Sephania Mungasyeghe
Tasinifu ya MA (Kiswahili)
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Novemba 2021
UCHAMBUZI WA MICHAKATO YA KISINTAKSIA KATIKA UUNDAJI WA SENTENSI CHANGAMANI ZA KISWA
Sephania Mungasyeghe Kyungu
Iliyowasilishwakwa Ajili ya Kukamilisha Sehemu ya Masharti ya Kutunukiwa Digrii ya MA (Kiswahili) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Novemba 2021
UTHIBITISHO
Aliyesaini hapa chini anathibitisha kuwa ameisoma tasinifu hii yenye mada: Uchambuzi wa Michakato ya Kisintaksia katika Uundaji wa Sentensi Changamani za Kiswahili, na anapendekeza ikubalike na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya utahini.
...
Dkt. Luinasia E. Kombe
(Msimamizi)
Tarehe:
IKIRARI
NA
HAKIMILIKI
Mimi, Sephania Mungasyeghe Kyungu, ninathibitisha kuwa tasinifu hii ni kazi yangu halisi na haijawahi kuwasilishwa na haitawasilishwa katika chuo kikuu kingine chochote kwa ajili ya kutunukiwa digrii kama hii au digrii nyingine yoyote.
Saini: ......................................................
Haki ya kunakili tasinifu hii inalindwa na Mkataba wa Berne, Sheria ya Hakimiliki ya mwaka 1999 na matamko mengine ya kitaifa na kimataifa. Kwa maana hiyo, ni milki dhihini. Hairuhusiwi kunakiliwa kwa namna yoyote ile, ikiwa ni kazi nzima au sehemu ya kazi hii, isipokuwa kwa matumizi halali ya kiutafiti, kujisomea au tahakiki za kitaaluma, bila kibali cha maandishi cha Mkurugenzi wa Shahada ya Uzamili kwa niaba ya mwandishi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
SHUKURANI
Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na nchi kwa kunijalia afya njema ya roho, mwili na akili katika kuifanya kazi hii tangu hatua ya kwanza hadi kukamilika kwa tasinifu hii. Ama kwa hakika, ukamilifu wa tasinifu hii hautokani na urazini au tajiriba yangu mwenyewe, ila ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu.
Pili, ninaishukuru Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwa kuniteua na kuniamini kuwa miongoni mwa wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo ya MA (Kiswahili), kwa hisani ya Kampuni ya ALAF, Novemba 2020.
Tatu, ninamshukuru sana Msimamizi wangu, Dkt. L. Kombe kwa kuniongoza, kunielekeza, kunishauri na kunilea kitaaluma hadi kufanikisha kazi hii. Amenionesha ushirikiano mkubwa na amekuwa msaada mkubwa kwangu. Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, amani, baraka na kibali katika maisha yake.
Nne, ninawashukuru walimu wangu wa MA (Kiswahili) walionifundisha kipindi cha tamrini. Miongoni mwao ni Prof. P. Malangwa, Prof. S. Omari, Dkt. M. Hans, Dkt. E. Mosha, Dkt. A. Buberwa, Dkt. R. Chipila, Dkt. M. Mashauri, Dkt. G. Mrikaria, Dkt. F. Mwendamseke, Dkt. E. Mahenge, Dkt. R. Kidami, Dkt. A. Msigwa, Dkt. A. Mnenuka, Dkt. Z. Limbe na Dkt. M. Kibiki. Ushauri na miongozo yao ya kitaaluma na kijamii kwa hakika sitaisahau. Mungu awabariki sana. Kando na hao, ninawashukuru wafanyakazi wote wa TATAKI, wahadhiri na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kunipa msaada wa hali na mali.
Tano, ninaishukuru familia yangu, kwanza baba yangu mzazi Mungasyeghe Kyungu na mama yangu mzazi Helena Mwasyika kwa malezi yao mema ambayo yamenichochea kuwa na ari ya kujiendeleza kielimu. Pia, ninawashukuru kaka zangu Azimio, Lazaro, Patrick, Yona na dada zangu Tumaini na Sophia pamoja na mdogo wangu Mordekai. Mungu azidi kuwabariki na kuwapa kibali kwa kila kitu mkifanyacho.
Sita, ninawashukuru wanafunzi wenzangu wa MA (Kiswahili) wa mwaka 2019-2021 kwa jamala zao kwangu, hasa wale wa mkondo wa isimu. Kadhalika, ninawashukuru ndugu, jamaa na marafiki wote ambao kwa namna moja ama nyingine wamechangia katika kufanikisha kazi hii. Ninatambua mchango wao. Mungu awabariki sana. Aidha, kwa kuwa wapo watu lukuki walionisaidia katika kukamilisha kazi hii, kutokana na wingi wao siwezi kuwataja wote. Ninaamini kwamba hawatakereka pindi watakaposoma shukurani hii bila kuona majina yao.
Mwisho, ninapenda kukiri kuwa waliotajwa hapa hawatawajibika kwa kasoro au makosa yoyote yatakayogundulika katika tasinifu hii.
TABARUKU
Kwa baba yangu mzazi,
Mungasyeghe Kyungu
Kwa mama yangu mzazi,
Helena Mwasyika
Kwa kaka zangu,
Azimio, Lazaro, Patrick, Yona na Mordekai
Kwa dada zangu,
Sophia na Tumaini.
ORODHA YA VIFUPISHO NA ALAMA
E Kielezi
H Kihusishi
KB Kishazi Bebwa
KBE Kishazi Bebwa Elezi
KBN Kishazi Bebwa Nomino
KBV Kishazi Bebwa Vumishi
KH Kirai Kihusishi
KK Kishazi Kikuu
KN Kirai Nomino
KT Kirai Kitenzi
KV Kirai Kivumishi
MN Muundo wa Ndani
MNJ Muundo wa Nje
N Nomino
Na. Namba
NMV Nadharia ya Muundo Virai
NR Nadharia Rasmi
S1 Sentensi ya Kwanza
S2 Sentensi ya Pili
SA Sentensi Ambatani
SC Sentensi Changamani
SGZ Sarufi Geuzi Zalishi
SS Sentensi Sahili
t Kitenzi Kishirikishi
T Kitenzi Kikuu
taz. Tazama
Ts Kitenzi Kisaidizi
U Kiunganishi
UT Kiunganishi Tegemezi
UTM Kiunganishi Tegemezi Maalumu V Kivumishi
W Kiwakilishi
ÆŸ Umbo Kapa
Inaonesha Uhamishaji wa Kiambishi Rejeshi
Inaonesha Kishazi Kubebwa Ndani ya S1
- Inaonesha Mpaka wa Mofimu
{} Inaonesha Unukuzi wa Kiambishi
[] Inaonesha Kishazi au Sentensi
IKISIRI
Utafiti huu ulilenga kuchunguza michakato ya kisintaksia katika uundaji wa sentensi changamani za Kiswahili, kwa kueleza namna sentensi hizo zinavyoundwa na kubainisha michakato inayotumika kuunda sentensi hizo. Data za utafiti huu zilipatikana maktabani katika riwaya na magazeti. Mbinu ya usomaji matini ilitumika kukusanya data, kisha data hizo zilichambuliwa kiuelezi. Utafiti huu ulitumia mkabala wa kitaamuli na kuongozwa na Nadharia Rasmi ya Chomsky (1965). Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa sentensi changamani zina miundo tofautitofauti. Mosi, kuna sentensi changamani zinazoundwa kwa kishazi kikuu na kishazi bebwa nomino. Sentensi hizi huundwa kwa kuchopeka kiunganishi tegemezi kama vile kuwa, kwamba na kama kwenye kishazi cha pili ambacho hukifanya kishazi hicho kufanya kazi kama nomino. Pili, kuna sentensi changamani zinazoundwa kwa kishazi kikuu na kishazi bebwa vumishi, hizi huundwa kwa kupachika kiambishi rejeshi kwenye sehemu ilipodondoshwa nomino radidi, kisha kiambishi hicho huhama na kupachikwa kwenye kitenzi kilicho karibu na kisabiki chake au kwenye mzizi AMBA. Mageuzi haya hukifanya kishazi kilicho na kiambishi rejeshi kufanya kazi ya kukumusha nomino ya kishazi cha kwanza. Tatu, kuna sentensi changamani zinazoundwa kwa kishazi kikuu na kishazi bebwa elezi. Sentensi hizi huundwa kwa kupachika viunganishi tegemezi maalumu kama vile kama, ili, kwani, nge, na ki mahali nomino radidi ilipodondoshwa au mwanzoni tu mwa kishazi cha pili. Mageuzi haya hukifanya kishazi kilichopachikwa kiunganishi tegemezi kufanya kazi ya kueleza zaidi kuhusu kitenzi cha kishazi cha kwanza. Pia, matokeo yanaonesha kwamba kuna michakato mitatu ya uundaji wa sentensi changamani nayo ni: uchopekaji, udondoshaji-chopezi na udondoshaji-chopezi hamishi. Michakato hii ni tofauti na ile iliyoelezwa na Wesana-Chomi (2017) ambayo ni ujalizaji na urejeshaji. Matokeo ya utafiti huu yana mchango katika sintaksia ya Kiswahili kwa kuwa yanaonesha namna sentensi changamani zinavyoundwa, zinavyochanganuliwa na michakato inayotumika kuziunda. Utafiti huu unapendekeza kuwa tafiti zenye mrengo kama huu zinaweza kufanywa kwenye lugha zingine za Kibantu kwa lengo la kuchunguza michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi changamani za lugha hizo.
YALIYOMO
Uthibitisho i
Ikirari na Hakimiliki ii
Shukurani . iii
Tabaruku… v
Orodha ya Vifupisho na Alama vi
Ikisiri. viii
Orodha ya Vielelezo xii
SURA YA KWANZA: UTANGULIZI WA JUMLA 1
1.1 Utangulizi 1
1.2 Usuli wa Tatizo la Utafiti 1
1.3 Tatizo la Utafiti 4
1.4 Malengo ya Utafiti 4
1.4.1 Lengo Kuu 4
1.4.2 Malengo Mahususi 4
1.5 Maswali ya Utafiti 5
1.6 Umuhimu wa Utafiti 5
1.7 Mawanda ya Utafiti 5
1.8 Mpangilio wa Tasinifu 5
1.9 Muhtasari 6
SURA YA PILI: MAPITIO YA MAANDIKO NA NADHARIA 7
2.1 Utangulizi 7
2.2 Sentensi Changamani 7
2.3 Michakato ya Kisintaksia 9
2.4 Pengo la Utafiti 11
2.5 Nadharia ya Utafiti 12
2.5.1 Hatua ya Kwanza ya Sarufi Geuzi Zalishi 12
2.5.2 Nadharia Rasmi 14
2.6 Muhtasari 15
SURA YA TATU: METHODOLOJIA YA UTAFITI 16
3.1 Utangulizi 16
3.2 Eneo la Utafiti 16
3.3 Wango, Sampuli na Usampulishaji 17
3.3.1 Wango 17
3.3.2 Sampuli 17
3.3.3 Usampulishaji 18
3.4 Mbinu ya Ukusanyaji Data 20
3.5 Vifaa vya Utafiti 20
3.5.1 Kalamu ya Risasi 21
3.5.2 Kalamu ya Wino na Shajara 21
3.5.3 Kompyuta Pakatwa 21
3.6 Uchambuzi wa Data 22
3.7 Kanuni za Kiitikeli 23
3.8 Kikwazo cha Utafiti 23
3.9 Muhtasari 23
SURA YA NNE: UWASILISHAJI NA UCHAMBUZI WA DATA 25
4.1 Utangulizi 25
4.2 Namna Sentensi Changamani za Kiswahili Zinavyoundwa 25
4.2.1 Sentensi Changamani Zenye Muundo wa Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Nomino 26
4.2.2 Sentensi Changamani Zenye Muundo wa Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Vumishi 29
4.2.3 Sentensi Changamani Zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Elezi 33
4.3 Michakato ya Uundaji wa Sentensi Changamani za Kiswahili 37
4.3.1 Uchopekaji wa Viunganishi Tegemezi 37
4.3.2 Udondoshaji-chopezi 41
4.3.3 Udondoshaji-chopezi Hamishi 47
4.4 Muhtasari 52
SURA YA TANO: MUHTASARI, MCHANGO, MAPENDEKEZO NA HITIMISHO 53
5.1 Utangulizi 53
5.2 Muhtasari wa Matokeo ya Utafiti 53
5.3 Mchango wa Utafiti 54
5.4 Mapendekezo ya Tafiti Fuatizi 55
5.5 Hitimisho 55
5.6 Muhtasari 56
MAREJELEO 57
VIAMBATISHO 60
ORODHA YA VIELELEZO
Kielelezo Na.1: Miundo ya SC za Kiswahili 26
Kielelezo Na. 2: MNJ wa SC za Kiswahili Zenye KK na KBN 28
Kielelezo Na. 3: MNJ wa SC ya Kiswahili Zenye KK na KBV 32
Kielelezo Na. 4: MNJ wa SC Kiswahili Zenye KK na KBE 34
Kielelezo Na. 5: MNJ wa SC Kiswahili Zenye KK na KB 36
Kielelezo Na. 6: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Uchopekaji wa UT 38
Kielelezo Na. 7: MNJ wa SC ya Kiswahili IIiyoundwa kwa Uchopekaji wa UT 41
Kielelezo Na. 8: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji- chopezi wa Vipashio 43
Kielelezo Na. 9: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji- chopezi 45
Kielelezo Na.10: Muhtasari wa Udondoshaji-chopezi Jinsi Unavyounda SC za Kiswahili 46
Kielelezo Na.11: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji- chopezi Hamishi 48
Kielelezo Na. 12: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji- Hamishi 50
Kielelezo Na.13: Muhtasari wa Mchakato wa Udondoshaji-chopezi Hamishi 51
Kielelezo Na. 14: Muhtasari wa Matokeo ya Lengo la Pili 54
SURA YA KWANZA
UTANGULIZI WA JUMLA
1.1 Utangulizi
Utafiti huu ulichunguza michakato ya kisintaksia katika uundaji wa sentensi changamani za Kiswahili. Sura hii imejikita katika kujadili taarifa za awali zinazohusu utafiti huu. Hivyo, vipengele vilivyojadiliwa katika sura hii ni usuli wa tatizo la utafiti, tatizo la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti na mawanda ya utafiti. Kabla ya kuhitimishwa kwa sura hii, mpangilio wa tasinifu hii na muhtasari wa sura hii umeelezwa.
1.2 Usuli wa Tatizo la Utafiti
Sintaksia ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na kanuni na michakato ya uzalishaji wa tungo. Kanuni hizo zinahusu namna maneno yanavyopangwa ili kuunda tungo kama vile: virai, vishazi na sentensi (Crystal, 2008; Matei, 2008; Tallerman, 2011). Besha (1994) anaeleza kuwa sintaksia hujishughulisha na uchambuzi na ufafanuzi wa muundo wa sentensi za lugha. Hata hivyo, sintaksia haijishughulishi tu na muundo wa sentensi za lugha, bali pia sheria na kanuni zinazotawala miundo hiyo na uhusiano wa maneno hayo katika tungo husika. Kwa kuzingatia muundo wa sentensi, kuna aina tatu za sentensi: sentensi sahili (kuanzia sasa, SS), sentensi ambatani (kuanzia sasa, SA) na sentensi changamani (kuanzia sasa, SC) (Obuchi na Mukhwana, 2015; Matei, 2008; Wesana-Chomi, 2017). Utafiti huu ulishughulikia SC ambayo ni aina ya sentensi inayoundwa na kishazi huru kimoja na kishazi tegemezi kimoja au zaidi (Massamba, Kihore na Hokororo, 1999). Tazama mfano wa (1) kwa ufafanuzi zaidi.
(1) Mtoto aliyekuja jana, ameondoka leo.
Katika mfano wa (1), sehemu ya tungo iliyoandikwa kwa hatimlazo ni kishazi bebwa (kuanzia sasa, KB) na iliyokoza ni kishazi kikuu (kuanzia sasa, KK).
Katika sintaksia ya Kiswahili SC imeelezwa kwa mawanda tofauti na wataalamu mbalimbali. Baadhi yao ni Massamba (2004), Habwe na Karanja (2004) na Matei (2008) ambao wamefasili SC na kutoa mifano. Wote wanaelekea kukubaliana na fasili ya Massamba na wenzake (wameshatajwa) kwamba SC ni aina ya sentensi ambazo huundwa na kishazi huru kimoja na kishazi tegemezi kimoja au zaidi. Wataalamu wengine wameeleza maana ya SC na kuongeza kipengele cha michakato inayohusika na uundaji wa SC. Miongoni wa wataalamu hao, yumo Wesana-Chomi (2017) ambaye ameeleza muundo wa SC pamoja na michakato ya uundaji wake ambayo ni urejeshaji na ujalizaji.
Kuhusu mchakato wa urejeshaji, Wesana-Chomi (keshatajwa) anaeleza kwamba hutumika kuunda SC zenye vishazi rejeshi kama mojawapo ya viambajengo vyake. Tazama mfano wa (2) kwa ufafanuzi zaidi.
(2) [Polisi wamemkamata mfungwa] S₁ [aliyetoroka jela jana.] S₂
Wesana-Chomi (keshatajwa) anafafanua mfano wa (2) kuwa SC ni matokeo ya mchakato wa urejeshaji ambao huunganisha sentensi mbili, sentensi ya kwanza (kuanzia sasa, S₁) na sentensi ya pili (kuanzia sasa, S₂) kwa kukunjia S₂ katika kirai nomino (kuanzia sasa, KN₂) cha S₁. Anaongeza kuwa katika mfano wa (2), sentensi zilizounganishwa ni S₁ na S₂ kama inavyoonesha katika mfano wa (3).
(3) [Polisi wamemkamata mfungwa] S₁ [Mfungwa alitoroka jela jana] S₂
Kuhusu mchakato wa ujalizaji, anaeleza kuwa SC huundwa kwa KK kimoja na kishazi bebwa nomino (kuanzia sasa, KBN) kimoja ambacho katika muundo wa nje (muundo wa kawaida) hutanguliwa na vitegemezo kama vile kama, kwamba na kuwa kama mfano wa (4a-b) wa SC unavyoonesha.
(4) a. [Wengi wamepata tetesi] S1 [kuwa Cheusi ni mke wa Hamisi.] S2
b. [Juma ameleta habari] S1 [kwamba mgonjwa amefariki asubuhi.] S2
Katika mfano wa (4a-b), KBN kimeandikwa kwa hatimlazo na kimetokea kama kiambajengo cha S1. Hivyo, kishazi tegemezi cha (4a) kinajaliza nomino tetesi ya S1 ilhali kishazi tegemezi cha (4b) kinajaliza nomino habari ya S2. Ifahamike kwamba kabla ya sentensi kuwa hivyo zilivyo katika muundo wa nje (kuanzia sasa, MNJ) wa (4a-b), zilikuwa kama inavyooneshwa katika muundo wa ndani (kuanzia sasa, MN) wa mfano wa (5).
(5) a. [Wengi wamepata tetesi.] S₁ [Cheusi ni mke wa Hamisi.] S₂
b. [Juma ameleta habari.] S₁ [Mgonjwa amefariki asubuhi.] S₂
Wesana-Chomi (2017) anaeleza kuwa katika kuunganisha S₁ na S₂, kiambajengo S₂ hukunjiwa katika muundo wa kiambajengo cha S₁ kama inavyooneshwa katika (4a-b). Katika muundo kama huo, KB (S₂) hufanya kazi kama kijalizo cha nomino.
Ukiyachunguza maelezo hayo kuhusu mchakato wa ujalizaji, utabaini kuwa yanaelekea kuchanganya mchakato wa kimuundo na kidhima. Ujalizaji kuwa dhima ni suala linalodokezwa pia na Philipo na Kuyenga (2018) ambao wanaeleza kuwa ujalizaji ni dhana iliyobuniwa na wanasarufi ili kuelezea uhusiano unaojitokeza pale kauli mbili au zaidi zinaposhikamanishwa kuwa kauli moja. Hali ikiwa hivyo, kauli moja hufanya kazi kama kijenzi mahususi cha kauli nyingine. Maelezo haya yanashadidia madai kwamba ujalizaji si mchakato wa uundaji wa SC bali ni matokeo ya uongezaji wa kiambajengo fulani katika sentensi za Kiswahili. Ikiwa ujalizaji si mchakato bali ni dhima, mtafiti alitaka kufahamu ni mchakato gani hutumika kuunda sentensi zilizopo kwenye mfano wa (4a-b).
Baada ya mtafiti kusoma michakato ya uundaji wa SC iliyoelezwa na Wesana-Chomi (keshatajwa) na kuangalia miundo yake, alibaini kwamba muundo wa SC za Kiswahili zinazoundwa kwa urejeshaji na ule anaouita ujalizaji ni tofauti. Vilevile, kadiri mtafiti alivyozidi kusoma alibaini kuwa kuna SC ambazo hazikuundwa kwa michakato aliyoitaja Wesana-Chomi (keshatajwa), kama mfano wa (6) unavyoshadadia maelezo haya.
(6) Serengeti wakicheza vizuri watapewa zawadi.
Sentensi katika mfano wa (6) ni SC ambayo haikuundwa kwa urejeshaji wala ujalizaji kama anavyoeleza katika michakato ya uundaji wa SC. Mfano huu unadokeza kuwa huenda ipo michakato mingine mbali na anayoitaja Wesana-Chomi (keshatajwa).
Kadhalika, michakato anayoitaja Wesana-Chomi (keshatajwa), haijawekwa wazi inatumikaje kuunda SC za Kiswahili, kama ilivyoelezwa katika michakato ya uundaji wa aina nyingine za sentensi. Kwa mfano, SA huundwa kwa mchakato wa uambatanishaji. Mchakato wa uambatanishaji umeelezwa unavyotumika kuunda SA (Wesana-Chomi, 2017; Kombe, 2018, 2019). Hivyo, kulihitajika uchunguzi wa michakato ya kisintaksia ya uundaji wa SC na namna inavyotumika kuunda sentensi hizo ili kuziba pengo la maarifa lililoachwa na wanaisimu tangulizi walioshughulikia SC za Kiswahili. Ndiyo maana utafiti huu ukafanyika.
1.3 Tatizo la Utafiti
SA na SC huundwa kwa vishazi viwili au zaidi. Ili kuweka pamoja vishazi hivyo na kuunda sentensi, ni jambo lenye namna ya pekee na ni la kimchakato. Namna na mchakato unaotumika kuunda sentensi ndiyo unaotupatia SA au SC katika MNJ. Wataalamu wanakubaliana kwamba SA huundwa kwa mchakato wa uambatanishaji (Wesana-Chomi, 2017; Kombe, 2018, 2019) na SC huundwa kwa michakato ya urejeshaji na ujalizaji (Wesana-Chomi, keshatajwa). Hata hivyo, uchunguzi wa miundo kadhaa ya SC uliofanywa katika utafiti wa awali unaonesha kuwa ujalizaji si mchakato wa kisintaksia wa uundaji wa SC za Kiswahili, bali ni matokeo ya uongezaji wa kiambajengo fulani katika sentensi. Hali hiyo inaonesha kuwa kulihitajika uchunguzi wa namna SC zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuziunda. Hivyo, utafiti huu ulilenga kuchunguza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato inayotumika kuunda sentensi hizo ili kuongeza maarifa ya kisintaksia kuhusu aina hizo za sentensi.
1.4 Malengo ya Utafiti
Utafiti huu ulikuwa na malengo ya aina mbili, lengo kuu na malengo mahususi.
1.4.1 Lengo Kuu
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza michakato ya kisintaksia katika uundaji wa SC za Kiswahili.
1.4.2 Malengo Mahususi
Malengo mahususi ya utafiti huu yalikuwa kama ifuatavyo:
Kueleza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa.
Kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda SC za Kiswahili.
1.5 Maswali ya Utafiti
Ili kufanikisha malengo tajwa hapo juu, utafiti huu ulikusudia kujibu maswali yafuatayo:
SC za Kiswahili zinaundwaje?
Ni michakato gani ya kisintaksia inatumika kuunda SC za Kiswahili?
1.6 Umuhimu wa Utafiti
Kwa kuzingatia umuhimu wa taaluma ya sintaksia na maendeleo yake, matokeo ya utafiti huu yatakuwa na manufaa ya namna tatu. Mosi, utafiti huu utawasaidia wataalamu wa sintaksia, kwani utakuwa rejeleo muhimu kwa watakaofanya tafiti kuhusu michakato ya kisintaksia katika tungo mbalimbali. Pili, utafiti huu unakusudiwa kuwasaidia waandishi wa vitabu, hususani vya sarufi ya Kiswahili kuongeza kipengele cha michakato ya kisintaksia pindi wanapofafanua SC za Kiswahili, kipengele ambacho kimekuwa kikipuuzwa kwa muda mrefu. Hivyo, utafiti huu umejaribu kuziba pengo hili la maarifa ya sintaksia. Tatu, matokeo ya utafiti huu, yatawasaidia wanasintaksia kujua michakato ya uundaji wa SC za Kiswahili.
1.7 Mawanda ya Utafiti
Utafiti huu ulikusudia kuchunguza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi hizo. Namna SC za Kiswahili zinavyoundwa ilichaguliwa kwa kuwa ni miongoni mwa vipengele ambavyo ni changamani. Pamoja na uchangamani wake, kipengele hiki bado kilikuwa kimeshughulikiwa kijumlajumla katika sintaksia ya Kiswahili. Ama kuhusu michakato ya uundaji wa SC, ilichaguliwa kutokana na uchunguzi wa awali kuonesha kuwa michakato inayotajwa na Wesana-Chomi (2017) inasailika kisintaksia. Hivyo, mawanda haya yameziba pengo la maarifa lililoachwa katika uundaji SC za Kiswahili.
1.8 Mpangilio wa Tasinifu
Tasinifu hii ina sura tano. Sura ya kwanza inatoa picha ya jumla ya sura zinazofuata kwa kuanzia utangulizi wa jumla ambao ndani yake kuna vipengele vidogovidogo kama vile: usuli wa tatizo la utafiti, tatizo la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti, mawanda ya utafiti pamoja na mpangilio wa tasinifu. Sura ya pili inahusu mapitio ya maandiko ambapo umetolewa ufafanuzi wa dhana muhimu katika mada ya utafiti na tafiti tangulizi kuhusu michakato ya uundaji wa SC. Pia, Nadharia Rasmi ya Chomsky (1965) iliyoongoza utafiti huu imejadiliwa. Sura ya tatu imeelezea methodolojia ya utafiti iliyotumika katika utafiti huu, hususani mchakato wa kukusanya na kuchambua data ulivyofanyika pamoja na uwasilishaji. Vipengele vilivyojadiliwa ni: eneo la utafiti, wango, sampuli na mbinu ya usampulishaji, mbinu ya ukusanyaji wa data, vifaa vya utafiti, uchambuzi na uwasilishaji wa data, kanuni za kiitikeli na vikwazo vya utafiti. Sura ya nne imewasilisha na kuchambua data iliyokusanywa kutoka maktabani. Vipengele viwili vimejadiliwa ambavyo ni uwasilishaji na uchambuzi wa namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia ya uundaji wa sentensi hizo. Sura ya tano inahusisha vipengele kama vile: muhtasari, matokeo, mchango, mapendekezo ya tafiti fuatizi na hitimisho. Aidha, kabla ya kuhitimishwa kwa kazi hii, marejeleo yaliyotumika yamebainishwa. Mwisho kabisa, kuna viambatanisho.
1.9 Muhtasari
Sura hii imefafanua utangulizi wa jumla wa utafiti huu. Katika sura hii, vipengele vya usuli wa tatizo la utafiti, tatizo la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti, mawanda ya utafiti pamoja na mpangilio wa tasinifu vimefafanuliwa. Sura inayofuata inahusu mapitio ya maandiko pamoja na nadharia iliyotumika katika utafiti huu.
SURA YA PILI
MAPITIO YA MAANDIKO NA NADHARIA
2.1 Utangulizi
Sura hii inahusu mapitio ya maandiko mbalimbali kuhusiana na mada ya utafiti na tatizo la utafiti na inafafanua nadharia iliyotumika katika utafiti huu. Sura hii imegawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza inahusu ufafanuzi wa SC za Kiswahili. Sehemu ya pili imeeleza michakato ya kisintaksia ya SC za Kiswahili. Sehemu ya tatu ni pengo la kiutafiti lililoonesha haja ya kuwapo kwa utafiti huu. Mwisho, sehemu hii imeeleza nadharia iliyotumika kwenye utafiti huu ambayo ni Nadharia Rasmi ya Sarufi Geuzi Zalishi iliyoasisiwa na Chomsky (1965).
2.2 Sentensi Changamani
SC ni aina ya tungo ambayo inaundwa na kishazi huru kimoja na kishazi tegemezi kimoja au zaidi (Massamba, 2004; Matei, 2008; Matinde, 2012; Obuchi na Mukhwana, 2015; Saluhaya, 2016; Wesana-Chomi, 2017). Msingi wa aina hii ya sentensi ni utegemezaji wa vishazi. Kishazi huru kinaweza kuwa tegemezi kutokana na upachikaji wa baadhi ya maneno au viambishi na hivyo kuzalisha SC kama mfano wa (7a) unavyoonesha.
(7) a. Wanafunzi wakisoma watafaulu mitihani.
Mfano wa (7a) ni sentensi moja katika MNJ lakini katika MN ni SS mbili (taz. Chomsky, 1965). Hapa kuna sentensi ambayo imepoteza sifa yake kutokana na kupachika kiambishi cha masharti {-ki-}. Sentensi hizo katika MN ni kama zinavyooneshwa katika mfano wa (7b na c).
(7) b. Wanafunzi watasoma.
c. Wanafunzi watafaulu mitihani.
Kwa hivyo, sentensi ya mfano wa (7b) imekuwa tegemezi kimuundo na kimaana kwenye sentensi (7c) baada ya kupachikwa kiambishi cha masharti {-ki-}.
Kwa kuwa vipashio vikuu vya SC ni vishazi huru na vishazi tegemezi, itafaa hapa tueleze kwa kifupi dhana ya kishazi. Maelezo hayo yatachangia kuweka msingi wa uelewa kuhusu mada ya utafiti huu.
Kishazi ni kipashio cha kimuundo chenye kiima na kiarifu (Radford, 1997; Massamba na wenzake, 1999; Matei, 2008). Maelezo haya yana maana kwamba kishazi kinaweza kusimama kama sentensi kamili, hasa pale kitenzi cha kishazi husika kinapokuwa na uarifishaji kamili. Naye Wesana-Chomi (2017) anaongeza kuwa kipashio cha lazima katika kishazi ni kitenzi. Hata hivyo, tutanabahishe kwamba si kila kitenzi kina sifa ya kuwa kishazi; kitenzi chenye sifa ya kuwa kishazi ni tungo kitenzi. Hii ni kwa sababu tungo kitenzi huwa na viambishi ambavyo vina uamilifu wa kisintaksia kama vile kuonesha upatanisho katika tungo, kuonesha mtenda au mtendwa na kadhalika. Kwa mfano, anakuja, amechoka hivi si tu vitenzi bali ni tungo kitenzi.
Kuna aina mbili ya vishazi ambavyo ni vishazi huru na vishazi tegemezi (Jerono, 2003; Matei, 2008; Wesana-Chomi, keshatajwa). Wataalamu hawa wanaelekea kukubaliana kuwa kishazi huru ni aina ya kishazi ambacho kinaweza kusimama peke yake katika mawasiliano na kikaleta maana bila utegemezi wa kishazi kingine. Mfano wa (8) unadhihirisha fasili ya kishazi huru.
(8) Mama anasonga ugali.
Mfano wa (8) unaonyesha kuwa kishazi huru hakihitaji kishazi kingine ili kukamilisha maana, kwa kuwa taarifa inayoelezwa na kishazi hiki ni kamili.
Kishazi tegemezi kimeelezwa kwa upana katika utafiti huu ikilinganishwa na kishazi huru. Hii inatokana na ukweli kwamba msingi wa SC ni utegemezaji wa vishazi. Dhana ya kishazi tegemezi imeshughulikiwa na wataalamu anuwai. Miongoni mwao ni Hudson (1971). Hudson (keshatajwa) anaeleza kuwa vishazi tegemezi ni vile vinavyotegemezwa ndani ya sentensi kuu. Hii ina maana kwamba vishazi tegemezi huwa vinabebwa katika muundo wa sentensi kuu. Kwa kuwa vishazi tegemezi huwa vinabebwa katika muundo wa sentensi kuu, katika utafiti huu tutaviita KB. Uainishaji wa vishazi tegemezi kama KB kisintaksia unaungwa mkono na Tallerman (2011), Wesana-Chomi (2017) na Chipalo (2021). KB kinaweza kuwa kiambajengo cha ziada au lazima kwenye KK (Chipalo, 2021). Chunguza mfano wa (9) kwa ufafanuzi zaidi.
(9) Tumepata taarifa kuwa Aisha anampenda mwanao.
Mfano wa (9) tungo iliyoandikwa kwa hatimlazo ni KB ambacho kinajaliza kishazi ambacho hakijalazwa ambacho ni KK.
Kwa ujumla, maelezo haya yalisaidia kupata maarifa kuhusu mada ya utafiti huu hasa kwa kuwa SC vijenzi vyake vikuu ni KK na KB. Pamoja na umuhimu wa maelezo ya wataalamu kuhusu SC, ufafanuzi wao hauweki bayana ni kwa namna gani vishazi vinabebwa ndani ya vishazi vingine na hatimaye kupata KK na KB ambavyo kwa pamoja huunda SC. Ni kutokana na pengo hili utafiti huu ulinuia kujaribu kuliziba kwa kuchunguza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi hizo.
2.3 Michakato ya Kisintaksia
Mchakato ni mfululizo wa shughuli zinazosababisha kitu fulani kufanyika ili kutimiza lengo fulani (Longhorn, 2011; TUKI, 2013; Wamitila, 2016). Katika mawanda ya sintaksia, dhana ya michakato ya kisintaksia tunaweza kuifasili kama shughuli inayoweka vipashio vya lugha pamoja ili kuunda tungo fulani yenye maana inayokubalika. Maelezo haya yanashadidiwa na Tallerman (2011) anapoeleza kuwa vipashio vya kisintaksia hujumuishwa pamoja kiulalo au kiusilisila (wima) kwa kufuata michakato.
Michakato iliyoelezwa katika sintaksia ya Kiswahili kwamba ndiyo inayohusika na uundaji wa SC ni urejeshaji na ujalizaji (Wesana-Chomi, 2017). Urejeshaji unatokana na dhana ya urejeshi. Aidha, urejeshi huo hutokea katika kitenzi na hutokea pale tendo fulani linaporejeshwa kwa mtenda wa tendo, mtendwa wa tendo na mtendewa wa tendo (Wesana-Chomi, keshatajwa). Mfano wa (10) unafafanua zaidi.
(10) Kisu kilichopotea kimepatikana.
Mfano wa (10), mtajwa ni kisu na kiambishi {-cho-} hurejelea nomino hiyo na hujulikana kama kiambishi rejeshi. Urejeshaji huu huzalisha tungo rejeshi ambazo zimeelezwa na Mekacha (1987) kama mojawapo ya tungo tegemezi. Anaendelea kueleza kuwa tungo tegemezi ni sentensi iliyoshushwa hadhi na kutegemezwa ndani ya sentensi nyingine. Hii ina maana kwamba tungo tegemezi haitokei peke yake bali hutokea kama kiambajengo cha sentensi kuu. Urejeshaji umeelezwa na Wesana-Chomi (k.h.j) kama moja ya michakato inayotumika kuunda SC. Chunguza mfano wa (11) kwa ufafanuzi zaidi.
(11) [Polisi wamemkamata mfungwa] S₁ [aliyetoroka jela jana.] S₂
Anaeleza kwamba sentensi ya (11) ni matokeo ya mchakato wa urejeshaji ambao unaunganisha sentensi S₁ na S₂ kwa kukunjia S₂ katika KN₂ cha S₁ kama mfano wa (12) unavyoonesha.
(12) [Polisi wamemkamata mfungwa.] S₁ [Mfungwa alitoroka jela jana.] S₂
Maelezo ya Mekacha (1987) na Wesana-Chomi (2017) hayaweki bayana namna mchakato huu unavyotumika kuunda SC za Kiswahili kisintaksia. Ili kujaribu kuziba pengo hili la maarifa ya SC, utafiti huu ulichunguza namna SC zinavyoundwa.
Ujalizaji kwa mujibu wa Wesana-Chomi (keshatajwa) huunda SC kwa kishazi kikuu kimoja na kishazi nomino kimoja ambavyo katika MNJ hutanguliwa na vitegemezi kama vile: kama, kwamba na kuwa. Tazama mfano wa (13a-b) kwa ufafanuzi zaidi.
(13) a. [Julia amepata tetesi] S1 [kuwa Cheusi ni mke wa Hamisi.] S2
b. [Jumanne ameleta habari] S2 [kwamba mgonjwa amefariki leo
usiku.] S2
Mifano ya (13a-b) vishazi nomino vimeandikwa kwa hatimlazo na kutokea kama viambajengo vya S1 vikiwa vimekunjiwa ndani ya S₁ hizo. KB cha (13a), kinajaliza nomino tetesi ya S1 ilhali KB cha (13b), kinajaliza nomino habari ya S1. Ifahamike kwamba kabla ya sentensi kuwa hivyo zilivyo katika MNJ wa (13a-b), zilikuwa kama inavyoonesha katika MN wa (14a-b).
(14) a. [Julia amepata tetesi.] S₁ [Cheusi ni mke wa Hamisi.] S₂
b. [Jumanne ameleta habari.] S₁ [Mgonjwa amefariki leo usiku.] S₂
Wesana-Chomi (keshatajwa) anaeleza kuwa katika kuunganisha S₁ na S₂ kiambajengo S₂ hukunjiwa katika muundo wa S₁ kama inavyoonesha katika (13a-b). Katika muundo kama huo, KB S₂ hufanya kazi kama kijalizo cha nomino.
Maelezo hayo kuhusu ujalizaji yanaelekea kuchanganya kati ya mchakato wa kimuundo na kidhima. Kuhusu dhana hii kuwa ya kidhima kunadokezwa pia na Philipo na Kuyenga (2018) ambao wanaeleza kuwa ujalizaji ni dhana iliyobuniwa na wanasarufi ili kuelezea uhusianao unaojitokeza pale kauli mbili au zaidi zinaposhikamanishwa kuwa kauli moja. Hali ikiwa hivyo, kauli moja hufanya kazi kama kijenzi mahususi cha kauli nyingine. Maelezo haya yanashadidia madai kwamba ujalizaji si mchakato wa uundaji wa SC bali ni matokeo ya mchakato wa kisintaksia wa uundaji wa SC za Kiswahili. Hali hii ilimsukuma mtafiti kutaka kufahamu mchakato upi unatumika kuunda sentensi zilizopo kwenye mfano wa (13a-b). Kwa kuwa ujalizaji si mchakato wa kimuundo bali ni matokeo ya mchakato wa kisintaksia wa uundaji wa SC za Kiswahili, palihitajika uchunguzi wa kisintaksia utakaobainisha mchakato unaotumika kuunda SC kama hizo.
Vilevile, katika mchakato wa urejeshaji na ujalizaji pamoja na mifano yake imebainika kuwa kuna miundo mingine ambayo haifanani na sentensi zilizotajwa katika mifano hiyo. Kwa ufafanuzi zaidi tazama muundo wa SC ya (6), (11) na (13a-b). Miundo hiyo inadokeza kuwapo kwa michakato zaidi ya ile iliyoelezwa na Wesana-Chomi. Ili kubaini mchakato huo ililazimu kufanyika kwa utafiti huu ili kubaini ni mchakato upi hasa unatumika kuunda SC kama ile ya (6).
Utaratibu unaotumika katika michakato ya uundaji wa sentensi katika lugha ya Kiswahili hususani SC haujawekwa bayana. Ingawa katika aina zingine za sentensi kama SA imeshughulikiwa, mchakato wa uambatanishaji umeelezwa namna unavyotumika kuunda SA hatua kwa hatua (Wesana-Chomi, 2018; Kombe, 2017, 2019). Maelezo haya yanadokeza kwamba michakato ya uundaji wa sentensi ina utaratibu wake kama ilivyoelezwa katika uambatanishaji lakini kwa upande wa SC hilo halijawekwa wazi. Jambo hili pia lilihitaji utafiti ili kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa.
2.4 Pengo la Utafiti
Maelezo ya wataalamu hawa ni muhimu katika kuujenga utafiti huu kwani yametoa mwanga kuhusu michakato ya kisintaksia inayohusika na uundaji wa SC za Kiswahili. Kutokana na maelezo ya wataalamu hao, shauku ya utafiti huu ni kutaka kufahamu namna SC za Kiswahili zinavyoundwa, jambo ambalo lilielezwa juu juu na Wesana-Chomi (2017). Michakato iliyobainishwa na wataalamu hao ilionekana kusailika kisintaksia, suala ambalo kwa uelewa wa mtafiti halikuwa limeshughulikiwa. Kutofanyika huko kungesababisha kuwapo kwa pengo la maarifa katika SC za Kiswahili. Hivyo, utafiti huu ulinuia kuchunguza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia ya uundaji wa sentensi hizo ili kuziba pengo lililoachwa na mapitio tangulizi.
2.5 Nadharia ya Utafiti
Utafiti huu uliongozwa na Nadharia Rasmi (kuanzia sasa, NR) ya Sarufi Geuzi Zalishi (kuanzia sasa, SGZ) ya Chomsky (1965). SGZ imeelezwa jinsi ilivyoanza hadi kufikia hatua ya pili ambayo imetumika katika utafiti huu. Nadharia ya SGZ iliibuka ili kushughulikia baadhi ya mambo ambayo hayakuweza kuelezwa na Nadharia ya Muundo Virai (kuanzia sasa, NMV) iliyojishughulisha na vijenzi vya tungo katika lugha. Baadhi ya mambo ambayo hayakuweza kushughulikiwa ni tungo zenye uhusiano kama inavyooneshwa katika mfano wa (15a-b).
(15) a. Kurwa analima shamba.
b. Shamba linalimwa na Kurwa.
Mfano wa (15) katika NMV, (a) na (b) zingechanganuliwa kama tungo tofauti ilhali tungo hizo zote mbili zina maana sawa. Katika kushughulikia suala hili, Chomsky (1957) alianzisha SGZ ambayo iliweza kushughulikia tungo ya (15a-b) jinsi zinavyoweza kuchanganuliwa. Hata hivyo, kushughulikia tungo za namna hiyo haikuwa kazi rahisi kutokana na lugha yenyewe kuwa changamani. Kwa hivyo, SGZ ilikuwa na hatua tano zote hizo zilitokana na uchangamani wa lugha yenyewe. Katika sehemu hii hazikujadiliwa hatua zote, bali imejadiliwa hatua ya kwanza na ile ya pili. Uchaguzi huu ni kwa sababu hatua ya kwanza ndiyo iliyochangia kuibuka kwa hatua ya pili ambayo ni NR iliyotumika katika utafiti huu.
2.5.1 Hatua ya Kwanza ya Sarufi Geuzi Zalishi
Hii ilijitokeza kati ya (1957-1965). Hatua hii ilitambulishwa na Chomsky (1957) baada ya kutoa chapisho lake lililojulikana kama Syntactic Structures. Hatua hii ilinuia kutanzua mambo makuu matatu. Mosi, muundo mmoja kuakisi maana tofauti. Pili, miundo miwili isiyofanana kisintaksia kuakisi maana moja. Tatu, kushughulikia miundo miwili kisintaksia inayofanana kuakisi maana mbili tofauti. Mambo hayo matatu ambayo hayakuweza kushughulikiwa katika NMV, kwa ujumla wake ndiyo yaliyomsukuma Chomsky kuanzisha Nadharia ya SGZ. Chomsky aliona kwamba mambo hayo yanaweza kushughulikiwa kwa kuonesha kwamba lugha ina ngazi mbili za kiuchanganuzi ambazo ni MN na MNJ. Chomsky (1957) anaendelea kueleza kuwa, MN ndiyo wenye dhamana ya kuweka bayana mshikamano dhahania wa vipashio ambavyo ndiyo msingi wa maana kamili ya sentensi wakati MNJ ni muundo wa tungo kama inavyojidhihirisha katika utendaji. Anaongeza kufafanua kuwa kanuni za jumla za uambajengo huunda MN wa sentensi ambao hupitia mageuzi mbalimbali na hatimaye kuzalisha MNJ wa sentensi. Kwa hiyo, mageuzi ni mchakato wa kubadili MN ili kupata MNJ. Katika hatua hii sintaksia ina vitengo vinne vyenye kushikamana na kukamilishana ambavyo ni: MN, kitengo cha mageuzi, MNJ na kanuni za kifonolojia.
Katika hatua hii ya kwanza ya SGZ, kanuni za mageuzi ni za aina tatu. Mosi, kanuni zenye kuhusisha dhima za sentensi, mathalani, swali, ukanushi na kadhalika. Pili, kanuni zenye kuhusisha michakato ya kimofolojia, kwa mfano, njeo, hali na zinginezo. Pia, kanuni zinazohusu upanuzi wa SS, SC, SA. Hatua hii ilikifanya kitengo cha mageuzi kuwa na uzito kwani mageuzi yote yalifanyikia katika kitengo hiki.
Katika hatua hii, Chomsky (1965) alipata changamoto kutoka kwa wanafunzi wake kwa kuwa hakuhusisha kitengo cha maana. Wanafunzi wake walihoji suala la muundo bila kuhusisha maana. Hapa yaelekea wanafunzi wake hawakukubaliana na Chomsky kuhusu suala la vitengo vya kisintaksia kutokuwa na kitengo cha maana. Hii inadhihirika pale Katz na Fodor walipotoa chapisho lao la The Structure of Semantic Theory (1963) ambalo lilikitambua kitengo cha semantiki kama kitengo muhimu katika ufafanuzi wa lugha. Changamoto hiyo ilimsukuma Chomsky (1965) kuandika chapisho lililoitwa Aspect of the Theory of Syntax. Katika chapisho hilo alijibu changamoto ya kitengo cha maana kutokuwapo katika sintaksia, kwa kufanyia marekebisho nadharia yake ambayo wengine huita hatua. Marekebisho hayo yalizalisha NR ambayo ni hatua ya pili ya SGZ ambayo ndiyo imetumiwa katika utafiti huu.
2.5.2 Nadharia Rasmi
NR ni matokeo ya marekebisho ya nadharia ya kwanza (hatua ya kwanza). NR ililenga kuingiza taarifa ya maana katika Nadharia ya SGZ. Chomsky (1965) aliingiza taarifa ya maana katika MN kwa madai kuwa kisintaksia MN ndiyo unaodhihirisha maana kwa kuteua maneno yenye kubeba maana iliyokusudiwa.
Fauka ya hilo, Chomsky (keshatajwa) alifanya mabadiliko kadhaa. Mabadiliko hayo ni mageuzi yote yaliyokuwa yanafanyika katika hatua ya kwanza ya SGZ yaliingizwa kwenye kitengo cha msingi. Hivyo, sentensi katika MN ilipaswa ionekane kama ni SA, SS au SC. Vilevile, kipengele cha msamiati kiliingizwa katika kitengo cha msingi na MN ulifungamanishwa na maana. Kwa hiyo, MN unazalishwa na kitengo cha msingi chenye taarifa zote hizo. MN unapitia katika kitengo cha mageuzi na kuzalisha MNJ ambao unapitia katika kitengo cha kanuni za kifonolojia ili kupata uwakilishi wa kifonetiki. Jacobsen (1977) anaeleza kwamba kitengo cha mageuzi katika hatua hii kina mageuzi kama vile: uhamishaji au usogezaji, uchopekaji, udondoshaji na mengineyo ili kupata MNJ kutoka kwenye MN.
Utafiti huu uliongozwa na NR yenye misingi ifuatayo. Mosi, umilisi na utendi ndiyo maarifa yanayotawala uwezo wa binadamu kuzungumza lugha. Umilisi ni maarifa aliyonayo mtu kuhusu sarufi ya lugha fulani, kwa upande wa utendi ni ule uwezo wa mtu kutumia lugha katika miktadha anuwai. Kuhusu sarufi, Chomsky (1957) anafafanua kuwa ni maarifa au uwezo bwete alionao binadamu wa kuzalisha lugha. Anaongeza kuwa kila sentensi iliyoko akilini kwa msemaji iko kama taswira tu isiyosikika.
Pili, umilisi wa lugha ndiyo unaomwezesha msemaji kuelewa ama kuzalisha sentensi ambayo hakuwahi kuisikia hapo awali. Anaongeza kuwa sarufi ndiyo inayotawala semo zetu na ndiyo inayoweka mipaka ya tungo zinazokubalika au zisizokubalika katika lugha husika. Aidha, semo za binadamu hutawaliwa na maarifa yake juu ya kile kinachokubalika na kanuni ya sarufi husika.
SGZ inasisitiza uzalishaji wa sentensi nyingi zisizo-ukomo kwa kutumia kanuni chache. Matumizi ya NMV yanawezesha kupatikana kwa vishazi ndani ya sentensi wakati wa kuzalisha sentensi zisizo-ukomo (Chomsky, 1965). Anaongeza kuwa uwezo wa kuzalisha sentensi zisizo-ukomo unatokana na kufahamu kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua kutokana na kuwa na umilisi wa lugha yake.
NR ilitumika kuchambua jinsi SC zinavyoundwa. Kwa kuwa nadharia hii inaeleza kwamba sarufi ndiyo inayoweka mipaka ya tungo zinazokubalika na zisizokubalika katika lugha ya binadamu. Hivyo, mtafiti alitumia nadharia hii kufafanua namna SC zinavyoundwa kutoka MN kwenda MNJ ili zikubalike ambazo ndizo zinazotumika kwenye matini za kawaida na mazungumzo ya kawaida.
Aidha, NR ilitumika katika utafiti huu katika kubainisha michakato ya kisintaksia ya uundaji wa SC za Kiswahili. Kwa kutumia misingi yote miwili ambapo kwa mujibu wa nadharia hii uzalishaji wa sentensi huzingatia kanuni zinazojulikana kutokana na umilisi wa msemaji katika lugha yake. Hivyo, mtafiti aliitumia nadharia hii kufafanua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato inayotumika kuunda sentensi hizo.
2.6 Muhtasari
Sura hii imegawanyika katika sehemu nne. Sehemu ya kwanza ilihusu ufafanuzi wa dhana ya SC ili kujenga uelewa kuhusu mada ya utafiti huu. Sehemu ya pili ilihusu tafiti tangulizi za Kiswahili zilizohusu michakato ya uundaji wa SC. Sehemu ya tatu ilifafanua nadharia ambayo imetumika katika utafiti huu. Nadharia iliyoelezwa katika sehemu hii ni SGZ ambapo hatua mbili zilifafanuliwa ya kwanza na pili. Kati ya hatua hizo, hatua iliyotumika katika utafiti huu ni NR. Vilevile, sehemu hii ilieleza pengo la kiutafiti ambalo hatimaye lilimchochea mtafiti kufanya utafiti huu. Sura inayofuata inajadili methodolojia ya utafiti ambayo imeeleza jinsi data za utafiti huu zilivyokusanywa, zilivyochambuliwa na kuwasilishwa.
SURA YA TATU
METHODOLOJIA YA UTAFITI
3.1 Utangulizi
Sura hii inaeleza methodolojia ya utafiti iliyotumika katika mchakato wa ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa data. Methodolojia hii inajumuisha: eneo la utafiti, wango, sampuli na usampulishaji, mbinu ya ukusanyaji wa data, vifaa vya utafiti, uchambuzi wa data, kanuni za kiitikeli na vikwazo vya utafiti.
3.2 Eneo la Utafiti
Data za utafiti huu zilipatikana maktabani. Maktaba zilizotumika kupata data za utafiti huu ni Maktaba ya Dkt. Wilbert Chagula na Makavazi ya TATAKI, zote zinapatikana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilichopo katika wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam. Maktaba hizi zilitumika kukusanya SC za Kiswahili katika matini teule ili kuchambua namna zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuziunda.
Mtafiti alichagua kufanyia utafiti wake maktabani kwa sababu data sahihi za kisarufi zinapatikana katika lugha ya maandishi kuliko lugha ya mazungumzo. Madai haya pia yanaelezwa na Meyer (1996) kwamba lugha ya mazungumzo hukiuka sana kanuni za kisarufi ili kufanikisha mawasiliano katika mazungumzo. Anaongeza kuwa mashartizuizi ya kisarufi hukiukwa kwa sababu za kipragmatiki. Naye Kortmann (1997) anaeleza kuwa kilongo cha mazungumzo aghalabu hutumia kiimbo na ishara zingine za kiisimu katika kueleza maana. Kwa kuzingatia maelezo ya Meyer na Kortmann, lugha ya maandishi ilikuwa zana bora zaidi katika kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia ya uundaji wa sentensi hizo.
Maktaba za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zilichaguliwa kwa kuwa zimesheheni machapisho mbalimbali ya Kiswahili ambayo ndiyo yaliyokusudiwa na mtafiti. Kwa hiyo, mtafiti alikuwa na uhakika wa kupata matini andishi za kifasihi na magazeti ambazo ndizo zilikusudiwa kutumika kama chanzo cha data.
3.3 Wango, Sampuli na Usampulishaji
Taratibu za kupata sampuli ya utafiti huu zilizingatiwa. Taratibu hizo ni uteuzi wa wango ambalo baadaye lilitupatia sampuli na mbinu ambazo zilitumika kupata sampuli kutoka kwenye wango.
3.3.1 Wango
Wango ni jumla ya watu au vitu vinavyofanyiwa utafiti ambavyo vyaweza kuwa binadamu au viumbe vingine vyenye uhai na visivyo hai (Oladipo na wenzake, 2015; Ponera, 2019). Kombo na Tromp (2006) wanatanabahisha kuwa watu au vitu vinavyotumika kutoa data za utafiti vinapaswa kuwa na uhusiano na mada inayofanyiwa utafiti. Hivyo, katika utafiti huu wango lilikuwa ni matini zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Hii ni kwa sababu, matini zilizoandikwa ni chanzo sahihi cha data kuliko matini za mazungumzo kwani mara nyingi matini andishi hufuata kanuni za kisarufi tofauti na matini za mazungumzo (Mayer, 1996; Kortmann, 1997).
3.3.2 Sampuli
Sampuli ni sehemu ya wango ambayo imeteuliwa itumike katika kusaka majibu ya tatizo (Dawson, 2002; Kothari, 2009). Sampuli ya utafiti huu ilikuwa kazi mbili za fasihi ambazo ni riwaya ya Haramu iliyoandikwa na Bwana (2004) na Mwendo iliyoandikwa na Lema (2004). Katika kila riwaya ilisomwa sura moja. Uteuzi wa riwaya ulitokana na utajiri mkubwa wa SC zinazotokana na lugha ya masimulizi (Mlacha, 1991). Matini zingine za kifasihi kama tamthiliya na ushairi hutumia sentensi fupifupi ambazo aghalabu huwa ni SS. Hivyo, isingekuwa rahisi kupata SC zilizokuwa zinatarajiwa ili kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi hizo.
Kadhalika, mtafiti alitumia sampuli ya magazeti rasmi mawili ambayo ni Mwananchi linalochapishwa na Mwananchi Communications Ltd na Nipashe linalochapishwa na The Guardian Ltd. Kwa kuwa magazeti hayo yanatolewa kila siku na mtafiti alikusanya data kwa siku thelathini (30), hakusoma magazeti kila siku. Aliteua tarehe moja kwa kila gazeti la Juni mwaka (2021) kati ya zile siku thelathini alizotumia kukusanya data. Katika kila gazeti alisoma kurasa mbili.
Licha ya kwamba riwaya za Kiswahili ni nyingi na magazeti rasmi yanatoka kila siku, mtafiti aliamua kuteua riwaya mbili na magazeti mawili na kuchagua tarehe moja tu ya magazeti ya mwezi Juni mwaka (2021). Hii ni kwa sababu mtafiti aliona sampuli hiyo inaweza kumpa SC za kutosha kukidhi malengo ya utafiti.
3.3.3 Usampulishaji
Usampulishaji ni mchakato wa kuteua sampuli kutoka katika chanzo kikuu cha data, yaani wango (Kombo na Tromp, 2006; Kothari, 2009; Ponera, 2019). Kuna aina mbili za usampulishaji ambazo ni usampulishaji nasibu na usio nasibu. Usampulishaji nasibu ni ule ambao mtafiti hatumii vigezo katika mchakato wa kuteua sampuli na usampulishaji usio nasibu ni ule ambao mtafiti anatumia vigezo fulani katika kuteua sampuli. Utafiti huu ulitumia usampulishaji nasibu na usio nasibu.
Ili kupata sampuli faafu, mbinu ya usampulishaji lengwa ilitumika kuteua sampuli iliyotumika katika utafiti huu. Kwa mujibu wa Tavakoli (2012), usampulishaji lengwa ni mbinu ya usampulishaji ambayo mtafiti hujiwekea vigezo au sifa atakazozitumia kuteua sampuli ambayo anaamini kwamba itampa data anayoihitaji, kwa kuzingatia taarifa au uchunguzi wa awali. Vigezo vitatu (03) vilizingatiwa: matini yenye lugha ya kisimulizi/kimaelezo, matini rasmi na matini zilizosukwa vizuri na kufuata kanuni za uandishi wa sarufi ya Kiswahili. Matini zilizochaguliwa kutokana na vigezo hivyo ni riwaya na magazeti rasmi. Kwa kuzingatia mbinu hii, kila riwaya na gazeti rasmi lilikuwa linafaa kutumika kama chanzo cha data. Kutokana na wingi wake mtafiti asingeweza kutumia matini zote kama chanzo cha data. Hivyo, mtafiti alilazimika kutumia mbinu nyingine ya usampulishaji ambayo ni usampulishaji nujumu.
Ili kupata sampuli wakilishi katika kundi la riwaya na magazeti rasmi, mbinu ya usampulishaji nujumu ilitumika. Usampulishaji nujumu ulitumika kumsaidia mtafiti kuchagua sampuli kutokana na wango lililopo karibu naye linalofikika kirahisi au linalopatikana kirahisi (Tavakoli, 2012). Kwa kutumia mbinu hii, mtafiti alimwomba Mkutubi wa Makavazi ya TATAKI kumpatia riwaya sita (6). Baada ya kuona riwaya zote sita zimesheheni SC, mtafiti alitumia mbinu ya usampulishaji nasibu sahili ili kuzipunguza zibaki mbili (02). Hii ni kwa sababu mtafiti angepata data nyingi ambazo asingeweza kuzichambua kama inavyostahili kulingana na muda uliowekwa wa utafiti huu.
Usampulishaji nasibu sahili ni mchakato wa kuteua sampuli ambapo kila mtoataarifa au kitoataarifa kina nafasi sawa ya kuteuliwa kuwa sampuli ya utafiti (Ary na wenzake, 2010). Kwa kutumia mbinu hii, majina sita (06) ya riwaya yalipewa namba, kisha namba zikaandikwa kwenye vikaratasi. Ili kuepuka upendeleo kutoka kwa mtafiti, Mkutubi wa Makavazi aliombwa kumsaidia mtafiti kuchagua vikaratasi viwili (02) kutoka katika kundi la riwaya ili kupata sampuli wakilishi katika utafiti. Namba za riwaya zilizo chaguliwa kutokana na mbinu hiyo ni riwaya ya Haramu ya Bwana (2004) na Mwendo ya Lema (2004). Katika matini hizi mtafiti alikusanya SC za Kiswahili na kisha kuzichambua ili kufahamu namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi hizo.
Vilevile, kwa kutumia mbinu ya usampulishaji nujumu, majina sita (06) ya magazeti rasmi aliyopatiwa matafiti, aliyapa namba kulingana na alivyopewa. Gazeti lililotajwa la kwanza lilipewa jina na namba na kuendelea hivyo hadi sita. Baada ya kitendo hicho, karatasi hizo zilikunjwa na kuwekwa mezani. Baada ya kufanya hivyo, mtafiti alimwomba muuzaji amsaidie kuchagua vikaratasi viwili tu kati ya sita. Magazeti yaliyochaguliwa kutokana na mchakato huo ni gazeti la Mwananchi linalochapishwa na Mwananchi Communications Ltd na Nipashe linalochapishwa na The Guardian Ltd.
Kwa kuwa magazeti hayo huchapishwa kila siku, usampulishaji nasibu sahili ulitumika tena kupata tarehe moja kati ya tarehe za mwezi Juni mwaka (2021). Tarehe za mwezi Juni mwaka (2021) ziliorodheshwa kwenye vikaratasi. Kila tarehe ndani ya mwezi huo iliandikwa kwenye kikaratasi chake, kisha vikaratasi hivyo vilikunjwa na kuokotwa kikaratasi kimoja tu kati ya vikaratasi thelathini (30). Tarehe iliyoandikwa kwenye karatasi iliyookotwa ndiyo tarehe ambayo magazeti husika yalisomwa ili kupata data. Tarehe iliyochaguliwa kutokana na mchakato huo ni 26. 06. 2021.
3.4 Mbinu ya Ukusanyaji Data
Mbinu za ukusanyaji data ni njia zimsaidiazo mtafiti kupata taarifa za kiutafiti zitumikazo kutoa mjumuisho (Kombo na Tromp, 2006). Uchaguzi wa mbinu gani itumike katika kukusanya data za utafiti hutegemea taarifa zinazohitajika na mtafiti ambazo ndizo zinatumika kufikia mahitimisho ya utafiti wake. Kwa kuwa utafiti huu unahusu michakato ya kisintaksia ya uundaji wa SC za Kiswahili, mbinu ya usomaji wa matini ilitumika kukusanya data.
Uchaguzi wa mbinu ya usomaji wa matini ulichochewa na maelezo ya wataalamu kama Meyer (1996) na Kortmann (1997) wanaoeleza kwamba matini zilizoandikwa ni faafu zaidi katika sarufi kwa kuwa matini za mazungumzo hukiuka kanuni nyingi za kisarufi. Kwa msingi huo, mbinu ya usomaji wa matini ndiyo ilikuwa mwafaka katika kukusanya data zinazohusu michakato ya uundaji wa SC za Kiswahili. Ili kupata SC hizo, mtafiti alisoma sura ya kwanza kwa kila riwaya teule, kwa sababu riwaya zina utajiri mkubwa wa SC. Kwa hiyo, sura kwanza tu ilitosha kupata SC zilizotarajiwa na mtafiti kutoka kwenye matini ya riwaya. Pia, alisoma kurasa mbili kwa kila gazeti teule. Katika gazeti la Mwananchi alisoma kurasa mbili ya 19 na 20 na gazeti la Nipashe kurasa mbili ya 3 na 19. Kurusa hizo zilichaguliwa kwa kuwa zilisheheni maelezo ambayo ilikuwa rahisi kupata SC zilizotarajiwa katika matini za magazeti.
Mtafiti alisoma matini teule katika sehemu teule kwa kufuata hatua zifuatazo. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kusoma kwa kina sehemu teule kuanzia mwanzo hadi mwisho ili kujua SC zilizopo. Hatua ya pili ilikuwa kusoma tena kwa kina sehemu teule katika matini teule ili kuweka alama kwenye SC zilizotumika. Hatua ya tatu ilikuwa kusoma tena kwa kina sehemu zilizowekwa alama kuwa ni SC, ili kuzidondoa kwa ajili ya kujibu maswali ya utafiti. Hatua ya nne ilikuwa ni kuzipanga data kimatini (yaani kila data ya matini ilipangwa) kwa kutumia kalamu ya wino na shajara. Baada ya hapo, uchambuzi wa data ulifuata.
3.5 Vifaa vya Utafiti
Vifaa vya utafiti hutegemea aina ya utafiti, lakini aghalabu baadhi ya vifaa hivi kama si vyote ni kalamu na karatasi, shajara, tepu rekoda na vifaa vyake, video/kamrekoda na vifaa vyake, kamera na vifaa vyake, kompyuta na vifaa vyake, hojaji na dodoso, vifaa vya kupimia na kuhesabu, darubuni, vionambali na kadhalika (Mulokozi, 1983). Kwa kuzingatia aina ya utafiti huu, mtafiti alitumia vifaa vifuatavyo:
3.5.1 Kalamu ya Risasi
Kalamu ya risasi ilitumiwa na mtafiti kuweka alama kwenye data zilizohitajika kwenye matini teule za riwaya na magazeti. Data hizo ambazo ziliwekewa alama baadaye zilinukuliwa kwa kalamu ya wino na kuandikwa kwenye shajara. Kifaa hiki kilitumika kuweka alama kwenye matini teule kwa kuwa ni rahisi kufuta alama zilizowekwa na aina hii ya kalamu. Kwa hivyo, kwa kuwa matini teule zilikuwa ni za maktaba, mtafiti alitakiwa kuzifuta alama hizo kwa ajili ya matumizi mengine ya maktaba. Kwa msingi huu, kalamu ya wino ilikuwa mwafaka katika utafiti.
3.5.2 Kalamu ya Wino na Shajara
Kalamu ya wino na shajara vilitumika kwa ajili ya kunukuu data kutoka kwenye matini teule. Vifaa hivi pia vilitumika kuzipanga data kutoka matini moja hadi nyingine. Taarifa zitakazokusanywa ni SC za Kiswahili. Sababu za kuviteua vifaa hivi ni kwamba kwa namna vilivyo vinaweza kutumika kwa urahisi, muda wowote na mahali popote hususani maktabani. Hapa mtafiti alihitaji kuzinukuu taarifa zinazohusu SC katika matini teule bila kurejea kwenye matini husika.
3.5.3 Kompyuta Pakatwa
Kompyuta pakatwa ilitumika kuingiza data zilizonukuliwa kwenye matini kwa kalamu ya wino na shajara. Pia, kompyuta pakatwa ilitumika kuchambua data. Sababu za kuteua kifaa hiki ni kwamba ni rahisi katika uchambuzi wa data na uandishi wa ripoti ya utafiti. Kifaa hiki kimesheheni programu anuwai za kiuandishi ambazo kwazo zisingeweza kupatikana katika kifaa kingine kama simu.
Kwa ujumla, vifaa vyote vilivyotumika katika utafiti huu vilisaidia kurahisisha mchakato wa kukusanya na kuchambua data za utafiti. Hii ilitokana na jinsi vifaa hivi vilivyokamilishana kwani kila kifaa kilikuwa na ubora na udhaifu katika mazingira fulani. Kwa hiyo, sehemu ambayo kifaa fulani kilikuwa na udhaifu katika mchakato wa ukusanyaji wa data, kifaa kingine kilitumika ili kuzipa pengo lake. Hii ndio sababu na faida ya kutumia vifaa anuwai katika utafiti huu.
3.6 Uchambuzi wa Data
Uchambuzi wa data ni kuipanga na kuitafsiri data-ghafi kwa utaratibu maalumu ili kuifanya iwe na maana pamoja na kupata matokeo ya utafiti (Yogesh, 2006). Katika utafiti huu, data zilichambuliwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli baada ya kuzikusanya kutoka maktabani. Mkabala wa kitaamuli ni ule unaotumia maelezo badala ya takwimu (Mligo, 2012).
Katika mkabala wa kitaamuli, mtafiti alitumia mbinu ya kimuktadha. Waasisi wa mbinu ya kimuktadha ni Glaser na Strauss (1967) ambao wanaeleza kwamba mtafiti anapochanganua data zake kwa mbinu hii kwa lengo la kuibuka na seti fulani ya maelezo kuhusiana na jambo ambalo analitafiti, hana budi kuyafikia mambo manne. Mosi, seti hiyo iwe inaendana na muktadha wa eneo linalotafitiwa; hivyo maelezo yalenge kuwafaa watu wa muktadha unaotafitiwa. Pili, seti hiyo iwe inaeleweka, hasa na watu wa eneo hilo. Tatu, seti ilenge kutumika katika maisha ya jumla ya walengwa hao. Nne, seti iruhusu kunyumbuka yaani mtumiaji aweze kuidhibiti, kuibadili, kuipindisha na kuielekeza kulingana na wakati. Mtafiti alitumia mbinu hii kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato inayotumika kuziunda sentensi hizo kwa kujikita katika muktadha wa kisintaksia. Muktadha unaorejelewa hapa ni ule wa kuangalia kama kipashio fulani kimechopekwa, kimedondoshwa au kimehamishwa katika MNJ. Mbinu hii pia ilitumika kurejelea dhana kisintaksia zaidi kuliko kisementiki au kimofolojia wakati wa uchambuzi wa data ili watu muktadha wa kisintaksia waweze kuelewa kwa urahisi.
Mtafiti, aliongozwa na NR ambayo inasema kwamba ili kuzalisha sentensi lazima ujue kanuni ambayo inatokana na umilisi wa mtu na lugha yake. Kadhalika, mtafiti alichambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa na kubainisha michakato inayotumika kuunda sentensi hizo, kwa kuongozwa na NR. Kwa kuwa kwa mujibu wa nadharia hii, michakato ya uundaji wa sentensi ina taratibu au ruwaza zake ambazo ndizo zinaifanya sentensi fulani ikubalike. Katika utafiti huu, zile ruwaza ndizo zinazoonesha namna ya uundaji wa SC za Kiswahili na kisha tumebainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi hizo. Uchambuzi ulifanyika kwa njia ya maelezo, sentensi za mifano na michoroti.
3.7 Kanuni za Kiitikeli
Utafiti wowote wa kitaaluma lazima uzingatie matakwa, miiko na maadili ya kijamii (Creswell, 2012; Ponera, 2019). Kwa kuwa utafiti huu ni wa kitaaluma, mtafiti alizingatia na kufuata taratibu zote za kufanya utafiti zilizowekwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwamo kuomba kibali cha kukusanya data. Kibali hicho kilipelekwa kwenye mamlaka husika zilizomruhusu mtafiti kufanya utafiti huu. Pia, masuala mengine ya kiitikeli kama vile ukweli na uwazi yalizingatiwa.
3.8 Kikwazo cha Utafiti
Mtafiti alikumbana na kikwazo cha mfumo mpya wa kuomba kibali kwa njia ya mtandao ambao bado haukuwa rafiki kutokana na upya wake. Kutokana na upya huo, mtafiti aliomba kibali mwezi Februari mwaka (2021), alikipata mwezi Mei mwaka (2021) ilhali alitarajia akipate mwezi Machi mwaka (2021). Kwa sababu hiyo, muda wa kukusanya data ilibidi aisogeze mbele hadi Juni mwaka (2021). Licha ya kuwapo kwa kikwazo hicho katika hatua ya ukusanyaji wa data, hakikuweza kuathiri matokeo ya utafiti huu.
3.9 Muhtasari
Katika sura hii methodolojia ya utafiti iliyotumika katika mchakato wa ukusanyaji na uchambuzi wa data imewasilishwa. Vipengele vya methodolojia vilivyojadiliwa katika sura hii ni: eneo la utafiti, wango, sampuli na usampulishaji, mbinu za ukusanyaji wa data, vifaa vya utafiti, uchambuzi wa data, kanuni za kiitikeli na kikwazo cha utafiti. Sura inayofuata inahusu uwasilishaji na uchambuzi wa data. Katika sura inyofuata data za utafiti zimewasilishwa kwa kutumia maelezo, sentensi mbalimbali za mifano na michoroti kwa kuongozwa na NR.
SURA YA NNE
UWASILISHAJI NA UCHAMBUZI WA DATA
4.1 Utangulizi
Sura hii inahusu uwasilishaji na uchambuzi wa data zilizokusanywa na mtafiti kutoka maktabani. Sura hii imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza imewasilisha data inayochambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa, na sehemu ya pili imebainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda sentensi hizo. Mwisho ni hitimisho.
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza michakato ya kisintaksia katika uundaji wa SC za Kiswahili. Lengo hili lilikuwa na malengo mahususi mawili. Mosi, kueleza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa. Pili, kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda SC za Kiswahili. Ili kufanikisha malengo mahususi ya utafiti huu, kulikuwa na maswali yafuatayo: Mosi, SC za Kiswahili zinaundwaje? Pili, ni michakato gani ya kisintaksia inayotumika kuunda SC za Kiswahili? Sehemu hii imeanza na kuwasilisha na kuchambua data inayohusu namna SC za Kiswahili zinavyoundwa.
4.2 Namna Sentensi Changamani za Kiswahili Zinavyoundwa
Sehemu hii inakusudia kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa kutoka MN kwenda MNJ kwa kuongozwa na NR. Data za utafiti huu zinaonesha kuwa SC za Kiswahili zina miundo mbalimbali. Miundo hiyo ni ile yenye KK na KB kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 1.
SC
KK KB
nomino kivumishi kielezi
-kama -ye- -sababu
-kuwa -po- -sharti
-kwamba -o- -kusudi
Kielelezo Na. 1: Miundo ya SC za Kiswahili
Kielelezo Na. 1 kinaonesha kwamba SC za Kiswahili zinaundwa na KK na KB. Ifahamike kwamba muundo huo unaweza kubadilika, yaani badala ya kuwa KK na KB ikawa KB na KK. Aidha, kielelezo kinaonesha vitambulishi vya kishazi husika chini ya aina ya KB. Sehemu zinazofuata zinaeleza zaidi namna SC za Kiswahili zinavyoundwa kutoka MN kwenda MNJ. Sehemu ya (4.2.1) imeanza kwa kuchambua SC zenye muundo wa KK na KBN.
4.2.1 Sentensi Changamani Zenye Muundo wa Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Nomino
KK hufasiliwa kwa kujiegemeza kisemantiki zaidi ambapo hufasiliwa kama ni kishazi kinachoweza kutumika peke yake na kuleta maana kamili katika mawasiliano bila kutegemea kishazi kingine (Wesana-Chomi, 2017). KK ni kiambajengo kikuu cha SC ambacho huambatana na vishazi vingine ambavyo vimeshushwa hadhi na kuwa bebwa. Miongoni mwa vishazi hivyo ni KBN. Hiki ni kishazi ambacho hufanya kazi kama yambwa, kazi ambayo aghalabu hufanywa na nomino au kirai nomino. Kutokana na kazi hiyo kishazi hiki hufahamika kama KBN.
Data za utafiti huu zinaonesha kuwa kuna SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBN. Katika MNJ wa SC za Kiswahili, KBN hutanguliwa na kiunganishi tegemezi (kuanzia sasa, UT) kama vile kwamba, kuwa na kama kama anavyoeleza Wesana-Chomi (2017) ingawa haweki wazi namna SC za Kiswahili zenye muundo huu zinavyoundwa. Utafiti huu umeonesha namna SC za Kiswahili zenye muundo huo zinavyoundwa. Tazama mfano wa (16a) kwa ufafanuzi zaidi.
(16) a. [Walimtangaza]S1 [kwamba yeye ni chapa nguvu] S2 (Lema, 2014: 3)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Mfano wa (16a) unaonesha kuwa SC hiyo imeundwa na KK na KBN katika MNJ. Hii ni kwa sababu S2 ina UT kwamba. Hii ina maana kwamba katika MN, sentensi hiyo ilikuwa na vishazi vikuu viwili kama inavyooneshwa katika data ya (16b). Kati ya vishazi hivyo, hakuna kilichokuwa kimetegemezwa ndani ya kishazi kingine.
(16) b. [Walimtangaza] S1 [yeye ni chapa nguvu] S2
Kwa kuwa kitenzi walimtangaza kina tabia ya kuhitaji yambwa, palihitajika mchakato wa kisintaksia wa kuunda tungo hii. Ili kufanikisha hili, mchakato wa uchopekaji ulifanyika kama inavyooneshwa katika hatua ya kwanza (1).
Hatua ya 1: Uchopekaji wa UT kwamba kwenye S2:
[Walimtangaza] S1 [kwamba yeye ni chapa nguvu] S2.
Katika hatua ya kwanza UT kimechopekwa kwenye S2 ili sentensi hiyo ifanye kazi ya kujaliza kitenzi walimtangaza. Katika hali kama hii S2 hujaliza maana ya kitenzi kikuu cha S1, kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na nomino. Kutokana na uchopekaji wa UT kwenye S2 huifanya sentensi hiyo kubebwa ndani ya kitenzi cha S1. Baada ya uchopekaji, hatua inayofata huwa ni kuunganisha S1 na S2 kwa kutumia UT kwamba, kama inavyooneshwa katika hatua ya pili (2).
Hatua ya 2: Uunganishaji wa S1 na S2:
Walimtangaza kwamba yeye ni chapa nguvu.
Baada ya vipashio vilivyopo katika S1 na S2 kama inavyooneshwa kwenye hatua ya kwanza kuonekana vinaweza kuunganishwa kwani vinashikamana, hatua inayofuata huwa ni uunganishaji wa vipashio hivyo. Pindi uunganishaji huu unapotokea katika MNJ huifanya S2 kufanya kazi kama kijalizo cha kitenzi. Kazi hii aghalabu hufanywa na nomino na hubebwa ndani ya kitenzi cha S1. Hii ndiyo sababu S2 huchukuliwa kama KBN. Tazama kielelezo Na. 2 kwa ufafanuzi zaidi.
S1
KN1 KT1
T1 S2
N1 UT KN2 KT2
W t2 KN3
N3
ÆŸ walimtangaza kwamba yeye ni chapanguvu
Kielelezo Na. 2: MNJ wa SC za Kiswahili Zenye KK na KBN
Pia, kwa mujibu wa data za utafiti huu madai ya Wesana-Chomi (2017), kwamba SC za Kiswahili zenye KK na KBN huundwa kwa mchakato wa ujalizaji, hayana mashiko kisintaksia. Wesana-Chomi amejenga madai yake kuhusu muundo wa SC zinazoundwa kwa mchakato wa ujalizaji kwa kutumia data ya (17a-b).
(17) a. [Wengi wanasema] S1 [kuwa cheusi ni mke wa Hamisi] S2
b. [Juma ameleta habari] S1 [kwamba mgonjwa amefika asubuhi] S2
Chanzo: Wesana-Chomi (2017)
Ukichunguza kwa makini sentensi za mfano wa (17a-b) kutoka kwa Wesana-Chomi (2017) hazina tofauti kimuundo na ile ya mfano wa (16a) ya maktabani. Kama ilivyoelezwa katika mfano wa (16), S2 hufanya kazi ya kujaliza S1 kutokana mchakato wa uchopekaji wa UT kwenye S2 kama vile: kama, kuwa na kwamba katika MNJ. Kishazi cha S2 (KBN) aghalabu hufanya kazi ya kujaliza kitenzi kikuu cha S1 au KN2 cha S1.
Kwa kuzingatia maelezo haya, kutokana na data ya (16) kutoka uwandani ujalizaji si namna mojawapo ya uundaji wa SC za Kiswahili bali ni dhima mojawapo ya ruwaza za kisintaksia. Kadhalika, data ya (16) inadhihirisha mawazo ya Philipo na Kuyenga (2018) wanaosema kuwa dhana ya ujalizaji ilibuniwa na wanasarufi mapokeo ili kueleza uhusiano unajitokeza pindi kauli mbili zinaposhikamanishwa ikiwa kauli moja inafanya kazi kama kijenzi mahususi cha kauli nyingine. Pia, data ya (16) inaonesha kwamba ikiwa sentensi mbili zitashikamanishwa kwa kutumia UT, aghalabu S2 hufanya kazi ya kujaliza sentensi nyingine kama ilivyoelezwa katika data ya (16).
4.2.2 Sentensi Changamani Zenye Muundo wa Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Vumishi
Data za utafiti huu zinaonesha kuna SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na kishazi bebwa vumishi (kuanzia sasa, KBV). KK kimeshaelezwa katika sehemu ya (4.2.1). Kuhusu KBV, Mekacha (1983) anakiita kishazi rejeshi ambapo anaeleza kuwa ni tungo tegemezi iliyoshushwa hadhi na kutegemezwa ndani ya tungo nyingine. Anaongeza kuwa tungo tegemezi haitokei peke yake bali hutokea kama sehemu ya sentensi, na kimuundo tungo tegemezi huwa kiambajengo cha sentensi nyingine. Mtaalamu huyo ameeleza namna tungo tegemezi rejeshi inavyoundwa kwa kutumia mkabala wa SGZ ingawa habainishi anatumia hatua ipi hasa. Pia, ametaja hatua mbili tu za namna tungo tegemezi inavyoundwa ambazo ni uwakilishi na uambishi. Hata hivyo, anatanabahisha kwamba lengo la chapisho lake ni kuibua mjadala kuhusu sintaksia ya tungo rejeshi. Kwa hiyo, katika kueleza namna tungo tegemezi ambazo kwa pamoja zinaunda SC ya Kiswahili, utafiti huu unatofautiana kwa kiwango fulani na Mekacha (1983). Tazama mfano wa (18a) kutoka maktabani.
(18) a. Mtoto aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita. (Lema,
2004: 13)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Katika data ya (18) tungo tegemezi iliyoandikwa kwa hatimlazo ni tungo iliyoshushwa hadhi kama ilivyoelezwa na Mekecha (keshatajwa). Hii ina maana kwamba katika MN, tungo iliyoandikwa kwa hatimlazo katika (18a) ilikuwa na hadhi sawa na hiyo ambayo haijaandikwa kwa hatimlazo kabla ya mageuzi kama inavyooneshwa katika (18b).
(18) b. i) Mtoto alikwenda kumuita.
ii) Mtoto alikuwa anacheza hapo nyumbani.
Katika data ya (18b), mtoto anayezungumziwa katika S1 na S2 ni yuleyule. Kwa kuwa mtoto anayezungumziwa ni yuleyule, nomino moja hudondoshwa ili kuondoa uradidi. Aghalabu nomino inayodondoshwa ni ile ya S2 kama inavyooneshwa katika hatua ya kwanza.
Hatua ya 1: Udondoshaji wa nomino radidi (mtoto) ya S2:
Mtoto [mtoto alikuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Nomino radidi mtoto ya S2 katika hatua ya kwanza imekatwa kuonesha imedondoshwa. Hii hufanyika ili kuondoa uradidi na kuleta ushikamani katika tungo husika. Kutokana na kudondosha nomino radidi katika S2 mahali nomino hiyo ilipokuwa panabaki wazi kama inavyooneshwa hapa chini.
Mtoto [. alikuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Hivyo, huhitajika kupachika kipashio kingine ambacho kitaziba pengo hilo. Aghalabu kiambishi rejeshi ndicho hupachikwa ili kuziba pengo la nomino iliyodondoshwa kama inavyooneshwa katika hatua ya pili (2).
Hatua ya 2: Upachikaji wa kiambishi rejeshi kwenye pengo la nomino iliyodondoshwa:
Mtoto [-ye- alikuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Wataalamu wa sintaksia kama Mekacha (1983) na Wesana-Chomi (2017) wanachanganya hatua ya kwanza na ya pili kana kwamba ni hatua moja au inafanyika kwa wakati mmoja. Wao wanadai kwamba nomino inayojirudia katika S1 na S2 hubadilishwa au kugeuzwa na kuwa kiambishi rejeshi ambapo Mekacha (1983) anaviita viwakilishi. Ukweli ni kwamba nomino inayojirudia katika S1 na S2 hudondoshwa ili kuondoa uradidi katika tungo. Kutokana na udondoshaji huo, nomino iliyodondoshwa huhitajika kufidiwa kwa kuchopeka kiambishi rejeshi. Mekecha (1987) ameiita hatua hii uambishaji ambapo anaeleza kuwa kirejeshi huambishwa kwa namna tofauti. Licha ya kwamba kiambishi rejeshi {-ye-} ni kipashio cha kimofolojia katika hatua hiyo lakini kina uamilifu wa kisintaksia wa kugeuza tungo tenzi kufanya kazi kama kikumushi. Kwa msingi huu, kipashio hicho kilifaa kuelezwa kisintaksia zaidi kuliko kimofolojia kama anavyofanya Mekacha. Kisintaksia kiambishi rejeshi hupachikwa kwenye nomino iliyodondoshwa ili kuziba pengo kama ilivyooneshwa katika hatua ya pili katika data ya (18).
Ukitazama tungo ya hatua ya pili katika data ya (18) inaonesha kiambishi {-ye-} kipo peke yake ilhali kwa kawaida katika Kiswahili kiambishi rejeshi huambatanishwa kwenye kitenzi kikuu, kisaidizi au kwenye umbo maalumu la AMBA. Hivyo, kiambishi hicho huhitajika kuhama ili kiambatanishwe ndani ya kitenzi kilicho karibu na kisabiki chake. Tazama hatua ya tatu kwa ufafanuzi zaidi.
Hatua ya 3: Uhamishaji wa kiambishi rejeshi kwenda karibu na kisabiki chake
Mtoto [ ye aliyekuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Baada ya uhamishaji wa kiambishi rejeshi kutoka mahali kilipokuwa na kupachikwa kwenye kitenzi, hukifanya kitenzi cha kishazi hicho kuwa bebwa. Uhamishaji huo ndio unaozalisha SC ya Kiswahili yenye muundo wa KK na KBV, kama inavyooneshwa hapa chini katika MNJ.
Mtoto aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita.
Tungo ambayo huwa na kiambishi rejeshi ndiyo imeitwa KBV. Kishazi hiki kimechukuliwa kama KBV tofauti na kishazi bebwa rejeshi kama walivyokuwa wakikichukulia hapo awali wataalamu kama vile Mekacha (1983). Hii ni kwa sababu kishazi hiki hufanya kazi ya kuvumisha nomino ya KK kama inavyooneshwa kwenye kielelezo Na. 3.
S1
KN1 KT1
N1 S2 Ts T
KN2 KT2
N TS T KE
E1 E2
Mtoto ÆŸ aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita
Kielelezo Na. 3: MNJ wa SC ya Kiswahili Zenye KK na KBV
Kwa mujibu wa data za utafiti huu, maelezo yaliyotolewa na Mekacha (1987) na Wesana-Chomi (2017) kuhusu namna SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBV zinavyoundwa yanasailika. Mathalani, Wesana-Chomi anadai kwamba nomino radidi hugeuzwa na kuwa kirejeshi. Data za utafiti zimeonesha kwamba nomino radidi haigeuzwi na kuwa kirejeshi badala yake inadondoshwa na kufidiwa na kiambishi rejeshi ambacho hupachikwa pale nomino radidi ilipokuwa.
Kadhalika, data za utafiti huu zinasaili madai ya Mekacha kwamba kiambishi rejeshi huambishwa kwenye kitenzi. Kwa muktadha wa kisintaksia, kwa kuwa kiambishi rejeshi kina uamilifu wa kugeuza kitenzi kufanya kazi kama kikumushi cha nomino kama inavyodhihirika katika mfano wa (18) hatua ya tatu (03) ilifaa kurejelewa kama uchopekaji kuliko uambishaji ambao umekaa kimuktadha wa kimofolojia. Kwa mantiki hii, hatua ya uambishaji anayoisema Mekacha (keshatajwa) ijulikane au itambulike kama uchopekaji wa kiambishi rejeshi kwenye kitenzi badala ya uambishaji ambayo ni dhana ya kimofolojia.
4.2.3 Sentensi Changamani Zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Elezi
Data za utafiti huu zinaonesha kwamba baadhi ya SC za Kiswahili zinaundwa na KK na kishazi bebwa elezi (kuanzia sasa, KBE). Data za utafiti huu, zinaonesha kwamba katika MNJ, KBE hutanguliwa na viunganishi tegemezi maalumu (kuanzia sasa, UTM). Vinaitwa UTM kwa sababu huwa vinaonesha masharti, kusudi, sababu, namna au wakati tendo linapofanyika. Kwa mfano, kwa sababu, kama, ili, kwani, nge, ki na mithili ya. Tazama mfano wa (19a) kutoka maktabani kwa ufafanuzi.
(19) a. [Mtoto mmoja wa kike, alifika] S1 [ili ashinde na Felisia] S2 (Lema, 2004:
18)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Mfano wa (19a) unaonesha SC imeundwa na KK na KBE. Hii ni kwa sababu S2 ina UTM cha sababu ambacho kimeifanya tungo ya S2 kuwa bebwa kwenye tungo ya S1. Hii ina maana kwamba katika MN, S2 ilikuwa ni tungo yenye hadhi sawa na S1 kabla ya kuchopeka UTM kama inavyooneshwa katika (19b).
(19) b. [Mtoto mmoja wa kike, alifika] S1 [mtoto mmoja wa kike, ashinde na
Felisia] S2
Data ya (19b) inaonesha kwamba KN cha S1 na S2 ni kilekile. Kwa kuwa KN kinachozungumziwa ni kilekile katika sentensi zote mbili, udondoshaji wa KN kimoja hufanyika ili kuondoa uradidi katika tungo. Aghalabu ikiwa kuna vipashio radidi kwenye tungo basi kipashio cha S2 ndicho hudondoshwa kama inavyooneshwa katika hatua ya kwanza.
Hatua ya 1: Udondoshaji wa KN ya S2:
[Mtoto mmoja wa kike, alifika] S1 [mtoto mmoja wa kike, ashinde na Felisia] S2
KN radidi cha S2 kimekatwa, kuonesha kimedondoshwa. KN kilichodondoshwa hurejelewa kwa kupachika UTM cha sababu ili kufidia udondoshaji huo, kama inavyooneshwa katika hatua ya pili.
Hatua ya 2: Uchopekaji wa UTM kwenye S2:
[Mtoto mmoja wa kike, alifika] S1 [ili ashinde na Felisia] S2
Uchopekaji wa UTM ili katika S2 unaifanya S2 kufanya kazi ya kueleza sababu ya mtoto mmoja wa kike kufika nyumbani kwa kina Felisia. Matokeo ya uchopekaji wa kipashio hicho katika S2 huifanya sentensi hiyo kufanya kazi ya kujaliza S1. Hatua inayofuata huwa ni kuunganisha S1 na S2 kwa kutumia UTM hicho. Tazama hatua ya tatu (03) kwa ufafanuzi.
Hatua ya 3: Uunganishaji wa S1 na S2 kwa kutumia UTM ili:
Mtoto mmoja wa kike, alifika ili ashinde na Felisia.
Huu ndio MNJ wa tungo iliyoundwa na KK na KBE ambapo KBE imepoteza hadhi ya kuwa KK kama ilivyokuwa katika MN. Hii imesababishwa na upachikaji wa UTM kinachoifanya tungo hiyo kuwa bebwa kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 4. na kufanya kazi ya kueleza sababu ya mtoto mmoja wa kike kufika kwa kina Felisia.
S1
KN1 KT1
N1 KV T S2
V KH UTM KN2 KT2
E. sababu T KH
H KN N H KN
N N
Mtoto mmoja wa kike alifika ili ÆŸ ashinde na Felisia
Kielelezo Na. 4: MNJ wa SC Kiswahili Zenye KK na KBE
Pia, kuna SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBE zinazoundwa kwa kuchopeka UTM bila kudondosha kipashio chochote katika MN kama katika hatua ya pili ya tungo Na. 19. Tazama mfano wa (20a) kutoka maktabani kwa ufafanuzi zaidi.
(20) a. [Hamiata alinuna kabisa] S1 [kwani Felisia alikuwa amemuaibisha] S2 (Lema, 2004: 4)
Chanzo: Data za Maktabani
Mfano wa (20a) inaonesha kwamba S1 haina hadhi sawa na S2. Hii ni kwa sababu S2 ina UTM cha sababu. Maelezo haya yana maana kwamba kabla ya kupachika UTM cha sababu S1 na S2 katika MN zote zilikuwa na hadhi sawa, kama inavyoonesha katika (20b).
(20) b. [Hamiata alinuna kabisa] S1 [Felisia alikuwa amemuaibisha] S2
Data ya (20b) inaonesha kuwa kitenzi cha S1 kina kielezi chake ambacho ni kabisa. Hata hivyo, kielezi hicho kinaonekana hakielezi wazi kwa nini hasa Hamiata alinuna bali kinaeleza namna tendo lilivyofanyika. Hivyo, huhitajika mchakato wa kisintaksia utakaowezesha kuwapo na maelezo toshelevu ya sababu za tendo la kununa kwa Hamiata. Kutokana na uhitaji huo, uchopekaji wa UTM cha sababu ya tendo hupachikwa kabla ya S2 kama inavyojidhihirisha katika (20c).
(20) c. [Hamiata alinuna kabisa] S1 [kwani Felisia alikuwa amemuaibisha] S2
Kutokana na kuchopeka UTM cha sababu kwani huifanya S2 kufanya kazi kama kielezi cha kitenzi cha S1 ambacho kinatoa maelezo toshelevu ya sababu ya kutendeka kwa tendo la kununa. UTM ndicho huunganisha S1 na S2 kama inavyooneshwa hapa chini katika (20d) ambao ni MNJ.
(20) d. Hamiata alinuna kabisa kwani Felisia alikuwa amemuaibisha.
Kutokana na kuunganisha S1 na S2, huku S2 ikiwa imechopekwa UTM huifanya S2 kufanya kazi ya kueleza sababu ya tendo la S2. Hivyo, S2 hubebwa ndani ya kitenzi cha S1 kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 5.
S1
KN1 KT1
N1 T E S2
UTM KN2 KT2
E. Sababu N2 Ts T
Hamiata alinuna kabisa kwani Felisia alikuwa amemuaibisha
Kielelezo Na. 5: MNJ wa SC Kiswahili Zenye KK na KB
Kwa muhtasari, namna SC za Kiswahili zinavyoundwa imebainika kwamba kila muundo una namna yake ya kuundwa. Ndani ya muundo mmoja kunaweza kujitokeza tofauti ndogondogo ya namna sentensi hizo zinavyoundwa. Pia, imebainika kuwa namna za uundaji wa SC ndizo zinazoifanya sentensi moja au mbili kati ya zinazounda tungo hiyo kufanya kazi ya kukumusha au kujaliza tungo nyingine.
4.3 Michakato ya Uundaji wa Sentensi Changamani za Kiswahili
Sehemu hii inajibu swali la pili la utafiti huu. Swali la pili lilikuwa; michakato gani inatumika kuunda SC za Kiswahili? Swali hili limeshughulikiwa kwa kuongozwa na NR ambapo michakato iliyobainika kutumika kuunda SC ni hii ifuatayo:
4.3.1 Uchopekaji wa Viunganishi Tegemezi
Kwa mujibu wa utafiti huu, uchopekaji ni mchakato unaorejelea hali ambayo kipashio fulani ambacho hakikuwapo katika MN wa tungo huongezwa katika MNJ na kubadili hadhi ya kisintaksia ya tungo husika. Hadhi inayorejelewa hapa ni ya kubadili KK kuwa KB. Data zilizochambuliwa katika (4.2) zimedhihirisha kwamba kuna SC za Kiswahili ambazo zinaundwa kutokana na uchopekaji wa viunganishi tegemezi. Kwa mujibu wa NR uchopekaji wa vipashio ambavyo havikuwapo katika MN wa tungo hubadili tungo fulani kutoka kwenye usibebwa kwenda bebwa. Imedhihirika kwamba uchopekaji hutumika kuunda SC zenye muundo wa KK na KBN na KK na KBE. Hata hivyo, uchopekaji wa viunganishi tegemezi vinavyounda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBN na KK na KBE ni tofauti. Tazama SC ya Kiswahili yenye muundo wa KK na KBN katika mfano wa (21a) kutoka maktabani.
(21) a. [Watu walisema] S1 [kwamba Wamakonde ni wacheza sindimba, Wamakonde wachonga vinyago] S2 (Lema, 2004: 8)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Mfano wa (21a) inaonesha kuwa S2 ni bebwa. Hii ni kwa sababu tungo hiyo haiwezi kujitegemea yenyewe kimaana kutokana na uchopekaji wa UT cha kawaida kwamba. Hii ina maana kwamba kabla ya uchopekaji wa kiunganishi kwamba, katika upande wa S2, sentensi hiyo ilikuwa na hadhi sawa na S1 kama inavyooneshwa katika (21b).
(21) b. [Watu walisema] S1 [Wamakonde ni wacheza sindimba, Wamakonde wachonga vinyago] S2
Katika (21b) kwa kuwa kitenzi cha S1 kinahitaji yambwa ili kuwa na uarifishaji kamili, palihitajika kufanyika mchakato wa kisintaksia wa kukijaliza kitenzi hicho ili kitoe taarifa kamili. Hivyo, mchakato uliofanyika ni wa kuchopeka UT kwamba kwenye upande wa S2 ambako kunaifanya sentensi hiyo kufanya kazi iliyopaswa kufanywa na nomino. Tazama mfano wa (21c) unavyoonesha uchopekaji wa UT.
(21) c. [Watu walisema] S1 [kwamba Wamakonde ni wacheza sindimba,
Wamakonde wachonga vinyago] S2
Kutokana na uchopekaji wa UT kwamba huifanya S2 kufanya kazi kama nomino ambapo S2 hii hubebwa kwenye kitenzi cha S1. Kadhalika, baada ya uchopekaji wa UT hiki katika S2 hufanya S1 na S2 kuunganishwa kwa kutumia kiunganishi hicho. Tazama mfano wa (21d) MNJ wa kwa ufafanuzi zaidi.
(21) d. Watu walisema kwamba Wamakonde ni wacheza sindimba, Wamakonde
wachonga vinyago.
Kwa hiyo, inadhihirika kwamba uchopekaji wa UT hicho kwamba katika muundo wa S2 wa nje ndiyo unaoifanya sentensi hiyo kuwa bebwa. Hatimaye tunapata SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBN katika MNJ. Katika muundo kama huu KBN hufanya kazi ya kujaliza kitenzi cha S1 kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 6.
S1
KN1 KT1
N1 T1 S2
UT S3 U S4
KN3 KT3 KN4 KT4
N3 t KN3 N4 t4 KN5
N N5
Watu walisema kwamba Wamakonde ni wachezasindimba ÆŸ Wamakonde ÆŸ wachongavinyago
Kielelezo Na. 6: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Uchopekaji wa UT
Aidha, data ya utafiti huu inaonesha kwamba UT vya kawaida aghalabu hutangulia KBN kama inavyoonesha katika data ya (22 a-b) kutoka maktabani.
(22) a. Alionekana kama aliyeelewa swali aliloulizwa na yule nesi. (Bwana, 2004:1)
b. Walimtangaza kwamba yeye ni chapa nguvu. (Lema, 2004: 3)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Kwa hiyo, SC zenye muundo wa KK na KBN zinaundwa kwa uchopekaji wa UT vya kawaida. Hii ni tofauti na madai ya Wesana-Chomi (2017) ambaye anasema kwamba sentensi zenye sifa hizi huundwa kwa ujalizaji. Data za utafiti huu zimedhihirisha kuwa SC hizi huundwa kwa mchakato wa uchopekaji. Kutokana na uchopekaji wa UT kwenye S2, huifanya S2 kuwa kama kijalizo cha KN2 ya S1 au kitenzi kikuu cha S1 (taz. kielelezo Na. 6).
Pengine kutokana na dhima hiyo, ndiyo iliyomchochea Wesana-Chomi kudai kwamba SC zenye muundo KK na KBN huu huundwa kwa mchakato wa ujalizaji. Hata hivyo, matokeo yanaonesha kuwa ujalizaji ni tokeo la uchopekeji wa UT katika tungo kama ilivyodhihirishwa katika data ya (21). Kwa hiyo, kisintaksia SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBN huundwa kwa mchakato wa uchopekaji wa UT kwenye S2. Uchopekaji huu huifanya S2 kufanya kazi ya kujaliza kitenzi au nomino ya S1.
Pia, mchakato wa uchopekaji wa UT umedhihirika kuunda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBE. Tofauti na uchopekaji wa UT vinavyojidhihirisha katika (22a-b), UT hivi huwa ni maalumu. Vinaitwa UTM kwa sababu huonesha: sababu, kusudi, sharti, namna na wakati kufanyika kwa tendo. UTM ni kama vile: ili, kama, kwa sababu, nge, kwani, mithili ya na kama. Mara nyingi UTM hutangulia KBE. Tazama mfano wa (23a) kwa ufafanuzi zaidi.
(23) a. [Hamiata alinuna kabisa] S1 [kwani Felisia alikuwa amemuaibisha] S2
(Lema, 2004: 4)
Chanzo: Data za Maktabani
Mfano wa (23a) unaonesha kwamba S2 haina hadhi sawa na S1. Hii ni kwa sababu S2 ina UTM cha sababu. Maelezo haya yana maana kwamba katika MN wa tungo hiyo S1 na S2 zote zilikuwa na hadhi sawa kabla S2 haijachopekwa UTM kama inavyoonesha katika mfano (23b).
(23) b. [Hamiata alinuna kabisa] S1 [Felisia alikuwa amemuaibisha] S2
Mfano wa (23b) unaonesha kuwa kitenzi cha S1 kina kielezi chake ambacho ni kabisa. Hata hivyo, kielezi hicho kinaonekana hakielezi wazi kwa nini Hamiata alinuna. Hivyo, huhitajika mchakato wa kisintaksia utakaowezesha kuwapo na maelezo toshelevu ya sababu ya tendo la kununa kwa Hamiata. Kwa sababu hiyo, uchopekaji wa UTM cha sababu ya tendo, ambacho ni kwani, kimepachikwa kabla ya S2 kama inavyojidhihirisha katika mfano wa (23c).
(23) c. [Hamiata alinuna kabisa] S1 [kwani Felisia alikuwa amemuaibisha] S2
Kutokana na kuchopeka UTM cha sababu kwani S2 inafanya kazi kama kielezi cha kitenzi cha S1 ambacho dhima yake ni kueleza sababu za kutendeka kwa tendo. Hatua inayofuata ni kuunganisha S1 na S2 ili kupata MNJ kama inavyooneshwa katika mfano wa (23d).
(23) d. Hamiata alinuna kabisa kwani Felisia alikuwa amemuaibisha.
Mchakato wa kuchopeka UTM kwenye S2, huifanya kushuka hadhi na kufanya kazi kama kielezi. Hatimaye tunapata SC yenye KK na KBE katika MNJ ambapo S2 hubebwa ndani ya kitenzi cha S1 kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 7.
S1
KN1 KT1
N1 T1 E S2
UTM KN2 KT2
E. Sababu N2 Ts T
Hamiata alinuna kabisa kwani Felisia alikuwa amemuaibisha
Kielelezo Na. 7: MNJ wa SC ya Kiswahili IIiyoundwa kwa Uchopekaji wa UT
4.3.2 Udondoshaji-chopezi
Kwa mujibu wa utafiti huu, imebainika kuwa udondoshaji-chopezi wa vipashio ni miongoni mwa michakato ya uundaji wa SC za Kiswahili. Udondoshaji-chopezi wa vipashio ni mchakato wa kuondoa kipashio radidi kinachojitokeza katika MN ili kuondoa uradidi ambapo kipashio kilichodondoshwa hurejelewa kwa kupachika kipashio kingine ili kuziba pengo. Udondoshaji-chopezi huu ndio hufanya tungo zilizokuwa na hadhi sawa katika MN kuwa na hadhi tofauti yaani tungo moja kubebwa ndani ya nyingine katika MNJ. Imebainika kwamba mchakato huu hutumika kuunda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBE na KK na KBV. Tazama mfano wa (24a) kwa ufafanuzi zaidi.
(24) a. [Mtu mwingine tunamwita mwizi] S1 [kwa sababu tumemkamata akiiba]
S2 (Mwananchi, 26/06/2021: 19)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Mfano wa (24a) ni SC yenye muundo wa KK na KBE. S2 inaeleza zaidi kwa nini hasa mtu mwingine tunamwita mwizi. Hii ni kutokana na udondoshaji uliofanyika katika MN na kuchopeka UTM kwa sababu katika MNJ. Hii ina maana kwamba kabla ya mchakato wa udondoshaji-chopezi, S1 na S2 za mfano wa (24a) zilikuwa na hadhi sawa kama inavyooneshwa katika MN wa (24b).
(24) b. [Mtu mwingine tunamwita mwizi] S1 [Mwizi tumemkamata akiiba] S2
Katika (24b) nomino mwizi, inajitokeza katika S1 na S2. Ili kuondoa uradidi, nomino moja hudondoshwa kama inavyooneshwa katika (24c).
(24) c. [Mtu mwingine tunamwita mwizi] S1 [mwizi tumemkamata akiiba] S2
Katika (24c) nomino mwizi ya S2 imekatwa kuonesha kwamba imedondoshwa. Nomino hiyo imedondoshwa ili kuondoa uradidi katika tungo. Nomino hii iliyodondoshwa hurejelewa kwa kupachika UTM cha sababu ili kufidia nomino hiyo iliyodondoshwa. Tazama uchopekaji wa UTM kwa sababu katika (24d).
(24) d. [Mtu mwingine tunamwita mwizi] S1 [kwa sababu tumemkamata akiiba] S2
Kutokana na upachikaji huo S2 inakuwa bebwa. S2 hiyo hufanya kazi ya kueleza sababu ya tendo la S1. Kwa hiyo, hubebwa ndani ya kitenzi cha S1 kama inavyooneshwa katika data (24e) ya MNJ.
(24) e. Mtu mwingine tunamwita mwizi kwa sababu tumemkamata akiiba.
Mchakato huu wa udondoshaji-chopezi huifanya sentensi iliyokuwa kuu kuwa bebwa. Hatimaye tunapata SC yenye muundo wa KK na KBE kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 8.
S1
KN1 KT1
N1 KV T KN2
V N2 S2
UTM KN3 KT2
E. Sababu N3 Ts T
Mtu mwingine tunamwita mwizi kwa sababu ÆŸ tumemkuta akiiba
Kielelezo Na. 8: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji-chopezi
Pia, data za utafiti zinaonesha kwamba udondoshaji-chopezi vipashio unatumika kuunda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBV. Tazama mfano wa (25a) kwa ufafanuzi zaidi.
(25) a. [Baadaye walihamia chumbani] S1 [ambako mengi yalifanyika kati yao] S2 (Mwananchi, 26/06/2021: 20)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Mfano wa (25a) S2 haina hadhi sawa na S1. Hii ni kutokana na udondoshaji-chopezi uliofanyika wa kiima cha S2 na kufidiwa na umbo AMBA lenye kiambishi rejeshi {-ko} lililoifanya S2 kuwa bebwa. Hii ina maana kwamba S2 ilikuwa na hadhi sawa na S1 katika MN kabla ya mchakato wa udondoshaji-chopezi kutokea, kama inavyooneshwa katika (25b).
(25) b. [Walihamia chumbani baadaye] S1 [chumbani mengi yalifanyika kati yao] S2
Mfano wa (25b) unaonesha kwamba nomino ya S1 ndiyo hiyohiyo inayozungumziwa katika KN1 cha S2. Hivyo, ili kuondoa uradidi huo na kuleta ushikamani katika tungo, nomino moja hususani ile ya S2 hudondoshwa kama inavyoonesha hapa chini katika (25c).
(25) c. [Walihamia chumbani baadaye] S1 [chumbani mengi yalifanyika kati yao] S2
Katika (25c) nomino chumbani ya S2 imekatwa kuonesha imedondoshwa ili kuondoa uradidi. Aghalabu nomino inapodondoshwa huhitaji kipashio kingine ili kufidia pengo linaloachwa na udondoshaji huo. Kutokana na udondoshaji huo hupachikwa kiambishi {-ko} ili kufidia nomino ya S2 iliyodondoshwa. Kiambishi hicho hupachikwa kwenye umbo AMBA. Kiambishi hicho kwenye umbo hilo hufanya kazi kama UT. Tazama mfano wa (25d) kwa ufafanuzi zaidi.
(25) d. [Baadaye walihamia chumbani] S1 [ambako mengi yalifanyika kati yao] S2
Data ya (25d) inaonesha kuwa udondoshajichopezi uliofanyika katika S2 umeifanya tungo hiyo kuwa bebwa kwa kuwa inafanya kazi kama shamirisho au kikumushi cha nomino ya S1. Pia, ukichunguza (25d) kielezi baadaye kimehama kutoka kwenye upande wa kiarifu kama ilivyokuwa katika (25b) kwenda kwenye kiima ili kukifanya UT chenye kirejeshi kiwe karibu kabisa na kisabiki. Hivyo, kutokana na mchakato huo S1 na S2 huunganishwa kama inavyooneshwa katika MNJ wa (25e).
(25) e. Baadaye walihamia chumbani ambako mengi yalifanyika kati yao.
Hapa udondoshaji-chopezi umeifanya S2 kuwa bebwa vumishi kwa kuwa inavumisha nomino ya S1. Matokeo yake ni kuundwa kwa SC yenye muundo wa KK na KBV kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 9.
S1
KN1 KT1
N1 T1 KN2 KE1
N2 S2 E1
UT KN3 KT2
W T2 KE2
E KV
V V
ÆŸ (baadaye) walihamia chumbani ambako mengi yalifanyika kati yao
Kielelezo Na. 9: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji-chopezi
Tumeeleza hapo awali katika utangulizi wa sehemu ya (4.3.2) kwamba udondoshajichopezi wa vipashio hutumika kuunda miundo miwili ya SC za Kiswahili. Hapa msomaji anaweza kujiuliza, ikiwa ndivyo inakuaje mchakato mmoja unazalisha aina mbalimbali za SC za Kiswahili tena zenye miundo tofauti. Majibu yake yanaweza kujibiwa kwa kielelezo Na.10
Udondoshaji-chopezi
Udondoshaji
[Kipashio kinachojirudia hasa kwenye S2]
Uchopekaji
[Ili kufidia au kuziba pengo la kipashio kilichodondoshwa]
UTM UT (AMBA+R)
+Sababu +amba-ye
+Kusudi +amba-cho
+Namna +amba-po
+Wakati +amba-o
SC: KK+KBE KK+KBV
Kielelezo Na. 10: Muhtasari wa Udondoshaji-chopezi Jinsi Unavyounda SC za Kiswahili
Kielelezo Na. 10 kinaonesha kwamba SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBE na KK na KBV huundwa kwa mchakato wa udondoshaji-chopezi. Kadhalika, kinaonesha kwamba vipashio vinavyochopekwa baada ya udondoshaji ndivyo vinavyotofautisha miundo ya SC hizo.
4.3.3 Udondoshaji-chopezi Hamishi
Kupitia data za utafiti huu, imebainika kuwa udondoshaji-chopezi hamishi wa vipashio ni miongoni mwa michakato inayotumika kuunda SC za Kiswahili. Kwa mujibu wa utafiti huu, udondoshaji-chopezi hamishi ni mchakato wa kudondosha kipashio kinachojirudia katika tungo na kupachika kipashio kingine cha ufidiaji, kisha kuhamisha kipashio hicho ili kuleta ushikamani katika tungo. Tazama mfano wa (26a) kwa ufafanuzi zaidi.
(26) a. Nguo alizovaa zilimfanya aonekane kijana. (Lema, 2004: 7)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Sentensi (26a) iliyoandikwa kwa hatimlazo ni tungo iliyoshushwa hadhi kutokana na mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi uliofanyika katika tungo. Hii ina maana kwamba tungo ya (26a) katika MN, S1 na S2 zilikuwa na hadhi sawa kabla ya mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi kama inavyooneshwa katika (26b).
(26) b. i) Nguo zilimfanya aonekane kijana.
ii) Nguo alivaa.
Katika tungo ya (26b) nomino nguo inajirudia kwenye S1 na S2. Inajirudia kwa sababu nomino nguo inayozungumziwa katika S1 na S2 ni ileile. Hivyo, udondoshaji unahitajika ili kuondoa uradidi. Tazama mfano wa (26c) unavyoonesha.
(26) c. [Nguo [nguo alivaa] zilimfanya aonekane kijana.]
Katika mfano wa (26c) nguo ya S2 inaonesha imekatwa kuonesha imedondoshwa ili kuondoa uradidi. Hii ina maana kwamba sehemu ilipokuwapo nomino nguo imebaki wazi na sehemu hiyo inapaswa kuzibwa kwa kupachika kipashio kingine kitakachoziba pengo hilo. Kipashio hicho ni kiambishi rejeshi {-zo-} kama inavyooneshwa hapa chini katika mfano wa (26d).
(26) d. Nguo -zo- alivaa zilimfanya aonekane kijana.
Mfano wa (26d) kiambishi rejeshi kimekaa peke yake na kipo mbali na kisabiki chake. Hivyo, kinahitaji kuhama na kupachikwa kwenye kitenzi kilichopo karibu na kisabiki chake kama inavyoonesha katika (26e).
(26) e. Nguo zo alizovaa zilimfanya aonekane kijana.
Kutokana na uhamishaji wa kiambishi rejeshi katika S2, huifanya sentensi hiyo kushuka hadhi na kuwa bebwa, yaani (KBV) ndani ya KN1 cha S1. Hivi ndivyo, SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBV zinavyoundwa kama inavyonesha katika MNJ wa (26f).
(26) f. Nguo alizovaa zilimfanya aonekane kijana.
Tungo ya (26f) inaweza kufafanuliwa zaidi na kielelezo Na.11 kinachoonesha jinsi S2 inavyofanya kazi ya kukumusha KN1 ya S1 kama inavyooneshwa katika kielelezo Na. 11.
S1
KN1 KT1
N1 S2 T1 KN3
KN2 KT2
N2 T2 Ts T1 N3
Nguo ÆŸ alizovaa zilimfanya aonekane kijana
Kielelezo Na. 11: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji-chopezi Hamishi
Pia, tazama mfano wa (27a) kutoka maktabani kwa ufafanuzi zaidi kuhusu namna mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi unavyotumika kuunda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBV.
(27) a. Mtoto aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita. (Lema,
2004: 13)
Chanzo: Data za Maktabani (2021)
Katika mfano wa (27a) iliyoandikwa kwa hatimlazo ni tungo iliyoshushwa hadhi baada ya mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi. Hii inamaana kwamba katika MN, tungo iliyoandikwa kwa hatimlazo katika (27a) ilikuwa na hadhi sawa na hiyo ambayo haijaandikwa kwa hatimlazo kabla ya mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi kama inavyooneshwa katika (27b).
(27) b. i) Mtoto alikwenda kumuita.
ii) Mtoto alikuwa anacheza hapo nyumbani.
Katika (27b) mtoto anayezungumziwa katika S1 na S2 ni yuleyule. Kwa kuwa mtoto anayezungumziwa ni yuleyule, nomino moja hudondoshwa ili kuondoa uradidi. Aghalabu nomino inayodondoshwa ni ile ya S2 kama inavyooneshwa katika (27c).
(27) c. Mtoto [mtoto alikuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Katika (27c) nomino radidi mtoto ya S2 imekatwa kuonesha imedondoshwa. Hii hufanyika ili kuondoa uradidi na kuleta ushikamani katika tungo husika. Kutokana na udondoshaji wa nomino radidi katika S2 mahali nomino hiyo ilipokuwa panabaki wazi kama inavyooneshwa katika (27d).
(27) d. Mtoto [..alikuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Hivyo, huhitajika kupachika kipashio kingine ambacho kitaziba pengo hilo. Katika mazingira kama haya kiambishi rejeshi ndicho hupachikwa ili kuziba pengo la nomino iliyodondoshwa kama inavyooneshwa hapa chini katika (27e).
(27) e. Mtoto [-ye- alikuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Tungo ya (27e) inaonesha kiambishi {-ye-} kipo peke yake ilhali kwa kawaida katika Kiswahili kiambishi rejeshi huchopekwa kwenye kitenzi kikuu, kisaidizi au kwenye umbo maalumu la AMBA. Hivyo, kiambishi hicho huhitajika kuhama ili kiambatanishwe ndani ya kitenzi kilicho karibu na kisabiki chake. Tazama (27f) kwa ufafanuzi zaidi.
(27) f. Mtoto [ ye aliyekuwa anacheza hapo nyumbani] alikwenda kumuita.
Baada ya uhamishaji wa kiambishi rejeshi kutoka mahali kilipokuwa na kupachikwa kwenye kitenzi, hukifanya kitenzi cha kishazi hicho kuwa bebwa. Uhamishaji huo ndiyo unaokamilisha SC ya Kiswahili yenye muundo wa KK na KBV kama inavyooneshwa hapa chini katika MNJ wa (27g).
(27) g. Mtoto aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita.
Tungo ambayo huwa na kiambishi rejeshi ndiyo huitwa KBV. Kishazi hiki aghalabu hufanya kazi ya kukumusha nomino ya KK kama inavyooneshwa kwenye kielelezo Na. 12.
S1
KN1 KT1
N1 S2 T1 KN2
KN2 KT2 N2
N TS T KE
E1 E2
Mtoto ÆŸ aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita
Kielelezo Na. 12: MNJ wa SC ya Kiswahili Iliyoundwa kwa Udondoshaji-chopezi Hamishi
Mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi ambao umebainishwa jinsi unavyounda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBV, Wesana-Chomi (2017) ameuita mchakato wa urejeshaji. Kwa hakika, kuuita mchakato huu urejeshaji hasa kwa kuwa nomino radidi inageuzwa na kuwa kirejeshi kunasailika rejea data ya (26) na (27) kwa ufafanuzi zaidi. Kwa sababu, kisintaksia nomino radidi hudondoshwa ili kuondoa uradidi na kuleta ushikamani katika tungo. Baada ya udondoshaji huo, uchopekaji hufanyika ili kufidia kipashio kilichodondoshwa. Kipashio hicho huwa ni kiambishi rejeshi. Ikiwa kiambishi hicho kipo mbali na kirejelewa chake huhamishwa ili kiwe karibu kisabiki au kirejelewa chake. Maelezo kutoka data ya (26 na 27) yanadhihirisha kwamba mchakato unaotumika kuunda SC za Kiswahili zenye KK na KBV ni udondoshaji-chopezi hamishi na si urejeshaji kama ilivyokuwa ikielezwa na Wesana-Chomi (2017). Mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi unaweza kuelezwa kwa muhtasari kwa kutumia kielelezo Na. 13.
Udondoshaji-chopezi Hamishi
Udondoshaji
[Kipashio kinachojirudia hasa KN cha S2]
Uchopekaji
[Kiambishi rejeshi ili kufidia KN cha S2 kilichodondoshwa]
Uhamishaji
Kiambishi ili kiwe ndani ya kitenzi kikuu au kitenzi kisaidizi kilicho karibu na kisabiki chake. Uhamishaji huo unaweza kuwa au
Kielelezo Na. 13: Muhtasari wa Mchakato wa Udondoshaji-chopezi Hamishi
Kwa muhtsari michakato inayotumika kuunda SC za Kiswahili, data za utafiti zinaonesha kwamba mchakato wa uchopekaji hutumika kuunda SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBN. Pili, imebainika kwamba mchakato wa udondoshaji-chopezi hutumika kuunda SC zenye miundo miwili ambayo ni: KK na KBE na KK na KBV. Kuhusu mchakato huu kuunda miundo miwili tofauti, imebainika kwamba kinachofanya iwe miundo tofauti licha ya kuundwa na mchakato mmoja ni tofauti ya vipashio vinavyochopekwa mara baada ya udondoshaji. Vipashio hivyo ni UTM kama vile: ili, kwani, kwa sababu ambavyo huunda SC za Kiswahili zenye KK na KBE na viambishi rejeshi ambavyo hupachikwa kwenye umbo maalumu la AMBA kama vile {-ko, -vyo, -cho} ambavyo huunda SC zenye muundo wa KK na KBV. Vilevile, imebainika kuwa kuna SC zingine ambazo huundwa kwa mchakato wa udondoshaji-chopezi hamishi, sentensi hizi ni zile zenye muundo wa KK na KBV. Katika mchakato huu nomino radidi ambayo aghalabu huwa ni ya S2 hudondoshwa. Nomino radidi iliyodondoshwa hufidiwa kwa kupachika kiambishi rejeshi ambacho hukaa sehemu ilipokuwa nomino iliyodondoshwa. Kwa kuwa kiambishi hicho lazima kikae karibu na kisabiki chake hulazimika kuhama ili kiwe karibu na kisabiki chake.
4.4 Muhtasari
Sura hii imewasilisha na kuchambua data kuhusu michakato ya kisintaksia katika uundaji wa SC za Kiswahili kwa kuongozwa na NR ya Chomsky (1965). Uwasilishaji na uchambuzi uliofanyika katika sura hii ulilenga kujibu maswali mawili: Swali la kwanza lilikuwa: SC za Kiswahili zinaundwaje? Aidha, swali la pili lilikuwa: michakato gani ya kisintaksia inatumika kuunda SC za Kiswahili? Maswali haya yamejibiwa kama ifuatavyo. Kwa mujibu wa data za utafiti huu imebainika kuwa kuna miundo anuwai ya SC za Kiswahili kama vile: KK na KBN, KK na KBV na KK na KBE na kila muundo una namna yake ya kuundwa. Kutokana na namna hiyo ndipo tunapata miundo tofauti ya SC za Kiswahili katika MNJ. Uchambuzi wa namna SC za Kiswahili zinavyoundwa umefanywa kwa kuzingatia NR. Pia, swali la pili limejibiwa kwa kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda SC za Kiswahili ambayo ni: Uchopekaji, Udondoshaji-chopezi na udondoshaji-chopezi hamishi. Sura inayofuata inahusu muhtasari, mchango, mapendekezo na hitimisho.
SURA YA TANO
MUHTASARI, MCHANGO, MAPENDEKEZO NA HITIMISHO
5.1 Utangulizi
Sura hii imewasilisha muhtasari wa matokeo ya utafiti, mchango, mapendekezo ya tafiti fuatizi na hitimisho la jumla. Sehemu za sura hii zimewasilishwa kwa kuzingatia malengo ya utafiti huu.
5.2 Muhtasari wa Matokeo ya Utafiti
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza michakato ya kisintaksia katika uundaji wa SC za Kiswahili. Lengo hili lilitoa malengo mahususi mawili. Mosi, kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa. Pili, kubainisha michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda SC za Kiswahili.
Matokeo ya lengo la kwanza yanaonesha kwamba kila muundo wa SC ya Kiswahili una namna yake ya kuundwa kutoka katika MN kwenda MNJ. Imebainika kwamba SC zenye muundo wa KK na KBN huundwa kwa kuchopeka UT kama vile kuwa, kwamba au kama. Vilevile, imebainika kwamba viunganishi hivi vinachopekwa ili kujaliza nomino au kitenzi cha S1.
Pia, imebainika kwamba SC za Kiswahili zenye muundo wa KK na KBV ina namna mbili za uundaji wake. Mosi, KN kinachojirudia hasa kwenye S2 hudondoshwa na kupachika kipashio kingine (kiambishi rejeshi) ili kufidia pengo lililoachwa na kipashio hicho. Uundaji wa namna hii hutokea kama na kama tu kiambishi rejeshi kimechopekwa kwenye umbo AMBA na kipo karibu na kisabiki chake. Pili, kudondosha KN kinachojirudia hasa cha S2 ili kuondoa uradidi na baada ya udondoshaji huo, upachikaji wa kipashio (kiambishi rejeshi) huhitajika ili kufidia pengo lililoachwa na udondoshaji huo. Baada ya upachikaji, hatua ya uhamishaji hufanyika ili kiambishi hicho kiwe ndani ya kitenzi. Uhamishaji huu hufanyika ili kutimiza sharti la NR linalotaka kirejeshi kukaa au kuwa karibu na kisabiki chake kwenye lugha ya Kiswahili.
Kadhalika, SC zenye muundo wa KK na KBE huundwa kwa kuchopeka UTM baada ya udondoshaji au hata bila ya udondoshaji kutegemeana na tungo husika. Aghalabu viunganishi tegemezi maalumu hutangulia KBE. UTM ni kama vile: nge, ki, kama, kwa sababu, ili, na kwani.
Lengo la pili lilikuwa ni kubainisha michakato ya uundaji wa SC za Kiswahili. Matokeo yanaonesha kwamba kuna michakato mitatu ya uundaji wa SC za Kiswahili ambayo ni: Uchopekaji, udondoshaji-chopezi na udondoshaji-chopezi hamishi. Matokeo hayo yanaweza kufafanuliwa kwa kielelezo Na. 14.
Michakato ya Uundaji wa SC za Kiswahili
Uchopekaji Udondoshaji-chopezi Udondoshaji-chopezi hamishi
SC: KK+KBN KK+KBE KK+KBE KK+KBV KK+KBV
Kielelezo Na. 14: Muhtasari wa Matokeo ya Lengo la Pili
5.3 Mchango wa Utafiti
Utafiti huu umeinufaisha taaluma ya sintaksia ya Kiswahili kwa kutoa maarifa mapya juu ya SC za Kiswahili. Maarifa hayo ni pamoja na kueleza namna SC za Kiswahili zenye miundo mbalimbali zinavyoundwa. Kabla ya utafiti huu kulikuwa na wataalamu anuwai waliokuwa wameeleza namna SC za Kiswahili zinavyoundwa, mmoja wao ni Wesana-Chomi (2017). Hata hivyo, utafiti huu ulieleza jinsi maelezo ya watangulizi hao yanavyopwaya kisintaksia kama inavyoelezwa katika sehemu ya (4.2.1, 4.2.2 na 4.2.3.) na kujaliza maarifa katika kipengele hicho. Uchambuzi na ufafanuzi wote katika utafti huu ulizingatia NR ya Chomsky (1965).
Kadhalika, kwa upande wa michakato ya kisintaksia inayotumika kuunda SC za Kiswahili kabla ya utafiti huu ilikuwa imetajwa na Wesana-Chomi (keshatajwa) ambayo ni urejeshaji na ujalizaji. Utafiti huu ulisaili michakato hii kwa kutumia NR ya Chomsky (1965). Utafiti huu haukuishia kusaili, bali ulibainisha michakato mitatu ambayo ni: uchopekaji, udondoshaji-chopezi na udondoshaji-chopezi hamishi.
Pia, utafiti huu umeinufaisha taaluma ya sintaksia kwa kuchanganua SC za Kiswahili kwa kuongozwa na NR ambayo inaonesha jinsi KB kinavyobebwa ndani ya KK. KB kimeoneshwa kama kimebebwa ndani ya kingine ili kuweka wazi uamilifu wake ambao ni kukumusha au kujaliza KK. Kabla ya utafiti huu, SC za Kiswahili zilikuwa zinachanganuliwa bila kuonesha ubebwa (taz. Wesana-Chomi, 2017; Philipo na Kuyenga, 2018). Uchanganuzi ambao hauweki wazi upekee wa SC ambao ni uwepo wa sentensi mbili au zaidi, huku moja ikiwa imebebwa ndani ya nyingine na kufanya kazi ya kukumusha au kujaliza tungo nyingine.
5.4 Mapendekezo ya Tafiti Fuatizi
Utafiti huu ulichunguza michakato ya kisintaksia ya uundaji wa SC za Kiswahili pekee. Hivyo, unapendekeza tafiti zingine za kiulinganishi zifanyike kuhusu michakato ya kisintaksia ya uundaji wa SC za Kiswahili na lugha zingine za Kibantu ili kufahamu kama michakato ya uundaji wa SC ni sawa au la baina ya lugha hizo. Pia, tafiti nyingine zenye mrengo kama huu zinaweza kufanywa kwenye lugha zingine za Kibantu kwa lengo la kuchunguza namna na michakato inayotumika kuunda SC za lugha hizo ili kuongeza maarifa ya kisintaksia katika lugha za Kibantu.
5.5 Hitimisho
Lengo kuu la utafiti huu, lilikuwa kuchunguza michakato ya kisintaksia katika uundaji wa SC za Kiswahili. Lengo hili lilikuwa na malengo mahususi mawili. Mosi, kuchambua namna SC za Kiswahili zinavyoundwa. Pili, kubainisha michakato ya kisintaksia ya uundaji wa SC za Kiswahili. Kuhusu lengo la kwanza, imebainika kwamba kila muundo wa SC ya Kiswahili una namna yake ya uundwaji. Aidha, kuhusu lengo la pili, imebainika kuwa kuna michakato mitatu ya uundaji wa SC za Kiswahili ambayo ni: uchopekaji, udondoshaji-chopezi na udondoshaji-chopezi hamishi.
5.6 Muhtasari
Sura hii ilijikita katika muhtasari wa matokeo ya utafiti, mchango, mapendekezo na hitimisho. Sura hii ilieleza vipengele vyake kwa kuzingatia malengo ya utafiti. Sehemu inayofuata inajikita kubainisha marejeleo ya kazi hii pamoja na viambatisho vya utafiti huu.
MAREJELEO
Ary, D., Jacobs, L.C., Sorensen, C. na Razavieh, A. (2010) Introduction to Research in Education. Belmont: Wadsthworth Cengage Learning.
Besha, R.M. (1994) Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Bwana, J.A. (2004) Haramu. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers.
Chipalo, A.J. (2021) Mwingiliano wa Vishazi Tegemezi na Vishazi Bebwa. Journal of Linguistics and Language in Education, Juz. 15:112-130.
Chomsky, N. (1957) Syantactic Structures. Mountain: The Hague.
Chomsky, N. (1965) Aspects of the Theory of Syntax. Cambridge: Mass MIT Press.
Cresswell, J.W. (2012) Education Research: Planning and Conducting and Evaluating Quantitative and Qualitative Research. Boston: Pearson Education.
Crystal, D. (2008) A Dictionary of Linguistics and Phonetics. UK: Blackwell Publishers Ltd.
Dawson, C. (2002) Practical Research Methods: A User -friendly Guide to Mastering Research Techniques and Project. Oxford: How to Book Ltd.
Habwe, J. na Karanja, P. (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Hudson, S. (1971) A Theory of Syntax for Systematic Functional Linguistics. Nertherlands: John Benjamins Publishing Company.
Glaser, B.G. na Strauss, A.L. (1967) The Discovery of Grounded Theory: Strategies for Qualitative Research. New York: Aldine de Gruyter
Jacobsen, B. (1977) Transformation of Generative Grammar. New York: North- Holland Publishing.
Jerono, P. (2003) Kishazi Huru Arifu cha Kiswahili: Mtazamo wa X-bar. Tasnifu ya Umahiri (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Nairobi, Nairobi.
Katz, J.J. na Fodor, J.A. (1963) The Structure of a Semantic Theory. Language, Vol. 39, No. 2. (Apr-Jun, 1963), pp. 170-210.
Kombe, L.E. (2018) “Uambatanishaji wa Vishazi katika Lugha ya Kiswahili: Uchunguzi wa Madai ya De Vos na Riedel (2017)”. Kioo cha Lugha, Juz. 4: 153-164.
Kombe, L.E. (2019) Uchambuzi wa Sintaksia ya Uambatanishaji katika Lugha ya Kiswahili. Tasnifu ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.
Kombo, D.K. & Tromp, D. I. (2006) Proposal and Thesis Writing: An Introduction. Nairobi: Paulines Publications Africa.
Kothari, C.R. (2009) Research Methodology: Methods and Techniques. New Delhi: New Age International (P). Limited Publisher.
Kortmann, B. (1997) Adverbial Subordination. A Typologyn and History of Adverbial Subordinators Based on European Languages. New York: Mourton da Gruyter.
Mligo, E.S. (2009) Jifunze Utafiti: Mwongozo Kuhusu Utafiti na Uandishi wa Ripoti yenye Mantiki. Dar es Salaam: Ecumenical Gathering.
Lema, E. (2004) Mwendo. Dar es Salaam: E&D Puplishers.
Longhorn, (2011) Kamusi ya Karne ya 21. Nairobi: Longhorn.
Massamba, D.P.B. (2004) Kamusi ya Falsafa na Isimu. Dar es Salaam: TUKI.
Massamba, M.P.B, Kihore, Y.M. na Hokororo, J.I. (1999) Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. (SAMAKISA). Dar es Salaam: TUKI.
Matei, A.K. (2008) Darubini ya Sarufi: Ufafanuzi Kamili wa Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Matinde, R.S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Education Publishers.
Mekacha, R.D.K. (1987) Tungo Rejeshi katika Kiswahili. Jarida la Mulika, Juz. 19: 83-91.
Meyer, C. (1996) “Coordinate Structures in English. World Englishes, Juz. 15: 11-27.
Mlacha, S.A.K. (1991) Linguistics Study of the Novel. Berln: Verlag Schreiber Publishers.
Mulokozi, M.M. (1983) Utafiti wa Fasihi Simulizi. (Muhadhara). Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Obuchi, S. M. na Mukhwana, A. (2015) Muundo wa Kiswahili: Ngazi na Vipengele. Nairobi: The Jomo Kenyatta Foundation.
Oladipo, R., Ikamari, L., Barasa, L. na Kiplang’at, J. (2015) General Research Methods. Nairobi: Oxfoward University Press.
Philipo, Z.T. & Kuyenga, F.E. (2017) Sintaksia ya Kiswahili: Nadharia ya Kisintaksia na Uchanganuzi wa Kiswahili. Dar es salaam: Karljamer Publishers Limited.
Ponera, A. S. (2019) Misingi ya Utafiti wa Kitamuli na Uandishi wa Tasnifu. Dodoma: Central Tangayika Press.
Radford, A. (1997) Syntactic Thoery and the Structure of English: A Minimalist Approach. Cambridge: Cambridge University Press.
Saluhaya, C.M. (2016) Nadharia ya Lugha Kidato cha Tano, Sita na Elimu ya Juu. Dar es Salaam: Ahmaddiyya Press.
Tallerman, M. (2011) Understanding Syntax. New Castle University: Hodder Education.
Tavakoli, H. (2012) A Dictionary of Research Methodology and Statistics in Applied Linguistics. Tehran: Rahnama Press.
TUKI (2013) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Oxford University Press.
Wamitila, K.W. (2016) Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide~Muwa.
Wesana-Chomi, E. (2017) Kitangulizi cha Muundo Viambajengo wa Sentensi za Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Yogesh, K.S. (2006) Fundamentals of Research Methodology and Statistics. New Delh: New Age International Ltd.
VIAMBATISHO
KIAMBATISHO NA. 1
Data za Utafiti za Sentensi Changamani
A. Data Kutoka Riwaya ya Haramu
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Rejeshi
Alikuwa amepona kabisa michubuko na majeraha mengine aliyoyapata kwenye ajali.
Ilikuwa ni sera ya ile hospitali kuwapima wagonjwa wote wanaolazwa kwa zaidi ya wiki moja.
Kwa hakika alikuwa mtoto mzuri ambaye alimvutia kila mtu kumbeba.
Mtoto alitabasamu alipomwona nesi akimtazama.
Hakutaka upweke ambao kwa bahati mbaya sana alijikuta nao.
Lakini hicho sicho kilichomtatiza yule nesi.
Kilichomsumbua ni ukimya uliotanda baada ya ajali.
Mtoto alikuwa ameletwa hospitali na msamaria mwema aliyesema amemwokota kwenye ajali ya barabarani huko Machinjioni.
Hata hivyo, hakuna hata mmoja aliyejitokeza kuulizia mtoto wala habari zake.
Ilitangazwa kuwa mzazi au mtu yeyote aliyepotelewa na mtoto wa kike mwenye umri wa kati ya mwaka mmoja na nusu na miaka miwili afike hospitalini au aende kituo chochote cha cha polisi.
Hakuna mtu yeyote aliyejitokeza.
Alionekana kama aliyeelewa swali aliloulizwa na yule nesi.
Alitabasamu mithili ya mtu ajuae jibu.
Jibu la kusikitisha lenye maelezo marefu ashindwalo kulitoa.
Je kama hakuna mtu atakayejitokeza kukuulizia mtoto mzuri itakuwaje?
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Nomino
Ilitangazwa kuwa mzazi au mtu yeyote aliyepotelewa na mtoto wa kike mwenye umri wa kati ya mwaka mmoja na nusu na miaka miwili afike hospitalini au aende kituo chochote cha polisi.
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Kielezi
Yule nesi alimwuliza yule mtoto kama vile alitarajia kupatiwa jibu.
B. Data kutoka Riwaya ya Mwendo
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Rejeshi
Walianza kuwa marafiki tangu walipokuwa darasa la tano.
Hamiata ni Mzaramo aliyezaliwa na kukulia hapa hapa Dar es Salaam.
Alilia tu alipoumia sana.
Na yeye anakaa tu anafurahia ninavyoaibika.
Kipindi kilipokwisha baada tu ya mwalimu kutoka nje, Hamiata alimfuata Felisia.
Akajaribu kumfariji rafiki yake kwa mkasa wowote ule uliompata.
Macho yakaonekana kama bakuli lililojaa maji.
Lakini amwambie nani kuhusu maumivu anayoyapata kwa sababu ya rafiki yake?
Basi kama ni hilo Felisia analotaka.
Kwani kutatokea nini kama Felisia asipokuwa rafiki yake.
Halafu swaiba na Pendo wanaoishi wote Kinondoni jirani kabisa na yeye.
Walishakubaliana kwamba ni lazima kila mmoja wao afahamu mwenzake anachokifanya, sasa jambo gani la ajabu limetokea?
Hamiata alisimama palepale aliposimama.
Wanafunzi kadhaa waliokuwa bado hawajaingia darasani walishangaa na kuulizana ni kitu gani kilikuwa kinamliza Hamiata.
Saa kumi, vipindi vilipokwisha, Hamiata aliondoka peke yake akaenda nyumbani.
Siku iliyofuata Felisia hakufika shule.
Sura yake ilikuwa giza kama lile linaloletwa na mawingu wakati wa masika kabla ya mvua.
Alihisi kuna jambo linatokea kati ya hao wanafunzi wawili.
Hakuna hata mwanafunzi aliyeinua macho kumtazama mwalimu.
Mwalimu alikuwa ameongozwa na mwanafunzi wa darasa la nne anayeishi karibu na Felisia.
Niliondoka vita ilipoanza.
Aliweka karibu na pale mwalimu alipokuwa amesimama.
Mzee Maji alivaa suruali na jinzi na shati la mikono mirefu la bluu lililombana kidogo.
Nguo alizovaa zilimfanya aonekane kijana.
Mzee Maji alifanya kazi ya ulinzi wa usiku katika duka moja la Mhindi lililopo babrabara ya Mosque.
Hakuna aliyeshangaa mwalimu aliposema tena kwamba Felisia hakufika shule.
Hilo halikuwa jambo alilotarajia.
Hakuweza kufahamu mara moja ni nini kilichomfanya Felisia afanane na mama yake vile.
Hakuna mtoto wa Kimakonde asiyechezwa ngoma.
Kila mtu ana jadi yake inayomtofautisha na mwingine.
Alijua mara mmoja kwamba ameuliza swali ambalo halikuwapendeza.
Niliondoka nikafata wazazi wangu waliokuwa huko Tanga pamoja na mdogo wangu.
Aliwaambia jinsi alivyofurahi na kuwafahamu na kuwa anatumaini kwamba Felisia atarudi shule.
Mwalimu alimpenda kwa bidii aliyoweka katika masomo yake.
Mwalimu Anastasia alimueleza kisa kilivyokuwa.
Jana yake alikuwa amesoma gazeti la Daily News kwamba huko Moshi vijijini kuna msichana wa darasa la sita aliyepelekwa hospitali akiwa amezimia kwa sababu ya kukosa damu.
Wazazi pamoja na wale waliomtahiri walijaribu kumuwekea dawa za kienyeji lakini hazikufaa kitu.
Mwenzake wa ukoo mmoja ambaye walikuwa watahiriwe pamoja na ambaye alitoroka usiku wa kuamkia siku ya kutahiriwa na kukimbilia kanisani ndiye aliyetoa habari kwamba mwenzake anachungulia kaburi.
Habari hizo alipata kutoka kwa mdogo wake mwenye umri wa miaka kumi na ambaye alifahamu mahali dada yake alipojificha.
Alianza kukerwa na tabia ya mwalimu huyu ya kumletea kesi ambazo hazimhusu.
Alipomsomea kesi hii na yeye alisikitika.
Huwezi piga vita jambo usilolielewa undani wake, ujue zuri la kuendeleza na baya la kuteketeza kwa moto mkali.
We mwenyewe unajua tunavyogongana vichwa hapa tukijiuliza sheria inavyosema katika mambo mengine.
Kwani kinachokataza sheria ya kutotahiri wasichana iwepo ni nini?
Sio sisi watu wazima tunaowatahiri?
Sema kinachotakiwa kufanya.
Huyo mtoto asifanyiwe anachokwenda kufanyiwa.
Jenga hoja inayoonesha mazuri au mabaya, yanayofaa na yasiyofaa, kama tohara kwa mfano.
Halafu weka mikakati ya vita dhidi ya yale yasiyofaa.
Walipofika nyumbani kwa Mzee Maji walimkuta anaongea kwa jirani.
Mtoto aliyekuwa anacheza hapo nyumbani alikwenda kumuita.
Huyo mnayemtafuta alijibu Mzee Maji.
Ilielekea ulikuwa wimbo wa ngoma, kwani kulikuwa na sehemu alizotilia mkazo na kutingisha kichwa.
Alipowatazama, macho yake yalionekana makali.
Mke wake alipomwona alimuambia.
Sababu ambazo sio za msingi kama ngoma haziwezi kukubalika.
Asipofika shule wiki hii nzima atakuwa amejifukuza.
Alipotoka kwenda chooni, alijifunika kanga kila mahali ili mwili wake usionekane.
Hamiata alimwambia mwenzake walipoonana.
Hamiata alimletea mwenzake madaftari ya masomo yote kila walipoachana.
Felisia alinakili kila muhtasari wa masomo yaliyofundishwa siku hiyo na kuanza kusoma.
Unasikia wanafunzi wengine wanavyokucheka.
Nilitamani ardhi ipasuke niingie ndani wakati nilipoona damu.
Nilishtuka ajabu niliposhindwa kujizuia.
Niliposhindwa kabisa niliogopa kweli.
He! mambo yalivyochachamaa ikabidi niende.
Natafuta nilipojikata sioni.
Nilikwenda nikafua gauni pale palipokuwa na damu.
Alilala kwenye chumba alimokuwa analala Joji.
Mtoto huyo jina lake Mene, alikuwa saa zote anacheza na rafiki zake aliowapata siku hiyohiyo alipofika.
Upo wakati alipomuacha asome.
Mambo ambayo asingetaja kabisa mbele yake wakati uliopita aliyaongea waziwazi tu.
Felisia alijiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
Aliwaonesha njia wakati walipokuja katika dunia ya watu na kuzurura katika mbuga na milima wakitafuta mahali pa kukaa.
Siku moja mwanamke huyu aliyekuwa mkubwa kuliko vitu vyote na ambaye aliwafahamu mizimu, kwani aliwaonesha njia wakati walipokuwa wanazurura mbugani wakitafuta mahali pa kukaa, alimchukua hadi msituni.
Kata tawi lake kubwa, unywe maji yatakayotoka.
Naishi katika giza nene ambamo mwanga umefichwa kama siri nene katika pepo zangu.
Ndani ya mti huu, ninamoishi mimi mzimu wako kuna wimbo.
Halafu nitakuonesha kifo kinachozidi upofu wa giza nene.
Wamakonde wote wanatokana na huyu mwanamke aliyekuwa mkubwa kuliko vitu vyote.
Na ndivyo hivyo iliyokuwa Mmakonde kuanza kuchonga mpingo akitafuta wimbo.
Mama Magdalena alipomaliza hadithi alikaa kimya.
Felisia aliita kwa hamu alipomuona tena rafiki yake baada ya siku tatu.
Hamiata alisema akiwa anamuigiza mwalimu anavyoongea wakati anapoona mwanafunzi wa kike anajilegeza au kuzubaa.
Kasema nikifika Mtwara tu, shangazi atanivisha shanga nyeupe alizotunga yeye mwenyewe.
Walipofika mwanafunzi alisema, kwao ni pale.
Halafu kuna wanafunzi waliosoma mambo hayo gazetini wakati wanaletwa shule na wazazi wao.
Furaha yao ikawa kama imeingiliwa na jambo geni lisilotakiwa kuingizwa katika uhusiano wao.
Baadaye Hamiata alitoa barua iliyokuwa imekunjwa hadi ikawa nyembamba kabisa na kufichwa katika mkunjo wa sketi kiunoni mwake.
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Nomino
Rafiki zake waliipenda hali hii na walimtangaza kwamba yeye ni chapa nguvu.
Wenzake wengine shuleni walisema kwamba Felisia ni kama swala kwa jinsi alivyoweza kukimbia chapuchapu bila kuchelewa wakati akishtushwa au kama amehisi hatari.
Hakutaka wanafunzi wenzake wajue kwamba anaumia.
Walikwisha kubaliana kwamba ni lazima kila mmoja wao afahamu mwenzake anachofanya, sasa jambo gani la ajabu limetokea.
Hakuna aliyeshangaa mwalimu aliposema tena kwamba Felisia hakufika shule.
Watu walisema kwamba Wamakonde ni wacheza sindimba, Wamakonde wachonga vinyago.
Tunatarajia kwamba atafaulu vizuri na kwenda sekondari bila shida yoyote.
Alijua mara moja kwamba ameuliza swali ambalo halikuwapendeza.
Mwalimu alianza kuona kwamba hatafika popote akizungumzia namna hii.
Aliwaambia jinsi alivyofurahi kuwafahamu na kuwa anatumaini kwamba Felisia atarudi shule.
Jana alikuwa amesoma katika gazeti la Daily News kwamba huko Moshi vijijini kuna msichana wa darasa la sita alipelekwa hospitali akiwa amezimia kwa sababu ya kukosa damu.
Mtoto huyu mdogo alishaingiwa na woga mkubwa kwamba zamu yake ya kufa haikuwa mbali.
Shida ni kwamba hatuelewi hizi mila vizuri.
Baada ya kusalimiana tu aliwaambia kwamba Mama Magdalena amekwenda kuwaona ndugu huko kurasini kuwapa taarifa za mwali.
Sisi tunataka kufahamu kama mtamruhusu Felisia kufanya mtihani wa darasa la saba mwezi wa sita.
Mzee Maji, labda ungejua tu kwamba kuna sheria inayosema kwamba mtoto hawezi kuondolewa shule bila sababu na katika muda maalumu.
Sababu ambazo sio za msingi kama ngoma haziwezi kukubalika.
Nakuomba umuambie Felisia kwamba asipofika shuke wiki hii nzima atakuwa amejifukuza.
Siku ya kwanza, Hamiata alikuwa na wasiwasi kwamba hataweza kumuona rafiki yake.
Simuambii mtu ngo kwamba tunaonana.
Yeye alikwisha ahidi kwamba hiyo itakuwa kazi yake ili rafiki yake asibaki nyuma kimasomo.
Baba alimwambia kwamba nimekwenda Kurasini.
Ulijuaje kwamba hicho kitu kimetokea?
Felisia alimuona mama yake kama kabadilika.
Alihisi kwamba mama yake alimpenda zaidi kuliko kawaida.
Alikuwa ameanza kuwa na wasiwasi kwamba rafiki yake amemsahau.
Alijua kwamba Hamiata hakuleta chokoleti kwani angekuwa amebeba kifurushi, angalau kidogo.
Mama kaniambia kwamba mtoto wa kike akishapata matiti ni kwamba amekua.
Alifikiria kwamba rafiki yake amemuambukiza ugonjwa wake.
Lakini nilimuambia mama kwamba mimi sitaki kuwa mwali.
Mama kaniambia kwamba kabla sijawa mkubwa ni lazima nifundishwe.
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Kielezi
Yeye alizaliwa Tanga wakati baba yake akiwa mkata katani katika shamba la mkonge la mwera huko Amboni.
Siku moja Felisia alifika shuleni akiwa hana furaha.
Jambo hili lilikuwa la ajabu kwa sababu kila akigombana na wavulana hasa wale waliotaka kuonesha ubabe wao, Felisia anawachapa vizuri.
Alikuwa anatafuta maneno mazuri ili mwalimu Nyoni ampe ruhusa.
Hamiata alinuna kabisa kwani Felisia alikuwa amemuaibisha.
Anastasia aliuliza kama vile hakusikia.
Alionekana kama vile ana mwanya.
Mzee Maji alionekana kama vile anawaza sana.
Tukishamcheza ngoma atarudi.
Mwalimu Anastasia aliamua kuongea na mwalimu mkuu ili kusisitiza uzito wa jambo hili.
Ungetaka tuende lini tukawaone hao wazee?
Ilielekea ulikuwa wimbo wa ngoma, kwani kulikuwa na sehemu alizotilia mkazo na kutingisha mwili.
Alipotoka kwenda chooni, alijifunika kanga kila mahali ili mwili wake usionekane.
Asubuhi na mapema Hamiata alipita daftari zake ili aende nazo shule.
Mi nakwambia ingekuwa niko shuleni ningekufa kabisa.
Mama aliongea na Felisia kama vile ni mtu mzima.
Lakini alisikiliza, kwani sauti ya mama yake ilimfanya asikilize.
Mizimu walimheshimu, kwani aliwaonesha njia wakati walipokuja katika dunia ya watu na kuzurura katika mbuga na milima wakitafuta mahali pa kukaa.
Mtama ulizaa hata ukainama.
Alizaa watoto wengine wengi kwani mizimu walimpenda.
Aliuweka mpingo huo wenye umbo la mwanamke katika kizingiti cha mlango wake ili asisumbuliwe na mizimu wasiokuwa na mahali pa kukaa.
Tena aliuweka ndani ya nyumba yake ili apate baraka ya watoto wengi.
Alivaa mwanamke wa Kimakonde, ili ajae uzuri.
Bila shaka anatafuta Mmkonde aje naye ili aongee Kimakonde na baba.
Mama Felisia alisimama wima kama vile kapigwa na radi.
Alisema ni vizuri kwa sababu eti nitakapokua zaidi nitaweza kupata watoto.
Mi nimeskia walimu wakiongea.
C: Data kutoka Kwenye gazeti la Mwananchi
Nukuu ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Rejeshi
Mmoja niliyekuwa namdai alinijibu: Sorry kaka nimekwenda Morogoro kikazi
Nikamkumbuka janja aliyeiba njiwa bandani wa rafiki yetu usiku.
kila alipokanyaga hatu moja kutoka bandani aliongeza alama ya kidole cha sita kwenye nyayo kwa kutumia kidole cha shahada.
Tukaenda kumkwida dogo aliyekuwa na upekee wa vidole sita kila mguu.
Hata mtoto hulala anapoimbiwa muziki wenya ladha.
Hatofautiani na jini tunayemwona kwenye filamu za Bongo ambaye kabla hajaingia kufanya madhara anavua viatu na kupiga hodi.
Mdokozi anapojiita mwizi anajiongopea tu kama mpagazi kujiita mfanyabiashara.
Ni sawa unapomwona mtu akijiimbia akamwita msanii.
Na yule bibi anayeimba wakati akiosha vyombo tumuiteje?
Ieleweke maneno yanaweza kuwa utenzi unaoweza kuwa wimbo ambao unaweza kuwa sehemu ya muziki.
Kuna maandiko ambayo ndiyo yanayobeba ujumbe gani ambayo ndiyo utenzi na mkangosio.
Ikayaonesha mapaja yaliyojaa vyema kwenye miguu yake mirefu na yenye mvuto.
Ikafanya nguo aliyoivaa inyooke kwenye sehemu ya tumbo na kuishia kwenye sehemu ya nyonga zilizotanuka.
Allaini alijitahidi kujenga utulivu alipokaa.
Wakiwa katika meza ya chakula wakiangaliana ana kwa ana huku sahani yenye chakula ikiwa mbele yake na kipande kikubwa cha pizza kilichokaa pembetatu kikiwamo.
Akatafuna taratibu kipande alichokimega.
Alijua nipo na Chief Engineer niliyejuana naye baada ya kuja nyumbani kufanya uchunguzi wa wizi na hivi niko naye tena nikiwa nimemkaribisha kinywaji na chakula, anaweza kuniua.
Niko Smarti kama Marjeib anavyojiona yuko smati.
Nishafuta picha tulizoonekana tuki-kiss pamoja.
Kwa nini unachukua risk kwa ajili ya mtu asiyefanana na mumeo kimapato.
Siku zote mwanaume bora kwa mwanamke ni yule anayezifahamu hisia zake.
Haya ndiyo maisha tunayoishi nayo wanawake.
Unaonesha ni mtu unayejali.
Hisia zako nilizigundua mara tu nilivyokuona siku ya kwanza tulipoonana.
Nikajua ni mtu unayejali.
Kadiri muda ulivyoendelea ndivyo shaka hiyo alivyoiondoa.
Baadaye wakahamia chumbani ambako mengi yalifanyika kati yao.
Una muda gani tokea ulivyoanza kumjua Robert Sakaya?
Lilikuwa swali ambalo Zenaba hakulitarajia.
Huoni unakokwenda hakuhusiani na swali nililokuuliza?
Ninamjua zaidi ya miaka mitano iliyopita.
Ninachojaribu kufanya ni kuhakikisha nyaraka za Marjeib zinarudi.
Zenaba alijibu kwa sauti iliyopwaya.
Nadhani utapata majibu yote ya maswali unayotaka kuuliza.
Sitaweza kukabiliana na mtu ambaye namchukulia mkewe kisha nikazungumza naye kana kwamba hakuna kinachotokea kati yetu.
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Nomino
Inaeleweka kuwa fundi anaunda mtungi kwa wiki nzima.
Uongo ni fani kama wizi, umbeya au usengenyaji.
Akasaini kwenye kitabu cha wageni kwamba alikwenda kutazama kumbukumbu za kale.
Inanifanya niamini kuwa jini huyu si katili.
Kwa hiyo, utagundua kuwa muziki ni mchnganyiko mkubwa sana.
Aliamua kuanzisha mapema taswira ya uwepo wao hapo kuwa ni mapenzi zaidi.
Lakini alikwambia kama atakuwa na safari ya huko?
Mume wangu sijamwambia kama uliwahi kuja.
Zenaba alijibu kama sehemu ya kumfurahisha Allain ajiskie kuwa huru.
Data za Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Kielezi
Huyu tukimkamata tunamwadhibu ili kumuopoa na pepo lake.
Utapenda kinywaji gani wakati nikikupashia pizza?
Nitafurahi ukiniletea bia.
Unamaana gani ukisema hivyo?
Kwa nini unachukua risk kwa ajili ya mtu asiyefanana na mumeo kimapato?
Lakini hazitaweza kurudi endapo nitakosa ushirikiano wako.
D. Data za Utafiti kutoka gazeti la Nipashe
Data za Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Rejeshi
Alitokea kumpenda tangu siku ile alipomwokoa kwa jamaa anayetaka kumbaka.
Kila mmoja alimueleza mwenzake kilichomsibu moyoni.
Kwa sababu anayekataa kila barua inayoletwa hapo ndiye aliyeleta barua hiyo.
Kwa hiyo zile siku mbili walizotakiwa kuhama zilifutika.
Wale waliokuwa wakiionea familia hiyo kwa sababu ya kulipa kisasi waliufyata mkia.
Hapa kilichotakiwa ni kwamba mimi nife nikiwa ndani ya nyumba.
Walichunguza ni nyumba tu.
Mzee Mataulo, mwenyekiti wa kijiji hicho alikuwa mmoja wa viongozi waliotuhumiwa na rushwa, upendeleo na mengi yanayofanana na hayo.
Akaambiwa akaimu hadi hapo uchaguzi utakapofanyika baada ya miezi mitatu.
Waliokuwa wanadhihaki na kumuonea Mzee Ngoma kwa ajili ya binti yake, walianza kujipendekeza.
Ilikuwa ni mara ya kwanza Bishada kuondoka kwenye kijiji chao alichozaliwa kwenda mjini.
Alivyokuwa akikataa wanaume kijijini hapo.
Uhasama mkubwa uliozuka kiasi cha kuamuru kutimuliwa.
Alivyotaka kubakwa na kuokolewa na mtu asiyemfahamu.
Ndiye anayetarajia kumuoa.
Akaja kuwa msichana mzuri aliyeumbwa.
Mzee Ngoma na mkewe Fatuma wanapata mtoto wa kike Bishada ambaye anaondokea kuwa tishio kwenye kijiji cha Mtakuja kwa urembo wake.
Fuatilia kisa hiki ambacho kitakuacha mdomo wazi.
Spika Job Ndugai amesema Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itaanza kuwaita na kuwahoji watu wanaolipaka Bunge matope.
Amesema watu hao wanajumuisha wanaosambaza taarifa alizoziita za upotoshaji.
Kauli hiyo ya Spika Ndugai ni majibu kwa mwongozo ulioombwa na mbunge wa Mbagala (CCM).
Abdala Chaurembo aliyelalamika kuchafuliwa na chombo kimoja cha habari kuhusu mgawanyo wa mali za lililokuwa jiji la Dar es Salaam.
Kumbe lengo lao ni kumfatilia mtu mmoja tu wanayemtaka wao.
Katika maelezo yake Spika Ndugai, alisema hakuna anayelidai Bunge.
Hakuna anayedai.
Kwa nini mnaamini vitu ambavyo havipo?
Miongoni mwa waliotajwa katika tangazo hilo linalolalamikiwa na Spika Ndugai, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Mahakama kuu imeamuru Sh. Milioni 350 walizolipa faini Mbowe na wenzake zirejeshwe.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na mahakama hiyo na Jaji Ilvin Mgeta, aliyekuwa akisikiliza rufani hiyo.
Hakuna shahidi aliyesema nini kilitokea Mwananyamala na kwamba tukio lilitokea muda nrefu.
Mashahidi hawakwenda kutoa taarifa popote wakati tukio lilipotokea.
Tofauti na wakili wa walalamikaji Peter Kibatala alivyodai kuwa hukumu iliandikwa kwa kurasa chache.
Shahidi wa kwanza alieleza mahakama alivyokuwa anawasiliana na Dotto ambaye alikuwa eneo la mkutano.
Kwa hiyo, hakuna chochote kilichopungua upande wa Jamhuri kwa sababu Dotto alikuwepo eneo la tukio tu.
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Nomino
Alijua kabisa kuwa hiyo itakuwa barua ya mwisho.
Kijiji kizima kilijua kuwa Bishada amepata mchumba.
Kuna wengine walidhani kuwa Denny bado anaishi kwenye nyumba ya mjomba wake.
Alibainisha kuwa tangazo hilo linalosambaa katika mitandao ya kijamii ni la mwaka 2018.
Alisema amebaini jeshi la polisi lilichochea vurugu kwa wananchi hao baada ya kupiga mabomu ya machozi na kusababisha mitafaruku.
Alisema Mbowe alikuwa anatoa hoja na malalamiko yake kwamba chama chake na wanachama wake wananyanyasika namana gani.
Msemo alidai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ilizingatia Sheria ikiwamo kuchambua ushahidi wa pande zote mbili.
Aliendelea kujibu hoja za rufani kwamba kuainisha ushahidi inategemea na mwandishi wa hukumu.
Alidai kuwa shahidi wa kwanza alieleza mahakamani alivyokuwa akiwasiliana na Dotto ambaye alikuwa eneo la mkutano.
Awali Kibatala alidai mahakamani hapo kwamba mahakama ya Kisutu ilikosea kuwapa adhabu Mbowe na wenzake aliiomba Mahakama Kuu itengue hukumu hiyo.
Data ya Sentensi Changamani zenye Kishazi Kikuu na Kishazi Bebwa Kielezi
Denny alimwandikia barua na kumwambia kwa sababu hatokuwa na mshenga.
Ni kwa sababu ilikuwa bado siku mbili tu wafurushwe kwenye kijiji hicho kama binti yao Bishada atakuwa hajaolewa au kuchumbiwa.
Wale waliokuwa wakiionea familia hiyo kwa sababu ya kulipa kisasi waliufyata mkia.
Mimi ningeumia sana ungeumia wewe au mashamba ya mjomba wangu.
Waliokuwa wanadhihaki na kumuonea Mzee Ngoma kwa ajili ya binti yake, walianza kujipendekeza.
Hata wewe mwenyewe usingekubali kwenda.
KIAMBATISHO NA. 2
VIBALI VYA UTAFITI
0 Comments