
Mfano wa jiko la mkaa

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Maketi Msangi.
Wanandoa
wawili wakazi wa mtaa wa Bunkango, Nshambya manispaa ya Bukoba mkoani
Kagera, maarufu kama mama Osward na baba Osward wamekutwa wakiwa
wamefariki dunia ndani ya nyumba walimokuwa wakiishi usiku wa kuamkia
jana, chanzo cha vifo hivyo kinatajwa kuwa ni jiko la mkaa.
Mwenyekiti
wa mtaa wa Bunkango, Anath Abas amesema kuwa alipata taarifa kuwa mtoto
wa wanandoa hao ameshindwa kwenda shule baada ya kugonga mlango wa
chumba walimokuwa wamelala wazazi wake kwa muda mrefu bila mafanikio, na
kuamua kutoa taarifa kwa jirani.
"Nilifika
eneo la tukio nikagonga mlango haufunguliwi, nikaita hawaitiki,
nikainama chini nikachungulia, nikamuona mama Osward amelala chini na
mume wake amelala kitandani" amesema mwenyekiti huyo.
Amesema
baada ya kuona pako kimya aliwaita viongozi wenzake pamoja na baadhi ya
wananchi wakasukuma mlango kwa nguvu na kukuta tayari wanandoa hao
wamepoteza maisha.
Diwani
wa kata Nshambya na Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gibson amesema
kuwa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa mtendaji wa kata yake,
alitoa taarifa polisi kwa hatua zaidi, huku akiwaasa wananchi wake
kuacha tabia ya kupikia ndani.
"Tumeambiwa
mwanamke alirejea nyumbani usiku, akawasha jiko la mkaa na kumenya
ndizi, na kisha kuingiza jiko hilo kwenye chumba kisha wakafunga mlango
na madirisha na kupumzika" amesema Godson Gibson.
Akizungumza
kwa njia ya simu Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Maketi
Msangi amekiri kuwepo kwa tukio hilo, na kwamba uchunguzi wa awali
umeonesha kuwa vifo vya wanandoa hao vimetokana na jiko la mkaa.
"Uchunguzi
wa awali umeonyesha vifo vyao vimetokana na kuvuta hewa yenye sumu
inayotokana na mkaa, lakini tunasubiri uchunguzi wa kitabibu ili
kujiridhisha kama kweli hicho ndo chanzo cha vifo hivyo na baada ya hapo
miili ya marehemu itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi" - Kaimu
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Maketi Msangi.
0 Comments