Header Ads Widget

Responsive Advertisement

VIPENGELE VINAVYOJENGA NA KUKUZA TOFAUTI KATI YA FASIHI YA WATOTO NA YA WATU WAZIMA


Kwa Mukhtasari
FASIHI ya watoto ni sanaa inayotumia lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyo chini ya umri wa miaka 18.

Kama ilivyo katika sanaa nyinginezo, mvuto ni kitu cha msingi katika fasihi, japo sifa hii ni kipengele muhimu zaidi ambacho kimepania kutofautisha fasihi ya watoto na ile ya watu wazima. 
Noun (2010), anasema kwamba fasihi ya watoto ni dhana inayorejelea utunzi unaowalenga watoto pekee. Huweza kuwa ama hadithi, ushairi, visakale au drama ambazo zimetungwa kwa ajili ya watoto wadogo na vijana.
Fasihi ya watoto hivyo basi inajikita katika mambo matatu makuu; yaanimhusika mkuu lazima awe ni mtoto, dhamira yake iwahusu watoto na lugha sahili itumiwe kuendeleza msuko. 
Sigh (2002) anasema kuwa fasihi ya watoto lazima iwe inaonyesha matendo na maisha ya mhusika kinaganaga, isawiri mhusika akitia hamasa na pia lazima iwe inaburudisha. 
Japo ni vigumu kuweka mipaka dhahiri baina ya fasihi ya watoto na fasihi ya watu wazima kutokana na sababu za mwingiliano, kuna baadhi ya vipengele ambavyo vinajenga na kukuza utofauti kati ya aina hizo za fasihi:

Matini 
Katika fasihi, kuna miundo mbalimbali kama vile changamano, sahili na rejea. Ikiwa wazo kuu la kazi litakosa kuwalenga watoto, basi huenda utunzi huo usipokelewe vyema.
Kazi ambayo inakusudiwa kuwa ya watoto sharti iwe na lugha rahisi inayoendana na hadhira ya watoto.
Miundo migumu ya sentensi na ploti changamano haipendekezwi kutumiwa katika fasihi ya watoto isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Mtoto atashawishika zaidi kuendelea kuisoma kazi fulani endapo hatakabiliwa na ugumu wowote wa msamiati na misemo katika usomaji wake.

Uhusika 
Katika fasihi ya watoto, kuna wahusika ambao ni watu wazima wenye kuvaa uhusika wa watoto na sehemu ambapo ilitegemewa awepo mhusika mtoto akawekwa mtu mzima.
Japo kwa upande wa fasihi ya watu wazima hali hii hujitokeza pia, watoto hufikiria tofauti kabisa na watu wazima. Hivyo basi, kazi inayoendana na fikira zao itakuwa imefanikiwa kuiteka pakubwa saikolojia ya watoto ambao ni walengwa wa kazi hiyo. 
Mtoto atakapoona kuwa wahusika wakuu katika kazi ya fasihi ni watoto, anaweza kushawishika zaidi kuisoma kazi hiyo kwa hamu ya kutaka kuridhisha matamanio yake. Watoto hupenda hali ambapo mhusika mkuu husawiriwa kuwa shujaa. 
Katika kuzikabili changamoto zinazomkumba, mhusika huyo anafaa kuwa kielelezo cha maadili.
Wahusika wanapochorwa, ni lazima kuwe na mhusika mwema na mhusika mwovu kwani hali hii huwavutia sana watoto kuliko watu wazima.
Ni vyema wahusika kama wanyama wapewe uhai na sifa za utendaji kwa sababu watoto hufurahia sana wanapoiga sauti na milio ya wanyama mbalimbali. 
Jambo hili hukosekana katika fasihi ya watu wazima ambao wana uwezo wa kufasiri  mambo na kutambua vigezo vinavyotofautisha ubaya na uzuri, ukweli na uongo  kutokana na ukomavu wa urazini wao. 

Taharuki 
Kama chombo muhimu katika fasihi, taharuki itamfanya msomaji wa hadithi aendelee kuizamia kwa lengo la kujua kile kinachofuatia.
Fantasia huleta mvuto wa kipekee katika fasihi ya watoto na hivyo kuwafanya kufurahia kazi ambazo huwatoa nje ya ulimwengu wa kawaida.
Huenda sifa hii isidhihirike kwa uwazi katika fasihi ya watu wazima. Fantasia ni hali ya kuwepo kwa mambo ya ajabu ajabu yasiyotarajiwa kutokea katika maisha ya kawaida. 
Japo hali hii hujitokeza katika fasihi ya watoto na ya watu wazima, ubainifu wake katika kazi za watoto ni wa kiwango cha juu. 

Falsafa 
Kazi ambayo ni fasihi inayowalenga watoto ni lazima iwe na mtazamo wa watoto na mambo yanayowavutia watoto. Hii ni kutokana na kwamba kazi nyingi za kifasihi hutungwa na watu wazima ambao pia ni waandishi wa fasihi ya watoto.
Hivyo, hutokea mwingiliano mkubwa wa mawazo na kushindwa kubaini yapi ni mawazo ya watoto na yapi ni ya watu wazima.
Ili hali hii ya mwingiliano iweze kuepukika, ni dhahiri kwamba kunahitajika kuwepo kwa sheria madhubuti na zenye kutekelezeka zitakazodhibiti kazi hizi mbili zisiweze kuingiliana, hasa kwa watunzi na wasomaji.
Watunzi wa fasihi ya watoto wanastahili kujikita katika fasihi hiyo tu na wale wa fasihi ya watu wazima pia wajikite katika fasihi ya watu wazima tu ili kuwapa wasomaji urahisi wa kujua mipaka ya kazi hizo.

Uwasilishaji 
Mada zinazowahusu watoto huwasilishwa kwa njia inayovutiasana tofauti na ilivyo kwa watu wazima. Watoto wengi wanapenda kazi zinazosimulia matukio ya safari.
Kazi yoyote inayohusu mada hizi itakuwa imefanikiwa pakubwa kuitwa fasihi ya watoto.
Ni lazima utunzi unaowalenga watoto uwe mfupi na ya kiutendaji kwani kazi ndefu huwachosha watoto na hivyo kupoteza mvuto kabisa kwa hadhira.
Pia kazi za fasihi ya watoto huwa na michezo kwani watoto hupenda kunasibishwa na mazingira hayo. 
Michezo huwafanya watoto wasichoke kuisoma au kuisikiliza kazi hiyo. Mwisho wa hadithi katika fasihi ya watoto unastahili kuibua hisia za furaha badala ya huzuni.
Funzo kuu lapaswa kumshajiisha msomaji na kujenga hali ya kujiamini ndani yake anapojitayarisha kukabiliana na maisha utu uzima. 

Post a Comment

0 Comments