Header Ads Widget

Responsive Advertisement

ELIMU MITINDO NININI PDF

Dhana ya Elimu – Mitindo
Elimu Mitindo ni dhana iliyoundwa na maneno mawili; ‘elimu’ na ‘mtindo’ na maneno haya yanapotenganishwa yanaleta maana tofauti kila moja. Kabla ya kuendelea zaidi ni muhimu kuangalia kwa undani zaidi dhana ya ‘mtindo.’ Njogu na Chimerah (2011:384) wanasema kuwa “mtindo ni namna au jinsi ya kufanya kitu na ndio unaomtofautisha fanani mmoja na mwingine…mtindo ni ubingwa wa kuoanisha fani na maudhui.” Maana hii inaonesha kwamba mtindo ni namna ya kufanya kitu kwa mfano kuandika, kucheza, kupamba, kuzungumza na hata kula kula. katika kipengele cha pili cha maana ya mtindo kulingana na wataalamu hawa ni dhahiri kwamba kila mtu ana mtindo wake. Kwa mfano pengine kila mtu ana namna yake ya kula, kwa mfano mwingine anakula haraka haraka kuliko mtu mwingine.
Katika muktadha wa fasihi mzungumzaji au mwandishi kuteua baadhi  ya miundo ya lugha katika gimba la lugha  inayohusisha  vipengele vingine nje ya miundo ya lugha.
Nao Leech na Short (1981) wanadai kuwa mtindo ni namna lugha inavyotumiwa na mtu fulani, kwa malengo fulani katika muktadha fulani. wakiendelea kufafanua dhana ya mtindo, Wafula na Njogu (2007:97) wanasema kuwa “kifasihi, mtindo unaelezwa kwa kuainishwa na madhumuni ya msanii. Madhumuni ni dhamira na mtindo ni jinsi dhamira zinavyowasilishwa…maudhui yanapaswa kuwasilishwa katika mtindo unaoafikiana nayo.”
Njogu na Chimerah (khj.47) wanasema kuwa mtindo ni ufundi wa kupanga na kupangua. Pia ni ujuzi wa kujieleza…mtindo hutumiwa kupeleka mbele maudhui na dhamira, pamoja na kusanifu kazi nzima ili kuleta ufanisi. Kauli hii inalenga kutuaminisha kwamba  katika lugha na fasihi mitindo ni dhana ambayo hutumika kufafanua uhusiano baina ya maudhui na namna ya kuyafikisha maudhui hayo ambapo njia ya kuyafikisha maudhui hayo ni fani.
Kwa mujibu wa Longhorn (2013:91) wanasema kuwa “Elimumitindo ni taaluma inayohusu mitindo ya uandishi wa tanzu au waandishi fulani.” Maana hii haijitoshelezi katika muktadha huu kwani haijataja fasihi wala lugha ambayo ndiyo kiunzi kikuu cha elimumitindo.
Hornborrow & Wareing (1998:164) wanapofasili elimumitindo kama somo wanasema kuwa wanasema ni matumizi ya ala za lugha kuchambulia matini za kifasihi; Kujadili matini kwa kutumia vigezo yakini kuliko vigezo vya kibinafsi. Katika fasili hii wataalam hawa wanajaribu kufafanua kwamba kuna nduni mahusus katika kuchambua matini za kifasihi na hivyo elimu mitindo inalenga pia kuweka msisitizo katika ujumi wa nduni za lugha kwa mfano urari wa vina na  mizani.
Wales (2001:371) anadai kuwa elimumitindo  ni taaluma inayojishughulisha na ufafanuzi wa nduni za matini  na umuhimu wa dhima za nduni hizo katika uchambuzi wa maana wa matini hiyo.
Kwa ujumla Elimumitindo ni taaluma inayochunguza mitindo ya lugha iliyotumika katika matini na namna mitindo hiyo inavyosaidia kupata maana ya  matini. Katika Elimumitindo kinachokusudiwa zaidi ni kubaini mitindo iliyotumika na kufafanua namna ilivyotumika na inamaanisha nini katika ulimwengu wa fasihi.




Hornborrow, J. na Wareing, S.  (1998). Patterns in Languages. An Introduction to Language  and Literary Style. London: Routledge.
Leech, G na Short. (1981). Style in Fiction. Essex: Longman Group Limited.
Longhorn. (2013). Kamusi ya Karne ya 21. Nairobi: Longhorn.
Njogu, K na Chimerah, R. (2011). Ufundishaji wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Wafula, R.M na Njogu, K. (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Wales, K. (2001). Dictionary of Stylistics. Essex: Longman.

Post a Comment

0 Comments