Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MKUDE ,HAJIBU IMEBAKI STORI SIMBA

Na EMANUEL MASSHELE imebaki stori! Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya uongozi wa klabu ya Simba kusema kuwa hauna matatizo na wachezaji wake, Jonas Mkude na Ibrahim Ajib, juu ya kuongeza mikataba mipya. Wawili hao wanatarajia kumaliza mikataba yao mwezi Mei mwakani, lakini siku za hivi karibuni wamekuwa wakihusishwa na kutakiwa na mahasimu wa Simba, Yanga, kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Manara, amesema kwamba wachezaji hao wamekuwa wakihudhuria mazoezi kila siku tangu maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na wamesema hawana mpango wa kuondoka Simba kwa hivi sasa. Manara alisema wachezaji hao jana waliungana na wenzao kwenda kambini Morogoro ambako timu hiyo imeweka kambi kujiandaa na mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu. “Tupo nao (Mkude na Ajib) tangu Jumatano na hawajawahi kukosekana hata siku moja mazoezini, sisi wenyewe tunashangaa hizo taarifa za kwamba wamegoma zinatoka wapi,” alisema Manara. Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alithibitisha ujio wa wakala wa Mkude anayejulikana kwa jina la Poul kuwasili nchini akitokea Afrika Kusini kwa ajili ya mazungumzo kwa lengo la kusaini mkataba mpya. Alisema amefanya mazungumzo na wakala huyo ambaye aliwasili nchini juzi kwa lengo la mazungumzo na kuingia mkataba mpya na mchezaji wao huyo. “Kila kitu kitakuwa sawa juu ya wachezaji wetu na ambao wanamaliza mikataba na wanaohitajika na benchi la ufundi, kama Mkude na Ajib tutamalizana nao kwa ajili ya mikataba mipya,” alisema Pope.

Post a Comment

0 Comments