Azimio la Kazi ni nini?
Ni mwongozo unaoandaliwa na Mwalimu ambao unaonesha mpangilio wa kufundisha mada mbalimbali katika Muhtasari wa somo husika.
Mwongozo huu unatokana na Muhtasari wa vitendo vya masomo (kwa elimu ya awali) au somo na uonesha mpangilio wa Mada Kuu na Mada Ndogo ambazo zitafundishwa darasani kwa muda uliopangwa.
Kwa ujumla Azimio la kazi ni mpangilio au utaratibu unaomwezesha mwalimu kuchanganua muhtasari wa somo na kupanga mada na jinsi atakavyozifundisha katika kipindi cha wiki, mwezi na muhula. Azimio la kazi huonesha njia atakazotumia mwalimu katika ufundishaji wake katika kila mada, na vifaa atakavyohitaji.
Hivyo, azimio la kazi ni mpango wa ufundishaji kwa kipindi fulani.
UMUHIMU WA AZIMIO LA KAZI
- Kuandaa andalio la somo kunahitaji rejea ya azimio la kazi
- Ufundishaji unahitaji kwenda na mtiririko mzuri wa mada
- Kutoa nafasi ya kufanya marekebisho ya mwelekeo inapobidi
- Huonesha wapi mwalimu alipofikia hivyo kumpa nafasi mwalimu anayempokea somo lake kujua pa kuanzia
- Huonesha zana na vifaa vya kumsaidia mwalimu katika ufundishaji wake
- Humuonesha mwalimu muda wa kufundisha kila mada
- Huonesha malengo ya ufundishaji wa somo hilo katika muda aliopanga na jinsi alivyojitahidi kuendana na muda huo
VIPENGELE MUHIMU VYA AZIMIO LA KAZI
Muhula:
Sehemu hii huandikwa namba ya muhula ambapo azimio la kazi litatumika
Mwezi:
Huandikwa jina la mwezi ambapo mada fulani zitafundishwa
Ujuzi:
Ni maarifa, stadi na muelekeo anaoupata mwanafunzi baada ya kujifunza mada husika.
- Maarifa, ni utambuzi anaoupata mtu au mwanafunzi baada ya kujifunza jambo fulani
- Stadi, ni ule uwezo wa mwanafunzi kutumia viungo vyake vya mwili kufanya jambo linalotokana na somo alilojifunza, mfano kucheza, kuumba vitu mbalimbali, kufanya majaribio katika maabara, ufaraguzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
- Mielekeo, inahusu mabadiliko yanayohusu stadi za maisha.Hii ni pamoja na mwanafunzi anavyobadili mwelekeowake kutokana na mambo aliyojifunza.
Wiki:
Sehemu hii huandikwa idadi ya wiki katika mwezi fulani ambapo sehemu fulani ya mada itafundishwa
Idadi ya vipindi:
Huandikwa idadi ya vipindi watakavyofundishwa katika idadi ya juma au majuma yaliyooneshwa
Mada kuu:
Hapa huandikwa mada kuu husika kama inavyoonekana katika muhtasari wa somo
Mada ndogo:
Hapa hujazwa mada ndogo kama ilivyo katika muhtasari wa somo
Vitendo vya ufundishaji:
Hapa hujazwa vitendo atakavyofanya mwalimu katika kujiandaa kufundisha mada husika na atakavyowashirikisha wanafunzi katika harakati za kufundisha na kujifunza
Vitendo vya ujifunzaji:
Hapa hujazwa vitendo vitakavyofanywa na wanafunzi kwa maelekezo ya mwalimu. Vitendo hivyo ama ni vya kujiandaa kujifunza katika muhula ufuatao au wakati uliopo wa muhula
Vifaa/zana:
Katika sehemu hii mwalimu anapaswa kuonesha vifaa au zana mbalimbali atakazotumia wakati waufundishajiwa mada ili kuweza kufanikisha ufundishaji na kuweza kufikia lengo lako mahsusi
Rejea:
Hapa mwalimu ataonesha vitabu alivyotumia kama rejea katika mada anayofundisha
Maoni:
Katika safu hii mwalimu atatoa maoni yake kuhusu mafanikio aliyoyaona, matatizo yaliyojitokeza na mapendekezo ya kuboresha ufundishaji.

0 Comments