HAKUNA namna! Zikiwa zimesalia siku chache dirisha dogo la usajili kufungwa Alhamisi wiki hii, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, atalazimika kuchukua uamuzi mgumu wa kuwatosa nyota takribani tisa kwenye kikosi chake cha sasa.
Yanga, ambayo juzi ilifungwa mabao 2-0 na JKU katika mechi ya kirafiki, italazimika kufanya mabadiliko ya bila kupenda kutokana na kiwango duni kilichooneshwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.
Lwandamina hana namna nyingine ya kutengeneza kikosi bora kama hatatembeza panga kwa baadhi ya nyota wake wanaoonekana kushuka kiwango.
Katika mchezo huo, Lwandamina alianzisha kikosi cha pili ili kupima uwezo wa kila mchezaji kabla ya kuunda kikosi chake cha kwanza atakachokitumia katika mashindano mbalimbali.
Ili Lwandamina aweze kupata kikosi bora kitakachoweza kutetea ubingwa Ligi Kuu Bara na baadaye kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, anahitaji kufanya uamuzi mgumu kwa kuwatema baadhi ya nyote ili aweze kusajili wachezaji wapya, ambao watakuwa na uwezo zaidi ya wao.
Taarifa za uhakika ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, nyota takriban tisa wanaweza kuondoka Yanga, huku wale wenye mikataba mirefu wakitakiwa kutolewa kwa mkopo ili wakakuze viwango vyao.
Wachezaji ambao wanatakiwa kupitiwa na uamuzi mgumu wa Lwandamina ni pamoja na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub Cannavaro, ambaye kiwango chake kinaonekana kushuka.
Cannavaro, aliyejiunga na Yanga katika msimu wa 2006 wa Ligi Kuu Bara akitokea Malindi ya Zanzibar, amekuwa akiwekwa benchi na Kocha Hans van der Pluijm, kwani alicheza mechi tatu mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Nyota wengine ambao wametajwa kuwa katika orodha ya kuachia nafasi zao Yanga ni pamoja na Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Said Juma ‘Makapu’, Matheo Anthony, Geofrey Mwashiuya, Obrey Chirwa na Malimi Busungu, huku kipa Ally Mustapha Barthez’ akionekana kutakiwa kuwekwa chini ya uangalizi maalumu.
Chanzo hicho kilisema kwamba, wachezaji wameonekana hawana msaada kwa timu hiyo, kwani Lwandamina anatakiwa kufanya usajili wa haraka ili aweze kutengeneza kikosi kitakacholeta ushindani.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wanaonekana kutoridhishwa na kiwango cha wachezaji hao, hasa baada ya kucheza chini ya kiwango dhidi ya JKU.
“Kocha Lwandamina amefanya jambo zuri sana, kwani tumeona wale waliokuwa wakilalamika juu ya kukosa nafasi katika kikosi cha Pluijm, nasi kama viongozi tumemuachia madaraka yote yeye na mkuu wake, Pluijm, waamue ila tumewaambia wafanye haraka ili wachezaji hawa wapate nafasi ya kusajiliwa na timu nyingine,” alisema.
Katika hatua nyingine, Lwandamina alisema aliamua kuwachezesha wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza ili kujua uwezo wao kisoka.
“Hatukuwa na malengo ya kushinda, kwani nilikuwa nahitaji kujua uwezo wa kila wachezaji, sasa nimewaona, nakwenda kuwafanyia kazi,” alisema Lwandamina.
Alisema mpira ni mchezo wa makosa, hivyo amewasoma vizuri wachezaji wake na ametambua upungufu upo katika idara ipi na atafanyia kazi kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, utakaoanza Jumamosi hii.
0 Comments