Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SERIKALI YAWAKUMBUKA WAANDISHI WA FASIHI KUGHARAMIA UCHAPISHAJI WA RIWAYA




 Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Wizara yake itatenga bajeti kwa ajili ya mtu yeyote mwenye muswada wa kuandika riwaya ambazo zitashindanishwa na muswada utakaoshinda utagharamiwa uchapishaji wake na Wizara.

Amesema hayo Jijini Dodoma alipokutana na wawakilishi wa Mwandishi wa Kitabu cha Hesabu kilichoandikwa kwa kutumia mitaala ya Kenya, Uganda na Tanzania, David Inzofu ambapo amesema lengo ni kuona kunakuwa na Watanzania wengi wanaojitokeza kuandika vitabu.

Kwa mujibu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo, Profesa Mkenda pia amemuagiza Kamishna wa Elimu kuhakikisha kitabu hicho kinapitiwa na wataalamu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ili kama kuna sehemu ya kuboresha kiweze kuboreshwa.

Amesema lengo la kumsaidia mwandishi huyo ni kuongeza hamasa kwa Watanzania wengi zaidi kuandika vitabu na kuhamasisha usomaji.

“Tunataka kusaidia waandishi ambao wanataka kuandika riwaya. Tunaposema elimu yetu tunataka iakisi mahitaji ya nchi yetu na utamaduni wetu tungependa pamoja na wanafunzi kusoma vitabu vya nje wasome pia vilivyoandikwa na Watanzania,” amesema.

Amesema kumekuwepo na maoni ya kutumia Kiswahili kufundishia katika siku zijazo, hivyo kunahitaji maandalizi ili kuweza kufika huko, Watanzania wenyewe waandike vitabu wawe tayari, uwezo na uzoefu wa kutafsiri vitabu vya Kiingereza kuwa vya Kiswahili.

“Tungependa kukuza Kiswahili na hii inahitaji maandalizi, hivyo lazima kuwe na vitabu vingi vya Kiswahili, huwezi kuanza kutumia lugha ya Kiswahili huku vitabu vikiwa vya Kiingereza,”amesema.

Amesema mwalimu huyo ametafsiri kitabu hicho kwa lugha ya Kiswahili na kwamba  itabidi Serikali imsaidie ili Baraza la Kiswahili lihakiki kitabu hicho.

Kwa upande wao, mmoja wa wawakilishi wa mwandishi wa kitabu hicho, Novatus Makunga amemshukuru Waziri Mkenda kwa kukubali kupokea nakala hizo kwa ajili ya kuvipitia.

Amesema hiyo inaonyesha nia njema ya Serikali iliyo nayo kushirikiana na wadau wengine wa elimu katika kuendelea kuboreaha elimu nchini

Post a Comment

0 Comments