Rombo. Naibu Waziri wa Maji nchini Tanzania, Maryprisca Mahundi amesema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kuunda mamlaka ya maji safi Rombo hatua ambayo itasaidia kuboresha utoaji wa huduma na kumaliza tatizo la maji katika Wilaya hiyo.
Alieleza hayo Jana
Jumatatu Desemba 14, 2020 wakati akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya usambazaji maji Wilaya ya Rombo Kiliwater na kubainisha kuwa lengo la Serikali ni kuona huduma ya maji inapatikana na kero ya maji inakwisha.
Amebainisha kuwa mchakato wa uundwaji wa mamlaka hiyo umekamilika na kinachosubiriwa ni waziri wa Maji, Jumaa Aweso kufanya uteuzi wa meneja wa mamlaka hiyo.
"Serikali ina nia njema na Kiliwater na imeendelea na michakato ya kuona ni namna gani wananchi wataendelea kupewa huduma ya maji kwa ubora na ufanisi zaidi ya ilivyo kwa sasa, michakato ya kuunda mamlaka imeshafanyika, kwa sasa muda sio mrefu waziri atafanya uteuzi ili kukamilisha uundaji wa mamlaka ya maji Rombo,” amesema.
Amesema kipindi cha nyuma ilikuwa rahisi Kiliwater kutoa huduma lakini kwa sasa imeelemewa na kwamba ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa, haina budi kuundwa kwa mamlaka ya maji.
Amewatoa hofu watumishi wa kampuni hiyo kutokana kuundwa kwa mamlaka na kueleza kuwa hakuna atakayefukuzwa kazi wala kuonewa.
"Lengo ni kuona ushirikiano unaendelea kuwepo haimaanishi Kiliwater ikibadilika kuwa mamlaka watumishi mtafukuzwa kazi hapana labda uwe haukidhi sifa zinazohitajika kwa sasa, lakini niwahakikishie, hakuna ambaye ataonewa kila mmoja atapata haki yake na stahiki zake zote zitazingatiwa,” amesema
Akizungumzia mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Chala, naibu waziri huyo amesema utagharimu zaidi ya Sh30 bilioni na utaanza mapema mwaka 2021.
Meneja wa Kiliwater, Prosper Kessy amesema moja ya changamoto zinazowakabili ni uzalishaji wa maji usiokidhi mahitaji na kwamba wana upungufu wa lita za ujazo 13,000 wakati wa unyevu na 22,000 wakati wa kiangazi.
Chanzo Gazeti la mwananchi

0 Comments