Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Dhamira za NGANO na NGOMEZI na nafasi yake katika jamii







Waandishi
Juma Hasheem
Na
Sephania Kyungu
BAK ,UDSM. 2019

@masshele

Makala hii tumeigawa katika sehemu kuu tatu, ambapo sehemu ya kwaza ni utagulizi ambapo tutafasili dhana mbalimbali zilizojitokeza katika swali, sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo tutabainisha dhamira mbalimbali zinazopatikana katika ngano na ngomezi pamoja na nafasi ya dhamira hizo kwa jamii ya leo na mwisho ni hitimisho la makala


Dhana ya Dhamira kwa mujibu wa Samwel (2015), anadai kuwa dhamira ni mada, lengo, kusudi au wazo kuu linalozungumzwa katika kazi ya fasihi. Samwel (keshatajwa), anaendelea kusema kuwa kazi ya fasihi huweza kuwa na dhamira za kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni. Mfano ndoa, elimu, kazi, ukombozi.

 Pia Samwel (keshatajwa), anaongeza kwa kusema kuwa dhamira hizi huweza kuelezwa kwamba msanii anakusudia kuelimisha jamii juu ya dhana na sifa za kiongozi bora, kuonya jamii juu ya madhara ya mapenzi shuleni, kuelekeza jamii juu ya umuhimu wa dini katika jamii, kuiasa jamii kuwa na uaminifu katika ndoa na kadhalika. Hivyo mtazamo wetu juu ya dhamira tuaungana na Samwel (keshatajwa), katika fasili yake kwani anadadavua kwa kina kuhusu dhana ya dhamira.


Aidha dhana ya ngano kwa mujibu wa Wamitila (2004), anadai kuwa ni hadithi za kimapokeo ambazo hutumia wahusika wa aina mbalimbali (Wanyama, miti, watu a mazimwi) kusimulia tukio au kisa fulani chenye mafunzo.

Vilevile baadhi ya ngano zimekuwa zikitungwa maalum kwa dhamira ya kuchoma au kuumiza ili kuwafanya watu waachane na matukio yaliyopita na kufundisha staha. Pia Mulokozi (2017), hatofautiani sana na fasili ya Wamitila (keshatajwa), juu ya fasili ya ngano, aidha Mulokozi (keshatajwa), anashadidia fasili yake kwa kutoa mifano kama vile Hadith ya Wairaq wa Tanzania” (1978), Watoto Wanaofanana, Shani Omari na Mrikaria (2006).


Fauka ya dhana hiyo pia kuna dhana ya ngomezi Wamitila (2004), anadai kuwa hii ni Istilahi inayotumiwa kwa maana ya fasihi ya ngoma. Katika jamii nyingi za Kiafrika, ngoma zilitumiwa na hutumiwa kupitisha ujumbe fulani. Katika lugha ya Kiswahili kuna msemo wa “mbiu ya mgambo ikilia ina jambo” ambao umejengwa kwenye utambuzi wa umuhimu wa njia hii ya mawasiliano.


Hapa kuna pande au baragumu inayowasilisha ujumbe maalum. Wamitila (keshatajwa), anaendelea kueleza kuwa ngomezi huelezwa kama fasihi ya ngoma kwa sababu katika jamii inayohusika midundo fulani ya ngoma huwakilisha maneno au kauli fulani. Katika fasihi ya ngoma hatuwezi kuacha kumzungumzia Nketia (1963), ambaye alifanya utafiti kuhusu ngoma katika jamii za Afrika Magharibi, ambapo alidai kwamba ngoma iliangaliwa kama chombo cha kupeleka ujumbe miongoni mwa wanajamii. Pia alieleza kuwa kuna aina tatu za upigaji ambapo kuna upigaji wa kiishara, upigaji wa uchezaji na upigaji wa kalima.


Baada ya kuangalia fasili za dhana mbalimbali, katika sehemu hii tutabainisha dhamira mbalimbali zinazojitokeza katika kipera cha ngano na utazu wa ngomezi pamoja na nafasi zake katika jamii ya leo. Kwa kuanza na kipera cha ngano zifuatazo ni dhamira na nafasi ya ngano katika jamii ya leo.
Mosi, dhamira ya upendo, kwa mujibu wa Okpewho (1992), anaeleza kuwa hizi ni hisia za mtu kwa mtu au kitu.

 Katika fasihi simulizi kuna upendo kwa familia au upendo kati ya mwanaume na mwanamke unaotokana na kuvutiwa na uzuri wa mwanamke kwa mume kwa maana ya kuonyesha harshi. Katika ngano tunaona pia dhamira hii inajitokeza hususani kwa upendo wa mnyama na mnyama wakiwa wanawakilisha binadamu. Mfano katika hadithi ya Kamera Chui na Paa (1978) dhamira hii inajitokeza pale msimulizi anaposema:


                          “…Chura aliona huruma nyingi akataka kumtetea paa.
                               Paa akapaza sauti yake akafanya kama mnyama
                               mkubwa sana anayeunguruma kuliko chui
                               akauliza “mama paa mbona unawasiwasi”, paa
                              akajibu chui alinambia nile majani halafu nikishiba
                              eti niwe kitoweo chake, chura nae akajibu
                  oooh usiogope…”
Katika dhamira hiyo ya upendo kwa mujibu wa Samwel (keshatajwa), anadai kuwa dhamira hii huimiza wanajamii kuwa na utu wema kwa wengine, pia kuwahimiza wanajamii kutofanya mambo ambayo hata wao wasingepeda wafayiwe kwani mara nyingi ubaya haujengi bali unabomoa. Pia mwisho wa ubaya ni aibu.



Pili, dhamira ya uganga na uchawi, Samwel (keshatajwa), anadai uganga unachukuliwa kuwa ni ile hali ya kupata tiba asilia juu ya matatizo ambayo yameshindwa kupata tiba ya kitaalamu. Waganga katika jamii mbalimbali za Kiafrika kwa kawaida hutumia mitishamba, mizimu, miungu na mengine yanayofanana na hayo ili kutoa tiba.

Uchawi kwa upande mwigine unaelezwa kama ujuzi katika mambo ya kimila yaayompa uwezo mtu kumdhuru mwigine. Hivyo wakati ambapo uganga huonekana kama dhana chanya uchawi huonekana kama dhana hasi. Dhamira ya uganga na uchawi imejitokeza sana katika kipera cha ngano. Mfano Samwel (2012), katika Hadithi ya Katope tunaona mwanamke aayeitwa Asimba anapata suluhisho la tatizo lake kwa kutumia uganga.

 Mfano katika hadithi hiyo msimulizi anasema:
                         “….Hatimaye Asimba akaamua kusafiri kwenda kijiji
                               cha mbali kutafuta mganga atakae mpa mtoto.
                               alifika katika kijiji kimoja ambapo alimpata
                              mganga wa kumsaidia, mganga yule alimfanyia
                              dawa Asimba na kumtengenezea mtoto wa udongo..…..”
Dhamira hii haijitokezi tu katika Hadithi ya Katope bali inajitokeza hata katika ngano nyingine ambayo ni ya Tamaa Mbaya. Samwel (2012), anaelezea hadithi ya “Mtoto Yatima na Shangazi Yake” pia katika hadithi hii tunaona dhamira ya uchawi inajitokeza pale msimulizi anaposema:
                        “…Walipotoka kwenda ngomani huku nyuma
                             akatokea bibi kizee aliyemgusa binti yatima
                             na fimbo yake, Binti yatima akabadilika akawa
                             mzuri sana akawa amevalia gauni pana refu zuri
                             na viatu vizuri….”
Mbali na hadithi hizo tulizozitumia hapo juu kuna hadithi nyingine dhamira ya uchawi inajitokeza kama vile Kisa cha Mtoto Mchoyo na Hadithi ya Kibuyu cha Ajabu Samwel (2012). Nafasi ya dhamira hii katika jamii ni kuwaonya wanajamii kuto acha tamaduni zao ambazo licha ya kubezwa na watu mbalimbali bado zina mchango kwa jamii.


Hii ni kwa mujibu wa King’ei na Kisovu (2010)
Tatu, nafasi ya mwanamke katika jamii, dhamira hii imewashughulisha wataalam mbalimbali akiwemo Samwel (2015), na Luto (2015), katika fasihi andishi. Aidha katika kipera cha ngano mwanamke anachorwa kama kiumbe dhaifu, kiumbe msaidizi, mtu mwenye roho mbaya na kama mlezi wa familia.

 Mfano Samwel katika Hadithi ya Katope (2012), anamsawiri mwanamke kama mlezi wa familia, msanii anasema:
                           “….Ikawa kila mara mtoto yule anapoenda kucheza
                 mbali na nyumbani mama yake huwa makini
                              kuangalia mawingu ili asinyeshewe na mvua…”
Pia Samwel katika Hadithi ya Mtoto Yatima na Shangazi yake (keshatajwa) msanii anasema:
                             “…Shangazi huyo alikuwa na mabinti wawili shangazi
                  hakukubali mabinti wake kufanya kazi na badala
                  yake alitaka binti yatima afanye kazi zote binti
                              yatima alikuwa anateswa sana na shangazi
                              yake pamoja na mabinti zake…”


Aidha katika kisa hiki mwanamke anachorwa kama mtu mwenye roho mbaya ambaye anakosa utu kwa mtoto yatima, Nafasi ya dhamira hii katika jamii ni kuikumbusha jamii kwamba suala la malezi ni jukumu la wazazi wote wawili pia inaiasa jamii kuachana na roho isiyo ya utu kwani haijengi bali inabomoa. Hii ni kwa mujibu wa Samwel (2015).


Nne, dhamira ya uchoyo, ubinafsi na ulafi, kwa mujibu wa Samwel (2015), anaeleza kwamba katika jamii za Waafrika uchoyo, ubinafsi na ulafi ni mambo yasiyokubalika hivyo ngano nyingi zilikemea uchoyo, ubinafsi na ulafi kama mambo yasiyokubalika. Mfano Samwel katika Kisa cha Mtoto Mchoyo (2012), msanii anasema:
                                “…Wazazi wake wakawa wanamwomba
                                  maembe hakuwapa ikawa anawatupia              
                                  maganda na makokwa tu…...
                                  Mazimwi yakaamua kumuadhibu
                                  kwa kumfanya kitoweo…”
Aidha Samwel kwenye kisa cha Mtoto Yatima na Shangazi Yake (keshatajwa) ubinafsi unajitokeza pale msanii anaposema:
                                  “…Shangazi yake binti yatima akawatoa mabinti
                                     zake wawili wakajaribu kiatu kile lakini
                                    hakikuwatosha………... kiatu kilimtosha sawasawa
                                    binti yatima walinzi walifurahi sana na
                                    kupiga mbiu kuashiria kuwa binti
                                    aliyetafutwa na mfalme amepatikana…”


Pia dhamira hii inajitokeza katika Samwel (2012) Kisa cha Koba Kuwa na Magamba Yaliyopasuka Pasuka” Visa hivyo kusudi lake ni kuwaonya wanajamii kutokuwa na tabia ya uchoyo, ubinafsi na ulafi huweza kuwaletea madhara.


Tano, dhamira ya uzazi, Samwel (2015), anaeleza kwamba suala la uzazi ni muhimu sana na kwamba mtu ambaye amekosa watoto huonekana kama mtu ambaye hajatimia. Katika jamii za jadi za Kiafrika kuzaa kulionekana kama njia pekee ya kuacha urithi. Suala la umuhimu wa uzazi linajitokeza sana katika kipera cha ngano. Mfano katika “Hadithi ya Katope” Samwel (2012), anasema:
                                        “…Asimba na Kachupa waliishi kwa muda mrefu
                                           katika ndoa yao bila kupata mtoto kutokana
                                           na hilo wakaanza kudharauliwa katika jamii
                                           kwa kukosa Watoto wa kuwarithi…”
Katika kisa hiki tunaona namna ambavyo suala la uzazi linavyopewa kipaumbele na jamii na kwamba mtu ambaye hana mtoto alionekana kama hana mrithi na hajatimia.

 Suala hili linajitokeza katika Mrikaria na Omari (2006), kisa cha Sungura na Fisi Mrikaria wanasema:
                                            “…Hapo ndipo fisi aligundua kuwa alidanganywa
                                              aliona huzuni sana kwa kudanganywa hata
                                              akawachinja Watoto wake wote mwenyewe…”
Katika kisa hiki tunaona namna suala la kukosa watoto linavyo hudhunisha na kujiona kama mkiwa. Nafasi ya dhamira hii katika jamii ya leo ni kusisitiza umuhimu wa uzazi kwani hamna njia nyingine ya kuendeleza kizazi isipokuwa kuzaa, hususani katika jamii za Kiafrika hii ni kwa mujibu wa Samwel (2015).


Sita, dhamira ya kifo, Samwel (2015), anaeleza kuwa kazi mbalimbali za fasihi simulizi zinajadili kifo kwa namna kuu mbili, kwanza chimbuko la kifo na pili kufa si mwisho wa kuwapo kwa mtu, mtu hata akifa anaendelea kuwapo. Suala la kufa si mwisho wa kuwapo linajitokeza katika ngano mbalimbali ikiwemo Kisa cha Mtoto Mchoyo, Samwel (2012), anasema:
                                           “…Mtoto aliyebaki mtini akila maembe aligundua
                                           kuwa ule mti ulikuwa ni makazi ya mazimwi,
                                           mazimwi hayo yalikuwa yamekwenda
                                           kunywa pombe kilabuni, yaliporudi mtini
                                           walimwona mtoto akiwa katika makazi
                                           yao akila maembe…”
Pia suala la kifo si mwisho wa kuwapo linajitokeza katika kisa cha “Kibuyu cha Ajabu” Samwel (2012), anasema:
                                            “…Ilipobaki mishale miwili akaomba mizimu
                                              imsaidie ili mshale wa kumi na moja uweze
                                              kukichoma kibuyu…”
katika visa hivyo vinaonyesha katika jamii ya Kiafrika kuwa kufa si mwisho wa kuwapo.

Aidha nafasi ya dhamira hii ya kufa si mwisho wa kuwapo kwa mujibu wa Mulokozi (2017), inasisitiza kutunza na kuhifadhi amali za jamii ikiwemo mila na desturi za kiafrika katika masuala ya kiimani.


Aidha katika utanzu wa Ngomezi, kuna dhamira na nafasi mbalimbali zinazojitokeza katika jamii ya leo.
Mosi, dhamira umoja na mshikamano, Nketia (1963), anaeleza kwamba fasihi ya ngoma imekuwa ikitumika kwa malengo mbalimbali hata hivyo malengo hubadilika kulingana na wakati wa jamii husika.

Nketia (Keshatajwa), anataja malengo ya fasihi ya ngoma katika jadi za Kiafrika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa vijiji vya mbali, kuwaleta watu pamoja kama vile kuitisha mikutano. Aidha Ushe (2012), akimnukuu Ebeze (2002), anabainisha matumizi ya fasihi ya ngoma katika jamii nyingine za jadi za Kiafrika kuwa ilitumika pia wakati wa sherehe. Hivyo katika fasihi ya ngoma tunaona suala la mshikamano miongoni mwa jamii za jadi za Kiafrika linasisitizwa sana.

Nafasi ya dhamira kwa mujibu wa Mng’aruth (2008), ni kuhimiza umoja na mshikamano kama msingi wa Maisha bora na amani katika jamii.
Pili, dhamira ya uongozi, Mng’aruth (2008), anaeleza kwamba fasihi ya ngoma hutumiwa kutangaza kuwasili kwa viongozi. Nae Ushe (keshatajwa), anabainisha matumizi ya fasihi ya ngoma katika jamii nyingine za jadi za Kiafrika kuwa ilitumika wakati wa sherehe kama vile sherehe za kusimika watawala na machifu. Hivyo katika fasihi ya ngoma tunabaini kwamba masuala ya uongozi yanapewa kipaumbele hususani kushirikiana kati ya viongozi na raia wake. Nafasi ya dhamira hii kwa mujibu wa Mulokozi (keshatajwa), anadai kuwa ni kuendeleza na kukuza harakati za kisiasa na kijamii.


Tatu, dhamira ya imani za jadi za Kiafrika, Mng’aruth (Keshatajwa), anaeleza kwamba katika utamaduni zipo ngoma za aina mbalimbali ambazo huwasilisha ujumbe maalum. Anaendelea kueleza kuwa midundo yake inaposikika hata kwa mbali, msikilizaji au mtazamaji huelewa maana iliyomo.

Mfano bora hapo ni ngoma ya “pungwa” ambapo anaeleza kwamba katika ngoma hii waswahili huamini kuwa mashetani wapo na huwakumbusha watu jambo hili litokeapo ngoma fulani huchezwa kwa midundo ya kipekee ambayo huwasiliana na mashetani hao. Lengo la ngoma hizi huwa ni kupunguza mashetani.

Nafasi ya dhamira hii kwa mujibu wa Mulokozi (keshatajwa), ni kukuza na kutunza imani za jadi za Kiafrika.
Nne dhamira ya vita, Mng’aruth (keshatajwa), anaeleza kwamba milio ya ngoma kwa midundo maalum huashiria kuasili kwa adui au tangazo la vita. Mng’aruth (keshatajwa), anaendelea kueleza kuwa mdundo wa kutangaza vita unatofautiana na ule wa kutangaza mwisho wake ili kuondoa utatanishi. Katika fasihi ya ngoma tumebaini kwamba dhamira hii inajitokeza sana katika fasihi ya ngoma za jadi ya Kiafrika katika kipindi cha nyuma kabla ya wakoloni kulikuwa na vita vya utawala ndiyo maana ngomezi nyingi zilihusu taarifa za vita.


Mfano ufuatao ni wa ngomezi ya vita kutoka kwa wa Akan wa huko Ghana uliotafsiriwa na Mulokozi (2017).
                                        “Walinzi imara kama chuma
                                          Moto umezao mataifa fimbo
                                          ya chuma iliyopindika tumeichapa
                                          bahari je, tutashinda na wangwa?
                                          Je, mto uwapo mkubwa, utazidi bahari
                                          njooni walinzi, njooni walinzi, njooni
                                          walinzi kwa wingi wenu nzige kwa utiriri
                                          tukweapo jabali, lameguka mapande mawili
                                         njooni walinzi, njooni walinzi katika wingi wenu”
Nafasi ya dhamira hii katika fasihi ya ngoma ni pamoja na kujenga ujasiri miongoni mwa askari, pia kujenga tabia ya umoja na mshikamano. Mulokozi (2017), anaizungumzia nafasi hii.


Kwa ujumla, fasihi ya ngano inatumika kwa kiasi kikubwa na jamii katika kujenga tabia ya jamii kuhifadhi amali za jamii kuendeleza harakati za jamii kutokana na mawazo yanayopatikana katika ngano hizo. Pia tumebaini kwamba katika utanzu wa ngomezi hautumiki sana hapa Afrika Mashariki unatumika sana katika jamii za Afrika Magharibi.

Hii imepelekea wanafunzi wengi wa fasihi hususani fasihi ya Afrika mashariki kutouelewa utanzu huu kama fasihi na badala yake wanautambua kama ni aina ya Sanaa za maonesho ama kama ala ya muziki.





                                                                 MAREJELEO
Kamera, W. D (1978) Hadithi za Wairaq. Arusha: EALB publishers.

King’ei, K &Kisovu, C (2005) Msingi wa Fasihi Simulizi. Nairobi: Kenya Literature Bureau.

Luto, M. C (2015) “Matatizo ya Mwanamke katika Kidagaa Kimemwozea na Nyuso za Mwanamke.  Tasnifu ya uzamili Chuo Kikuu cha Nairobi: Haijachapishwa.
Mng’aruth, K. T (2008) Fasihi Simulizi na Utamaduni. Nairobi: Jomo kenyata Foundation.

Mulokozi, M. M (2017) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: KAUTTU.
Nketia, J. H (1963) Drumming in Akan Communities. London: Thomas Nelson Ltd.
Samwel, M (2012) “Mabadiliko katika Majigambo: Uchunguzi wa majigambo ya jadi na Bongofleva” Tasnifu ya uzamivu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Haijachapishwa.
Samwel, M (2015) Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Meveli Publisher.
Okpewho, I (1963) African Oral Literature. New Delhi: Indiana University Press.
Wamitila, K.W (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus.



          

Post a Comment

0 Comments