- Serikali imependekeza kuongezeka na kupunguza kodi katika michezo mbalimbali ya kubahatisha.
- Hatua hiyo inatarajia kuongezea serikali mapato na kuweka usawa katika kodi hizo za michezo.
Lengo la kupunguza kodi ya mshindi ni kuongeza wachezaji kwenye mchezo huo na kuzuia wasicheze mtandaoni katika mataifa mengine. Picha| Mtandao.
.
Dar es Salaam. Serikali imependekeza mabadiliko katika Sheria ya Michezo ya Kubahatisha kwa kuongeza kodi katika baadhi ya michezo na kupunguza kodi katika baadhi ya sehemu ili kuendeleza michezo nchini.
Miongoni mwa kodi zilizopunguzwa ni kodi katika mapato ya ushindi wa mchezo wa kubahatisha (winnings).
Katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali mwaka 2021/22, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema leo (Alhamisi Juni10, 20201) bungeni Jijini Dodoma kuwa Serikali inapendekeza kupunguza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Gaming tax on Winnings) kutoka asilimia 20 hadi asilimia 15 kwenye Michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (Sports betting).
“Lengo lake ni kuongeza wachezaji kwenye mchezo huo na kuzuia wasicheze mtandaoni katika mataifa mengine ambayo hayatozi gharama hiyo,” amesema Dk Nchemba.
Mbali na ahueni hiyo, bado Serikali imeendelea kukomalia mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha baada ya kupendekeza kuongeza viwango vya kodi katika maeneo mengine.
Katika bajeti hiyo inayotarajiwa kuanza Julai mosi mwaka huu, Serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha kodi katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (sports betting) kwa mapato ghafi (Gross Gaming Revenue - GGR) kutoka asilimia 25 ya mauzo ghafi hadi asilimia 30 ya mauzo ghafi.
Dk Nchemba amesema ongezeko la asilimia 5 litapelekwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kwa ajili ya kuendeleza michezo nchini.Katika upande wa michezo ya kubahatisha ya kompyuta, Dk nchemba amesema Serikali inapendekeza kutoza kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha inayoendeshwa kwa kompyuta (Virtual Games).
Mbali na kodi hiyo, Serikali pia inapendekeza kutoza kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha iliyo chini ya majaribio.
“Lengo la hatua hizi ni kuleta usawa wa utozaji kodi katika michezo ya kubahatisha. Hatua hizi za marekebisho ya michezo ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh14.92 bilioni,” amesema Dk Nchemba
x
0 Comments