Uungwana ni vitendo, Makonda onyesha vyeti mambo yais
Kwa ufupi
Tangu madai haya yaanze kutolewa, Makonda ambaye amejitanabaisha kuwa mtu safi na mwadilifu hajajibu chochote, watu wamesubiri sana na wengine wameanza kungalia kwa Rais John Magufuli aliyemteua kuona kama atasema lolote.
By Glory masshele
Kwa takriban wiki mbili sasa kumekuwa na madai kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa alitumia vyeti vya kidato cha nne vya mtu mwingine hadi akafanikiwa kuendelea na elimu ya vyuo vya kati na hatimaye kufika chuo kikuu.
Tangu madai haya yaanze kutolewa, Makonda ambaye amejitanabaisha kuwa mtu safi na mwadilifu hajajibu chochote, watu wamesubiri sana na wengine wameanza kungalia kwa Rais John Magufuli aliyemteua kuona kama atasema lolote.
Lakini, bado hatuoni kauli wala hatua zikichukuliwa kubainisha ukweli. Tukumbuke kuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye sasa ni mbunge wa kuteuliwa, Anne Kilango Malecela alivyotenguliwa kwa kosa la kusema uongo, kesho yake tu mtu alitangazwa kutimuliwa.
Ni kweli kwamba tuhuma hizi zimeibuliwa wakati alipotangaza majina ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya. Inawezekana waliotajwa ndiyo hao hao walioibua kashfa hii au inawezekana ni watu wengine wenye mapenzi mema.
Kwa hiyo, Makonda kama kiongozi muungwana anapaswa kuthibitisha kama madai hayo ni kweli au uongo. Huu siyo wakati wa kujificha kwenye kivuli cha vita ya dawa za kulevya.
Kwa wiki zote hizi mbili na ushei, Makonda amekuwa akiibukia kwenye majukwaa tofauti na kuyahusisha madai hayo na vita ya dawa za kulevya. Hiyo vita yenyewe ya dawa za kulevya ina mjadala mpana, sitaufanya kwa leo.
Sawa, hata kama ni madai yatokanayo na vita ya dawa za kulevya, basi awajibu hao wanaomzushia kwa kuwaonyesha vyeti vyake halisi? Tatizo nini kama vyeti vipo?
Mara utamsikia yuko kwenye tamasha hili anajitetea hivi, mara yuko msikitini anajitetea hivi, mara yuko kanisani analia machozi kuwa anazushiwa. Hayo yote yangekuwa na maana sana iwapo angeweka mezani vyeti vyake vya shule. Huo ndiyo uungwana.
Mtu kufeli mtihani siyo kosa la jinai, lakini kutumia cheti cha mtu mwingine kama ni kweli hilo ni kosa. Mbaya zaidi cheti hicho kinapomwezesha kupata madaraka makubwa katika jamii. Halafu anayatumia madaraka hayo kujionyesha kuwa mwadilifu huku akiwananga wenzake.
Maana ni afadhali mtu ukae kimya tu ufunike kombe mwanaharamu apite, lakini ilifika mahali Makonda akawa anajiona kuwa kauli yake ni kama kauli ya Mungu. Sasa huu ni wakati wa kuonyesha ujeuri kwa wanaomzushia kuhusu elimu yake ili nao wafunge midomo wakose hoja.
Tatizo linakuja pale, hata mamlaka zinazohusika na elimu zinapoamua kukaa kimya, mfano wizara ya elimu na hasa Baraza la Mitihani la Taifa linalotangaza kila siku kusaka watu wanaotumia vyeti vya wengine na kufikia hatua ya kuwataka wanancdhi watoe taarifa, nalo liko kimya. Kulikoni?
Si lazima mamlaka hizo zijitokeze kumkandamiza au kumtetea, bali zinatakiwa zijitokeze kueleza ukweli wa suala hilo ili kutumiliza hali ya hewa na kama kuna watu wanaomzushia Makonda waonekane na hata kuchukuliwa hatua.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, kumekuwa na uhakiki wa vyeti wa watumishi wa umma, uhakiki umekuwa mrefu, watu wanakaguliwa mara mbilimbili, ili kubaini pia watumishi hewa. Watu wamesimamishwa kazi, wengine wamekimbia na wengine wameshitakiwa mahakamani. Je, uhakiki huo hauwahusu wateule wa Rais?
Kama hauwahusu, basi zoezi zima halina maana, kwa sababu viongozi ndiyo wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wengine. Utaulizaje cheti cha mtumishi wakati wewe umeshindwa au umekataa kuonyesha chako?
Mbona mkurugenzi mmoja wa halmashautri alipoteuliwa na kulalamikiwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa hana sifa, Rais Magufuli baada ya kumwapisha alimwambia onyesha vyeti vyako na akaonyesha na vikapigwa picha.
nadhani utaratibu huo ndiyo ungekutumika kujibu hoja kama hizo badala ya kuzipotezea.
Uhakiki umesababisha Serikali ishindwe kutoa ajira mpya, mishahara haijapanda, halafu unasikia madai kuwa mteule mmoja hana cheti. Kama ni kweli hii ni aibu kwa Serikali na hakuna haja ya kujisafisha ila kuonyesha vyeti halali au kukubali kuwajibika.
Pia, Serikali ingetumia taarifa za watu mbalimbali kama waliosikika mara kadhaa wakidai kuwa na ushahidi wote wa madai hayo. Wangepewa ushirikiano na kuonyesha walicho nacho ili ukweli ujitenge kutoka kwenye uzushi.
Pamoja na yote hayo, bado narudia wito wangu kuwa Makonda ajitokeze hadharani na vyeti vyake halali na kuweka bayana ukweli, maana uongo ukisemwa sana unaaminika kuwa kweli, sasa kabla haujaaminika, Makonda aonyeshe uungwana kwa kuweka wazi historia yake ya elimu
0 Comments