Sephania Kyungu
sephaniakyungu06@gmail.com
Owomugisha Rominate
rowomugisha8@gmail.com
Ikisiri
Makala hii inalenga kuchambua usawiri wa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile. Haja ya kuchambua usawiri wa mhsika Kichaa katika riwaya hii imetokana na madai ya Mbatiah (1978) ambaye anasema kwamba usawiri wa wahusika katika riwaya ya Mzingile si halisia. Mwandishi wa makala hii anaona kwamba licha ya kwamba wahusika wengi katika riwaya ya Mzingile kama vile Kakulu, Mzee, Kipofu na Mwanamke ambao si halisi, wapo ambao ni halisia akiwemo mhusika Kichaa. Makala hii inachambua usawiri wa mhuska Kichaa kwa kuangalia hali halisi ya Kichaa katika jamii. Ili kukidhi azima hii, makala hii iliongozwa na Nadharia ya Uhalisia katika uchambuzi wa usawiri wa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile. Makala hii imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao unajumuisha maelezo kuhusu mada, nadharia, mbinu ya ukusanyaji wa data na suala la Kichaa katika jamii. Sehemu ya pili ni usawiri wa mhusika Kichaa, na mwisho ni hitimisho.
1. Utangulizi
Riwaya ya Mzingile ni miongoni mwa riwaya za majaribio (taz. Mbatiah, 1978 na Njogu, 2014). Mbatiah anaongeza kuwa usawiri wa wahusika katika riwaya ya Mzingile hauna uhalisia. Anaendelea kueleza kuwa riwaya ya Mzingile imejikita kabisa katika masuala ya kidhanaishi, bila kujishughulisha na masuala ya kijamii. Maelezo haya yana maana kwamba mambo yanayoongelewa kwenye riwaya hizi mbili hayaakisi jamii tunayoishi. Mahitimisho ya namna hii ni jumla mno. Kutokana na madai kama haya, makala hii ikaona ipo haja ya kuyachunguza mahitimisho hayo kwa kuchambua usawiri wa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile kwa kujiegemeza katika Nadharia ya Uhalisia.
Nao, Bulaya na Mkumbwa (2014) wanazungumzia sifa za riwaya ya majaribio wanasema zina sifa ya kuwa na mparanganyiko wa matukio; yaani hayapangwi katika hali ya kujengana, matumizi ya fantasia na mazingaombwe, mwingiliano matini, uchanganayaji wa historia na ubunifu, matumizi ya wahusika na mandhari ya kidhanaishi mambo ambayo msingi wake mkuu upo katika visasili. Maelezo haya yanadokeza suala la wahusika katika riwaya za majaribio kwamba ni la kidhainshi yaani ni wa kufikirika. Mawazo kama haya ni ya kijumla sana ambayo yanadhirisha ombwe la maarifa ya uhalisia hakiki kuhusu suala la wahusika katika riwaya za majaribio kama vile Mzingile. Hali hii ndiyo iliyotoa raghba kuandikwa kwa makala hii ili kujaribu kuziba pengo la maarifa ya uhalisia hakiki katika riwaya za majaribio kama vile Mzingile kwa kujikita katika wahusika.
Aidha, Njogu (2014) amegusia suala la wahusika katika riwaya ya Mzingile kwa kueleza kwa muhtasari wahusika wanaopatikana katika riwaya hizo. Muhtasari huo kwa kweli unaelezwa bila kujiegemeza katika nadharia yoyote. Mhusika Kichaa anayelengwa kushughulikiwa katika makala hii ameelezwa pia kwa muhtasari bila uchambuzi wowote. Hali hii inaonesha kwamba suala la wahusika bado ni pengo katika riwaya hizo. Makala hii inakusudia kupunguza ombwe la maarifa kuhusiana na wahusika katika riwaya ya Mzingile kwa kuchambua usawiri wa mhusika Kichaa kwa kuongozwa na Nadharia ya Uhalisia.
2 Nadharia ya Uhalisia
Makala hii inaongozwa na Nadharia ya Uhalisia ambayo inaangazia uhusiano uliopo baina ya yale yanayozungumziwa katika kazi ya fasihi na jamii iliyomkuza mwandishi. Imetubidi kutumia nadharia hii kutokana na kuwapo kwa madai kwamba riwaya za majaribio kama vile Mzingile usawiri wake wa wahusika si halisi ambapo makala hii inachukulia kuwa haya ni mahitimisho ya jumla mno. Mahitimisho ambayo yanalionekana kwamba yamefikiwa bila uchaunguzi wa kina unaongozwa na Nadharia ya Uhalisia ili kujua ikiwa ni kweli kwamba mambo yaliyomo katika riwaya za majaribio si halisia ikiwemo wahusika wake au la.
Kwa mujibu wa Wafula na Njogu (2007), Nadharia ya Uhalisia iliasisiwa na Gustav Flaubert (1821-1880). Msisitizo wa Gustav Flaubert ulikuwa katika fikra za mtu na ubainishwaji wa matatizo ya kijamii katika uhalisia wake. Nadharia ya uhalisia iliibuka kwa lengo la kupinga Nadharia ya Ulimbwende ambayo ilishindwa kuyasawiri maisha kama yalivyo, Wanauhalisia waliamini kwamba fasihi inapaswa kuyasawiri maisha kama yalivyo bila kupotosha wala kutia chumvi (Msokile,1993; Mbatiah, 2001; Wafula na Njogu, 2007; Mulokozi, 2017).
Larkin (1992) anaunga mkono mawazo makuu ya Nadharia ya Uhalisia, kwa kusema kwamba jukumu la msanii ni kuwarudisha wasomaji katika ulimwengu wa kawaida na kwamba ulimwengu atakao uumba mwandishi unapaswa uwe wa kweli na halisi. Hii ina maana kwamba msanii hana uhuru wa kuingiza ubunifu ambao haupo kwenye jamii. Mawazo haya yanashadadiwa pia na Wamitila (2003) ambaye anasema Nadharia ya Uhalisia inasisistiza usawiri wa mambo kwa uaminifu na usahihi wake katika jamii.
Aidha, baadhi ya misingi ya Nadharia ya Uhalisia kulingana na Wafula na Njogu (2007) ni pamoja na:
Fasihi isawiri na kueleza mambo kwa kuzingatia uhalisia wake.
Fasihi ieleze mambo ya kihistoria yasababishayo mabadiliko chanya kwa jamii.
Fasihi itoe picha halisi ya jamii bila ya kudunisha au kutia chuku.
Fasihi ioneshe matumaini kwa binadamu kuweza kushinda matatizo yake yanayomzunguka katika mazingira yake.
Makala hii ilitumia msingi wa kwanza na wa pili katika kuchambua usawiri wa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile kwa kuangalia namna anavyosawiriwa katika kazi hiyo na hali halisi katika jamii. Jambo ambalo litasaidia kuondoa mawazo ya jumla kuhusu usawiri wa wahusika katika riwaya za majaribio kwamba si halisia.
3 Methodolojia
Data za makala hii zimepatika kwa njia ya usomaji wa matini ambapo mwandishi alisoma riwaya ya Mzingile ili kuweza kuelewa namna mhusika Kichaa anavyosawiriwa. Hivyo, ili kuweza kuelewa hili mwandishi alisoma riwaya hiyo mwanzo mpaka mwisho na kuweka alama sehemu zinazomhusu mhusika Kichaa pamoja na namna anavyosawiriwa. Data zimewasilishwa kwa njia ya maelezo yaliyoshadididwa na nukuu kutoka katika matini teule.
4 Suala la Kichaa katika Jamii
Kwa mujibu wa Resani (2017) akirejelea kamusi Elezo Huru anasema Kichaa ni mtu ambaye kisayansi amepata madhara katika mfumo wa ubongo. Madhara hayo yanaweza kuwa yameletwa na ugonjwa, ajali au matumizi ya kemikali zinazoweza kuharibu mfumo wa kawaida wa ubongo. Kuna magonjwa mengi na tofauti ya akili yananyoathiri ubongo wa binadamu na magonjwa hayo husababisha huzuni kupindukia, wasiwasi, kutojali chochote katika maisha ya Kichaa ambaye hutenda kinyume na matarajio ya jamii inayomzunguka. Kadhalika, magonjwa ya akili huathiri jinsi mtu anavyowaza na kuhisi, kuona, kunusa na kusikia. Maelezo haya yana ukweli kwani Kichaa anaweza kukaa kutwa sehemu chafu na bila kufikiria madhara ambayo yanaweza kumpata kwa sababu. Pia, kichaa anaweza kukaa katika eneo la chafu bila kujali kwa sababu ya kuathirika kwa mfumo wake wa upumuaji.
Aidha, Resani anaongeza kuwa dalili za ugonjwa wa akili ni pamoja na mtu kukosa hamu ya kutenda mambo ya kawaida ya kila siku. Hivyo, mtu hujikuta hawezi mambo kama vile kuoga, kufua, au kupika. Katika ipindi hiki unamkuta mtu anaongea yeye mwenyewe bila kujijua. Kwa ufupi, Kichaa hufanya mambo ambayo si ya kawaida. Makala hii inalenga kuchambua ikiwa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile anasawiriwa kama vichaa wengine walivyo katika jamii.
5.0 Usawiri wa Kichaa katika Riwaya ya Mzingile
Usawiri wa mhusika ni namna msanii anavyomchora mhusika katika kazi ya fasihi. Kuna njia anuwai ambazo zinaweza kutumika kumaizi namna mhusika fulani anavyosawiriwa katika kazi za fasihi kama vile mwitiko wake kwa wengine, mwitiko wake yeye mwenyewe, kile anachosema yaani kauli yake mwenyewe, matendo yake kwa wengine na mwonekano wake. Kwa hiyo, ili kubaini namna mhusika Kichaa anavyosawiriwa katika riwaya ya Mzingile, makala hii ilitumia njia hizo kama inavyofafanuliwa katika sehemu inayofuata.
5.1 Kichaa kama Mtani wa Watoto
Mtani ni mtu ambaye ana uhuru wa kumfanyia mwenzie masihara katika mazingira mwafaka bila kuzusha sokomoko (TUKI, 2019). Katika riwaya ya Mzingile msanii anatusimulia kuwa Kichaa ni mtani wa watoto. Dondoo lifuatalo linadhihirisha maelezo haya:
“Leo nawasikia wapitao karibu na kibanda changu wakisema “kichaa chake kimetulia”, Natabasamu. Ni vizuri kuwa kichaa. Ni vizuri kuogopwa na ni vizuri kuwa mtani wa watoto wapendao kucheka”.
(Mzingile, 2011: 32)
Dondoo hili linaonesha Kichaa ni mtu ambaye anapenda kucheka na watoto kwa kuwa wanapenda hivyo. Katika hali halisi vichaa huwa na tabia ya kutaniana na watoto kwa kuwa wao huwapa ushirikiano kuliko watu wazima ambao huwabagua kutokana na hali zao. Kadhalika, watoto huwa wanapenda kutaniana na vichaa kwa kuwa utani huo si rahisi kuupata kwa watu wazima. Kwa hivyo, katika hali kama hiyo Kichaa hujiona amepata marafiki na watoto hujiona wamepata rafiti. Katika mazingira kama hayo huzuka suala la kutaniana kati yao. Kwa hiyo, usawiri unaojihidhirisha katika riwaya ya Mzingile una uhalisia kwani unatupa picha halisi ya mhusika Kichaa kama alivyo katika jamii.
5.2 Kichaa kama Mtu Huru
Mtu huru ni yule ambaye hafungwi na chochote; yaani hayupo chini ya kitu au mtu yoyote. Katika riwaya ya Mzingile, msanii anamsawiri Kichaa kama mtu huru ambaye hafungwi na maadili ya kidini au kijamii. Maadili ambayo mara nyingi humfunga mtu asifanye yale atakayo kwa kuhofia kukiuka maadili hayo. Dondoo lifuatalo linadhihirisha haya:
DAIMA nilitaka kuwa kichaa. Lakini akili timamu ziliniusia usiwe! Nilitamani sana kuogelea katika bahari ya nusu urazini, kati ya kuwa na kutokuwako, kati ya ndoto na hali halisi, kati ya uhuru n ufungwa. Daima nilitaka kuwa asili ya kicheko cha furaha na uchungu…. Naam, nilitka uhuru wangu. Uhuru wa kuwa katika kutokuwako.
(Mzingile, 2011:30)
Dondoo hili linaoenesha kwamba Kichaa ni mtu uhuru. Hii inatokana na ukweli kwamba Kichaa hafungwi na maadili ya kidini na kijamii. Kupitia dondoo hilo, mwandishi anatuonesha kwamba mtu hawezi kuwa huru kama si Kichaa kwa sababu anafungwa na maadili ya dini na kijamii. Maadili haya yanamtaka mtu kufanya hiki na kutofanya kile. Kwa mfano, maadili ya dini ya kikatoliki Padri haruhusiwi kujihusisha na ngono licha ya kwamba hutamani kufanya hivyo ila anafungwa na maadili hayo. Kadhalika, katika maadili ya kijamii mtu haruhusiwi kutukana, kutembea uchi na kadhalika. Kwa upande wa kichaa hufungwi na maadili hayo.
Resani (2017) anashadidia maelezo haya anaposema Kichaa anapenda lugha ya matusi. Kadhalika, Kichaa anaweza kushinda jalalani, kula chakula kichafu, kutokuoga na mengine yanayoendana na hayo. Yote haya anayafanya bila kufungwa na maadili ya kijamii ambayo hayaruhusu mambo hayo. Maleezo haya yanaonesha kwamba Kichaa ni mtu mwenye uhuru wote, yaani anaeza kufanya lolote bila ufungwa wowote. Hii inaonesha kwamba usawiri wa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile unaendana na hali halisi ya jamii ambapo Kichaa anaweza kufanya lolote bila ufungwa wowote. Hii ndio sababu mwandishi anasema “nataka kuwa kichaa” yaani kuwa huru.
5.3 Kichaa kama Mtu Anayeishi kwenye Nyumba Mbovu
Katika riwaya ya Mzingile mhusika Kichaa anasawiriwa kama mtu anayeishi kwenye nyumba chakavu. Hili linajidhihirisha kupitia mazungumzo ya mhusika Mimi na Mzee. Dondoo lifuatalo linadhihirisha hilI:
“Nitokako nyumba kama hii haziko tena.”
“Kwa nini!”
“Zimechakaa mtindo. Wakati nikiwa mdogo niliziona. Lakini baadaye ilitolewa amri zivunjwe zote. Mijini na mashambani. Badala yake nyumba mpya za kisasa zilijengwa.
“Ha!”
Kusema kweli nyumba kama hii ikionekana itafikiriwa ya kichaa. Itavunja heshima ya wananchi.
“Ina maana kuna mafundi kunizidi mimi?”
Wapo, tena wengi.”
Ha! Wanatumia muda gani kujenga hizo nyumba mpya.?”
(Mzingile, 2011: 25)
Kupitia mazungumzo ya mhusika Mimi kuhusu nyumba ambayo Mzee anaishi, inaonesha kuwa Kichaa anasawiriwa kama mtu anayeishi kwenye nyumba za ajabu. Hii inatokana na namna nyumba ya Mzee ilivyo ambapo dondoo hili linaonesha ni nyumba za zamani ambazo ziliachwa kukaliwa na watu kitamboo na kwamba mtu yeyote anayeendelea kuishi katika nyumba hizo hufananishwa na Kichaa. Aghalabu nyumba hizo huwa ni makazi ya mijusi, popo na viumbe wengine wanaopenda kuishi kwenye mapango. Kadhalika, nyumba hizi huwa zinavuja, hazipo imara. Nyumba aliyokuwa anaishi Mzee ilikuwa na sifa zinazoelekeana na hizi. Hii ina maana kwamba msanii alikuwa sahihi kumsawiri mhusika Kichaa kwa sababu hata katika maisha ya kawaida Vichaa huishi katika nyumba za aina hiyo. Aidha, Kichaa huamini kuwa nyumba hiyo inafaa kama za wengine na hata anapoambiwa kwamba nyumba yake ni mbovu huwa anawashangaa wanaomshangaa.
5.4 Kichaa kama Mwanamapinduzi
Mapinduzi ni mabadiliko ya mbinu au hali kama vile kilimo, elimu na kadhalika (TUKI, 2019). Kwa hivyo, tunaposema mwanamapinduzi ni mtu anayepanga kuleta mabadiliko makubwa katika jamii kuhusu mambo anuwai ya kijamii. Katika riwaya ya Mzingile kupitia maneno ya Kichaa yanaonesha ni mwanamapinduzi. Dondoo lifuatalo linadhihirisha hilo;
“ULIMWENGU unahitaji, mwanga mpya!” Kichaa alipiga kelele na kisha akaongezea, “Lakini hiyo haitakuwa kabla ya uharibifu wa maafa!” Tulikuwa kilabuni tukinywa pombe. Watu walicheka. Mimi pia nilicheka, lakini maneno yake yaliamsha ari ya kutaka kujua asili ya mwanga.
(Mzingile, 2011: 8)
Dondoo hili linaonesha kwamba Kichaa alitaka kuleta mabadiliko ya hali ya watu kuamini visasili na kuanza kuamini ukweli. Hata hivyo, kitendo cha watu kucheka kama inavyooneshwa katika dondoo hili kina maana kwamba watu walimcheka Kichaa kwa sababu wanajua si rahisi kubadili visasili hivyo ambavyo tayari vilikuwa vimetawala akili za watu. Katika hali halisi si jambo la ajabu kumkuta Kichaa akiwa na lengo la kubadilisha hali ya kiuchumi katika familia yake kama vile kujenga ghorofa, kununua gari, kuwajengea nyumnba nzuri watoto wake kama anao. Hali hii inatokana na Kichaa kujiona kwamba yeye ni bingwa wa kila kitu. Hali hii haina tofuti na namna Kichaa anavyorajia kufanya mambo makubwa katika jamii. Katika dondoo hilo ambalo ni la kuleta mwanga mpya (ukweli), kimsingi suala la kuleta uhalisia na ukweli mpya katika jamii ambayo imefungwa na kisasili cha kuwapo kwa Mungu si jambo rahisi. Kulingana na Nadharia ya Uhalisia usawiri huu unatoa picha halisi ya Kichaa kama vile alivyo katika jamii kwa sababu matarajio yake yanaendana na Vichaa wanapatikana katika jamii zetu.
5.5 Kichaa kama Mtu Asiyeogopa
Katika riwaya ya Mzingile, mhusika Kichaa anasawiriwa kama mtu asiyeogopa kupitia matendo ambayo Kichaa anayoyafanya ambayo yanaonesha kwamba ni mtu asiyeogopa kama vile kuwavulia watu nguo. Dondoo hili linadhihirisha hilo kama ifuatavyo:
“Ni vizuri kuwa kichaa. Ni vizuri kuogopwa na vizuri kuwa mtani wa watoto wapendao kucheka. Wakati mwingine huwavulia watu nguo makusudi mazima na wakati mwingine huwakenulia meno hali ya macho yangu yakiwa mekundu.”
(Mzingile, 2011:32)
Dondoo hili imeonesha kwamba kichaa ni mtu asiyeogopa kitu kama vile maadili ya kijamii ambayo hayaruhusu mtu mzima kuvua nguo hadharani. Tabia hizi za Kichaa kutoogopa maadili ya kijamii kama kuvua nguo hadharani hutokana na kufanya mambo bila kuwa na uelewa na utashi wa akili. Resani (2017) anashadadia usawiri huu anaposema kuwa Kichaa huamini kwamba yeye ni bingwa wa kila kitu. Resani anaendelea kueleza kwamba Kichaa utamkuta akiongea chochote kinachotoka mdomoni hata kama kinaweza kuwakera watu wengine, lakini yeye hajali.
Aidha, katika maongezi ya Kichaa kuhusu dini yanaonesha kwamba hogopi. Kwani anaeleza kwamba itikadi na imani ya dini ni uzushi tu wa watu ambao hawayachunguzi mambo kwa kina. Usawiri huu unajidhihirisha kupitia simulizi anayotoa Kichaa kwamba siku moja aliingia kanisani kupitia dirishani alikaa kwenye altare. Masista walipokaribia alipiga chafya na masista hao wakaanza kukimbia ovyo na kudai kuwa Yesu amewatokea. Watu walisadiki habari hizo ingawa hazikuwa za kweli. Dondoo lifuatalo linaonesha namna Kichaa anavyoeleza jinsi uzushi huo ulivyopokelewa:
Nafikiri miaka kumi sasa imepita tangu walipobomoa kanisa hilo na kujenga kanisa kubwa la makumbusho. Maelefu ya wagonjwa wamefika kuubusu huo msalaba. Nimesikia baadhi wamepona. Padri wa kanisa hilo amenishauri mara nyingi mimi pia nikaubusu msalaba nipate kupona kichaa changu.
(Mzingile, 2011: 33)
Dondoo hili linaonesha namna uzushi unavyoenea kuhusu masuala ya imani. Kupitia kisa hiki cha Kichaa anaeleza ukweli mchungu bila hata kuogopa jinsi watu wasivyochunguza mambo kwa kina na kupokea kama yalivyo. Matokeo yake ni kuzuka kwa imani mbalimbali ambazo zimefanya mwanadamu kuwa mtumwa. Hii ina maana kwamba hulazimika kufuata masharti ya imani husika. Aidha, kuhusu kisa hicho Kichaa anaongezea kuwa:
“Je kisa hiki unakionaje? Kama wewe ni padri najua utacheka kwa mnuno. Uzushi? Ufurahi usifurahi sijali. Mimi ni kichaa na wachache wananiamini”
(Mzingile, 2011:33)
Dondoo hili linaonesha kwamba pamoja kwamba Kichaa anajua kwamba kisa hicho kina ukweli mchungu lakini hajali iwapo watu wanafurahi au hawafurahi. Hali hii ni kawaida kwa Kichaa kusema ukweli bila kuogopa. Utamkuta Kichaa akieleza mambo ambayo watu hawawezi kuongea hadharani lakini yenye huongea bila kuogopa chochote. Resani (2017) anadokeza pia kuhusu hili anaposema kwamba Kichaa utamkuta akiongea chochote tu kinachomtoka mdomoni bila kujali watu watakipokeaje na yeye atakuwa katika mazingira gani baada ya kusema jambo hilo. Hii inaonesha kwamba usawiri wa mhusika Kichaa katika riwaya ya Mzingile ni halisi kwa sabubu unatoa picha halisi ya Vichaa tunaoishi nao katika jamii.
6 Hitimisho
Makala hii imeangazia usawiri wa Kichaa katika riwaya ya Mzingile. Kwa kutumia mbinu anuwai za kubaini namna mhusika anavyosawiriwa katika kazi ya fasihi. Makala hii imebaini kwamba mhusika kichaa anasawiriwa kama mtani wa watoto, mtu huru, mtu anayeishi kwenye nyumba mbovu, mwanamapinduzi na kama mtu asiyeogopa. Aidha, imebainika kwamba usawiri wa Kichaa unaojitokeza katika riwaya ya Mzingile unaakisi uhalisia wa Vichaa waliopo katika jamii. Tofauti na madai ya wataalamu kama Mbatiah (1998) aliyesema usawiri wa wahusia katika riwaya ya Mzingile si halisi. Kwa hiyo, makala hii inatamatisha kuwa katika riwaya ya Mzingile kuna usawiri wa wahusika ambao si halisi kama vile usawiri wa Mzee, Kipofu, Kakulu na Mwanamke aliyemsaidia Mimi kumwongoza njiani na kuna wale ambao ni halisi kama vile Kichaa na Padri.
MAREJELEO
Bulaya, J na Mkumbwa, A. (2014) “Kufungamana kwa Fasihi Simulizi na Riwaya ya Kiswahili ya Kimajaribio: Uchambuzi wa Visa katika Binadamu”. Kioo cha Lugha, Juz. 12:100-112.
Kezilahabi, E. (2011) Mzingile. Nairobi: Vide- Muwa Publishers Limited.
Larkin, M. (1992) A Man and Society in Nineteenth Century Realism. London: Macmillan.
Mbatiah, M. (2001) Kamusi ya Fasihi. Nairobi: Standard TextBooks Graphics and Publishers.
Mbatiah, M. (1998) “Mienendo Mipya Katika Uandishi wa Kezilahabi: Nagona na Mzingile”. Mulika, Juz, 24: 1-13.
Mulokozi, M.M. (2017) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Kozi za Fasihi Vyuoni na Vyuo Vikuu. Dar es Salaam: KAUTTU.
Msokile, M. (1993) Misingi Ya Uhakiki Wa Fasihi. Nairobi: East Africa Education Publisher.
Njogu, G. W. (2014) Fumbo la Uhai na Kifo katika Riwaya za Euphrase Kezilahabi: Nagona na Mzingile. Tasnifu ya Umahiri (Haijachapishwa) Chuo Kikuu Cha Kenyatta, Nairobi.
Resani, M. (2017) Lugha na Ubongo: Athari za Kisaikolojia katika Kuibua Mitindo ya Matumizi ya Lugha. Mulika, Juz. 36:40-51.
TUKI (2019) Kamusi Ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Wafula, R. M. na Njogu, K. (2007) Nadharia za uhakiki wa fasihi. Nairobi: Jomo kenyatta foundation.
Wamitila, K. W. (2003) Kamusi ya Kiswahili, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication Ltd.

0 Comments