Kwa Mukhtasari
Fasihi ya watoto ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto na huweza kuwa hadithi, ushairi, visakale au drama.
FASIHI imeeleweka kama sanaa inayotumia lugha kuwasilisha ujumbe unaomhusu binadamu. Hata hivyo, ipo fasihi ya watoto ambayo siku za hivi karibuni imeanza kupata mashiko kutokana na tafiti pamoja na maandishi mengi yanayofanywa.
Fasihi ya watoto ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto na huweza kuwa hadithi, ushairi, visakale au drama.
Dhana mtoto ina utata katika kuieleza. Inaweza tu kufafanuliwa kwa kutegemea mwega wa mtoa maana hiyo. Hii ni kutokana na mawazo kuwa mtoto anaweza kufafanuliwa kwa njia mbalimbali kwa kutegemea sheria, dini, biolojia na hata saikolojia.
Kwa jumla tunaweza kueleza fasihi ya watoto kama sanaa inayotumia lugha kuwasilisha ujumbe unaowahusu watoto. Baadhi ya sifa za fasihi ya watoto ni pamoja na;
Msuko mwepesi
Misuko ya kazi za watoto huwa miepesi ili kumwezesha msomaji kuweza kufuata matukio yenyewe. Msuko huo mwepesi hutilia maanani sana matukio na aghalabu hukitwa kwenye muundo wa A-B-C-D. Muundo huu wa A-B-C-D ni muundo sahili, yaani wa moja kwa moja. Pengine muundo huu huzingatia kuwa mtoto akichanganyiwa matukio, anaweza kuchoka na kuacha kufuatilia kazi husika au labda hata asiielewe kabisa.
Ukubwa wa maandishi
Kazi za watoto hasa vitabu huchapishwa kwa maandishi yenye ukubwa tofauti. Kazi inayowalenga watoto wadogo sana hasa wale ambao kwanza ndio wameingia katika ulimwengu wa usomaji huwa zimesheheni maandishi makubwa yanayoweza kuonekana. Iwapo mtoto ni wa kiwango cha kati yaani darasa la nne na tano maandishi yao bado yatakuwa makubwa lakini si kama yale ya darasa la pili.
Pia maandishi ya kazi za fasihi za watoto wa darasa la sita na saba yatakuwa madogo kuliko yale ya watoto wadogo zaidi.
Maandishi hayo pia hutiwa rangi ili yavutie macho ya watoto. Rangi zenyewe huwa za kupendeza na huteuliwa kiufundi. Hali hii huchangia kuvuta makini ya watoto na kuwachochea kuisoma kazi teule.
Matumizi ya fantasia
Fantasia ni hali ya kuwepo kwa mambo ya ajabuajabu katika kazi ya fasihi yasiyotarajiwa kutokea katika maisha ya kawaida. Ni dhana inayotumiwa kueleza kazi ya fasihi ambayo ina sifa ambazo zinakiuka uhalisia, Wamitila (2003). Fantasia huleta mvuto wa kipekee katika kazi za watoto na hivyo kufanya watoto wengi kufurahia sana kazi ambazo zina fantasia.
Lugha nyepesi
Kazi ya watoto huwa na lugha rahisi inayoendana na hadhira ya watoto. Lugha 'changa’ hutumiwa. Uchanga wake unakuwa katika hadhi ya tungo kama sentensi fupi. Miundo migumu na sentensi changamano hazipendekezwi kutumiwa katika fasihi ya watoto isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo. Wepesi wa lugha hutokana na umri na uwezo wa wasomaji. Urazini wa watoto kwa kawaida ni mdogo. Hivyo basi, sharti sentensi zinazotumiwa ziwe fupi, sahili na zenye kueleweka bila mkanganyo. Hata hivyo, usahili wa lugha haupaswi kuchukuliwa au kueleweka kuwa uchapwa au hali duni ya matumizi ya lugha.
Kazi nyingi huwa ni fupi
Aghalabu fasihi ya watoto huhusisha tungo fupi. Mtoto anapopewa kitabu asome, kwanza huangalia picha na baada ya hapo huangalia ukubwa wa kitabu. Ikiwa kitabu kina kurasa chache, hapo huhamasika kukisoma kwa sababu anajua atamaliza kukisoma kwa haraka. Kama ni kitabu kikubwa, mtoto hushikwa na uvivu hata kabla hajaanza kukisoma.
Kazi ndefu huwachosha watoto na hivyo huweza kupoteza mvuto kabisa kwa watoto. Hadithi za watoto hazina kina au undani wa kimasimulizi ambao hudhihirika katika fasihi ya watu wazima. Usimulizi hujikita katika maelezo ya mambo ambayo huwa ni muhimu tu katika kuijenga hadithi na kuubainisha muktadha wake.
Husheni vielelezo; picha au michoro yenye rangi
Fasihi ya watoto huwa na vielelezo na picha tena zenye rangi. Hali hii huwafanya watoto kutosahau kwa urahisi kile walichosoma lakini pia huwasaidia kuhusisha matukio katika hadithi na ulimwengu halisi.
Wahusika na uhusika
Fasihi ya watoto huwa na wahusika na uhusika wa aina mbalimbali. Kuna kazi ambazo huwa na watoto kama wahusika wakuu. Vinginevyo, fasihi ya watoto hutumia kwa kiasi kikubwa wahusika wanyama. Wanyama hawa hufuata tabia za watu; wanazungumza na kutenda matendo ambayo kwa jumla yanahusishwa na watu.
Isitoshe, katika fasihi ya watoto, wahusika wanaweza kuwa mazimwi na majitu. Zimwi ni kiumbe ambaye anapewa sifa zinazokiuka sifa za binadamu na huwa na sifa hasi kama ulafi, ukatili, ubaya, uovu na kadhalika.
0 Comments