapo anadai kuwa uzuri au ibaya wa maisha baada ya kifo hutegemeana na matendo ya mtu alipokuwa duniani. Kama mtu alitenda mema ataishi vizuri peponi na kama alitenda mabaya atapata shida huko peponi katika kitabu chake cha Kielezo cha Fasihi kwenye shairi la Mbinguni; mwandishi anazungumzia maisha ya akhera ambapo anaeleza kwamba maisha ni matamu kwa wenye kutenda mema hapa duniani (uk.45), vilevile anaeleza kuwa maisha ya akhera ni ya furaha na hakutakuwa na kufa tena. Huko ni mahali ambako misiba yote haitakuwako tena. Kila mtu atakuwa hana huzuni hata tahayari kucheka.... kila mtu ataridhishwa... faradhi ya mauti itakoma.
Fauka ya hayo, falsafa hii pia inajitokeza katika kitabu cha Kusadikika mwandishi anasema:
     "...Wanadamu hawakuahidiwa aishi katika ulimwengu, aushi yao haipatikani ila katika maisha ya milele, ambayo hana budi kuandaliwa vema na kila mtu kwa bidii zote..."( uk4)
Pia katika Adili na Nduguze mwandishi anasema:
"...Adili alitumika kuwa maisha ni safari na dunia ni matembezi kwa mwanadamu, masikani yao ya milele ni peponi, hapana mtu ambaye atabaki duniani..".( uk.21).
Hivyo, katika falsafa hii, Shaaban Robert alitaka jamii itambue kwamba maisha hayaishi tu hapa duniani bali kuna maisha mengine baada ya kifo ambayo kwayo hutegemea na matendo ya mwanadamu duniani.
2.4 Falsafa ya Ndoa
Hiki ni kipengele kimojawapo cha falsafa ya Afrika kinachojitokeza katika kazi nyingi za kifasihi. Temples (1945) anaeleza kuwa katika maisha ya Mwafrika, ndoa na mimba ni vyanzo vya uhai na hudumishwa kwa kuwa na mtoto ama watoto. Anaendelea kueleza kuwa ili maisha ya ndoa yaendelee na yazidi kuwa na amani na upendo ni lazima suala  mimba na watoto lihusike kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wa Shaaban Robert anaamini kuwa ili ndoa iendelee kuwepo utu ni jambo la msingi, aidha, anadokeza kuwa suala la fedha na utajiri haviwezi kusimamisha ndoa isipokuwa utu. Katika kitabu cha Utenzi wa Adili Shabaan Robert anasema:
      "Hata hivyo ukiweza,
      Samahani kumfanyia,
      Faida itatuliza,
   Kuwajia yeye nawe.

Mkeo mpe heshima,
mhesabu kama mama,
mzaa watoto wema,
ulivyozaliwa wewe.
Katika utenzi huu mwandishi anaonyesha namna utu ulivyo nguzo kwenye suala la ndoa. Kwa upande wake anaona kwamba kitu cha msingi kwenye ndoa ni kuheshimiana, kusameheana na kuvumiliana. Suala la watoto ni majaliwa ya mwenyezi Mungu. Pia mtazamo huu unapatikana kwenye kazi zake kama vile riwaya ya Kufikirika ambapo mhusika Mfalme na Malkia walivyovumiliana katika ndoa licha ya kutopata watoto.
Hivyo, katika falsafa hii Shaaban Robert kuhusu suala la ndoa anaitaka jamii kuthamini ndoa na kuachana na mtazamo kuwa watoto ndio nguzo kuu ya ndoa, badala yake jamii iamini kuwa upatikanaji wa watoto ni majaliwa ya mwenyezi Mungu.
2.5 Falsafa ya Uganga na Uchawi
Samwel (2015) anaeleza kuwa jamii nyingi zinatofautisha dhana ya uganga na uchawi. Uganga unachukuliwa kuwa ni ile hali ya kupata tiba asilia juu ya matatizo ambayo yameshinda kupata tiba kitaalamu, anafafanua kuwa waganga katika jamii mbalimbali za Kiafrika kwa kawaida hutumia miti shamba, mizimu, miungu na mengine yanayofanana na hayo ili kutoa tiba. Kwa upande wa Shaaban Robert kwa namna alivyosawiri waganga yaelekea huamini kwamba waganga wanaweza kutibu kama ambavyo Waafrika wengi wanavyoamini hususani kwa wale ambao hawajapokea imani ya Kikristo wala Kiislamu. Falsafa hii inaitokeza katika riwaya ya Kufikirika pale anaposema:
"...mbiu maalumu ilitangaza habari kwa watu kuwa Waganga wote walitakiwa na Serikali ya Kufikirika. Upesi kama iwezekanavyo watu hao lazima wafike kwa Mfalme Mtukufu wa Kufikirika. Mtu yeyote mweledi wa dawa, utabiri au dua akikosa kutii wito wa Mfalme Mtumufu bila udhuru mwema, lazima atahukumiwa uhalifu na kutotii amri ya serikali wakati wa jambo kubwa la taifa na la haraka linalotaka msaada wa kila mganga. Mtu asiyehudhuria lakini akiweza kujitetea katika mashtaka kwa sababu za kutosha kama vile ugonjwa na mambo mengine ambayo hayaepukiki serikali itamsamehe; lakini akishindwa kufanya hivo na ikiwa itathibitika kuwa ni mhalifu hasira ya Mfalme Mtumufu wa Kufikirika itakuw juu yake pasipo huruma. Waganga wote walitakiwa wakutane kwa Mfalme Mtukufu baada ya siku 30 za tangazo...". ( Uk.4)
Katika nukuu hii, mwandishi anadokeza mtazamo wake juu ya uganga ambapo licha ya waganga hao kuitwa wote kujaribu kutibu ugumba wa Mfalme na utasa wa Malkia kwa kutumia mitishamba na dawa nyinginezo  lakini hawakuweza kumtibu.
Hivyo, Shaaban Robert ana mtazamo tofauti kuhusu suala la uganga na uchawi kwamba waganga hawawezi kutibu badala yake matatizo hayo yanaweza kutibiwa kwa njia nyingine.
2.6 Falsafa Mwandishi Kuhusu Mwanamke
King'ei (1993) anaeleza kuwa tungo nyingi katika fasihi ya Kiswahili zimekuwa zikimsawiri mhusika wa kike kwa njia hasi kuanzia tendi au tenzi za zamani kama vile: Utenzi wa Mwanakupona na Utenzi wa Al-Inkishafi. Hata hivyo, baadhi ya kazi chache katika fasihi huwaonesha wahusika wa kike kwa njia chanya mfano mzuri ni huu wa riwaya ya Shaaban Robert unaoitwa Wasifu wa Siti Binti Saad na katika kazi zake nyingine za kishairi. Kwa mfano mwandishi anamsawiri Siti kama mhusika anayefaa kuigwa na wanawake wengine hata katika jamii ya sasa. Sifa mojawapo ni kuwa mwenye bidii mithili ya nyuki ama mchwa. Shaaban Robert anasema:
   "...Utamu wa mazao ya jasho lake ulipozidi naye alizidi, naye alizidi kufanya kazi kwa bidii vileviel. Mwendo wake ulikuwa kama huu siku zote. Alihudhuria katika taarabu kadha wa kadha katika mji wa Unguja akaimba mchana na usiku kama kurumbizi ..." (uk.16).
Hapa mwandishi Shaaban Robert anaonesha mtazamo chanya kuhusu mwanamke jambo ambalo ni tofauti na watunzi wengine. Aidha katika shairi la Ua mwandishi anamsawiri mwanamke kama ni kiumbe mwenye thamani kubwa katika jamii. Kwa mfano
    " E Ua langu manuka, katika maisha yangu,
     Na faraja ya uzito, kila aina machungu,
  Kwangu ua hili shoto, na kulia pia yangu,
nalifumuapo woto, ni pambo la Ulimwengu,
Ua hili kama skito, ua hili kufu yangu".

"Ni ua kweli sio ndoto  ua ni kipenzi change
ni ua lenye mnato, limevuta moyo wangu
tokea mimi moto, ni lenye mapenzi yangu
ua li kando ya mto, neema kubwa ya Mungu
ua lina zari fito, zenye kiwiti cha mbingu".
Kwa kutumia zanda kama ua pamoja na taswira nyingine Shaaban Robert anamsawiri mwanamke kuwa kiumbe wa thamani kuu pia anabainisha wazi kwamba uhusiano wa mwanamke na mwanaume hukamilika na kufana tu katika asasi na mazingira ya ndoa. kama Waswahili wasemavyo, "Mwanamke ni anga la nyumba" na hapa Shaaban Robert anakumbusha hilo kwa kusimulia jinsi mke mzuri anavyompa mumewe fahari, furaha, amani na hata imani. Katika shairi hili inatahadharishwa kuwa kumfananisha mwanamke na kitu cha kupendeza kama ua sio kumdunisha wala kumuonesha kuwa ni kitu cha kumvutia na kumpumbaza tu mwanamke. Hili si kweli hata kidogo. Lengo la mwandishi ni kuonesha mwanamke ni mwezi wa mwanaume na kwamba wote wawili wanakamilishana na upendo kati yao ndiyo msingi wa utu wao.
2.2.0 Mtazamo wa  Shabaan Robert Kuhusu Maisha kwa Ujumla
Mnenuka (2011) anaeleza kwamba maana na dhana ya maisha na mustakabari wake ni miongoni mwa masuala yaliyowasumbua na yanayoendelea kuwasumbua wanafalsafa na wataalamu mbalimbali kwa sababu ya kutokukubaliana kwao. Hii ni dhahiri kuwa mawazo yatolewayo bado hayawaridhishi wataalamu hao na umma kwa ujumla. Anaendelea kueleza kuwa baadhi ya watu mashuhuri ambao wameathiri mitazamo mikubwa kuhusu maisha na muktasari wake ni pamoja na Gautama Siddhartha anayefahamika kama Buddha (?563-?483 KK) na mwingine ni Confucius (551-479KK) kwa upande wa Mashariki ya mbali; Yesu (?0-?33KK) na Mohammed (?570-632Bk) kwa upande wa Mashariki ya Kati, Democritus (460-? KK), Plato (?427-347 KK), Socrates (?470-399 KK ) na Aristotle (384-322 KK), John Locke (1632-1704 BK), Hegel (1770-1831 BK), Marx (1818-1883 BK) Kwa upande wa nchi za Magharibi. Sheria, mitazamo na maisha ya watu wa Ulaya na Marekani vimeathiriwa na mawazo ya wanafalsafa hao waliotajwa hapo juu, kama ilivyo kwa mifumo ya maisha ya watu wa Mashariki ilivyoathiriwa na falsafa za baadhi ya wataalamu waliotajwa hapo juu na hata Mashariki ya Kati. Afrika, kwa upande wake, imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ontolojia za jamii zao  pamoja na wanafalsafa walioathiri Ulaya na Marekani pamoja na Mashariki ya Kati kupitia ukoloni wa Kiarabu na Kizugu kwa viwango tofauti. Kwahiyo, barani Afrika kuna watu walioathiriwa na ontolojia za jamii zao, wanafalsafa wa Mashariki ya Kati kama vile Yesu na Mohammed na wapo wale walioathiriwa na wanafalsfa wa Mashariki ya mbali na Ulaya na Marekani,  wapo walioathiriwa na mchanganyiko wa falsafa hizo kwa kujua au kutokujua. Athari hizi zinajitokeza pia katima kazi za sanaa hususani fasihi. Ili kufanya sehemu hii kuwa rahisi, ni vyema kuchambua vipengele kimoja bada ya kingine kwa hivyo mjadala huu utagawanyika katika vipengele kadhaa kama itakavyofafanuliwa hapa chini.
 2.2.1 Maisha ni Nini
Kama ilivyodokezwa hapo awali, swali hili ni miongoni mwa maswali yaliyojadiliwa na wanafalsafa wengi bila kupata mwafaka. Swali hili linajadiliwa pia na mwanafasihi wa Kiswahili ambaye ni Shaabani Robert. Kwa upande wake anaamini kuwa haki ni suala jema na anadai kuwa pakiwepo haki basi dunia itakuwa sehemu nzuri ya kuishi kama wazo hilo linavyojitokeza katika shairi lake la Haki. Anasema:
                            HAKI ni jambo aula, walimwengu kutumia,
                               Haki dawa ya mazira, nuru katika Dunia,
                             Na pindi ikitawala, udhalimu hukimbia. (Uk.1)
Pamoja na kutambua umuhimu wa haki, msanii huyu hadokezi njia za kuipata haki hiyo kana kwamba mtu anaweza kupata haki bila kudai. Badala yake, katika shairi lake la Mbegu za Mungu anadai kuwa anayetenda haki anampendeza Mungu na anayefanya vitendo vya dhuluma anajiharibia mbingu. Kama anavyooeleza katika shairi lake la Mbegu za Mungu anasema:
                                        Dhuluma mbaya, haina [M ]zungu,
                                      Wa kufika mbele ya Mungu,
                                    Haitafaa katika mbingu. (Mashairi ya Shaaban Robert, uk.19).
Kwa hiyo, Shaaban Robert anashindwa kudokeza suluhisho la kudai haki kwa nguvu, pengine hii inatokana na athari za wanafalsafa kama vile Mohammed ambaye ndiye aliyemuathiri kwa kiasi kikubwa.
Aidha, Shaaban Robert anayatazama maisha kama sehemu inayokaliwa na watu wenye tabia mbaya na nzuri. Miongoni mwa mashairi yanayodokeza wazo hili ni kama vile: Kitendawili cha Dunia, Tumeharibika pamoja na Ulimwengu na Dunia kutoka katika vitabu vya Insha na Mashairi na Almasi za Afrika. Mfano kutoka katika ubeti wa pili wa shairi la Ila  kama ifuatavyo:
                            Huimba Mwezi na Jua,
                           Umaskini na Mali,
                           Au Bahari na Hewa;
                            Hali na Baridi kali,
                            Na Fahari na Ukiwa,
                            Na Huruma na Halali;
                           Na Milima ya kukwea,
                           Na Mito na Majabari. (Insha na Mashairi, uk.45).
Katika shairi hilo na mengine yaliyotajwa hapo juu, Shaaban Robert anadokeza kwa ufupi pande mbili zinazosigana katika maisha hapa duniani. Kuna masikini lakini pia kuna wenye mali, haramu lakini pia kuna halali. Ameeleza baadhi ya tofauti za msingi za maisha ya watu hapa duniani kuwa binadamu wanatofautiana katika maisha. Kwa hiyo, kuhusiana na tofauti za watu hapa duniani Shaaban Robert anafanana na wanafasihi wengine kama vile Mulokozi.
Aidha, Shaaban Robert anaona njia nzuri ya kuleta amani na afueni ya maisha hapa duniani ni kumuomba Mungu. Wazo hili linajitokeza katika mashairi yake kadhaa kama vile shairi la Okoa Wanadamu kama ubeti huu unavyodhihirisha wazo hilo:
Mungu mtenda mambo,
Okoa wanadamu,
Maisha yao tambo,
Na daima magumu. (Mashairi ya Shaaban Robert, uk.20)
Katika mtazamo huu tunaona kwamba mwandishi kwa kiasi kikubwa ameathiriwa na  mtazamo wa Mtume mohammed kuhusu swala la maisha.
2.2.2 Chanzo cha Maisha ni Nini
Kuhusu chanzo cha maisha Shaaban Robert kwa upande wake anaamini kwamba binadamu anazaliwa kama baadhi ya wanyama wengine lakini mipango hiyo hupangwa na Mungu. Hii inatokana na hoja zinazojengwa na mkondo anaoutumia ambao ndiyo hasa unafafanua kila kitu, yaani kuamini kuwa binadamu hana uwezo wa kufanya kitu kwa uhuru wake kwa sababu kila kinachotokea kinapangwa na Mungu. Shaaban Robert anadai kwamba kabla na baada ya kuzaliwa uhai wa mtu hauko mikononi mwa binadamu, bali kuna uwepo mkubwa zaidi unaoweza kuamua kuwepo au kutokuwepo kwa binadamu, yaani kama ni mtoto, azaliwe au asizaliwe, aishi au afe, kama ataishi kwa muda gani na afanye nini hapa duniani, wazo hili linapatikana katika shairi lake la Tulivyo kama ilivyoelezwa hapo juu. Wazo hili limejitokeza pia katika shairi la Mwanzo na Akheri anapotoa wazo la jumla kuhusu ualfa na uomega wa Mungu kwa kila kitu duniani kama shairi linavyosema:
                                          BARA na bahari vilivyomo vyote,
                                           Mwenyewe kahari ulimwengu wote,
                                           Hanayo chanjali pahali popote,
                                            Wa kwenda urari wa kati wowote. (insha na mashairi, uk. 27).
Mshairi huyu anatuambia kuwa Mungu ndiye mwanzo wa kila kitu, ikiwa ni pamoja na binadamu, yaani kutungwa mimba, kuzaliwa, kuishi na hatimaye kufa. Mwanzo wa hayo tunayaona katika shairi lake la Jalala ambapo anaeleza ukuu wa Mungu katika kutoa uhai au kuondoa kama anavyosema:
MWANA sijampa jina, amefariki ghafla,
Ni kaziye Maulana, sina welevu na hila,
Na kuomba Mungu Bwana, ipe pazuri pahala,
Rohoyo huyu kijana, samehe dhana na ila. (Almasi za Afrika, uk.52).
Kama ilivyodokezwa hapo awali, mkondo wa falsafa ambao ameegemea ni ule unaoamini kuwa binadamu hana nafasi ya kuathiri chochote hapa duniani bila idhini au nguvu kutoka kwa Mungu, anaamini kuwa kifo cha mtoto ambaye hakubahatika kupata hata jina ni mapenzi ya Mungu. Kwa hiyo, binadamu anaishi na kuongozwa na uwepo ambao namzidi nguvu kwa kila kitu. Uwezo huo unaitwa Mungu. Hivyo kwa kiasi kikubwa, tunaona kwamba Shaaban Robert ameathiriwa sana na mtazamo wa mtume Mohammed kuhusu chanzo cha maisha.
2.2.3 Maisha Baada ya Kifo nini Kinatokea
Shaaban Robert anaamini kuwa baada ya kifo binadamu huendelea kuishi katika roho mpaka siku atakaporudishiwa mwili ili kukabiliwa na adhabu au starehe ya pepeoni. Ikiwa mtu alifanya makosa mbalimbali ataadhibiwa na ikiwa alifanya matendo mazuri basi atatuzwa, ndio maana Shaaban Robert anasisitiza umuhimu wa kuishi vizuri ili akapate tuzo huko mbinguni badala ya kutupwa jehanamu ambako atateswa milele na milele kama mashairi yake mengi yanavyosema. Mfano wa mashairi hayo ni: Shairi la Matendo na Fidia na Utenzi wa Neema nyingi Ajabu. Kwa mfano katika Utenzi wa Neema nyingi Ajabu anaeleza thawabu anayoipata mtu aliyefata mafundisho ya dini na baada ya kufa na adhabu inayotolewa kwa mtu ambaye hakuzingatia amri za Mungu na kutenda mabaya alipokuwa akiishi hapa duniani anasema:
                             Adhabu iliyokuu,
                            Ni moto chini na juu,
                             Haifai kusahau,
                            Kuwa hili litakuwa. (Almasi za Afrika, uk.45)
                       
                       
                             Dini anayefuata,
                           Njia njema atapita,
                           Na daraja ya sitara,
                           Kwake pana itakua. (Almasi za Afrika uk.49)
Vilevile, katika utenzi huohuo anasisitiza kuwa macho na shetani kwa sababu shetani anatabia ya kushawishi watu ili wafanye makosa yanayomchukiza Mungu. Mara baada ya kuanguka, yaani binadamu kufanya dhambi, shetani hukimbia na kumuacha binadamu katika dhambi kama utenzi unavyoeleza:      Jihadhari na Ibilisi,
Usimpe nafasi,
Jilinde yako nafisi,
Ama utaangamia. (Almasi za Afrika uk.42).

Kuwa shetani huruka,
Mtu akishaanguka,
Ni neno lenye hakika,
Acha kumuandamia. (Almasi za Afrika uk.42)
Shaaban Robert anahusisha matendo mema na matendo mabaya na adhabu za hapahapa duniani na adhabu na thawabu za kiwango kikubwa zaidi, yaani adhabu ya moto ambayo haina mfano hapa duniani ama kwenda peponi kwenye starehe kubwa kuliko zile zinazopatikana hapa duniani, baadhi ya kazi zinazodokeza wazo hili ni Neema nyingi Ajabu, Matendo na Fidia na katika shairi la Akhera.
2.2.4 Mtazamo wa Shaaban Robert Umeathiriwa na Falsafa Gani?
Mnenuka() anaeleza kuwa Shaaban Robert kazi zake zinaonekana kuwa zimeathiriwa na imani ya dini ya Kiislamu kwa kiasi kikubwa. Msanii huyu anaiona dunia kwa kutumia macho ya dini ya Kiislamu. Mawazo mbalimbali ya Shaaban Robert yanapatikana katika falsafa ya dini ya Kiislamu. Shaaban Robert anatumia kazi zake nyingi kueleza falsafa hii ya dini ya Kiislamu. Kwa mfano, suala la utu ama falsafa ya wema kushinda ubaya limejadiliwa kwa kina katika kazi zake nyingi ambayo ndiyo msingi wa Uislamu.
3.0 Hitimisho
Makala hii imechambua falsafa na mitazamo mbalimbali ya Shaaban Robert katika kazi zake za kinathari na za kishairi, katika kazi nyingi za kishairi ndizo zinazoonekana kuathiriwa mno na falsafa ya utu pamoja na muktadha wa dini ya Kiislamu ukilinganisha na kazi nyingine za kinathari kama vile riwaya ya Kusadikika, Kufikirika na nathari nyingine. Aidha katika Makala hii imebainika kuwa kwa kiasi kikubwa falsafa ya mwandishi hutokana na mazingira yaliyomkuza mwandishi husika. Ingawa si mara zote falsafa ya mwandishi inatokana na mazingira yaliyomkuza.















                                                                   Marejeleo
Barry, p. (2002). Beginning Theory:  An Introduction  to Literally and Cultural Theory. Second Edition. Manchester: Manchester University Press. Toleo la kwanza lilichapishwa mwaka 1995.
Chuachua, R. (2011). Itikadi katika Riwaya za Shaaban Robert. Dar es Salaam: TUKI.
Finnegan, R. (1977). Oral Poetry: It's Nature, Significance and Social Context. Cambridge: Cambridge University Press.
King'ei, K. (1993). Kusadikika-Shaaban Robert. Nairobi: East African Educational Publishers L. T. D.
Mbiti, J.S (1990). African Religions and Philosophy. Oxford: Heinemann. Toleo la kwanza lilichapishwa mwaka 1975.
Mnenuka, A. (2011). "Falsafa ya Maisha katika Ushairi wa Mugyabuso Mulokozi na Shaaban Robert". Kioo cha Lugha. Juz.9. Dar es Salaam: TUKI.
Njogu, K.  na Chimerah, R.  (2017).  Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Okpewho, I. (1992). African Oral Literature: Background, Character, and Continuity. Bloomington & Indianapolis: Indiana University Press.
Robert, S. (1991). Maisha yangu na Baada ya miaka Hamsini. Dar es Salaam. Mkuki na Nyota Publishers.
                  (1951). Kusadikika. Nairobi: Evans Brothers.
                  (1951). Adili na Nduguze. London: Macmillan.
                  (1958). Wasifu wa Siti Bint Saad: Mwimbaji wa Unguja. London: Thomas.
                  (1967).  Insha na Mashairi. Nairobi: Nelson.
                  (1968). Kufikirika. Nairobi: O. U. P.
                  (1969). Utubora Mkulima. Nairobi: Nelson.
                   (1971). Mashairi ya Shaaban Robert. Nairobi: Nelson.
                   (1972). Almasi za Afrika. Nairobi: Nelson.
                    (1973). Kielezo cha Fasihi. Nairobi: Nelson.
  Samwel, M. (2015). Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Meveli Publishers.
Temples, P. (1945). Bantu Philosophy. Paris: Presence Africaine Publishers.
TUKI (2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI
Vazquez, A.S. (1973). Art and Society: Essay in Marxist Aesthetic. London: Merlin Press.



Post a Comment

0 Comments