Meli za kivita za Iran zaelekea Ghuba ya Aden
Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetuma msafara wake wa 46 wa meli za kivita katika Ghuba ya Aden.
Manwoari hizo za Iran zimeng'oa nanga katika Bandari ya Bandar Abbas kusini mwa nchi Jumatatu katika sherehe iliyodhudhuriwa na Admeri Habibullah Sayyari, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran. Msafara huo 46 wa meli za kivita za Jeshi la Wanamaji la Iran utakuwa na majukumu ya upelelezi na kutekeleza oparesheni baharini na unajumuisha manwoari mbili za Sabalan na Lavan.
Msafara huo wa 46 wa manwoari za Iran mbali na kulinda usalama na kusindikiza meli za kibiashara na za mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia utakuwa na jukumu la kulinda hadhi na nguvu za Iran ya Kiislamu na kukabiliana na propaganda chafu za maadui wanaoeneza chuki dhidi ya Iran.
Msafara wa 46 umeondoka baada ya msafara mwingine wa 45 wa meli za kivita za Jeshi la Wanamaji la Iran kurejea Bandar Abbas baada ya oparesheni ya miezi miwili katika maji ya kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jeshi la Wanamaji la Iran limeimarisha harakati zake katika maji ya kimataifa kwa lengo la kudumisha usalama na kulinda meli za kibiashara na zinazobeba mafuta. Wanamaji wa Iran wamefanikiwa pakubwa kuzuia hujuma nyingi za maharamia wanaolenga kuteka meli za Iran na za mataifa mengine katika maji ya kimataifa.
0 Comments