Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Sababu Mwamposa kujaza Uwanja wa Mkapa Dar


Umati wa watu uliojitokeza kwenye usiku wa mkesha wa Mtume Boniface Mwamposa wa kanisa la Arise and shine katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Ijumaa usiku. Na Mpiga Picha Maalum

Dar es Salaam. Kama ulidhani mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga ndizo pekee zinazojaza Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, utakuwa unajidanganya.

Baadhi ya makongamano ya dini yamethibitisha kuujaza uwanja huo hadi pomoni, hali ambayo wataalamu wa masuala ya kijamii wamesema watu wanajazana kwa sababu tano tofauti, wakiwemo wenye matatizo, wanaoamini na wanao kwenda kushuhudia na na kuhoji kinachofanyika.

Akizungumzia umati huo, mtaalamu wa saikolojia, Yisambi Mbuwi alisema watu waliokwenda katika mkesha ule wamegawanyika katika makundi tofauti, akisema miongoni mwao huenda wachache wakawa na hofu ya Mungu.

Mbuwi alisema kuna watu wamekwenda kwa kushawishiwa na marafiki zao au kufuata mkumbo, kusindikiza ndugu, wengine kwa kufuata miujiza au kumpeleka mgonjwa huku baadhi wamehudhuria kwa ajili ya kwenda kuangalia kinachofanyika na inawezekana miongoni mwao wakawa wapinzani wa Mwamposa.

“Kuna kundi limeenda kwa sababu linamwamini Mwamposa, wengine kwa sababu ya uhitaji kutokana na changamoto zinazowakabili, wengine ni wale waliokosa sehemu za kwenda wameamua kwenda ili kuonana na marafiki zao. Kundi jingine ni lile wanalokwenda kwa ajili ya ibada, kwa sababu Mwamposa yupo.

“Kisaikolojia maana yake ni mwitikio wa jamii, katika kundi la watu 10 wengine wanakuwa na mwitikio tofauti, hata kwenye miujiza baadhi wanakwenda wakiwa na sababu maalumu kama kupima imani ya mtumishi husika,” alisema Mbuwi.


Waujaza hadi nje

Juzi wafuasi wa Mtume Boniface Mwamposa waliujaza Uwanja wa Mkapa, wengine wakabaki nje.

Mwamposa, maarufu ‘Buldoza’ wa Kanisa la Arise and Shine (Inuka Uangaze), usiku wa kumkia jana aliendesha mkesha aliouita “Vuka na Chako Kabla ya Kuvuka Mwaka” ulioweka rekodi ya mahudhurio kwa kuujaza uwanja huo unaoweza kuchukua mashabiki 60,000 waliokaa, huku wengine wanaokadiriwa 20,000 wakikaa kwenye korido.

Mtume Boniface Mwamposa wa kanisa la Arise and Shine akiomba wakati wa mkesha wa ibada ya kufunga mwaka iliyofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam juzi Ijumaa usiku. Na Mpiga Picha Maalum

Kwa wapenzi wa soka, mbali na kuulinganisha umati huo na wa mashabiki katika mechi za Simba na Yanga zinapokutana au kwenye siku zake maalumu --Simba Day na Wiki ya Mwananchi, hali kama hiyo ilitokea katika mechi ya kufuzu Afcon ya Taifa Stars na Uganda, Machi 2019.

Tukio hilo lililozua gumzo katika mitandao ya kijamii, lilisababisha foleni katika barabara mbalimbali za kwenda uwanjani hapo kama vile Mandela, Kilwa na Chang’ombe kutokana na wingi wa magari, hasa daladala zilizokatisha ruti na kuamua kuelekea huko kupeleka wafuasi.

Hii ni kutokana na kuwepo maelfu ya watu wanaokwenda katika mkesha huo, tofauti ilivyozoeleka shughuli hiyo kufanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe.

Mbali na daladala, kulikuwa fursa kubwa ya kusafirisha abiria kwa bajaji na pikipiki na teksi mtandao kuelekea uwanjani, hatua ambayo ilisababisha wingi wa abiria katika vituo vya daladala na foleni barabarani.

Akizungumzia hali hiyo, Joseph Mwakalinga, dereva wa bodaboda eneo la Tabata Relini alisema, “jana (juzi) ilikuwa hekaheka, yule mwanaume (Mtume Mwamposa), alishika Jiji, maana foleni ya magari kuelekea Uwanja wa Mkapa ilikuwa balaa.

“Nimeshahudia daladala nyingine zikikatiza ruti na kwenda kwa Mkapa kwa nauli ya Sh 1,000 badala ya Sh600 kama ilivyozoeleka. Hata bodaboda tulipata riziki ya kupeleka abiria, nenda rudi za uwanja wa Mkapa hazikukauka kabisa,” alisema Mwakalinga.

Naye Hermeneglid Mfoi, dereva wa daladala inayofanya safari zake kati ya Mbagala-Ubungo Simu2000 alisema juzi ilikuwa siku ya neema kwao kwa kuwa walipata fedha nyingi kutokana na wingi wa watu, licha ya foleni iliyojitokeza mara kwa mara.

Kwa upande wake, John Joseph alisema Uwanja wa Mkapa ulifurika si kwa wakazi wa Dar es Salaam pekee, bali hata mikoa ya jirani ya Pwani na Morogoro walihudhuria mkesha huo.

Alisema kuanzia nje na ndani ya uwanja watu walikuwa wamejazana hadi kufikia juzi jioni.


Washinda uwanjani, wakesha

Watu walianza kuingia kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia juzi saa 12 asubuhi baada ya milango kufunguliwa.

Waumini waliotoka mikoani walikuwa wanaingia kwa kutumia milango ya D jirani na Uwanja wa Uhuru na wengine wakitumia mlango B jirani na ukuta wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce).

Makundi tofauti yaliendelea kuingia uwanjani hapo na ilipofika saa nne asubuhi umati ulipoongezeka, maofisa usalama wa uwanja huo waliweka utaratibu wa ukaguzi.



Maofisa hao walianza kumkagua kila anayeingia ili kuhakikisha hali ya usalama inakuwepo, lakini walionekana kuelemewa kutokana na idadi yao kuwa ndogo (wanne kwa geti moja) huku watu wakiendelea kuingia kwa wingi.

Magari aina Toyota Coaster yalionekana kushusha makundi ya watu kutoka Chalinze na Morogoro waliopokewa na kuelekezwa maeneo yaliyoandaliwa kwenye viti vya rangi ya machungwa.

Ilipofika kati ya saa nane mchana mabasi saba yaliyokodiwa ya kampuni ya Abood yaliingia uwanjani hapo na kushushusha abiria kutoka Morogoro, ambayo yaliwasubiri hadi mkesha ulipomalizika kisha kuwarudisha.

Vilevile wakazi wa Dodoma hawakuwa nyuma baada ya kukodi magari ya kampuni ya Shabiby takribani matatu yaliyowasili saa tisa alasiri uwanjani hapo.

“Makundi mengine ya watu yalionekana ndani ya maeneo ya viwanja, wakipata huduma ya udongo ulioombewa, mafuta ya upako pamoja na maji yaliyoombewa siku tatu,” alieleza mmoja wa waumini.

Kwenye saa 12 jioni, ofisa mmoja wa uwanja alisikika akisema wanafikiria kuufunga uwanja kwa sababu umati uliokuwa ndani ulikuwa unatosha juu.

Muda mfupi baadaye milango ilifungwa na kuzusha sintofahamu kwa mamia ya watu waliokuwa nje ya uwanja.

Ilipofika saa 1:00 usiku milango ilifunguliwa na kuwaruhusu waliokuwa nje kuingia ndani kisha kufungwa tena.

Hali ilibadilika baada ya kufunga milango mara ya pili kutokana na umati wa nje kulazimisha kutaka kuingia ndani.

Umati uliokuwa mlango D ulifanikiwa kusukuma lango na kuingia na geti, jambo lililosababisha watu kulaliana.

Hata hivyo, askari wa Suma- JKT na wale wa kutuliza ghasia (FFU) na wahudumu wa kanisa hilo walifanikiwa kuwaokoa bila madhara makubwa.

Muda mfupi baadaye geti lilifungwa kutokana na umati mkubwa na msongamano wa watu nje ya uwanja. Baadhi ya watu walizunguka kwa kutumia geti la Uwanja wa Uhuru lililokuwa na mkesha mwingine wa Kongamano la Usiku wa Sifa lililoandaliwa na Kanisa Katoliki.


Baada ya saa mbili usiku milango ilifungwa, huku uwanja ikionekana kufurika na saa tano usiku Mwamposa alipanda madhabahuni na umati uliokuwepo uwanjani hapo ulilipuka shangwe.

Katika mahubiri yake, aliuambia umati huo kwamba ilikuwa “siku muhimu ya kukanyaga mafuta ya upako kwa ajili ya kutembea na ushindi kwa mwaka ujao.”

Via mwananchi

Post a Comment

0 Comments