Hasira za China kwa uchokozi mpya wa Donald Trump
Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ameikasirisha mno China kwa kitendo chake kisicho cha kidiplomasia cha kuzungumza kwa simu na rais wa kisiwa cha Taiwan ambacho China inakihesabu kuwa ni sehemu isiyotenganishika na nchi hiyo.
Televisheni ya CNN ya nchini Marekani imeripoti kuwa, Donald Trump amekiuka ada ya marais wote waliomtangulia wa Marekani kwa hatua yake hiyo isiyotarajiwa ya kuzungumza kwa simu na Bi Tsai Ing-wen, rais wa serikali ya Taiwan. Karibuni hivi Donald Trump ataingia madarakani akiwa rais wa 45 wa Marekani, na tayari ameshavunja ada ya marais wote wa Marekani ambao walikuwa wanakwepa kuzungumza na marais wa Taiwan ili kuepusha hasira cha China.
Ukweli wa mambo ni kuwa tangu mwanzoni mwa miaka ya muongo wa 70 wa karne ya 20, Marekani iliitambua haki ya kujitawala ardhi ya China moja, mji mkuu wake ukiwa ni Beijing, ingawa hata hivyo imekuwa na uhusiano usio rasmi na Taiwan katika muda wote huo.
Kwa kweli Marekani imekubali kuwa kisiwa chenye ukubwa wa kilomita mraba 36 elfu cha Taiwan ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya China na inakiri pia kuwa, uingiliaji wowote ule wa kigeni katika masuala ya Taiwan ni sawa na kuingilia mambo ya ndani ya China. Hata hivyo, inaonekana Donald Trump amedharau makubaliano yote hayo na ameamua kuzungumza kwa njia ya simu na rais wa serikali ya kisiwa cha Taiwan, Bi Tsai Ing-wen kinyume na taratibu za marais waliomtangulia.
Ni jambo lililo wazi kuwa, kama katika mazungumzo hayo ya simu, Trump alizungumza na rais wa serikali ya Taiwan uhusiano wa kisasa na kiusalama baina ya pande hizo mbili na kama ana nia ya kuendeleza uhusiano wa kiusalama baina ya Marekani na Taiwan katika wakati na mazingira maalumu, basi jambo hilo litakuwa ni sawa na kuvunja makubaliano yote yaliyofikiwa huko nyuma kati ya China na Marekani.
Tabán inabidi kugusia pia nukta hii muhimu kwamba, miaka yote hii Marekani imekuwa ikipanua sana wigo wa uhusiano wake na Taiwan, lakini hadi sasa China haijalihesabu jambo hilo kuwa ni uingiliaji wa haki ya kujitawala ya nchi hiyo. Pamoja na hayo, hadi hivi sasa, Marekani imeshindwa kuiuzia Taiwan silaha za kisasa na kuna wakati china iliizuia Taiwan kushiriki katika Shirika la Afya Duniani licha ya kuweko mashinikizo makubwa .China iliionya Marekani kwamba, kushiriki katika mashirika na taasisi za kimataifa ni maalumu kwa ajili ya nchi kamili, wakati Taiwan ni sehemu isiyotenganishika na China na ni kisiwa chenye utawala wa ndani tu. Pamoja na hayo, mara kwa mara Marekani imekuwa ikisema kuwa, Taiwan na Hong Kong ni mifano miwili ya demokrasia na uchumi huru mbele ya vitisho vikubwa vya China ya kikomunisti. China imesema, Marekani inapaswa kujifunza na uzoefu wa huko nyuma ambapo kila iliipojaribu kukabiliana na China imeshindwa. Aidha imesema, Marekani ndiyo inayopata madhara makubwa hasa ya kiuchumi, kila inapoanzisha chokochoko dhidi ya China.
Hivi sasa pia na licha ya Beijing kukasirishwa na kitendo cha Donald Trump cha kuzungumza kwa simu na rais wa serikali ya Taiwan, lakini inaonekana kuwa China haitochukua hatua za haraka dhidi ya kitendo hicho, bali itaendelea kufuatilia kwa karibu utendaji wa Donald Trump kutoka chama cha Republican hasa kwa kuzingatia matukio yasiyosahaulika ya kihistoria ambapo ni serikali ya chama cha Republican cha nchini Marekani ndiyo iliyoanza kutambua umuhimu wa kuwa na uhusiano na China ya kikomunisti.
0 Comments