Header Ads Widget

Responsive Advertisement

NANI KUVAANA NA NANI LIGI YA MABINGWA ULAYA

HATIMAYE jumla ya timu 16 ambazo zitacheza hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zimepatikana.

Kwa mashabiki wa soka, hasa wale wanaofuatilia soka la Ulaya, hapo ndipo kwenye uhondo wenyewe, kwani vigogo hao watakuwa na safari ngumu ya kuitafuta robo fainali.

Hata hivyo, baada ya timu 16 kufuzu, kinachosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ni ile droo ambayo ndiyo itakayoweka wazi timu zitakazovaana kuisaka robo fainali.

Huenda kuna maswali mengi kwenye vichwa vya mashabiki wa kandanda kuhusu droo hiyo.



Itachezeshwa lini?

Kwa wale waliokuwa wakipasua kichwa juu ya swali hilo, droo hiyo itachezeshwa Desemba 12, Jumatatu ya wiki ijayo. Hafla ya mchakato huo itafanyika jijini Nyon, Uswis.

Droo hiyo inachezeshwaje?

Timu zilizomaliza katika nafasi ya kwanza katika kila kundi zitaweka sehemu yake na zile zilizokamata nafasi ya pili zitatengwa peke yake.

Itachaguliwa timu moja kutoka katika timu zilizoongoza katika makundi yao, na kisha mpinzani wake atatafutwa upande wa pili, kwa maana ya zile zilizokamata nafasi ya pili.

Hakuna timu itakayokutana na nyingine ya nchi moja. Washindi hao wa kwanza watacheza mechi zao za kwanza za hatua ya mtoano wakiwa nyumbani.



Ni timu gani zilizofuzu?

Walioongoza katika makundi yao ni Arsenal, Napoli, Barcelona, Atletico Madrid, Monaco, Borussia Dortmund, Leicester, na Juventus.

Walioshika nafasi ya pili ni PSG, Benfica, Manchester City, Bayern Munich, Bayer Leverkusen, Real Madrid, Porto, na Sevilla.

Timu za England zitakutana na nani?

Msimu huu, Ligi Kuu England imeingiza timu tatu katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mpaka kufikia hatua hiyo, ni Arsenal, Leicester na Manchester City ndizo zinazoipeperusha bendera ya England.

Arsenal walikuwa kinara wa Kundi A, haitawezekana kucheza na timu waliyokuwa nayo kwenye mechi za hatua ya mtoano, hivyo hawatakutana na Paris Saint-Germain.

Lakini pia, hawataweza kuvaana na Man City kwa kuwa wanatoka nchi moja.

Kuna uwezekano mkubwa wa Arsenal kukutana na aidha Benfica, Bayern Munich, Bayer Leverkusen, Real Madrid, Porto au Sevilla.

Leicester wanaweza kupangiwa na PSG au moja kati ya timu hizo ambazo zinaweza kukutana na Arsenal.

Man City, ambao walikuwa Kundi C na kumaliza wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Barcelona, huenda wakakutana na Napoli, Atletico Madrid, Monaco, Borussia Dortmund au Juventus.





Nani ana nafasi ya kusonga mbele kati yao?

Kwa haraka haraka ni ngumu, ni mapema mno kutabiri timu itakayosonga mbele kati ya hizo tatu.

Huenda takwimu za hatua ya makundi zikawa na nafasi nzuri ya kubashiri atakayetinga robo fainali.

Arsenal walifuzu wakiwa kileleni mwa Kundi A, ambapo katika mechi sita, walishinda nne, wakatoa sare mbili na kujikusanyia pointi 14.

Arsenal waliruhusu mabao sita pekee, huku wakiwa wamezifumania nyavu mara 18.

Itakumbukwa kuwa msimu uliopita, safari ya wakali hao wa Kaskazini mwa London katika michuano hiyo ilikomea katika hatua ya hii ya 16 bora.

Leicester City ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, walikuwa kinara wa Kundi G ambapo walipata pointi 13 katika michezo sita waliyoshuka dimbani.

Kikosi hicho cha kocha Claudio Ranieri kilishinda michezo minne, kikatoa sare mara moja na kufungwa mechi moja.

Mpaka kinamaliza hatua ya makundi, kilikuwa kimefunga mabao saba, huku kikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Kama ilivyokuwa matarajio ya wengi, Man City wamemaliza nyuma ya Barca kwenye Kundi C.

Walishinda mechi mbili, wakatoa sare mara tatu, na kisha kupoteza mchezo mmoja na matokeo hayo yamewafanya kuwa na pointi tisa.

Wamemaliza hatua ya makundi wakiwa na mabao 12, huku wakiwa wameruhusu mabao 10.

Msimu uliopita, matajiri hao wa Etihad waliishia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya kwa ngazi ya klabu.



Mechi zinaanza lini?

Kwa mujibu wa ratiba ya sasa ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), mechi za raundi ya kwanza zitaanza kuchezwa Februari 14, mwakani na zile za marudiano zitaanza kuchezwa Machi 7.

Facebook


London England


Post a Comment

0 Comments