PAMOJA na mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, kupewa nafasi kubwa ya kunyakua tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu, lakini kwa mujibu wa utafiti, si mchezaji mwenye thamani kubwa barani Ulaya.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kampuni ya Tafiti ya Uswisi, CIES na taarifa kuwekwa kwenye mtandao wao wa CIES Football Observatory, Ronaldo ana thamani ya pauni milioni 110 akizidiwa na hasimu wake, Lionel Messi mwenye thamani ya pauni milioni 161, huku Antoine Griezmann akiwa na thamani ya pauni milioni 115 na nafasi ya kwanza kushikwa na Neymar mwenye thamani ya pauni milioni 213.
Kiungo wa Liverpool, Philippe Coutinho, mwenye thamani ya pauni milioni 63 ameshika nafasi ya 10 katika orodha hiyo ya wachezaji ghali.
CIES wametumia njia za kisasa kupata thamani hizo za usajili katika ligi kubwa tano UIaya (Ligi Kuu England, La Liga, Serie A, Ligue 1, Bundesliga).
Utafiti huo umeangalia umri, mkataba wa mchezaji na klabu, nafasi yake kwenye timu ya taifa, uzoefu na uchezaji wake pamoja na mafanikio, matokeo na kiwango cha ushindani wa timu.
Beki wa Madrid, Raphael Varane, ana thamani ya pauni milioni 42 na Aymeric Laporte (41), hao wakiungana na nyota wanaokipiga La Liga, wakati Manchester United wana wachezaji wawili akiwemo David De Gea thamani yake ni pauni milioni 49 na Paul Pogba pauni milioni 106.
Mchezaji mmoja wa Serie A aliyeingia kwenye orodha hiyo, ni nyota wa Juventus, Leonardo Bonucci ambaye ana thamani ya pauni milioni 42, huku Ligue 1 wakiwa na nyota wawili wote kutoka PSG, ambao ni Marquinhos mwenye thamani ya pauni milioni 40 na Marco Veratti pauni milioni 62.
Wachezaji wengine kutoka Ligi Kuu England ni Sergio Aguero mwenye thamani ya pauni milioni 75, Eden Hazard pauni milioni 64, Kevin De Bruyne (60), Alexis Sanchez (59) na Harry Kane (53).
MADRID HISPANIA
0 Comments