
Dhana ya fasihi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama
ifuatavyo mathalani, Massamba (1999) anasema kuwa fasihi ni sanaa inayotungwa
au kubuniwa kwa lengo la kuifikishia ujumbe hadhira iliyokusudiwa kwa njia ya mdomo
au maandishi.
Aidha, Wamitila (2010) anafasili fasihi kuwa ni
sanaa inayotumia lugha kwa namna maalumu inayoathili na kupitisha ujumbe fulani
unaolenga hadhira. Fasili hii ina mapungufu yake kwa kuwa haiweki bayana lugha
hiyo ama ni ya mazungumzo au iko katika maandishi.
Kwa ujumla fasihi ni sanaa itumiayo lugha ama ya
mazungumzo au ya maandishi ili kuweza kufikisha ujumbe kwa hadhira
iliyokusudiwa. Hadhira hiyo inaweza kuwa ya watoto au watu wazima.
Pia, fasihi ya watoto imefasiliwa na wataaalamu
mbalimbali kama ifuatavyo: Weche (2010) anafasili fasihi ya watoto kuwa ni kioo
cha kumwongoza mtoto katika mambo mbalimbali yanayohusu maadili. Anaendela
kueleza kuwa fasihi hiyo haina budi kupinga tabia zisizokubalika na
kuzibainisha tabia hizo kwa watoto ili wazifahamu.
Wamitila (2008) anafasili fasihi ya watoto kuwa ni
ile fasihi ambayo kimsingi hurejelea matini au kazi ambazo hadhira yake kubwa
ni ya watoto.
NOUN (2010) wanaeleza kuwa fasihi ya watoto ni ile
fasihi inayomlenga mtoto na siyo mtu mzima.Wanaendelea kueleza kuwa fasihi hii
inaweza kuwa katika tanzu mbalimbali kama vile hadithi, ushairi, visakale na
drama.
Vilevile, Wamitila (2010) anafasili fasihi ya watoto
kuwa ni ile fasihi ambayo maudhui yake yamejengwa kwa ajili ya mtoto.
Fasili zote hufanya dhana ya fasihi ya watoto iwe
telezi yaani itazamwe kwa namna mbalimbali kwa kuwa hazimuweki bayana mtoto
anayezungumziwa ambapo kutokana na fasili hizo unaweza kujiuliza, Je mtoto
anayemaanishwa ni yupi? Ili kufahamu nani ni mtoto hatuna budi kuangalia
mitazamo ifuatayo:
Mtazamo wa kidini, katika mtazamo huu mtoto
anachukuliwa ni mtu yeyote anayeamini kuwapo kwa Mungu kupitia dini. Waumini
wote wa dini husika humuita Mungu kuwa ni baba, hivyo waumini wote huonekana
watoto mblele ya Mungu na kuishi kwa kufuata mafundisho yake.
Mtoto katika mtazamo wa kikatiba, katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania humtambua mtoto kama mtu yeyote aliye chini ya miaka
kumi na nane (18). Hivyo, yeyote aliye juu ya umri huo hachukuliwi kama mtoto
bali ni mtu mzima.
Mtazamo wa kibaiolojia na ukuaji, pia mtazamo huu
hutambua kuwa mtoto ni kiumbe chochote chenye viungo tete vinavyoendelea
kukomaa na hadi kufikia kipindi cha kubalehe na kuingia utu uzima. Hivyo,
mtazamo huu huona mtoto kama kiumbe chochote si lazima awe binadamu.
Mtazamo wa kihistoria, kijamii na kiutamaduni, kila
jamii ina namna yake ya kumtambua mtoto ni nani kupitia masuala mbalimbali. Kwa
mfano katika jamii ya Kitanzania hutenga mambo yanayofanywa na watoto na watu
wazima. Kwa mfano jando na unyago hufanywa na watoto na vijana. Vilevile katika
jamii mtoto ni mtu yeyote mwenye umri mdogo dhidi ya wakubwa au wazee. Hivyo,
wazee huwaona vijana ni watoto bila kujali umri wao.
Hivyo basi, mtazamo wa kikatiba ndio mtazamo unaofaa
zaidi katika kubainisha yupi hasa ni mtoto anayemaanishwa. Mtazamo huu hudai
kwamba mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka kumi na nane (18). Hivyo,
kutokana na mtazamo huu tunaweza kusema kuwa fasihi ya watoto ni ile fasihi
ambayo fani na maudhui yake humlenga mtu aliye chini ya miaka kumi na nane
(18). Hata hivyo ieleweke kuwa kwa kiasi fulani huweza kuwahusu watu wazima
yaani wale watu walio juu ya miaka kumi na nane.
Kwa kutumia kazi mbili za fasihi ya watoto ambazo ni
riwaya ya Zindera iliyoandikwa na
Erast G. Sabuni pamoja na tamthilia ya Kilio Chetu iliyoandikwa na Medical Aid Foundation, dhana ya fasihi ya
watoto inaweza kufasiliwa kama ifuatavyo:
Wamitila (20100 anatoa sifa mbalimbali ambazo
zinaweza kutumika kufasili dhana ya fasihi ya watoto kama ifuatavyo:
Fasihi ya watoto ni fasihi inayojikita zaidi
kujadili masuala mbalimbali ya watoto na malezi yao kwa ujumla. Dhamira nyingi
katika vitabu vya watoto na hulenga watoto kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano katika
riwaya ya Zindera masuala mbalimbali
ya watoto walemavu yamejadiliwa. Kwa mfano kutengwa kwa watoto wenye ulemavu wa
ngozi (albino). Kama ilivyokuwa kwa Zindera aliyekataliwa na baba yake. Kwa
mfano Nzeta anasema;
“Masikini”
ni kitoto cha kike lakini albino”
(Uk. 4)
Pia, Mpanduji mume wa Sara anasema;
“Albino!
Akamdondosha mtoto chini” (Uk)
Vilevile katika tamthilia ya Kilio Chetu inajadili
matatizo mbalimbali yanayowakabili watoto ikiwemo ukosefu wa elimu ya kijinsia
inayosababisha watoto kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI pamoja na mimba za
utotoni. Kwa mfano, Suzi anasema,
“Mie, kwanza
sikujua mambo haya, mama na mjomba walijua juu ya mambo haya ya mapenzi”
Hivyo, watoto huwalaumu wazazi kwa kutowahadharisha
mapema na kuwapatia elimu hiyo ya jinsia.
Mara nyingi fasihi ya watoto huwa na muundo sahili. Senkoro
(2011) anaeleza muundo ni mtiririko wa visa na matukio katika kazi ya fasihi.
Naye Wamitla (2010) anaeleza kuwa muundo wa fasihi ya watoto ni mwepesi
unaomwezesha kupata ujumbe kwa njia rahisi. Muundo huu hutumika ili kuwafanya
watoto waelewe kwa urahisimaudhui bila kuchanganyikiwa. Mfano katika riwaya ya Zindera imetumia muundo sahili (wa moja
kwa moja) kwani matukio yamepangwa kuanzia ndoa ya Mpanduji na Sara, kuzaliwa
kwa Zindera, matatizo aliyoyapatia na hatimaye kufanikiwa kuwa daktari. Hii
imesaidia watoto kufuata mafunzo kwa njia rahisi. Vilevile, katika tamthilia ya
Kilio Chetu muundo uliotumika ni wa
moja kwa moja ambapo tunaona toka mwanzo kuingia kwa DUBWANA (UKIMWI) na jinsi
watu walivyo kosa elimu ya ugonjwa huo na hatimaye kifo cha Joti na Suzi
kutokea.
Wahusika wakuu katika fasihi ya watoto mara nyingi
huwa ni watoto wenyewe. Njogu na Chimerah (2011) anaeleza kuwa wahusika ni
sehemu ya kazi na viumbe wa sanaa inyobuniwa kutokana na mazingira ya msanii.
Pia Wamitila (2010) anasema kuwa fasihi ya watoto lazima iwe na wahusika watoto
wenyewe. Hiyo ni kwa ajili ya kuonesha uhalisia wa yale yanayozungumziwa,
kujadiliwa na kutendwa na watoto wenyewe. Ketika tamthilia ya Kilio Chetu wahusika wakuu wote ni
watoto wenyewe. Kwa mfano Joti, Suzi, Anna na Mwarami ambao huonekana toka
mwanzo wa tamthilia hadi mwisho wakiwa wanalaumu madhara ya kukosa elimu ya
jinsia. Kwa mfano Suzi anasema;
“….naapa kwa
Mungu wangu, mimi na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa tusingetumbu…tu…”
Pia, katika riwaya ya Zindera mhusika mkuu ni mtoto mwenyewe ambapo tunaona Zindera kuwa
ndiye mhusika mkuu kuanzia mwanzo wa riwaya hadi mwisho (toka kuzaliwa kwake,
malezi yake na hatimae mafanikio yake ya kuwa daktari).
Mara nyingi fasihi ya watoto hutumia yatima kama
motifu. Ndalu na wenzake (2014) wanaeleza kuwa yatima ni mtoto aliyefiwa na
mzazi mmoja au zaidi. Pia, Wamitila (2010) amnaeleza kuwa haiwezi kuchunguzwa
bila ya kuchunguza nafasi ya mhusika au mtoto yatima au aliyetengwa na hivyo
hulazimika kufanya juhudi za kujiokoa au kuishia kuokolewa. Motifu hii
inatumika katika kazi nyingi za fasihi ya watoto kwa kukuza ujasiri na akili ya
kuweza kujinasua kwenye mtego fulani. Hata hivyo ieleweke kuwa pale ambapo
mtoto si yatima aghalabu huwa na upungufu au dosari fulani ya kimaumbile. Kwa
mfano motifu hii imetumika katika riwaya ya Zindera
pale ambapo Zindera alipotelekezwa porini. Licha ya changamoto alizopitia ikiwa
ni pamoja na kufiwa na walezi wake lakini mwishowe anakuwa daktari. Kwa mfano
mwandishi anaema:
“Katika hali ambayo haikutarajiwa,
moto mkubwa ulizuka kijijini kwao. Moto huo uliteketeza kabisa myumba ya
mwindaji Makale. Ni Pili pekee yake aliyenusurika kifo. Lakini Makale na mkewe
wote walifariki dunia”
Pia, katika tamthilia ya Kilio Chetu motifu ya yatima imetumika kwani tunamuona mhusika Suzi
ambaye alikuwa na mzazi mmoja tu wa kike.
Pia, fasihi ya watoto husheheni michoro, picha na
vielelezo mbalimbali. Ngugi (2011) anaeleza kuwa kazi nyingi za watoto lazima
ziwe na vielelezo, michoro pamoja na picha. Anaendelea kusema kuwa dhima yake
kuu ni kufikisha ujumbe kwa njia iliyorahisi. Kwa mfano, kuna mchoro
unaomuonesha Suzi akipigwa na mama yake baada ya kukutwa na vidonge vya majira
kwenye nguo zake shule (Uk. 10).. Pia, katika riwaya ya Zindera kuna vielelezo mbalimbali vilivyotumika ili kufanya ujumbe
uwafikie kwa urahisi kwa mfano kuna kielelezo kinachoonesha Sara akimficha
mwanae Zindera baada ya kuhisi kuna mtu anamfuatilia kwa nia ya kumdhuru
mwanae. (Uk. 15). Pia, vielelezo vingine viko katika ukurasa wa 2, 21, 28, 35,
45, 51, 58 na 65.
Fasihi ya watoto mara nyingi hutumia lugha rahisi
inayoeleweka kwa urahis. Wamitila (2010) anafafanua kuwa lugha ni nyenzo kuu
katika kazi yoyote ile ya fasihi. Anaendelea kueleza kuwa lugha nyepesi si
lazima kwa watu wazima kwani uwezo wao ni mkubwa. hivyo Hivyo, fasihi ya watoto
hutumia sentensi fupi na sentensi zisizochangamani. Lengo kuu la kutumia lugha
nyepesi ili kufikisha ujumbe kwa njia iliyo rahisi. Kwa mfano katika tamthilia
ya Kilio Chetu mwandishi anasema;
“Mwarami:
Mshikaji Joti ee, umetuanika juani hivi
Joti:
Kwani viti jamani?
Choggo: Eti
vipi? We sio tulikubaliana kukutana pale
kijiweni?” (Uk. 18)
Vilevile, kitabu cha Zindera tunaona kuwa lugha iliyotumika miongoni mwa wahusika wa
riwaya hii. Lugha hii imetumika ili maudhui yawafikie watoto kwa njia rahisi.
Kwa mfano, mwandishi anasema;
“Ahsante baba, Zindera alisema”
Zindera alisema sasa naweza kufanya upasuaji, nayafahamu maadhi mengi pamoja na
tiba yake!
Kwa kuhitimisha, fasihi ya watoto ina dhima kubwa
sana katika jamii si kwa watoto tu bali hata kwa watu wazima kwani licha ya
watoto kupata elimu inayohusiana na namna gani ya kuishi na jamii inayowazunguka
hususani watu wazima, lakini na fasihi hutoa njia mbalimbali zinazowasaidia
wazazi kufahamu jinsi ya kuishi na kulea watoto.
MAREJELEO
Medical
Aid Foundation (1995). Kilio Chetu.
Dar es Salaam: TPH.
NOUN (2010). Children
Literature. Lagos: National Open University of Nigeria.
Ngugi,
P. (2010). Language and Literacy
Education: The Stateof Chidrens in Kiswahili in Kenya. Berlin: Lambert
Academic Publishing.
Njogu,
k. na Chimerah, R. (2008) Ufundishaji wa
Fasihi, Nadharia na Mbinu, Nairobi:Jomo Kenyatta Foundation. Ngugi, P.
(2010). Language and Literacy Education:
The Stateof Chidrens in Kiswahili in Kenya. Berlin: Lambert Academic
Publishing
Mulokozi, M. M. (1996). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Ndalu na wenzake. (2014). Kamusi Teule ya Kiswahili. Dar es Salaam: EAEP.
Sabuni, E. G. (2008). Zindera. Dar es Salaam; Solution Publuishing.
Wamitila, K. W. (2010). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Niarobi: Focus Books. Wamitila,
K. W. (2008). Misingi ya Uchunguzi wa Fasihi.
Nairobi: Vide Muwa Publishers.
0 Comments