Header Ads Widget

Responsive Advertisement

FALSAFA ZA SHAABAN ROBERT







FALSAFA ZA SHEIKH SHAABAN ROBERT JUU YA DHANA YA UCHUMI.
👉🏿Salaam wapenda maandishi kwa kuyasoma na kuyaandika. Wapo wapenda maandishi hata kwa kuyatazama tu.Maandishi ni kitabu hata yawe mawili. Nakumbuka wakati nilipokuwa nasoma kitabu cha Sheikh Shaaban Robert kinachoitwa "KIELELEZO CHA INSHA"UK.79 nilipatazama na kupaona pahala ambapo Nguli huyu Mwenyezi amlaze pema,aliweka hadhiri kuwa, hata barua kutoka kwa mpenzi wako ndugu yangu ni kitabu hicho na tena kina manufaa yake. Akisisitiza matumizi ya vitabu na kuyapenda maandishi na namna yanavyoweza kunusuru kipande chochote cha ulimwengu huu na huo ujao kama ilivyowezekana kwenye ulimwengu ule wa jana,basi hata nami nikawaza kuwa naanzaje kuwa na afya njema, halafu nisiandike yaliyojiri juu ya umuhimu wa vitabu Mungu akipenda hapo halafu yake ?.Aliitaja barua humo,ili tu isadifu wakati wao wao . Leo hii hakuna waraka wa karatasi tukumbuke, Ila kuna kioo chenye herufi zisukwazo hata kuumbwa maandishi. Leo kuna mitandao mithili ya hii.HAPANA SHAKA KABISA, NISOMAPO RISALA YOYOTE MTANDAONI, HUHESABU MIMI KUWA NASOMA KITABU TU .WA BAADU.
👉🏿Mada yangu leo hii, ni kwamba nahitaji kufunua kurasa kadhaa za vitabu kadhaa vya HAYAATI SHAABAN ROBERT.Nataka kudondoa vijisehemu tu alivyojitokeza kiuchumi zaidi,huku nikilinganisha hili na lile ili tupate moja kamili. Wakati napitisha jicho kwenye aya za kiuchumi kwenye maandiko yake, basi haraka ikaja aya moja ya Kur-an kichwani, hata wewe hutoshangaa pale nitapoweka mambo kwa rangi nyeupe YA mbingu yaani hadharani.
👉🏿Niliposoma "ADILI NA NDUGUZE",Nilistaajabu Shaaban Robert akianza na kutuamsha na umuhimu wa kodi ilokorofika mahesabu yake.Anaangaza mambo mawili yaliyo tofauti kabisa kabisa pahala hapa,ambapo Mfalme " *Rai aliweza kujua tafsiri ya ndoto YA Ughaibu kuwa jumla ya kodi ilikuwa na kasoro,lakini hakuweza kujua maana ya ndoto ya Janibu, yaani, sababu ya kasoro ile. Mambo katika maisha yamo katika mwendo huu siku zote.Hayajulikani mpaka yamechunguzwa na kuthibitishwa kwanza.Rai alikuwa arifu wa mwendo huu. Kwa hivi, shauri hili liliachwa kwa Maarifa, Waziri Mkuu, kuchunguzwa.*".Kukorofika kwa kodi kunapaswa kuchunguzwa na kufuatilia.Kwakuwa, Mwendo huu wa kupata kasoro na kutojua chanzo cha kasoro katika mahesabu, ni mwendo uliopo katika maisha siku zote. Lakini kumbuka Mfalme Rai hufanikiwa haya kwakuwa ni "arifu" .Arifu maana yake ni mjuzi, mtambuzi, mbainishaji, wakati Waziri Mkuu wake Ni Maarifa.
👉🏿Katika kitabu hikohiko mwandishi akionesha sifa kuu za Mfalme Rai, anataja majanga makuu katika taifa lolote yanayoweza kuchochea udororaji kiuchumi pale aposema " *Kuondoa uvivu, ugoigoi na woga katika nchi ni kazi ngumu.Mambo haya yanapendwa sana na watu ingawa yana madhara kwao.*".Anamsifia Rai na kusimulia katika namna ya mnato wa masikizano na maafikiano, na si wa msuguano na masukumano. Anasimulia katika hali ikupayo sauti mbili.Wakati ya kwanza yakwambia fungu masikio, nako ya pili yasema funga macho. Namna ya masimulizi yenye msukumo kutoka ndani ya nafsi yenye kweli Na haki.Hahahaha! Si wajua bustani yenye maua tofauti Ndiyo yenye utajiri wa ridhaa na ukunjufu wa nafsi zetu. Wacha nikupambie kwa mfano huu. Azungumzwavyo Mfalme Rai,akili yangu ikahama kwenda madrasani wakati nadarasishwa somo la " *AL- 'ITIMAADU' ALAA NAFSY*" yaani " *KUFANYA MAMBO KWA NAFSI YAKO MWENYEWE*".Ni somo fulani hivi,lilikuwa latufunza kuacha kuagizia agizia katika kazi popote inapowezekana.Nakumbuka tulisoma shairi fupi la Kiarabu lisemalo " *Maa hakka jildaka mithlu dhufrik, fatawalla anta jamii'a amrik*" yaani " *Hakuna chenye kutosha kukuna ugozi wako mithili ya ukucha wako,basi tawalia mambo yako kwa amri yako*".Huwa nakumbuka tu mie kumbe huenda hata BWANA MSA natumia kanuni hino kumfuundisha Jamilah kulea mwanawe katika Riwaya ya " *KOSA LA BWANA MSA*",pale mtoto wa Jamila ajifunzae kutembea anapoanguka na mamaye kumkimbilia amwinuwe. Bwana Msa Asema " *Hapana usimwaribu mtoto.Mtoto aangukapo usimwinuwe ila mwambie inuka.*".Ohoo! Ya Bwana Msa yana kurasa zake, twendeni na Shaaban Robert.
👉🏿" *Adili. .....hakuacha kuhesabu kitu alichonunua wala alichouza. Vitu vyote, kilichoingia ndani,na kilichotoka nje vilitiwa daftarini kwa uangalifu. Mali bila daftari, hupotea bila habari. .............Hakika mtu anayehesabu mapato na matumizi yake hafi masikini*"UK.12.Kuandika mahesabu ni katika harakati za ufuatiliaji wa kuondoa kasoro za ukusanyaji wa mapato katika nchi au maisha binafsi.
👉🏿Baada ya nukta hizi habibi,nafsi yangu ikaridhika, basi nikafunua kurasa zake katika "SIKU YA WATENZI WOTE " ambamo anasema " *Shindano la wazimu, kati ya matajiri na masikini linaangamiza maisha ya mataifa katika ulimwengu.*"Ukiisoma vizuri Riwaya hii utabaini kuwa Hayaati Sheikh Shaaban Robert ndo kana kwamba alifahamu kuwa alikuwa anauaga ulimwengu mara kadhaa nimekuwa nikirudua kusema Na kuonesha.Humu ndimo anamotoa suluhu ya mwisho ya kiuchimi katika ulimwengu na kukusisitizia kuwa hakutokuwa na suluhu nyengine katu.Ni jambo la wazi kabisa,ukiwacha mamlaka ambayo Shaaban Robert anaiambia kugawa kwa adili,je! Vipi hali ya mwenye magari 15 na baiskeli 20 pale anapokupakia kwenye gari lake moja kukupeleka kwa mtawala ukaandamane kwakuwa maisha yako magumu. Vipi kwa mtu huyu kama angetoa baiskeli yake moja kwa ridhaa yake kukupa ili uzunguke kwa uuzaji wa machungwa? Vipi kama matajiri wote kwa mwaka wangekuwa wanatoa " *robo ya sehemu ya kumi ya mali yake?*".Kwa wasojua hii ndo iitwayo Zaka.Yaani mali yako kamili ikatwe vipande kumi,halafu tisa vyote vyako ila kimoja kikakatwa robo itayotolewa zaka na robo tatu ukarudishiwa mwenyewe? Ni dunia aloitamani Sheikh Shaaban Robert katika kazi yake hii ninayoiita mimi "MAAGANO".Kushindikana kwa
hili kama si mashindano ayaitayo Sheikh Shaaban Robert ya "wazimu" ni nini sasa? .
👉🏿Nimekuja kuona pia kwa wenye imani wamehusiwa kuwa kukosa baada ya jitihadi tele, hayo ni majaribu tu.
" *Ndugu zangu, katika Maisha yetu twajaribiwa na dhiki namna kwa na namna. Umasikini na njaa na uchi na maradhi ni mifano iliyo wazi.Sisi sote twatakia wengine vitu ambavyo hapana njia za halali za kuvipatia,lakini ushindi wetu juu YA majaribu na mateso umehakikishwa na Mwenyezi Mungu. Amina*".Ameyaorodhesha mashaka yote kwa msisitizo Wa kuiibia isimu ya Lugha ya Kiarabu katika orodha. Katika Kiswahili twasema " *baba, mama,kaka na dada*",wakati katika lugha ya Kiarabu twasema " *abii wa ummi wa akh wa ukht*".Sheikh Shaaban Robert anasema " *Umasikini na njaa na uchi na maradhi....*"akilenga kutaka vikaririke na "na" ilotiwa kila baada ya janga moja, ndiyo itayozindua na kutanabaisha uzito wa haya mambo.
👉🏿Haayati Sheikh Shaaban Robert atabiri mapigano na matengano baada ya ugunduzi wa rasilimali ya uchumi wa taifa ya seruji nyingi chini yake katika mapango ya Amboni. UK.83.
" *Nasema habari jambo ambalo kwa hakika litatokea, na ambalo likitokea litashangaza kabisa ulimwengu kwa manufaa yake.Baada ya huvumbuzi wa mambo mengi ya heri ulimwengu umekabiliwa na fujo na uharabu Wa mtengano. Kila mtengano huzaa mtengano.Hapana mwisho wa kizazi cha matengano.magunduzi yetu mema hayafaidiki kwa fujo* " .Sina hakika kama tangu miaka ya 1960 ambapo kitabu hiki akikiandika, tayari huko Amboni yamenukia machafuko, lakini nina hakika kuwa bado dunia imechafuka na kisa ni neema ya magunduzi ya seruji, gesi, mafuta na madini katika nchi mbalimbali katika dunia yetu na miji mbalimbali katika nchi yetu. MWENYEZI ATUPE NEEMA, ATUPE NA UTULIVU WA NYOYO ZETU. AMIN.
👉🏿Katika mengi niwezayo Kuandika,Sheikh Shaaban Robert anauvunja vunja umasikini kwa nyenzo YA ajaa ambayo ipo siku yake nitaiandikia makala ya peke yake In sha Allah nayo si nyingine ila " *URAFIKI*" .Anasema mhusika Ayub kumwambia Sarah UK.61 " *Urafiki,pia, husaidia sana katika maisha ya masikini;kuoneana huruma-kutendeana hisani ndogo, furaha ijayo kwa fadhili iliyotendwa. Na zaidi ya mambo haya yote mwili na raha huja furaha kuu-furaha ambayo uwezo wote wa maovu mtu hauwezi kuiharibu*"
👉🏿BASI ILE AYA NILOIKUMBUKA NI AYA NDEFU KULIKO ZOTE NDANI YA KUR-AN IKIJITAWALA KURASA NZIMA NA KUPINDUKIAKATIKA BAADHI YA MASHAFU NI (2:282)NA INAHUSU UCHUMI TU. JE! WADHANI NI JAMBO DOGO HILO?
👉🏿Chambilecho Mzee wangu Abdilatif Abdalla(Sauti Ya Dhiki) "Mambo yana mambo yake".Ni mwanagenzi nilotaka kujaribu kutenda ili niithibitishe siha yangu." *Kukosoa ndiyo adili yenyewe hiyo*"Shaaban Robert.Na mkosa kasoro ila akahitaji tu kunirukia basi ndo uanaume huo. "Wanaume ni wawili, arukiaye na arukiwaye "Kasema yeye pia Shaaban Robert.

Post a Comment

0 Comments