Wanaotaka kujiajiri watakiwa kutafuta maarifa na ujuzi kwanza.- Waliojiajiri watakiwa kuwaheshimu walioajiriwa kwa sababu siyo watu wote wanaweza kuwa wajasiriamali.
- Kujiajiri na kuajiriwa ni njia za kufikia malengo, muhimu chagua njia unayoona inakufaa wewe.
Dar es Salaam. Mwanzilishi wa kampuni ya Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amewashauri vijana wenye mpango wa kujiajiri katika shughuli za ujasiriamali kuajiriwa kwanza ili kupata ujuzi na maarifa ili kuepuka makosa mara baada ya kuanzisha biashara zao.
Mtambalike aliyekuwa akiongoza mada ya “Kipi bora, kujiajiri ama kuajiriwa” katika jukwaa la mtandaoni la #ElimikaWikiendi leo (Februari 8, 2020) amesema mtu akipata maarifa na ujuzi wa kutosha kabla ya kujiajiri ana nafasi nzuri kufanikiwa katika kile anachokifanya.
“Kosa tunalofanya wengi tunajiajiri mapema kwenye sekta ambazo hatuna ujuzi au ufahamu nazo. Jambo la msingi ni kujua unataka nini na kua tayari kuajiriwa japo kwa muda mfupi ili upate ujuzi husika kabla ya kujiajiri. Itakuokoa na makosa mengi sana,” ameandika Jumanne katika ukurasa wake wa Twitter.
Amesema vijana waliopo vyuoni na shuleni wanaotaka kujiajiri ni muhimu wakajenga msingi wa kuanza kujifunza na kujiandaa mapema na safari ya ujasiriamali tangu wakiwa shuleni.
Mfumo wa ajira nao umebadilika usibweteke usubiri kuajiriwa ukishamaliza chuo. Anza kujenga ujuzi wako mapema kama lengo lako ni kujiajiri. Tatizo la ukosefu wa ajira limelazimisha mabadiliko ya njia tunazopitia kufika malengo yetu. Ni muhimu kufahamu. #ElimikaWikiendi
32 people are talking about this
Amesema teknolojia pia imekuja na changamoto na fursa mpya kwenye mifumo ya kuajiri na kujiajiri na kwa kijana inabidi ufahamu na kujiandaa mapema kwa lolote.
Hata wale walioajiriwa makazini bado wana nafasi ya kujiajiri kwa shughuli za ziada ili kujiongezea kipato kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Amesema kama umeajiriwa na muda mwingi upo huru, jitahidi kujifunza taaluma mpya usidharau taaluma ambazo zinaonekana za watu wa kawaida ndiyo zenye pesa hizo.
“Jambo jingine la msingi sana ni kufahamu umuhimu wa “Urban Skills” ujuzi utakaokusaidia kuishi mjini. Kwa mujibu wa mtandao wa @LinkedIn ujuzi wa Videography (upigaji picha za video) ni miongoni mwao. Jifunze design, digital Marketing, etc (usanifu,masoko ya mtandaoni). Jifunze taaluma ambazo zitakupatia pesa haraka,” amesisitiza Mtambalike.
Amesema inawezekana kabisa mtu kuajiriwa na kujiajiri kwa wakati mmoja. Mfano asubuhi upo ofisini jioni unaendesha @Uber, asubuhi upo ofisini jioni unafanya kazi ya mteja kwenye @freelancer, asubuhi upo ofisini jioni una publish podcast yako online (unachapisha sauti yako mtandaoni) au unauza fanicha @instagram.
Wakichangia mada iliyoibuliwa na Mtambalike katika jukwaa hilo, baadhi ya wachangiaji wamesema siyo watu wote wanaweza kuwa wajasiriamali bali wengine wanatakiwa kuajiriwa na wajasiriamali wachache.
Mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Jamii Forums, Mike Mushi amesema “Bado nitasisitiza hili, yeyote anayetaka kujiajiri, kuwa mfanyabiashara au mjasiriamali ataelewa kwamba hawezi kufanikiwa bila kuheshimu sana watu walioajiriwa.”
Naye Michael Kimollo (@michael_kimollo) ameeleza kuwa kuajiriwa na kujiajiri ni njia tu za kumfikisha mtu anapotaka kufika kwenye maisha hakuna iliyo bora zaidi ya nyingine, “ni wewe tu kujiuliza ipi inakuelekeza na itakufikisha kwenye malengo yako.”
Muhimu ni kufahamu kuwa safari ya kujiajiri siyo rahisi inahitaji muda na maarifa ya kutosha katika kila hatua utakayopita.
“Na factor (jambo) kubwa ni kwamba wengi huongozwa ni 'mihemko' kwamba wakijiajiri katika sekta fulani basi watatoboa in a short time (kwa muda mfupi). However (Hata hivyo) wanapofika kwa ground (mtaani) mambo huwa ni tofauti kabisa which lead most of them kukata tamaa na kuwadiscourage others not to try (inawasababisha wengi wao kukata tamaa na kuwakatisha tamaa wengine wasijaribu,” amesema mchangiaji Kimson47 @RednetCompany

0 Comments