Dhima Ya Kamusi Katika Kufundisha Na Kujifunza Kiswahlli 1
I. Mbaabu
Utangulizi
Tunapoyatoa maoni na mapendekezo yetu kuhusu njia za
kuisahihisha Kamusi ya Kiswahili Sanifu KKS, inafaa tuwakumbuke
Watanzania wawili waliosahauliwa na historia licha ya kuiwekea KKS msingi imara.
Ndugu Samwel Chiponda aliyekuwa mfanyakazi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam na
Ndugu Abdulla Mohamed el Hathramy kutoka Idara ya Elimu Zanzibar wakishirikiana
na Makasisi J.S. Lemble wa Tanganyika na G.W. Broomfield2 wa Zanzibar
pamoja na maafisa wa utawala Frederick Johnson3 wa Tanganyika na P.
Sheldon wa Zanzibar ndio walikuwa wanachama wa Kamati ya Usanifishaji wa
Kiswahili iliyokamilisha kikao chake mjini Dar es Salaam tarehe 9 Oktoba, mwaka
1925. Bila shaka maoni ya Ndugu Chiponda na Hathramy pamoja na ujuzi wao wa
Kiswahili uliwaongoza wanachama wengine ambao wote walikuwa Wazungu.
Kamati ya Ndugu Chiponda na wenzake ilitoa mapendekezo kumi na
tisa (19) kuhusu njia za kusanifisha Kiswahili. Mapendekezo hayo yalipelekwa kwa
serikali za Tanganyika, Kenya, Zanzibar Burundi na Zaire (Congo), mabalozi
kadhaa, Chuo Kikuu cha London - School of Oriental and African Studies (SOAS) na
Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha Afrika ya Kusini, mashirika ya kutafsiri Biblia
pamoja na mabingwa wa Kiswahili na lugha za Kibantu wa wakati huo kama vile Sir
H.H. Johnson na Profesa Carl Meinhof. Katika pendekezo nambari 12 kamati
ilionelea ni bora kurahisisha tahajia za Kiswahili na kuwa na utaratibu maalum
wa kuyaandikia maneno ya Kiswahili ili kuepukana na hali ya kuwepo na njia mbili
au zaidi za kuliandika neno moja. Zifuatazo ni baadhi ya tahajia
zilizopendekezwa na kamati hiyo.
|
dhoruba
|
badala ya
|
dharuba
|
|
heshima
|
badala ya
|
hishima
|
|
hekima
|
badala ya
|
hikima
|
|
methali
|
badala ya
|
mithali
|
|
ishirini
|
badala ya
|
asharini
|
|
lakini
|
badala ya
|
ilakini
|
|
merikebu
|
badala ya
|
marikebu
|
|
hesabu
|
badala ya
|
hisabu
|
|
tisini
|
badala ya
|
tisaini
|
|
hasa
|
badala ya
|
haswa
|
|
sheria
|
badala ya
|
sharia
|
|
asili
|
badala ya
|
asli
|
|
labda
|
badala ya
|
labuda
|
|
sharti
|
badala ya
|
sharuti
|
|
nchi
|
badala ya
|
inchi
|
Kama tutakavyoeleza baadaye, baadhi ya mapendekezo haya
hayakuzingatiwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) katika kuitunga KKS
licha ya TUKI kuwa mrithi wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambayo
iliundwa kufanikisha mapendekezo ya Kamati ya Ndugu Chiponda na wenzake. Baada
ya mkutano huo wa usanifishaji wa Kiswahili kulikuwa na mashauriano na mikutano
kadhaa kati ya serikali za Afrika Mashariki kabla ya kuanzishwa kwa kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki katika mwaka 1930, Mmoja kati ya mikutano hiyo ni
mkutano wa 1928 mjini Mombasa ambao ulikubaliana na mapendekezo ya kamati ya
Ndugu Chiponda na wenzake Mapendekezo hayo yalikuwa ni pamoja na pendekezo la
kwanza la kutumiwa kwa lahaja ya Kiunguja "pamoja na marekebisho
yatakayohitajika" kuwa msingi wa Kiswahili sanifu.
Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na Makao Makuu
yake Dar es Salaam kati ya 1930 na 1942 ilipohamia Nairobi. Mwaka 1952 ilihamia
Kampala hadi 1962 ilipohama tena hadi Mombasa. Mwaka uliofuata kamati ilihamia
Dar es Salaam tena. Mwaka 1964 kamati ilivunjwa na badala yake kikaanzishwa Chuo
cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili ambacho kiligeuza jina kuwa Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili. Taasisi haikurithi vitaa na baadhi ya shughuli za Kamati
ya Kiswahili ya Afrika Mashariki tu, hali ilirithi wafanyakazi wa Kamati
wakiwemo Wilfed Whiteley, aliyekuwa Mkurugenzi wa kwanza wa TUKI. Katibu wa
mwisho wa Kamati, Jan Knappert. pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa mwisho wa
kamati J.W.T. Allen pia ni baadhi ya wafanyakazi wa Kamati walioajiriwa na
Taasisi5
Dhima ya kamusi sanifu ni kusanifisha lugha
Kwa watu wengi, wakiwemo walimu na wanafunzi wa lugha, muamuzi
wa mwisho wa kutegemewa kuhusu masuala ya tahajia, maana na sarufi (kama vile
ngeli za nomino) ni kamusi sanifu ya lugha hiyo. Ubora wa kamusi mara nyingi
hutegemea jinsi inavyoweza kuyashughulikia vilivyo masuala hayo. Kwa sasa KKS
inao upungufu wa maneno yanayotumiwa sana. Mtu yeyote anayejifunza lugha
huvunjika moyo anapoyakosa maneno anayotarajia kuyapata katika kamusi. Ili
kuwaridhisha watumiaji wengi, kamusi sanifu haina budi kuwa na maneno mengi
katika nyanja nyingi iwezekanavyo. Baadhi ya istilahi za sayansi na teknolojia
zinazotumika na watu wengi zinastahili kuwa katika kamusi kuambatana na
maendeleo ya jamii. Maana za istilahi hizo zinastahili kuelezwa bila ya kuegemea
mfumo wowote wa siasa.
Tatizo kubwa zaidi analokumbana nalo mwalimu na mwanafunzi wa
Kiswahili anapoitumia K.K.S ni ule ukosefu wa uamuazi kuhusu usanifu wa tahajia.
KKS inayo maneno mengi ambayo yamepewa tahajia zaidi ya moja. Ziko jozi za
maneno kama vile sharia - "tazama sheria"; desturi "pengine dasturi"; hesabu -
"pia hisabu". Kwa kutumia maneno yenye kuonyesha shaka kama vile "tazama",
"pia", na "pengine" KKS inampotosha mwanafunzi. Mwanafunzi wa Kiswahili anayo
haki kutarajia KKS impatie tahajia sanifu za maneno ya kawaida badala ya jozi
kama glopu/globu, drili/dereli, na spitali/hospitali. Vile vilejozi hizi za
tahajia ndizo zilikataliwa na kamati ya ndugu Chiponda na wenzake zaidi ya miaka
hamsini kabla ya kutungwa kwa KKS.
Bila shaka tofauti za kirnatamshi kutegemea mazingira ya mtu
binafsi na lahaja yake zipo na zitaendelea kuwepo kwa lugha yoyote ile. Hata
hivyo kamusi rasmi ya lugha sanifu inalo jukumu la kusanifisha maandishi kwa
kutumia tahajia sanifu. Katika utangulizi wa KKS imeelezwa kwamba "maneno katika
kamusi hii yameandikwa kufuatana na tahajia sanifu"6 . Hivyo ndivyo
kamusi rasmi ya lugha sanifu inavyopaswa kuwa. Utangulizi huo unaendelea:
Maneno pia, pengine na taz yametumiwa kuonyesha hali hiyo7 Kwa yale maneno yenye tahajia zaidi ya moja basi tahajia zote zimeonyeshwa.
Hebu sasa tuyachunguze maneno hayo yanayotumiwa kuonyesha
tahajia mbili zilizoko katika KKS. Maneno pia, pengine na tazama
yanaonyesha haJi ya kukosa uamuzi. Kusanifisha lugha ni kutoa uamuzi
inavyohitajika. Kwa kuyatumia maneno hayo KKS inaonyesha kwamba haina uhakika
ikiwa neno sanifu ni desturi na dasturi; hesabu au hisabu.
Neno tazama lamwelekeza anayetumia kamusi kwa neno ambalo KKS inalitambua
zaidi. Ukiangalia neno markebu unaongozwa: "tazama merikebu";
sharia "tazama sheria"; dharuba tazama dhoruba". n.k. Hivi ni kuonyesha
kwamba (labda) KKS inatambua tahajia merikebu, sheria hekima na
dhoruba, kuwa sanifu zaidi kuliko markebu, sharia, hikima na dharuba.
Ikiwa ni hivyo basi, yaonyesha kwamba neno la mwisho dharuba lililo-
kataliwa mwaka 1925 ndilo KKS imeamua kwamba ni zuri zaidi kuliko dhoruba
lililosanitishwa. Mwanafunzi wa Kiswahili hana budi kuyapima maneno yote mawili
na kuamua ni tahajia ipi atakayoitumia. Mara nyingi tahajia atakayoamua kutumia
ni ile anayoshauriwa na KKS kwa neno "tazama". Kwa mujibu wa kamusi hii.
nwanafunzi anaweza kuchagua tahajia yoyote na kuitumia kwa kuwa KKS haijamsaidia
kutoa uamuzi huo. Wanafunzi tofauti waweza kuchagua tahajia tofauti na tahajia
aliyoichagua mwalimu wao. Je huku si ni kuilemaza lugha?
Suala jingine ambalo linazushwa na dondoo la hapo juu kutoka
KKS, pamoja na matumizi ya maneno hayo yenye kuzusha shaka kwa mwalimu na
mwanafunzi wa Kiswahili ni iwapo tahajia zote mbili zimesanifishwa kama
inavyodaiwa katika utangulizi huo wa KKS. Kamati ya usanifishaji wa Kiswahili ya
Ndugu Chiponda na wenzake iliamua tahajia za baadhi ya maneno ziandikwe kama
tulivyotaja katika utangulizi, kwa mfano desturi, hekima, merikebu na
dhoruba. Je ni kikao kipi cha Kamati ya Kiswahili ya ya Afrika Mashariki
kilichoamua kwamba tahajia dasturi, hikifna na marikebu ni sanifu
baada ya kukataliwa 1925? Vilevile tunashuku iwapo ni kweli kwamba tahajia
dasturi, hikima, marikebu, dharuba, chandalua, dereli, glopu, spitali,
halambee, chokra, dreva, mazowea, finika na mengine mengi kama hayo
yalisanifishwa.
Nyingi kati ya tahajia zilizoorodheshwa juu hazipatikani katika
kamusi sanifu ya Kiswahili-Kiingereza iliyotungwa na Kamati ya Kiswahili ya
Afrika Mashariki chini ya uongozi wa katibu wake Frederick Johnson. Yaelekea
kwamba tahajia hizi ni maoni ya watunzi wa KKS wala si maoni ya Kamati
iliyokisanifisha Kiswahili. Kama tujuavyo TUKI haijawahi kuwa na vikao vya
kimataifa vya kusanifisha maneno ya kawaida ya Kiswahili kama walivyosanifisha
istilahi za taaluma mbalimbali. Iwapo hatuna sababu maalum na ushahidi wa
kutosha kwamba tahajia hizo zote zilisanifishwa, yafaa ziondolewe kabisa katika
KKS. Wakati umewadia wa kuifanya KKS kuwa kielelezo cha Kiswahili sanifu.
Wanaosanifisha lugha wanalo jukumu la kutofautisha kati ya tahajia sanifu na
zisizo sanifu. Ni maoni ya mwandishi kwamba jukumu hili sasa liko mikononi mwa
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili kama warithi wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki.
Baadhi ya maneno yenye zaidi ya tahajia moja yamekopwa kutoka
lugha ya kigeni, hasa Kiingereza. Taasisi inayafahamu maneno hayo ya Kiingereza.
Inajua nl tahajia ipi inayoshabihiana zaidi na neno asilia (neno lililokopwa).
Kwa mfano maneno spitali na hospitali yamekopwa kutoka neno
hospital la Kiingereza. Taasisi inakerwa na nini ndipo ikope
spitali, na glopu, na kusanifisha badala ya kukata yamuzi mara moja
kukopa hospitali na globu pekee? Ni nani katika lahaja sanifu ya
Kiswahili anayetumia neno halambee? Ikiwa ni matamshi ya hara, mbona basi
matamshi harambee linalotumiwa na baadhi ya Wakenya wa bara lisiongezwe?
Kwa utupi, msimamo thabiti kuhusu usanifishaji wa tahajia za Kiswahili
unahitajika.
Kila anayejifunza lugha ngeni, mathalani Kiingereza hufanya
jitihada za kujifunza tahajia kama vile saw (ona), sew (shona),
sow (panda), soul (roho) n.k. Lakini kuhusu lugha yetu ya taifa
KKS haijali ikiwa tutaandika drili au dereli. Kuruhusu na
kupendekeza Kiswahili kiandikwe kiholela "taz, horera", - kadri mtu anavyotaka
ni kushusha hadhi ya Kiswahili na dhana nzima ya usanifishaji. Baadhi ya hizi
tahajia za ziada bila shaka ni matamshi ya kilahaja au ya tabaka mbalimbali za
waliosoma na waliokosa elimu ya kutosha kuweza kutambua asili halisi ya neno
lililokopwa. Kwa hivyo inapendekezwa kwamba tahajia moja sanifu itumiwe kwa neno
moja. Ikiwa ni lazima, KKS inaweza kuwafahamisha wasomaji wake kwamba badala ya
kutamka neno hospitali, kwa mfano, baadhi ya watu hutamka spitali.
Lakini ni sharti ifahamike waziwazi kwamba tahajia sanifu ni moja na tahajia
hiyo ndiyo pekee inayostahili kuorodheshwa katika kamusi ya Kiswahili Sanitu.
Umuhimu wa kuidurusu kamusi
Nijambo la kawaida kuidurusu kamusi upya kila baada ya muda
maalum. Kwa lugha inayoendelea kukua na kupanua msamiati wake kwa haraka kama
vile Kiswahili, muda huo haupaswi kuzidi miaka kumi. Mbali na kuongeza maneno
mapya katika hilo toleo jipya, fursa hiyo hutumiwa
(1) Kurekebisha makosa yoyote ambayo huenda yalitokea katika toleo lililotangulia, na
(2) Kuandikiana mkataba mpya kati ya watungaji kamusi na wachapishaji8
Huu ni mwaka wa kumi na tatu tangu KKS ichapishwe kwa mara ya
kwanza (1981). Ni jambo lisilozusha ubishi kwamba tayari KKS imepitwa na wakati.
Njia mojawapo ya kuthibitisha ukweli huu ni kutazama makala yoyote kutoka
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ukiwemo ucangulizi wa KKS yenyewe. Baadhi ya
maneno yaliyotumiwa katika utangulizi huo, kama vile kitomeo, vitomeo na
kidahizo hayakuorodheshwa katika KKS. Mifano mingine ni maneno kama vile
ikama na kasma9, pamoja na neno leksikografia
lililotumiwa katika ukurasa wa kwanza wa barua ya Dkt. Mdee ya kutangaza warsha
hii. Pengine maneno hayamo katika kamusi kwa kuwa ni maneno ya kitaaluma au
istilahi. Wakati umewadia kuamua ni istilahi zipi zitakazokuwepo kwenye kamusi
ya kawaida kama KKS na zile ambazo zitaingizwa katika kamusi maalum za taaluma
mbalimbali. Maoni ya mwandishi ni kwamba baadhi ya istilahi za taaluma nyingi
zinastahili kuwa katika KKS kwa kuwa idadi ya watu ambao wanahitaji kuzifahamu
inaendelea kuongezeka kwa haraka kuambatana na maendeleo ya nchi zetu kielimu na
kiteknolojia. Neno laweza kuwa la kitaaluma leo, na kesho likawa la kawaida.
Hairidhishi kuyaacha nje maneno kama hayo ati kwa sababu ni ya kitaaluma huku
yakiendelca kutumiwa katika mawasiliano ya kawaida.
Maneno mengine ya kawaida kama vile nyanja na nyayo
ambayo ni nomino za hali ya wingi wa ngeli ya 14 (u) hupatikana lu katika
hali ya umoja - uwanja na wayo. Hata ingawa ni sahihi
kuyaorodhesha hivyo, hapana shaka kuwa wapo wanafunzi wengi wanaoitumia kamusii
hii ambao hawajui watayapata wapi maneno kama hayo. Haitoshi kutoa maelezo hayo
katika utangulizi kwa sababu pengine mtu hadewi asili au hali ya umoja wa neno
analolitafuta. Mwanafunzi wa Kiswahili atafaidika sana iwapo maneno kama hayo
yataorodheshwa katika KKS na kumfahamisha kwamba neno hilo ni nomino ya hali ya
wingi na kwamba maana yake inapatikana katika nomino (nomino yenyewe itajwe) ya
hali ya umoja.
Kamusi sanifu ifafanue lugha wala isifungamane na itikadi
Kamusi ya Kiswahili Sanifu ilipokuwa ikiandikwa, siasa za ujamaa
zilikuwa zikivuma sana nchini Tanzania. Yaonekana kwamba TUKI ilijitwisha mzigo
wa kufafanua na kusambaza siasa hizo kupitia KKS. Kwa mfano, maana moja ya neno
kabaila imeelezwa kuwa:
Mnyonyaji mwenye majumba mengi ya kupangisha na ardhi kubwa ya kupangisha au inayolimwa na watu wengine wengi kwa ajili ya faida yake.10
Neno linalomtisha na kumkera yeyote anayoitumia KKS katika
kufundisha au kujifunza Kiswahili ni Mnyonyaji. Kwa kutumia neno
mnyonyaji TUKI iliwashauri (na ingali yaendelea kuwashauri) Watanzania na
wengine wanaoitumia kamusi hii wasiutafute utajiri wa aina hiyo kwa kuwa wakiwa
na majumba ya kupangisha watakuwa wanyonyaji (sawa na kupe) wanaowanyonya wateja
wao. Neno mnyonyaji halijaorodheshwa, kwa hivyo itabidi utafute kitenzi nyonya
ndipo upate maelezo kwamba ni "kuishi kwajasho la mwingine".
Maelezo hayo yanampotosha mwanafunzi. Ili kuwa na majumba mengi
ya kupangisha ni lazima mtu awe na mali ili aweze kuyanunua au kuyajenga. Kama
tujuavyo, ni nadra sana kupata mali halisi bila jasho. Je, mwenye majumba hayo
anaishi kwa jasho la nani? Ni maoni ya mwandishi kwamba kizazi cha sasa
kinachotumia KKS kimedhulumiwa na TUKI kwa kutishwa kwamba wakitajirika watakuwa
wanyonyaji. Dhutuma hii ingeondolewa endapo maelezo yasiyoegemea siasa za upande
wowote yangeanzia: "mtu mwenye majumba mengi..."
Mfano mwingine kama huo ni neno bepari. Maana moja ya
neno bepari inaelezwa kuwa "mmojawapo katika tabaka la wanyonyaji"10
Misemo ya siasa hizo imetapakaa kote katika KKS. Mifano mingine ni kama
vile "ubepari ni unyama" "Ubwanyenye Uchwara:"11 na "Usiwe
kupejitegemee"12. Mifano hii michache inazusha suala la ikiwa siasa
na propaganda zinazoweza kubadilika wakati wowote ule zinastahili kuingizwa
katika kamusi. Kamusi hii hutumiwa zaidi na wanafunzi kuliko watu wazima. Vile
vile kamusi hii yaelekea huuzwa nakala nyingi zaidi nje ya Tanzania kama vilc
Kenya kuliko vile inavyouzwa Tanzania. (Kufikia 1989 ilikuwa imechapwa upya
matoleo 13 nchini Kenya zikilinganishwa na matoleo mawili tu, (1981 na 1988
nchini Tanzania). Inapendekezwa kwamba KKS isahihishwe kwa kutoa maelezo ya
maneno ya Kiswahili bila ya kueneza siasa.
Maneno yaliyotoholewa kutoka lugha nyingine
Ukopaji wa maneno ni mojawapo ya njia za kuongeza manepo ya
lugha. Kila lugha hukopa maneno kutoka lugha nyingine. Mengi kati ya maneno
ambayo Kiswahili kimekopa yanatokana na lugha ambazo zimeingiliana na Kiswahili
kama vile Kiarabu, Kihindi, Kiajemi, Kireno na Kiingereza. Mengi kati ya maneno
yaliyokopwa na Kiswahili ni maneno ya vitu, dhana au vyombo vipya ambavyo
havikuwepo katika utamaduni wa Waswabili. Ni nadra sana kwa lugba yoyote ile
kukopa maneno ya msamiati asilia ambayo hutarajiwa kuwa katika kila lugha kama
vile maji, mwezi, nyota, mkono, kichwa na jua.
Kamusi ya Kiswahili sanifu imekopa maneno ya Kiingereza
kupindukia. Tazama mifano ifuatayo:
|
sentafowadi
|
hedimistresi
|
|
zigizaga
|
steshenimasta
|
|
chakuleti
|
speapati
|
|
bucha
|
katekista
|
|
kondrati
|
bradha
|
Mifano hii (michache) inazusha masuala kadhaa. Je, ikiwa
tutakopa steshenimasta mbona tusikope piimasta (P.E. Master),
domitorimasta (dormitory master), sabjektimasta (subject master)
n.k. Iwapo tutakopa neno bucha (duka la nyama), mbona tusikope fama
(mkulima). travela (msafiri), sing'a (muimbaji) na maneno
mengine kama vile weka (mfanyakazi)? Jambo linalosisitizwa hapa ni kwamba
kukopa kuna mipaka yake. Tukikopa bila mpango itatubidi kulipa kwa kuipoteza
lugha tuliyotarajia kuitajirisha kwa lcukopa. Mwanafunzi wa Kiswahili
ataridhishwa na ukopaji wa istilahi kama vile aspirini, bakteria na
katheta, lakini atashangazwa na sababu za kukopa baadhi ya maneno ya
kawaida. Azimio nambari mbili (2) la Kamati ya Usanifishaji wa Kiswahili ya
Ndugu Chiponda na wenzake, (1925) lilipendekeza kutumiwa kwa maneno yenye asiJi
ya Kibantu kila inapowezekana katika shughuli za uundaji wa maneno mapya ya
Kiswahili. Je. tumeridhika kwamba hatuwezi kupata maneno yenye asili ya Kibantu
ndipo tukope maneno kama zigizaga na bucha?
Mzizi wa Kitenzi cha Kiswahili
Mzizi wa kitenzi cha Kiswahili ni ile sehemu ya kitenzi
inayobeba maana ya kitenzi hicho. Mzizi ni sehemu ambayo haibadiliki, na ambayo
haipasuliwi na viambishi awali au viambishi tamati katika myambuliko. Mzizi wa
kitenzi chenye asili ya Kibantu ni ile sehemu ya kitenzi ambacho
hakijanyambulishwa inayotangulia irabu a ya mwisho ya kitenzi hicho. Vitenzi
vyote vyenye asili ya Kibantu huishia kwa irabu (kiishio) a kabla
havijanyambulishwa. Mbali na maelezo hayo hatuwezi kusahau kwamba Kiswahili
kinazo kanuni zake za mfumo wa sauti unaosababisha mabadiliko ya sauti. Mfumo
huo ndio unatuwezesha kuelewa kwamba k hubadilika ikawa sh katika
mifano kama vile:
|
amka
|
amsha
|
|
mka
|
rusha
|
|
pika
|
mpishi12
|
Kamusi ya Kiswahili sanifu inatoa mifano kama vile kau
kuwa ndio mzizi wa kauka; toro kuwa mzizi wa toroka na mifano
mingine mingi, hasa ile inayoishia kwa konsonanti k. Labda waandishi wa
KKS walipoamua kutumia mizizi hiyo walikiri kubanwa na maelezo ya neno mzizi
kwamba haubadiliki. Neno amsha linapoundwa kutokana na neno amka
au (ku) rushwa kutokana na ruka hatuwezi kusema kwamba kiini
hubadilika kwa kuwa k ndiyo huwa sh na mabadiliko hayo
yanatar.ajiwa katika mazingira hayo ya mfumo wa sauti ya Kiswahili. Dhana ya
mzizi wa kitenzi kama inavyojidhihirisha katika KKS inahitaji kuchunguzwa upya.
KKS ina mifano ya mizizi kama vile kaz (mzizi wa kaza na kazan
(mzizi wa kazana)13. Bila shaka kuna tatizo hapa kwa kuwa maneno
yote mawili yana mzizi sawa. Tatizo hili iinatokana na matumizi ya 'kiambishi' -
hasa "kiambishi tamati" - ambacho ni sehemu ya kitenzi inayopatikana baada ya
mzizi kama vile pigia, pigika, pigisha, pigiwa n.k.
Kiambishi tamati kwa hakika ni kiungo cha kauli kama vile
kutendea, kutendeka na kutendana. pamoja na kiishio kama vile irahu a.
Sehemu hizi mbili, yaani kiungo cha kauli na kiishio zikitambuliwa vilivyo
labda tatizo hili la mzizi litatatuliwa. Viungo vya kauli ya kutendeka - k,
ik, ek, lik na lek - vyote huwa na konsonanti k kutangulia
kiishio u. Hii ndiyo sababu mizizi ya vitenzi vinavyoishia k
hufikiriwa kwamba ni vitenzi vya kauli ya kutendeka. Jambo hili likitambuliwa
KKS itakuwa na mizizi iliyo sahihi kama vile kauk mzizi wa kauka na
torok-mzizi wa toroka kwa kuwa kauka na toroka ni vitenzi
mbavyo bado havijanyambulishwa.
Pia yafaa ikumbukwe kwamba vitenzi vilivyokopwa havina mizizi
sawa na vitenzi vyenye asili ya Kibantu. Mofolojia ya vitenzi hivyo ni tofauti
na ya vitenzi asilia kwa kuwa neno zima ni mzizi. Kwa mfano, neno safiri
likinyambulishwa hutoa maneno kama vile:
|
msafiri
|
wasafiri
|
|
waliosafiri
|
usafiri
|
|
usafirishaji
|
kusafirisha
|
Kwa hivyo KKS haina msingi wala sababu za kutosha kuvunja neno
safiri na kueleza kwamba safir ndio mzizi wake. Mifano mingine ni
kama vile hubiri lililopewa mzizi hubir, tahiri lililopewa mzizi
tahur na samehe lililopewa mzizi sameh.
Hitimisho
Katika kumalizia, ni wazi kwamba KKS ina historia ndefu na
inastahili kujitajirisha na misingi iliyowekwa ha kamati ya usanifishaji ya
Ndugu Chiponda na wenzake pamoja na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na
kamusi zake. Pia mwandishi anatoa pongezi zake kwa serikali ya Tanzania kwa
kuianzisha na kuikimu Taasisi ya Uchunguzi wa Kishwahili ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, pamoja na wafanyakazi wa Taasisi kwa kazi yao ya kujitolea kwa dhati
kuhudia ulunwengu mzima wa Kiswahili.
Maelezo
1. Huu ni upanuzi wa Makala ya Mwandishi "Uchambuzi wa Kamusi ya
Kiswahili sanifu" iliyochapishwa katika UFUMBUZI toleo la tatu 1989:
26-32.
2. Mwandishi wa Sarufi ya Kiswahili. London: Sheldon
Press, 1931.
3. Aliyekuwa katika wa Kwanza wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki.
4. Rejea F, Johnson. "Report of the Committee for the
Standardization of Swahili Language" barua aliyowaandikia Katibu Mkuu na
Mkurugenzi wa Elimu, Dar es Salaam, Oktoba 16, 1925.
5. Tazama Ireri Mbaabu: Historia ya Usanifishaji wa
Kiswahili. Longman Kenya Ltd. 1991.
6. TUKI 1981. Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam:
OUP.
7. ibid
8. Kwa kila toleo wachapishaji wanastahili kuongeza asilimia ya
malipo wanaowalipa waandishi wa Kamusi hadi kufikia asilimia 50 na pengine
asilimia 60 ya mauzo yote.
9. Mbaabu 1991: 116
10. TUKI 1981: 94.
11. ibid: 18
12. Tazama Ireri Mbaabu: Sarufi za Kiswahili. Longman
Kenya Ltd. 1992: 158-164.
13. TUKI 1981:
105
0 Comments