@masshele swahili
Pambo la Lugha ni miongoni mwa diwani iliyoandikwa na nguli wa fasihi za Kiswahili Shaaban Robert mnamo mwaka 1946. Katika utangulizi wake anasema kuwa kitabu chaitwa Pambo la Lugha kwa vile ambavyo mashairi yasimulivyo habari zake kwa maneno ya vina au mlingano wa sauti ipendezayo masikio. Aidha, diwani hii ina jumla ya mashairi arobaini na tatu (43) yanayozungumzia kuhusu maisha, lugha na siasa. Katika kazi hii fani na maudhui yatahakikiwa.
KIINI
Katika sehemu hii fani na maudhui yatahakikiwa kwa kutumia diwani ya Pambo la Lugha ambapo sehemu inayoanza ni maudhui kisha kufuatiwa na fani.
Maudhui
Njogu na Chimerah (1999) maudhui ni ujumbe wa jumla kuhusu matukio, kitu, wahusika au hali ya maisha kama vile yavyojikeza katika kazi ya fasihi iwe riwaya, tamthiliya, shairi au wimbo. Katika sehemu hii vipengele vifuatavyo vitachunguzwa katika diwani hii ambavyo ni dhamira kuu, dhamira ndogondogo, ujumbe, falsafa, mtazamo wa mwandishi, nafasi ya mwanamke na mgogoro.
Dhamira
Wamitila (2004) anasema kuwa dhamira ni lengo la mtunzi katika utungo wake. Lengo hili hutokeza kuwa wazo kuu ambalo hukuzwa katika utungo unaohusika kuanzia mwanzo hadi mwisho. Katika kipengele hiki tutaangalia dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
2.1.1.0 Dhamira kuu
Katika diwani hii dhamira kuu ni maisha.
2.1.1.1 Dhamira Ndogondogo
2.1.1.1.1 Umuhimu wa Lugha ya Kiswahili
Katika diwani hii mwandishi anaeleza umuhimu na ufahari uliopo katika lugha ya Kiswahili ambapo kila Mswahili anapaswa kujivunia na kutembea kifua mbele huku akitumia lugha hii. Katika shairi la Kiswahili mwandishi anasema:
“Maneno ya uthabiti, maelezo ya jinsi,
Nyingi na tofauti, kwa ufasaha na wepesi,
Kama lulu na yakuti, johari na almasi,
Lenye ladha ya sauti, bado kuona kamusi,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.” (Uk. 29)
Vilevile, mwandishi anaonesha nafasi ya Kiswahili duniani ambayo ndiyo humfanya ajivunie lugha hii. Katika shairi la Kiswahili mwandishi anasema:
“Lugha kuu za dunia, jumla kumi na mbili,
Na hizo huhesabiwa, pamoja na Kiswahili,
Kwa haja kuwaridhia, watu mbalimbali,
Kwayo hakikupungua, yanipasa kukijali…” (Uk. 28)
Hivyo basi, kutoka na mashairi hayo mwandishi anasisitiza umuhimu wa lugha ya Kiswahili ambapo watu hawana budi kujivunia lugha hiyo kwa kuitumia na kuitangaza.
2.1.1.1.2 Suala la elimu
Katika diwani hii mwandishi anasisitiza umuhimu wa elimu katika jamii, ambapo anaona kuwa na elimu ni fahari na ni ufunguo wa maisha. Haya yanadhihirika katika Utenzi wa Adili, mwandishi anasema:
31
Elimu kitu kizuri,
Kuwa nayo ni fahari,
Sababu humshauri,
Mtu lakutumia. (Uk. 38)
52
“Elimu aliyenayo,
Amepata ufunguo,
Mbele ya mazuio,
Katika maishaye.” (Uk. 46)
Kutokana maelezo hayo, mwandishi anasisitiza umuhimu wa elimu katika jamii na anaona elimu ni kitu pekee ambacho huweza kumtoa mtu katika vikwazo mbalimbali.
2.1.1.1.3 Suala la mapenzi na ndoa
Mwandishi wa diwani hii shaaban Robert analiona suala la mapenzi kuwa na nafasi kubwa katika maisha ya mwanadamu, Lakini huweza kuleta mashaka au baraka. Hili linajidhihirisha katika shairi la Mapenzi ambapo anasema:
‘Yana nguvu halisi, kwa mtu yanapofika,
Hupenya moyo upesi, hayaachi yakishika,
Na shabaha hayakosi, yanapolenga hufika,
Hupunguza wasiwasi, ama hukuza mashaka,
Huweza na kufilisi, ama kuleta baraka,
Hasa katika nafsi, zinayoyataka.” (Uk. 7)
Vilevile, katika suala la ndoa mwandishi anaona kuwa ni suala muhimu la kuheshimiwa na hili linajidhihirisha katika shairi la Siku Tukufu, mwandishi anasema:
“Viumbe wamepewa, siku tatu tukufu,
Siku ya kuzaliwa, na siku ya kuja ufu,
Tatu siku ya kuoa, kadhalika maarufu,
Zote huheshimiwa, kwa namna badilifu.” (Uk. 1)
Hivyo basi, mwandishi anaona kuwa suala la mapenzi na ndoa katika jamii ni sehemu ya maisha.
2.1.1.1.4 Suala la Maadili
Mwandishi wa diwani hii anajaribu kugusia suala la maadili kwa kuonyesha namna ambavyo mtu hupaswa kuepuka ubaya, kuheshimu mke na kumheshimu mwalimu. Mathalani katika shairi la Choyo mwandishi anasema:
“Sasa natarajia, madeni kuyarudisha,
Ambayo nimepokea, watu kunikopesha,
Hazina za dunia, kuzitaka kumeniisha…” (Uk. 10)
Katika shairi hili mwandishi anasisitiza umuhimu wa kulipa madeni. Pia, suala la maadili limejitokeza katika Utenzi waAdili ambapo mwandishi anasema:
43
“Kila kukicha tazama,
Viungo vyako kusema,
Ulimi nena mema,
Pigo lisitujie.”
54
“Kadhalika mwalimu,
Mkuza yako fahamu,
Naye anasehemu,
Heshimayo apewe.”
62
“Mkeo mpe heshima,
Muhesabu kama mama,
Mzaa watoto wema,
Ulivyozaliwa wewe.”
(Uk. 46)
Katika utenzi huu mwandishi anafunza watu namna ya kuishi kwa maadili katika jamii.
2.1.1.1.5 Suala la Siasa
Katika suala hili mwandishi anasisitiza kuungana. Pia, masuala ya vita na kutokata tamaa. Kwa kurejelea shairi la Chama cha Afrika, mwandishi anasema:
“Upeke faida yake, nimekaa nikiwaza,
Heri leo nitanuke, haifai kuitunza,
Upeke ni makeke, hasa siku za juzi,
Itakapo watu wake, nchi kuiongoza.” (Uk. 9)
Vilevile, mwandishi ameonyesha masuala ya vita katika shairi la Chanzo ambapo anasema:
“Ingawa vita vigumu, yeye alivipenda,
Kwa moyo alizimu, daima mbele kwenda,
Moyo kuutia hamu, mashaka kuyashinda,
Ndilo linalolazimu, kila mtu kutenda.” (Uk. 61)
Vilevile, mwandishi ameeleza masuala ya udikteta katika siasa ambapo katika shairi la Hitler anasema:
“Hakungoja maamuzi, jambo alotafuta,
Nakifoche si wazi, namna kilivyopita,
Haya ndiyo mageuzi, nayayoleta na vita,
Udachi ya manazi, heshima haikupata.” (Uk. 6)
Katika sehemu hii mwandishi anasizitiza umuhimu wa ushirikiano katika siasa na namna uongozi mbaya ulivyo na madhara makubwa.
2.1.1.1.6 Suala la Kifo
Katika diwani hii mwandishi hakusita kujadili suala la kifo kwani ni sehemu anayopitia kila mwanadamu katika maisha yake. Hivyo, mwandishi hakusita kutumia ufundi wake kuongelea suala hili. Katika shairi la Mauti anasema:
“Ugonjwa hutibika, mauti hayana dawa,
Kizima huharibika, kufa na kupotea,
Umbile likiweka, mauti yanaondoa,
Hili hufanyika pote, katika dunia.” (Uk. 3)
Katika shairi hili mwandishi anatilia mkazo kuwa kifo hakikwepeki mahali popote duniani na kuona kuwa kila nafsi itaonja umauti.
2.1.1.2 Ujumbe
Wamitila (2004) anasema kuwa ni dhana itumikayo kueleza taarifa ambazo msanii au mtunzi hukusudia kuzifikisha kwa wasomaji wake au hadhira yake kama njia mojawapo ya kuhakikisha dhamira yake imetimia. Katika diwani hii ya Pambo la Lugha kuna mafunzo mbalimbali yanayopatikana, nayo ni kama yafuatayo:
Udikteta una maadhara makubwa katika maisha. Shairi la Hitler. (Uk. 5)
Tukipende na kukithamini Kiswahili. Shairi la Kiswahili. (Uk. 27)
Mwanamke si kiatu, katika shairi la Mwanamke si Kiatu. (Uk. 19)
Kila nafsi itaonja umauti, katika shairi la Mauti (Uk. 3)
Elimu ni ufunguo wa maisha, katika Utenzi wa Adili (Uk. 46)
2.1.1.3 Mtazamo wa Mwandishi
Kwa mujibu wa Wamitila (2004) matazamo ni namna au jinsi mtu anavyochukulia mambo au anavyofikiri juu ya jambo fulani kwa mtazamo wa kimapokeo na kimapinduzi. Mtazamo wa mwandishi huyu ni wa kimapinduzi kwa sababu anaona kuwa maadili, kuheshimu wanawake, kuithamini Kiswahili, elimu na kuungana ni mambo yanayochochea ujenzi wa jamii mpya.
2.1.1.4 Falsafa
Wamitila (2004) anaeleza kuwa falsafa ni mawazo aliyonayo mwandishi juu ya maisha ambayo hujitokeza katika maandishi yake. Mawazo hayo huyaamini na kuyashikilia kama ukweli unaoongoza maisha yake na jamii yake kwa ujumla. Katika diwani hii kuna falsafa juu ya utu, ukweli na kifo.
2.1.1.5 Nafasi ya Mwanamke
Katika diwani hii mwandishi ameweza kumtazama mwanamke kwa namna tofauti kama vile ifauatavyo:
Mwanamke anastahili kuheshimiwa katika jamii. Shairi la Mwanamke si Kiatu.
Mwanamke anahaki sawa na mwanaume, katika shairi la Mume na Mke. (Uk. 34)
Mwanamke ni muhimu katika maisha, katika shairi la Peke. (Uk. 2)
2.2 Fani
Wamitila (2016), anaeleza kuwa fani ni ufundi anaoweza kutumia mwandishi katika kuifinyanga kazi yake. Fani huusisha vipengele kama vile muundo, mtindo, matumizi ya lugha, wahusika, mandhari.
2.2.1 Mandhari
Mandhari ya diwani hii ni nchini Tnganyika wakati wa ukoloni wa Mwingereza, mapema sana baada ya vita vya pili vya dunia.
2.2.2 Muundo
Mulokozi (2017), anasema kuwa muundo ni msuko, mwingiliano na uwiano wa vipengele vyote vinavyojenga shairi au kazi ya sanaa. Aidha, anaendelea kueleza kuwa unahusisha idadi ya msitari, vipande au mshororo, beti, urari wa vina na mizani pamoja na kibwagizo.
2.2.2.1 Idadi ya Mishororo
Tarbia au shairi lenye mishororo minne. Mfano wa maishiri yenye muundo huu ni pamoja na shairi la Raha, Panya, Siku Tukufu, Wazo, Peke, Undugu, Kweli, Umashuhuri, Moshi, Mauti, Hidaya, Jina, Rairai, Ugani, Hitler, Chanzo.
Takhimisa au mishororo tano, mfano wa mashairi hayo ni pamoja na shairi la Kiswahili.
Mistari sita, kuna shairi la Mapenzi na shairi la Sumbuka.
2.2.2.2 Idadi ya Beti
Ubeti mmoja – shairi la Raha na shairi la Panya.
Beti mbili – shairi la Wazo, Siku Tukufu, Peke, Undugu, Kweli, Umashuhuri, Siri na Moshi.
Beti tatu – shairi la Mauti, Hidaya, Jinan na Rairai.
Beti nne – shairi la Ugeni.
Beti tano – shairi la Hitler.
Beti sita – shairi la Chanzo na shairi la Mapenzi.
Beti saba – shairi la Dunia na shairi la Siku ya Kusafiri.
Beti nane – shairi la Chama cha Afrika, Choyo na Sumbuka.
Beti tisa – shairi la Fujo na shairi la Kwa Mzuri.
Beti kumi – shairi la Mali Isiyokwisha, Urafiki, Maradhi, Kwa Fulani.
Beti kumi na moja – shairi la Mwanamke si Kiatu.
Beti kumi na sita – shairi la Washairi.
Beti kumi na nane – shairi la Ndoa ya Siri.
Beti ishirini – shairi la Waadhi.
Beti thelethini na moja – shairi la Kiswahili.
Beti arobaini na sita – shairi la Mume na Mke.
2.2.2.3 Urari wa Vina na Mizani
Katika diwani hii mashairi yote yana urari wa vina na mizani kuanzia mwanzo hadi mwisho.
2.2.3 Mtindo
Kwa mujibu wa Njogu na Chimeraha (1999) ni tabia ya utungaji inayompambanua mtunzi mmoja na mtunzi mwingine. Mtindo alioutumia mwandishi katika diwani hii ni pamoja na mtindo wa kimapokeo ambao unazingatia urari wa vina na mizani.
2.2.4 Matumizi ya Lugha
Mtunzi ametumia lugha rahisi uliosheheni yafuatayo:
2.2.4.1 Misemo
Katika diwani hii mwandishi ametumia misemo kama vile
“Ndugu hakatiliwi” Shairi la Undugu (Uk. 2)
“Mauti hayana dawa” shairi la Mauti (Uk. 3)
2.2.4.2 Matumizi ya Lugha ya Kiingereza
Katika diwani hii mwandishi ametumia pia lugha la kiingereza katika mashairi yake, mathalani shairi la Chama cha Afrika (Uk. 10), Ndoa ya Siri (Uk. 23)
2.2.5 Tamathali za Semi
2.2.5.1 Takriri.
Msokile (1993) anaeleza kuwa takriri ni moja kati ya vipengele vya matumizi ya lugha katika kazi za fasihi ambapo kunakuwa na marudiorudio ya herufi, silabi, neno, sentensi na wakati mwingine hata aya nzima hurudiwa.
“Hodihodi” katika shairi la Mwanamke si Kiatu (Uk. 19)
“Yaya i ! yaya i !” katika shairi la Ndoa ya Siri. (Uk. 23)
2.2.5.2 Tashihisi
Mulokozi (1996) anaeleza kwamba ni tamathali ya kukipa uhai na tabia za kibinadamu kitu ambacho hakina uhai na tabia hizo.
Mifano:
“Mapenzi yakihimili” (Uk. 7) shairi la Mapenzi
“Litakufa langu jina” (Uk. 11) shairi la Nasumbuka
2.2.5.3 Tashbiha
Gibbe (1980) anasema kuwa ni tamathali ambayo hulinganisha vitu viwili kwa kutumia viunganishi linganishi mbalimbali kama vile ‘mithili ya’, ‘kama’ na ‘kama kwamba.’ Lengo la kutumia tashbiha ni kujenga picha.
“Sura ya kufurahisha kama ile ya pepo”, shairi la Mume na Mke (Uk. 31)
“Umbo la kupendeza kama malaika”, , shairi la Mume na Mke (Uk. 31)
2.2.5.4 Sitiari
Msokile (1993) ni tamathali ya semi ambayo kwa kawaida huhusisha matendo, kitu au tabia ya vitu vyenye maumbile tofauti, ulinganisho huu unahusisha misingi au sifa zinazopatikana katika vitu vyote viwili ingawa sifa hizo haziwi kati ya kitu na kitu. Katika diwani hii sitiari imetumika pale ambapo mshairi anasema: “Mwanamke ni mwili”, shairi la Mume na Mke (Uk. 31)
2.2.5.5 Ishara na Taswira
Taswira hurejelea picha ijengekayo akilini mwa msomaji kutokana na athari ya lugha katika fasihi. Baadhi ya taswira zilizotumika ni pamoja na:
“Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa”, shairi la Kiswahili (Uk. 27). Hii ina maana kuwa mtu athamini kitu chake hata kama kinadharauliwa.
3.0 HITIMISHO
Kwa ujumla, mwandishi wa diwani hii amefaulu kimaudhui na kifani katika kufikisha ujumbe kwa jamaa, ambapo amezungumzia mambo mbalimbali yanayohusu jamii kama vile undugu, mapenzi, Kiswahili, ukweli, maradhi na ndoa. Katika kufikisha hayo, mwandishi ametumia fani mbalimbali kama vile matumizi ya lugha na tamathali za semi.
MAREJELEO
Gibbe, A. G. (1980). Shaaban Robert: Mashairi. Dar es Salaam. Tanzania Publishing House.
Msokile, M. (1993). Misingi ya Hadithi Fupi. Dar es Salaam University Press.
Mulokozi, M. M. (1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
______________(2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili Kozi za Fasihi Vyuoni na Vyuo Vikuu. Dar es Salaam: KAUTTU.
Njogu, K. na Chimerah, R. (1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Robert, S. (1945). Pambo la Lugha. Nairobi: Oxford University Press.
Wamitila, K. W. (2004) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: English Press.
______________(2016). Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide Muwa.
www.masshele.blogspot.com
0 Comments