Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Bainisha media mbalimbali za kisasa ambazo unaweza kuzitumia kufundisha stadi yoyote ya lugha.





Mkiwa ni walimu tarajali wa kufundisha Kiswahili wanafunzi wageni mnatarajiwa kutumia media za kisasa ili kufanikisha jukumu hilo.


Bainisha media mbalimbali za kisasa ambazo unaweza kuzitumia kufundisha stadi yoyote ya lugha.


Kisha chagua media moja na ueleze kwa ufasaha namna utakavyoitumia darasani kufundisha stadi ulioichagua.
Fafanua faida ya media hiyo katika kufanikisha ujifunzaji wa lugha ya kigeni.


Onyo hairuhusiwi kuiga ama kunakili makala hii kwaajili ya matumizi ya kitaaluma badala yake itumike kama mwongozo tuu na njia ya kukuongezea maarifa.

Info.masshele@gmail.com
Imehaririwa na Dk Msigwa




Katika makala hii tumeligawa katika sehemu kuu tatu, utangulizi, kiini na hitimisho, ambapo katika utangulizi tumefasili maana ya lugha ya kigeni, media za ufundishaji lugha na stadi za lugha, sehemu ya kiini tumebainisha media mbalimbali zinazotumika katika ufundishaji wa lugha za kigeni, jinsi zinavyotumika kufundishia stadi ya kusikiliza, kisha tumechagua media moja namna inavyotumika katika darasa la lugha ya kigeni au lugha ya pili na tumeeleza faida ya media hiyo katika ujifunzaji wa lugha ya kigeni na mwisho hitimisho.


Stern (1983), anafafanua kuwa lugha ya kigeni ni lugha ambayo mtu na kuitumia lakini wazungumzaji wake wazawa wapo nje ya nchi ya mjifunzaji huyo.


(Mtandao), lugha ya kigeni ni lugha ambayo unajifunza na kuitumia lakini wazungumzaji wake wako nje ya nchi au mbali na jamii anapokaa mwanafunzi huyo. Kwa mfano lugha ya Kiingereza ni lugha ya kigeni hapa Tanzania(www.masshele.blogspot.com/ 31707436/mbinu_za_ufundishaji_kiswahili_kwa wageni.


Kwa ujumla tunaungana na fasili hizi ambazo zinaelezea mambo ya msingi kuhusu dhana ya lugha ya kigeni.
Longman (1987) wanafasili kwamba neno media asili yake ni lugha ya Kilatini ambalo ni medius ambapo wanasema kwamba media ni zana, njia ambazo hutumika kuwasilishia ujumbe kwa kuona au kutamka.


Aidha Rossi na Biddle (1967), wanasema kuwa media ni kifaa chochote ambacho hutumika au kutumiwa kuwasilisha ujumbe ama taarifa kati ya mtu na mtu au watu na watu.


Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa media za kisasa ni njia za kisasa zinazotumika katika mawasiliano kati ya mwalimu na mwanafunzi katika darasa la kujifunzia lugha ya kigeni.


Massamba (2009) anaeleza kwamba stadi za lugha ni ujuzi anaoupata mtu katika kujifunza lugha mfano kusema, kuandika na kusikiliza.


Vilevile, TUKI (2013), wanaeleza kwamba stadi za lugha ni ujuzi au taarifa ya kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika katika lugha au maarifa jinsi ya kujifunza lugha.


Kutokana na fasili za wataalamu hao tunaweza kupata maana ya pamoja kwamba stadi za lugha ni vipengele mbalimbali ambavyo wajifunzaji wa lugha ya pili wanatarajia kujua ili waweze kutumia lugha katika mawasiliano.


 Vipengele hivi huwa ni vipya kwa mwanafunzi hivyo huhitaji kufundishwa kila kitu.


Kuna media mbalimbali za kisasa ambazo hutumika katika kufunza lugha ya kigeni. Katika sehemu hii tumebainisha media za kisasa ambazo hutumika kufundisha stadi mbalimbali za lugha ya kigeni.


Media ya televisheni, ( https//fluent.com/ blog/English/learn- English- Tv) wanaeleza kwamba televisheni inawasaidia wanafunzi kuimarika katika stadi mbalimbali mfano katika stadi ya kusikiliza, stadi ya msamiati na stadi ya mazungumzo. Wanaendelea kusema kuwa wanapoangalia televisheni unapata stadi ya kusikiliza, pia unaelewa msamiati ambayo haikuwa rafiki na hii inapelekea kujua msamiati mingi na kuweza kuelewa mazungumzo kutokana na ulichokiangalia.


Aidha umuhimu mwingine wa kutumia televisheni katika kufunza lugha ni kwamba mwalimu anapotumia televisheni kufunza lugha inawasaidia wajifunzaji kupata vyanzo mbalimbali vya kujifunzia.



Media ya video, kwa mujibu wa Loneogan (1984) na Stempleski (1991), wanaeleza kwamba video ni media ambayo inahusisha vielelezo mbalimbali vya kuona na kusikiliza katika darasa la kufunzia lugha mfano ramani na picha.

Wanaendelea kufafanua kwamba media hii inaweza kutumika wakati na muda wowote kulingana na mahitaji ya mwalimu. Kuna umuhimu wa kutumia media ya video katika ufunzaji wa lugha



Mosi, video inaleta msukumo kwa mjifunzaji lugha ya kigeni. Allan (1985)  anaeleza kuwa video ni media ambayo inahusisha media nyingine ndogondogo ambazo zinaweza kumshawishi na kumfurahisha mwanafunzi pindi anapojifunza lugha ya kigeni.


Allan anataja mfano wa vitu hivyo ni matukio ya kimichezo na stori.
Pili, inaonesha uhalisia wa kile anachojifunza. Hall (1989), anaeleza kwamba video inamwonesha mwanafunzi uhalisia wa kile anachojifunza.


Media ya Tovuti/  TUKI (2013)  wanasema kuwa tovuti ni nafasi katika mtandao wa kompyuta zinazopatikana taarifa mbalimbali. Wanaendelea kueleza kuwa taarifa hizo zinaweza zikawa zinahusu kazi na biashara.


Hauck (2007)  anaeleza kwamba tovuti inaweza kutumika katika ufunzaji na ujifunzaji wa lugha ya kigeni kwa kujua tamaduni za lugha lengwa. Aidha Thorne na Payne (2005)  katika tafiti zao kuhusu ujifunzaji wa lugha ya kigeni wanadai kwamba tovuti inasaidia katika mwingiliano na mawasiliano katika mfunzaji na mjifunzaji wa lugha lengwa ambapo katika tovuti hizo ndiko taarifa hupatikana zinazohusu lugha hiyo ambayo mwanafunzi anajifunza na jukumu la mwalimu ni kuhakikisha kuwa, anaweka taarifa muhimu kuhusu lugha hiyo katika tovuti husika ambayo mwanafunzi anaifahamu.


Media ya redio, Odera (2006)  anaeleza kuwa media ya redio inaonekana kuwa ni njia bora ya ufundishaji na ujifunzaji wa lugha. Mfano Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kiswahili katika madaraja mbalimbali.


 Anaendelea kueleza kuwa media ya redio inasaidia katika ufunzaji na ujifunzaji wa lugha kwa sababu mwanafunzi anauwezo wa kumudu msamiati na matamshi na kuiga jinsi ambayo mtoa mada au mwasilishaji anavyowasilisha.


Anaendelea kueleza kwamba somo linapotolewa kwa njia ya redio inakuwa somo la kuvutia zaidi na lenye mantiki. Pia, redio inashawishi au inawapa hamasa(motisha) wajifunzaji wa lugha. Bates (1984)  anaeleza kwamba redio inasaidia katika ufunzaji na ujifunzaji wa lugha kwa kuepuka kutumia lugha ya kwanza ( lugha mama).



Media changamani (muitimedia), Barker na Tucker (1990) wanaeleza kwamba media changamani ni mchanganyiko wa media mbalimbali. Lee  anasema kwamba media changamani ni matumizi ya teknolojia katika media mbalimbali kwa pamoja. Mfano kompyuta pamoja na sauti, kompyuta na CD na kompyuta na video au video tepu..


 Media changamani inarahisisha  mwingiliano baina ya mfunzaji na mjifunzaji. Gardner na MacNally (1995)  wanaeleza kuwa media hii inarahisisha mwingiliano baina ya mfunzaji na mjifunzaji wake. Pia inauwezo mkubwa kuhifadhi taarifa kidigitali. Media hiyo inauwezo mkubwa wa kuhifadhi data.



Katika ufunzaji wa lugha na ujifunzaji wa lugha stadi ya kusikiliza ndio inayoonekana kuwa stadi msingi wa stadi nyingine. Katika ufundishaji wa lugha ya kigeni kwa kutumia mbinu ya mawasiliano inamtaka mfundishaji na mfunzaji kutumia sana stadi ya kusikiliza kwani ndio msingi wa stadi nyingine. BAKITA (2017), wanaeleza kwamba kusikilizani kutega sikio ili kusikiliza kile linachosemwa.Katika stadi hii ya kusikiliza msikilizaji hanabudi kuwa na ufahamu sikuvu ili aweze kusikia kile kinacho semwa na kukipa maana.



Kutokana na ubainishaji wa media mbalimbali za kisasa tulizozizungumzia hapo juu zinatumika katika kufundishia lugha ya kigeni , tukiwa kama walimu tarajali ni vizuri tukatumia media changamani (multimedia) hususani katika stadi ya kusikiliza ambayo ndio msingi wa stadi nyingine.



Mambo ya kuzingatia kabla ya kuandaa media changamani katika mchakato wa ufundishaji stadi ya kusikiliza. Chapelle (2001), anaeleza mambo ya kuzingatia kabla ya kuandaa media mchangamani katika ufundishaji wa lugha ya kigeni. Kwa kutumia stadi ya kusikuliza.
Mosi, aina ya darasa, hapa Chapelle (keshatajwa), anaeleza kwamba muandaaji wa media changamani mfano video, michoro, picha, sauti hana budi kuangalia aina ya darasa yaani kuangalia umri wao, na jinsi watakavyashawishika kusikiliza somo husika kutokana na matumizi ya media husika.


 Kwa mfano kama darasa ni la watoto unapoandaa media changamani vizuri, kutumia video kwani watoto watasikiliza namna ya matamshi na watasikiliza namna ya matamshi na wakati huo huo watoto wataona kile kinachosemwa, mfano kuwa mada inahusu chakula unapoandaa media utashawoshika kuweka picha au video inayohusu picha na yenye sauti ya vyakula husika.



 Pili, mazingira ya darasa, hapo ni kwamba kabla ya kuandaa media mwalimu hana budi kuzingatia mazingira ya darasa lake kama yatakuwa rafiki kwa media husika. Mfano, media nyingi za kiteknolojia zinahitaji uwepo wa umeme kwa ajili ya kusukuma mitambo ili shughuli ya kufundisha iendelee, mfano komyuta mara nyingi ili kutumia kufundishia huhitaji sana darasa lenye umeme.


Tatu, daraja la wajifunzaji lugha, katika uandaaji wa media ni muhimu kujua daraja la wajifunzaji wa lugha kama ni daraja la chini, kati na juu ili kujua mtindo upi wauweke kwenye media ili kufundishia lugha lengwa ya kigeni.
Nne, idadi ya wajifunzaji. Kwa mujibu wa Chapelle (2001) anaeleza kwamba kabla ya uandaaji wa media  mwalimu hana budi kuzingatia idadi ya wanafunzi kama kubwa, ndogo au ya kati ili kama anatumia media ya sauti aweke somo lake katika sauti ambayo kila mtu atakuwa na uwezo wa kusikiliza na kuelewa nini kinachosemwa bila tabu yoyote.


Mfano sauti ndogo kutoonekana vizuri kwa video kwa wanafunzi walio mbali hivyo kupata stadi ya kusikiliza pekee ambayo inahusisha mlango wa fahari moja wakati. Ni vizuri katika ujifunzaji kutumia milango ya fahamu walau miwili, mfano masikio na macho.
Tano, mwitiko wa wanafunzi. Kwa mujibu wa Chapelle (2001) mwalimu hana budi kuangalia media ambayo wanafunzi watakuwa wanaonyesha namna wanavyopokea somo lakusikiliza.


Mfano, matumizi ya media mchanganyiko yanaruhusu mwitiko wa msomaji.
Namna ya kuandaa media changamani/mchanganyiko katika ufundishaji wa kusikiliza katika lugha ya kigeni. Katika uandaaji wa media changamani tutatumia video na sauti iliyorekodiwa uwandani katika mazungumzo ya daiyolojia, tanakilishi na projector (kipangama).


Namna ya kuandaa darasa la katika stadi ya kusikiliza kwa kutumia media mchanganyiko. Kwa mujibu wa tovuti ya /http//www.teachingenglish.org.uk/article/a-framewaork wanaeleza kuwa katika uandaaji wa somo la kusikiliza lazima kuwe na;


Mosi, kabla ya kusikiliza kwa mujibu wa tovuti tajwa hapo juu inaeleza kwamba kabla ya kuanza kufundisha stadi ya kusikiliza mwalimu hana budi kufanya yafuatayo. Mfano, kwanza kuhakikisha wajifunzaji wanakuwa makini ili kuelewa kwanza urahisi matini inayofundishwa. Wanaendelea kueleza kwamba ili wanafunzi wawe makini na unachowasilisha huna budi kuwapa motisha juu ya somo husika.



Pili, wakati wa kusikiliza matini kutoka katika media ya vedio ya sauti wanaeleza kwamba wakati wa kusikiliza kwanza mwalimu inatakiwa kuwahamasisha wanafunzi kukaa kimya ili waweze kusikiliza na kuona ili kupata uelewa wa jumla wa kile kinachosemwa. Wanaendelea kueleza kwamba hapa wakati wa kusikiliza video rekoda unaweza kuwauliza wanafunzi maswali kidogo sio sana juu ya kile kinachosemwa. Pili, hapa wanaeleza kwamba  mwalimu anatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaelewa kwa kina kile wanachokisikiza hapa mwalimu anaweza kusimamisha video rekodi kwa muda kidogo pindi wanafunzi wanaposikiliza pale ambapo mwalimu anahisi wanafunzi wake hawakuelewa vizuri.
Namna ya kupima ufahamu stadi ya kusikiliza kwa kutumia media mchanganyiko (multimedia). Mwalimu anapaswa kuwauliza maswali wanafunzi kulingana na kile walichokuwa wanakisikiliza kwa kutumia video rekoda, mfano wa maswali hayo mwalimu anaweza kuwauliza wanafunzi wabashiri maongezi yanayoweza kuendelea mbele kutokana na walivyoelewa mada. Kwa mujibu wa Wyat (1984) anaeleza kwamba ikiwa wanafunzi watashindwa kujibu mwalimu anaweza kurudisha nyuma kidogo video rekoda kwa ajili ya kujaliza kwa maelezo ya wazi zaidi tofauti na yale yanayosikika ili kurahisisha waelewe. Wyatt (1984) anaendelea kueleza kwamba mara baada ya kurudisha nyuma na kueleza pale ambapo mwalimu anahisi wanafunzi hawakuelewa huwaacha waendelee kusikiliza matini na baada ya hapo huwauliza wanafunzi maswali ya ufahamu kuhusu kile walichokisikia ili kuona kama wameelewa.



Kuna faida kadhaa za kutumia media mchanganyiko (multimedia) katika kufundisha lugha ya kigeni. Kuna baadhi ya wataalamu wanaeleza umuhimu wa matumizi ya media mchanganyiko (multimedia). Mfano, Richard (1985), Meskill (1996) na Lee (1996). Baadhi ya hoja wanazozitaja zinaeleza umuhimu wa media mchanganyiko ni kama vile:



Mosi, media mchanganyiko/changamani (multimedia) inamsaidia mwanafunzi kupata muunganiko wa taarifa/maarifa yaliyopita na mapya kuhusu anachojifunza.


 Kwa mujibu wa Richard (1985) anaeleza kwamba video rekoda, tape rekoda inamsaidia mwafunzi kukumbuka yaliyopita kuhusu lugha anayojifunza kutokana na kusimamisha video rekoda ili kuruhusu uelewa wa yanayofundishwa, kurudisha nyuma video rekoda ili mwanafunzi kukumbuka na kupata weledi zaidi wa yale yaliyopita.


Hii humsaidia sana mwananfunzi ukilinganisha na media zingine, mfano wa media ambazo matini inafundishwa haijapishwa wala kurekodiwa.
Pili, media mchanganyiko/changamani (multimedia) inamsaidia mwanafunzi kupunguza mambo yasiyo ya msingi kwenye darasa la kufundisha lugha. Kwa mujibu wa Richard (1985) anaeleza kwamba video rekoda au videoau tape rekoda ni tofauti na ufundishaji wa lugha bila kutumia media ya kisasa kwani katika ufundishaji wa lugha bila kutumia media kama video rekoda inapunguza uradidi kutokana na kwamba kile kilichorekodiwa kimepetia mchakato ambao umeridhia kwamba sasa matini ni mwafaka kwa wanafunzi. Hivyo, kutokana na uepukaji wa uradidi humsaidia mwanafunzi kuelewa kile kinachofundishwa bila kuchanganya na mambo mengine, pengine ambayo yangekuwa nje ya muda.


Tatu, media mchnganyiko/changamani ni media ambayo ina motisha kwa wanafunzi, Kwa mujibu wa Meskill (1996) anaeleza kwamba media changamani ni media nyenye motisha kwani inahusisha milango ya fahamu miwili ambayo ni macho na masiko, hivyo humpa hamasa mwanfunzi ya kusikiliza.


Nne, media changamani inahusisha media mbalimbali zenye ubora zinazoweza kutumika kufundisha lugha. Kwa mujibu wa Lee (1196) anaeleza kwamba media mchanganyiko inaweza kutumia media mbalimbali zenye ubora. Mfano, sauti, video, picha au michoro ili kulifanya somo la kufundisha lugha kwa kigeni kuwa na mvuto zaidi. Hivyo, kama mwalimu tarajali sina budi kutumia media changamani ambayo hainiwekei mipaka katika kutumia media moja na nyingine ili kuhakikisha kwamba somo linakuwa la kuvutia na linaloeleweka kutokana na media husika.



Tano, media changamani zina uwezo mkubwa wa kuhifadhi data za mwalimu anazofundishia. Kwa mujibu wa Barker na Tucker (1990) na Bunzeli na Morris (1992) wanaeleza kuwa mediachangamani jinsi ilivyo na uwezo wa kuhifadhi picha, michoro, sauti na video rekoda. Wanaendelea kueleza kuwa media hii ina uwezo wa kuhifadhi matini iliyochanganyikana na picha zinazoweza kutembea kulingana na teknolojia, kuhifadhi video yenye sauti ndani yake. Hivyo, kutokana na uwezo huo wa kuhifadhi mambo mengi na muhimu kuhusu somo husika hususani katika stadi ya kusikiliza.


Sita, media changamani inamsaidia mjifunzaji kutumia milango ya fahamu katika mchakato wa ujifunzajimhii ni kwa mujibu wa Perzylo (1993). Aidha, Adams na Corston (1993) wanadai kwamba mtu hukumbuka aliyosoma (matini) 10%,  alichokiona (picha mwendo) 20%, alichokiona na kusikia (matini sauti yenye picha mwendo) 30% , alichokiona, kusikia na kufanya (matini, sauti na picha mwendo na mwingiliano) 70%. Hivyo, kama mwalimu tarajali ni vizuri kutumia media inayohusisha kuona, kusikiliza pamoja na kufanya vitendo kwa wajifunzaji lugha. Mfano, katika video rekoda inahusisha kuona yaani picha mwendo pamoja na sauti ya lugha lengwa, hii humsaidia mwanafunzi kukumbuka zaidi kwani huhusisha milango ya fahamu kama vile macho na masikio.


Baada ya somo kuisha mwalimu unaweza kuwagawia wanafunzi kila mtu nakala yake kwa somo ulilofundisha ili kukumbuka na kuelewa zaidi walichosoma.

 Pia, mwalimu unaweza kutoa maswali machache na rahisi ya kupima ufahamu kuhusu kile walichokisikia.
Kwa kuhitimisha, ingawa media za kisasa zimeonekana kuwa na umuhimu mkubwa sana katika ufundishaji wa lugha ya kigeni katika stadi mbalimbali za lugha bado media hizi zimebaki kuwa changamoto kwa nchi zenye teknolojia ya chini, mfano Tanzania. Baadhi ya changamoto hizo ni gharama za media za kisasa, madarasa ya kufundishia, kukosa umeme, media hizi zikiwa zimerekodiwa zinakuwa hazibadiliki kulingana na mahitaji ya wanafunzi katika muktadha husika.














MAREJELEO
Adams, D. M. (1987). Communicating with Electronic Image: Transforming Attitudes, Knowledge and Perception. British Journal of Educational Technology 18: 15-20.
Ahmad, K. , Corbett, G. , Roggers na Sussex, R. (1985). Computer Language Learning nad Language Teaching. Cambridge: Cambridge University Press.
Allan, M. (1985). Teaching English with Video. Harlow, Essex: Longman.
BAKITA, (2015). Kamusi Kuu ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publisher Ltd.
Barker, J. na Tucker, R. N. (1990). The Interactive Learning Revolution: Multimedia in Education and Training. London: Kogan Page.
Broady, E na Le Duc, D. (1995). Learner Autonomy and the Video Camera: A Winder Role for Video Recording Activities? Language Learning Journal 11: 74 – 77.
www.masshele.blogspot.com/mbinu-za ufundishaji-lugha&wageni
Bunzel, M. J. na Morris, S. K. (1992). Multimedia Applications Development. New York: McGraw – Hill.
Chapelle, C. A. (2001). Computer Applications in Second Language Acquasition. Cambridge: CUP.
Corston, N. (1993). Video on Windows Multimedia Interactive Development Ltd.
Fox, J., Matthews, A. , Matthews, C. na Rope, A. (1990). Educational Technology in Modern Language Learning. Sheffield: Training Agency.

Gardner, J. na McNally, H. (1995). Supporting School – based Initial Teacher Training with Interactive Video. British Journal of Educational Technology 26: 30 – 41.
Hill, B. (1989). Making The Most of Video. London: CILT.
Lee, B. M. (1996). Using The Internent for English Learning and Research. English Teaching 44: 49 – 63.
Lonergan, J. (1984). Video in Language Teaching. Cambridge: Cambridge University Press.
Massamba, (2009), Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TATAKI.
Meskill, C. (1996). Listerning Skills Through Multimedia. In Journal of Education Multimedia and Hypermedia [online]. 1996, Vol. 2 na 5 [cit. 2014-06-15]. P. 179 – 201.
Odera, F. Y. (1996). School Radio Programmes: A Case Study of its Use in Selected Institution in Nyanza Provinced Kenya. Unpublished MPHil Thesis. Wales: Great Britain.
Perzylo, L. (1993). The Application of Multimedia CD – ROMs in School. British Journal of Educational Technology 24: 191 – 197.
Richards, J. C. (1985). The Concept of Language Teaching. New York: CUP.
Rossi, P. H. na Biddle, B. J. (1967). The New Media and Education: Their on Society. New York: Anchori Books.
Stern, H. H. (1983). Fundamental Concepts of Language Teaching. Oxford, England: Oxford University Press.
Stempleski, S. (1991). Teaching Communication Skills with Authentic Video. In Video in Second Language Teaching: Using Selecting and Producing Video for The Classroom, eds. S. Sterompleski and A. Arcario, pp. 7 – 24. Alexandria, Virginia: TESOL. Inc.
TUKI, (2013), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

Post a Comment

0 Comments