- Leksikolojia ni taaluma ya maneno kwa jumla
- Leksikografia ni taaluma ya leksikolojia inayohusu utungaji wa kamusi ya maneno ya lugha kwa jumla
JINSI tulivyong’amua katika makala iliyotangulia, idadi kubwa ya kamusi za istilahi zilizoundwa za Kiswahili ni ndogondogo.
Bila shaka, udogo huu unadokeza kwamba pamoja na
juhudi ambazo zimekuwa zikiendelea za uundaji wa istilahi za Kiswahili,
bado kuna upungufu mkubwa wa istilahi katika nyanja husika.
Ni bayana kwamba kuna vikwazo chungunzima katika
mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili ambavyo vinasababisha
upungufu huo wa istilahi.
Kwa mujibu wa baadhi ya wataalam na wanaisimu wa lugha
ya Kiswahili, tatizo kuu katika uundaji wa istilahi za Kiswahili
linatokana na kuegemea zaidi mbinu za leksikografia badala mbinu za
teminografia.
Mbinu ya Leksikografia na Teminografia
Hatuwezi kuangazia dhana ya uundaji
wa maneno pasipo kufafanua tofauti baina ya leksikolojia na teminolojia,
na baina ya leksikografia na teminografia ambalo ni suala tata
linalowakanganya wengi wakiwemo mabingwa wa lugha na tafsiri.
Tutafafanua dhana hizo ifuatavyo:
Leksikolojia - Hii ni taaluma ya maneno kwa jumla.
Teminolojia – Ni taaluma ya istilahi au maneno yanayohusishwa na dhana katika uwanja mahsusi wa maarifa.
Leksikolojia
na teminolojia ni taaluma za jumla kwa maana kwamba hazihusiani moja
kwa moja na masuala ya utumizi wa lugha. Hatahivyo, leksikografia ni
lekskolojia tumizi kwa maana kwamba inahusu maneno katika mazingira ya
utumizi wa lugha.
Kwa mujibu wa Mdee (1997),
leksikografia ni taaluma ya leksikolojia inayohusu utungaji wa kamusi ya
maneno ya lugha kwa jumla. Huu ni mchakato wa kukusanya maneno ya
lugha, mengi kadiri ya mahitaji ya mtumiaji wa kamusi aliyelengwa, na
kuyaorodhesha katika muundo wa kamusi kama vidahizo na kufasili maana
zake kwa mujibu wa matumizi halisi ya lugha.
Kulingana na ISO CD (704:1997),
Teminografia inaweza pia kuitwa teminolojia tumizi kwa maana kwamba ni
taaluma ya ukusanyaji, uchakataji na uhifadhi wa istilahi za fani
mahususi ya maarifa kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa.
Kutokana na fasili hii, teminografia
haihusiki na uundaji wa istilahi bali ukusanyaji, uhifadhi wa istilahi
katika njia mbalimbali kama vile kamusi au hazina data ya istilahi.
Marejeo
Masebo, J. A. (2010). Nadhari ya Lugha Kiswahili 1.Dar-Es Salaam: Nyambari Nyangwine Publisher.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers.
0 Comments