na
Hashim
Juma
Ikisiri
Watunga kamusi huwa na malengo mbalimbali. Baadhi ya malengo hayo ni haja ya kueleza na
kufafanua dhana mpya, kumsaidia mtumiaji kamusi kuwa na uelewa zaidi, haja ya kutaka
kumsaidia mtumiaji kuwa na idadi kubwa ya msamiati inayorejelea dhana moja, kumsaidia
mtumiaji wa kamusi kufahamu historia za maana za maneno, haja ya kutaka kuonesha matumizi
ya maneno, na haja ya kutaka kutoa maana za maneno. Hata hivyo, malengo hayo ili yaweze
kutimizwa kwa kiwango kikubwa yanategemea matumizi ya nadharia za maana. Lengo la makala
haya ni kujadili jinsi nadharia za maana zinavyokidhi malengo ya watunga kamusi. Pia, katika
kujadili hili makala haya yatakuwa na mpangilio ufuatao; kipengele cha utangulizi ambacho
kimehusisha nadharia mbalimbali za maana, kipengele cha namna nadharia za maana
zinavyowasaidia watunga kamusi katika kutimiza malengo yao na mwisho ni hitimisho.
1.0Utangulizi
Katika kipengele hiki nimeelezea nadharia mbalimbali za maana kwa kuwaangalia, waasisi wake
na misingi ya nadharia hizo. Miongoni mwa nadharia za maana ni:
1.2 Nadharia ya Dhana/Taswira
Nadharia hii hudai kuwa, maana ya kiyambo ni dhana au taswira inayoibuliwa na kiyambo hicho
akilini mwa mwanalugha pindi kiyambo hicho kinapotumika (Palmer, 1976: Lyons, 1987:
Akmajian na wenzie, 2010). Hii ina maana kwamba, maneno ni alama ya mawazo yaliyomo akilini
mwa watumiaji wa lugha inayohusika. Kimsingi, nadharia hii ina misingi ya kisaikolojia kwa
kuhusisha suala la dhana inayoibuliwa katika ubongo ama akilini mwa mwanalugha. mfano,
maana ya neno mtoto ni ile picha au taswira inayojengeka kuhusishwa na kiyambo hicho katika
ubongo wa mwanalugha.
1.3 Nadharia ya Uelekezi
Nadharia hii iliasisiwa na wanafalsafa waliodai kuwa njia nzuri ya kufafanua maana ya kitu ni
kuonyesha kwa kidole kile kinachorejelewa (Resani, 2014). Katika nadharia hii uelekezi hutumika
kama mbinu ya msingi inayotumiwa kuwaonesha watu vitu halisi katika mazingira wanamoishi.
1.4 Nadharia ya Matumizi
Hii ni nadharia yenye mkondo wa kimawazo ya wanafalsafa. Mwanafalsafa anayehusishwa moja
kwa moja na nadharia hii ni Lodwig Wittgenstein (1953) katika kitabu cheke cha Philosophical
Investigation (Reimer, 2010: Akmajian na wenzie, 2010, Kahigi, 2019). Wittgenstein anaeleza
kuwa, ni kosa kubwa kuweka mipaka ya maana kama ambavyo nadharia za maana kama dhana,
mwitiko na kitaja zinavyofanya, kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuweka mipaka ya thamani
ya umbo lenyewe la kiisimu na hivyo kinachopaswa kuzingatiwa ni matumizi yake. Hivyo, haja
ya kuuliza hili neno lina maana gani bali angalia neno hilo linatumikaje. Tobing (2010) anaeleza
kuwa, maana za maneno hazitakuwa na uvulivuli kama zitakitwa katika muktadha wa matumizi.
Pia, Fodor (1980) anaeleza kuwa, nadharia hii haibagui umbo lolote la kiisimu lenye maana kwani
kwenye Kiswahili kuna maneno kama vile ‘na’ ‘ya’ ‘wa’ ‘kwa’. Mfano neno na linapata maana
kama litahusishwa na muktadha wa tungo mathalani, Baba na mama wanalima, neno na ambalo
ni kiunganishi linapata maana kama, neno linalotumika kuunganisha maneno katika tungo. Hivyo,
maneno kama hayo yanaweza kuelezwa vizuri kwa kutumia nadharia ya matumizi.
2.0 Jinsi Nadharia za Maana zinavyowasaidia Watunga Kamusi katika Kutimiza malengo
yao
Kimsingi, watunga kamusi hutumia nadharia za semantiki kama sehemu ya kufanikisha malengo
yao, makala haya yamezingatia malengo ya watunga kamusi hususani watunga kamusi ya lugha
(wahidiya) na malengo hayo ni kama yafuatayo:
2.1Haja ya kutaka kuonesha matumizi ya Maneno mbalimbali
Watunga kamusi huwa la kusudio la kutaka kuonesha namna ambavyo neno fulani linavyoweza
kutumika. Uoneshaji wa matumizi ya maneno katika kamusi humsaidia mtumiaji kufahamu
mawanda ya neno husika kwani kila neno huwa na mipaka yake kimatumizi. Lengo hili huwa linatimizwa na watunga kamusi pindi wanapotumia nadharia ya matumizi ambayo msingi wake ni
‘maana ya neno ni matumizi yake katika lugha’. Tazama mifano ifuatayo kwa ufafanuzi zaidi.
Neno Maana
i. Na neno linalotumika kuunganisha maneno katika
tungo: Baba~mama.
ii. Mbuzi mnyama anayefanana na swala, anayefugwa kwa
ajili ya kutoa nyama au maziwa: Mama
amenunua mbuzi jike na dume
Chanzo TUKI, 2014
Katika mfano wa (i-ii) hapo juu, kuna kategoria mbili za maneno ambazo ni tofauti, kuna
kiunganishi na nomino. Mathalani neno na linapata maana kama litahusishwa katika muktadha wa
tungo. Mfano: Baba~mama wanalima, matumizi ya na katika tungo (i) ni kuunganisha maneno
yenye hadhi sawa katika tungo. Kadhalika, neno mbuzi limefasiliwa kama mnyama anayefanana
na swala, anayefugwa kwa ajili ya kutoa nyama au maziwa. Maana ya mbuzi imetolewa kwenye
kamusi kwa kuzingatia muktadha wa matumizi ya neno hilo. Lengo hili huwa linatimizwa na
watunga kamusi kwa kutumia nadharia ya matumizi ambapo neno limepewa maana kutokana na
jinsi linavyotumika.
2.2 Humsaidia Mtumiaji kuwa na idadi kubwa ya Msamiati inayorejelea dhana moja
Watunga kamusi wanapaswa kumsaidia mtumiaji wa kamusi kumuorodheshea msamiati
mbalimbali inayorejelea dhana moja. Kimsingi, msamiati huo ni ule wenye mahusiano ya
sinonimia mathalani pesa/hela/faranga. Mtumiaji anapokutana na maneno kwenye kamusi
humsaidia kuwa na ukwasi wa msamiati na kumfanya aweze kuyatumia katika miktadha
mbalimbali. Lengo hili huwa linatimizwa na watunga kamusi kwa kutumia nadharia ya matumizi
ambapo mtumiaji atalazimika kutofautisha matumizi ya maneno hayo kulingana na muktadha.
2.3 Haja ya kutaka kutoa maana za Meneno
Watunga kamusi hutoa maana za maneno ili ziweze kumsaidia mtumiaji wa kamusi. Maana za
maneno ambazo zinapatikana kwenye kamusi hutokana na vyanzo mbalimbali vya data, mathalani
kukusanya makongoo, kupitia kamusi tangulizi na kuwahoji watu (Mdee, 2006). Hivyo, katika
vyanzo vya upatikanaji data, watu au jamii wana nafasi katika kutoa maana za maneno kwani
watunga kamusi hulazimika kuwahoji watu au jamii ili waweze kupata maana za maneno. Lengo
hili linaweza kutimizwa na watunga kamusi kupitia nadharia ya dhana/taswira ambapo wahojiwa
wanakuwa na dhana fulani akilini mwao kuhusiana na maneno wanayoulizwa. Hivyo, maana ya
maneno hayo watakayoulizwa yatatokana na dhana walizonazo katika akili zao. Tazama mifano
ifuatayo kwa ufafanuzi zaidi.
Mfano (i), maana ya neno mpira itatokana na dhana ambayo ipo kichwani kwa mhojiwa,
ambapo mhojiwa anaweza kusema kuwa mpira1
ni kitu cha mviringo kinachodunda na
kinachotumiwa katika michezo mbalimbali. Mpira2
ni mti ambao hutoa utomvu mzito
mweupe unaogandishwa na kutengenezwa vitu mbalimbali kama vile magurudumu.
Chanzo (TUKI 2014).
Katika mfano (i) hapo juu, tunaona kuwa kuna maana mbili tofauti juu ya dhana mpira, ambapo
maana hizo mbili zimetokana na dhana ambazo zimejengeka akilini mwa watumiaji lugha juu ya
neno mpira.
2.4 Haja ya kutaka Kuhifadhi historia za Maana za Maneno
Watunga kamusi wanapaswa kuhifadhi maana za maneno ili watumiaji waweze kufahamu maana
hizo. Mdee (2006) anaeleza kuwa, maana ya neno huweza kupangwa kufuatana na kigezo cha
kihistoria. Maneno yenye uhusiano wa Kipolisemia maana zake hupangwa kwa kuzingatia kigezo
cha kihistoria. Tazama mifano ufuatao kwa ufafanuzi zaidi.
1. mdomo
i.
-sehemu ya mwili wa binadamu inaopatikana kwenye kichwa
ii.
-sehemu ya juu ya chupa iliyo wazi
2. mguu
i.
-wa binadamu
ii.
-wa meza
Katika mfano (i-ii) hapo juu, maana za maneno zilizopangwa kwa kuzingatia kigezo cha kihistoria,
ambapo maana ya kwanza ya maneno tajwa hapo juu, ndiyo maana ya msingi ambayo ilianza,
kisha ndipo ikaja maana ya pili ambayo imekuja kutokana na mnyumbuliko wa maana ya kwanza.
Hivyo maneno yenye uhusiano wa kipolisemia maana zake huwekwa kwa kufuata kigezo cha maana kihistoria. Lengo hili linatimizwa na watunga kamusi pindi watumiapo nadharia ya
matumizi ili neno kichwa na mguu liweze kueleweka lazima likitwe katika muktadha wa
matumizi ili lipate maana. Mfano; mguu wa meza umevunjika. Kufanya hivyo tungo hiyo itakuwa
haileti utata wa kimaana.
2.5Lengo la kumsaidia mtumiaji kamusi kuwa na uelewa zaidi ya Maneno
Watunzi wa kamusi hawana budi ya kutafuta namna ambayo itamuwezesha mtumiaji wa kamusi
aweze kuelewa zaidi maana za maneno. Kamusi zenye picha humsaidia mtumiaji kuelewa zaidi
kutokana na matumizi ya picha kwenye kamusi. Baadhi ya maneno katika kamusi huitajika
kupewa ufafanuzi kwa kutumia picha ili kumrahisishia msomaji aweze kuielewa zaidi juu ya dhana
husika. Tazama mifano ifuatayo kwa ufafanuzi zaidi.
Neno Maana
i. Mwewe Ndege mkubwa anayefanana na tai ambaye
hukamata vifaranga wa kuku.
ii. Mnandi Ndege mkubwa mwenye rangi nyeupe tumboni,
shingo ndefu na miguu mifupi kama ya bata na
hukaa baharini, mtoni au ziwani akiwinda samaki.
Chanzo: TUKI, 2014
Katika mfano (i-ii) hapo juu, neno mwewe na mnandi yamepewa ufafanuzi wake kwa kuwekewa
picha ili zimsaidie mtumiaji wa kamusi aweze kuelewa zaidi juu ya dhana mwewe na mnandi.
Watunga kamusi hutimiza lengo hili kwa kutumia nadharia ya uelekezi ambayo ina muelekeza
mtu kwa kutumia picha ili aelewe zaidi kuhusu neno fulani.
2.5 Haja ya kueleza na kufafanua dhana mpya
Kimsingi, dhana mpya zinazoingiwa kwenye kamusi huitaji ufafanuzi wa kimaana. Chuwa (1995)
anaeleza kuwa, dhana mpya katika kamusi huitaji kufafanuliwa zaidi kwani dhana hizo zinakuwa
ngeni kwa watumiaji wengine hivyo watunga kamusi hulazimika kutolea ufafanuzi maneno hayo.
Pia, Wamitila (2010) anaeleza kuwa, yapo maneno ambayo ni mapya kwa watumiaji wengine
ambayo huitaji kupewa ufafanuzi. Tazama mfano (i-ii) kwa ufafanuzi.
Neno Maana
i.
Ng’aure Paka wa Kike
ii.
Mafurudhati Hali ya kuwa nana tabia ya
usahaulifu na kupuuza mambo ya
Kimsingi anayotakiwa kufanya mtu.
Chanzo Wamitila (2010).
Katika mfano (i-ii) hapo juu, ni dhana mpya kwa watumiaji wengine na zimeingizwa kwenye
kamusi na kupewa ufafanuzi. Hivyo, lengo la kueleza na kufafanua dhana mpya huwa linatimizwa
na watunga kamusi kwa kutumia nadharia ya dhana/taswira ambayo hulitazama neno.
3.0 Hitimisho
Makala haya yameangazia Nadharia za Maana, Malengo ya watunga kamusi, na Namna ambayo
nadharia za semantiki zinavyowasaidia watunga kamusi katika kutimiza malengo yao. Kuhusu
nadharia za semantiki ambazo zinakidhi malengo ya watunga kamusi nadharia ya dhana/taswira,
nadharia ya uelekezi na nadharia ya matumizi. Kadhalika, makala haya yamebaini kuwa, nadharia
ya matumizi inayotumika kwa kiwango kikubwa na watunga kamusi pindi wapoingiza maana za
maneno kwenye kamusi. Pia, makala haya yamebaini kwamba, kuna uwezekano wa kuwa na neno
moja kutumia nadharia mbili katika kupata maana, mathalani, neno; mbuzi, kata, ota. Kimsingi,
maneno hayo yanaweza kutumia nadharia ya matumizi na nadharia ya dhana/taswira katika kupata
maana zake.
MAREJELEO
Chuwa, A.R. (1995). Dhima ya Kamusi katika Kubainisha Kamusi ya Vihisishi. Vol 4 no 2:
Taasisi ya Taalima za Kiswahili.
Fodor, J. D (1980). Semantics. Theories of Meaning in Generative Gramma. London Harvard
University Press.
Kahigi, K. K. (2019). Misingi ya Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili. Dar es Salaam: KAUTTU.
Mdee, J. S. (2006). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Palmer, R. M. (1976). Semantics. Volume 2. London: Cambridge University Press.
Reimer, N. (2010). Introducing Semantics, New York, Cambridge University Press.
Resani, M (2014). Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili. Dar es Salaam: Karljamer Print
Technology.
Tobing, S. S (2010). Semantics Change and Meaning shift analysis of Film Making terms, Tasnifu
ya Strata 1 Digrii ya Isimu Chuo Kikuu cha Diponegoro.
TUKI, (2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam: Oxford University Press.
Wamitila, K. W. (2010). Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide Muwa.
0 Comments