Header Ads Widget

Responsive Advertisement

KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI WAKATI WA WAINGEREZA , VYOMBO VYA HABARI TANZANIA BARA






Katika makala  hili, tumeligawa katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao utabeba fasili ya vyombo vya habari pamoja na historia fupi ya utawala wa Muingereza nchini Tanganyika. Sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo tutaeleza mambo makubwa yaliyofanywa na utawala wa Mwigereza katika kukuza Kiswahili kwa ujumla na Kiswahili katika vyombo vya habari. Mwisho ni hitimisho la swali. Kwa kuanza na utangulizi
Waingereza walianza kuitawala Tanganyika miaka ya 1920. Utawala wa Mwingereza ulifuata ule wa Wajerumani ambao waliitawala Tanganyika kabla ya vita ya kwanza ya dunia. Baada ya Mjerumani kushindwa katika vit ya kwanza ya dunia, Muingereza alikabidhiwa Tanganyika na baadhi ya makoloni ambayo yalikuwa ya Mjerumani, na hili lilifuatia makubaliano ywliyowekwa katika mkataba wa Verssaile.
Vyombo vya habari kwa mujibu wa Wikipeda, ni vyombo vya vya mawasiliano vinavyolenga watu wengi iwezekanavyo kwa shabaha ya kuwapatia habari au burudani. Kwa mfano magazeti, televisheni au 'internet".
Waingereza walipofika Tanganyika walikuta Mjerumani akiwa ameshafanya mambo mengi yakiwemo yale ya kiutawala, kibiashara na kielimu. Massamba (2012), anasema Waingereza walikuwa ni watawala ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Yafuatayo ni baadhi ya mambo makubwa aliyoyafanya Muingereza katika kukuza na kuendeleza Kiswahili wakati wa utawala wake.
Mosi, walipitisha na kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika shule za awali (msingi). Katika kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa usawa na kiwango kimoja katika makoloni yao ya Afrika Mashariki, Muingereza aliona haja ya kuchagua lugha moja ya kienyeji ili kutolea elimu. Kati ya lugha nyingi za kibantu, Kiswahili kilionekana kinafaa zaidi. Hivyo walipitisha lugha ya Kiswahili kuwa lugha lugha rasmi ya kufundishia katika elimu ya awali. Kuchaguliwa kwa lugha ya kiswahili kulifanya watumiaji wake kuongezeka. Mathalani wote waliojiunga na shule za wakoloni iliwalazimu kujifunza Kiswahili. Lakini pia walimu wa shule hizo ambao aghalabu walikuwa si waswahili walilazimika kujifunza Kiswahili ili waweze kuwasiliana na wanafunzi wao shuleni. Vilevile kutumika kwa kiswahili shuleni kulichochea uandishi wa vitabu na machapisho yahusuyo lugha ya Kiswahili.
Jambo la pili lililofanywa  na Waingereza ni kuisanifisha lugha ya Kiswahili. Baada ya Waingereza kuchagua lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia, waligundua kuwa lugha hii ilikua na lahaja nyingi sana. Hivyo waliamua kuchagua lahaja moja kati ya zile nyingi na kuisanifisha ili itumike katika nyanja zote rasmi ikiwemo utawala na elimu. Usanifishaji ulifanyika chini ya Kamati ya  Lugha ya Afrika mashariki (The interterritorial Swahili Language Committee). Kamati iliteua lahaja ya Kiunguja ambayo ilitumika kama kiunzi cha lugha ya Kiswahili. Usanifishaji wa Kiswahili ulisadia sana kupata lugha rasmi ya kutumika katika miktadha rasmi.  Kiswahili sanifu kilianza sasa kuandikwa na kuzungumzwa kwa ufasaha na hivyo kukuza na kuendeleza lugha ya kiswahili.
Jambo la tatu ni Kuanzishwa kwa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki yaani The Interterritorial Swahili Language Committee. Kamati hii iliundwa mwaka 1925 na ikaanza rasmi shughuli zake mwaka 1930 chini ya katibu mkuu wa kwanza Frederick Johnson. Kamati hii ilifanya kazi nyingi sana ambazo kwa ujumla wake zilisaidia kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Baadhi ya shughuli zilizofanywa na kamati hii ni pamoja na; kusanifiaha othografia ya Kiswahili, kuchapisha machapisho mbalimbali ya lugha ya Kiswahili na kuwatia moyo na kuwapa ushauri waandishi ambao ni wenyeji wa lugha ya Kiswahili. Vilevile kamati ilikuwa inafanya masahihisho ya vitabu  vilivyotumika kufundishia shuleni kila mara ilipohitajika. Walitafsiri vitabu na machapisho mbalimbali katika lugha ya kiswahili. Kazi zote hizi zilizofanywa na kamati ya lugha zilisaidia kuinua wabobezi wa lugha ya Kiswahili na vilevile kufanya watumiaji wa Kiswahili kuongezeka na lugha kuenea zaidi.
Jambo lingine ni kuandaa kamusi za kiswahili pamoja na kiswahili na kiingereza. Baadhi ya kamusi zilizoandaliwa na kutolewa wakati wa Muingereza ni A standard Swahili-English Dictionary, A standard English-Swahili  Dictionary na Kamusi ya Kiswahili-Kiswahili. Kamusi zote hizi zilihaririwa na Frederick Johnson ambaye alikua ndie katibu mkuu wa Kamati ya Lugha ta Afrika Mashariki. Kamusi hizo zilisaidia katika ujifunzaji lugha ya Kiswahili na hasa kwa wale ambao hawakuwa wenyeji wa lugha ya Kiswahili. Vile ilikuwa njia ya kuhifadhi maneno na msamiati wa lugha ya Kiswahili na kuupanua kwa kuwekea maana yake pamoja na maana nyingine za ziada. Kwa namna hii lugha ya Kiswahili ilikua na kupata hadhi ya juu tofauti na awali.
Ama kwenye uwanja wa Habari Waingereza walifanya yafuatayo;
Kwanza ni kuchapisha magazeti kwa lugha ya Kiswahili. Mwaka 1923 Waingereza walichapisha gazeti la Mamboleo. Kwa mujibu wa Stummer (1998), anasema kuwa hili lilikuwa gazeti la kwanza kuchapishwa kwa lugha ya Kiswahili katika utawala wa Mwingereza na maudhui yake yalihusu makala ya elimu, habari za ndani, matangazo ya serikali pamoja na hadithi za kufurahisha. Hivyo gazeti lilichangia kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Kwani hapa ndio ulikua mwanzo wa lugha ya Kiswahili kutumika kwenye uwanja wa habari, hali iliyoendelea hata baada ya wakoloni hao kuondoka Tanganyika.
Vilevile mwaka 1937 walianzisha gazeti la Kwetu ambalo lilichapishwa kwa lugha ya Kiswahili. Stummer (1998) anaeleza kuwa gazeti hili lilikuwa la kwanza kuchapishwa Tanzania na Waafrika wenyewe ambapo walifanikiwa kuchapishwa nakala 1000 na kurasa zote ziliandikwa kwa lugha ya Kiswahili isipokuwa ukurasa wa mbele ulitafsiriwa kwa lugha ya kiingereza na maudhui yake yalihusu mambo muhimu ya kijamii kama vile ubaguzi wa rangi, ugandamizaji wa kiuchumi na habari za Ulaya za kisiasa. Kutokana na mada zote kuchapishwa kwa lugha ya Kiswahili na gazeti lilisomwa na wenyeji wengi na hivyo illichangia kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili. Kuchapishwa kwa gazeti la kiswahili kulifungua njia kwa lugha ya Kiswahili kutumika katika vyombo vya habari.
Kuanzishwa kwa redio mwaka 1950. Stummer (1998), anasema kuwa redio ilianzishwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya habari. Idadi kubwa ya watu na serikali kulihitaji chombo maalumu kwa ajili ya propaganda ikisababisha mjadala kuhusu kuanzishwa kwa mifumo ya utangazaji Tanganyika. Lakini kutokana na uharibifu mkubwa uliotokana na machafuko ya vita ya pili ya dunia azma hii iliahirishwa hadi 27/08/1942 hadi 1950. Ambapo mhandisi  aliyejulikana kwa jina la Thorney Croft kutoka shirika la utangazaji la British Broadcasting corporation (BBC) kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya kuanzishwa chombo cha utangazaji. Alikuja na mkakati uliotambuliwa kwa jina la Thorney Croft plan na ulikuwa na mahitimisho haya; serikali ya Tanganyika haikuwa na ulazima wa utangazaji kwa wale wasiokuwa Watanzania. Hatimaye tarehe 01/07/ 1951 chombo cha utangazaji kilianzishwa kikiitwa 'Sauti ya Dar es salaam' chini ya idara ya maendeleo ya jamii chini ya kiongozi wake C. A. L Richard. Radio hii ilitoa matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa na kiingereza kwa kiasi kidogo, lengo likiwa kuwafikia wenyeji wengi ambao wengi wao hawakujua kiingereza na aghalabu walikua hawajui kusoma magazeti.
Kwa kuhitimisha, pamoja na mambo yote yaliyofanywa na Muingereza katika kukuza na kueneza Kiswahili, haikumaamisha kuwa hili ndilo lilikuwa lengo lao la msingi. Massamba  na Wenzake (2012), wanasema Waingereza walichukua hatua ya kukiendeleza Kiswahili ili kupata njia au namna ya kukuza utawala wao na maslahi yao kiujumla.
Received from miss happy J.
IKS / UDSM

Post a Comment

0 Comments