Nadharia za uhakiki wa fasihi
Nadharia ya UMUUNDO
Nadharia ya UHALISIA
Nadharia ya umarx
Nadharia ya UHALISIA mpya
Nadharia ya umuundo mpya
Nadharia ya ufeministi
Nadharia ya kisaikolojia
Nadharia ya natorojia
NADHARIA ZAKI-MARX
Anachokisema mhakiki kuhusu kazi anayoizingatia, hutegemea kwa kiwango kikubwa, dhana anazozileta katika kazi hiyo. Aghalabu, dhana hizi haziwi za moja kwa moja, lakini mhakiki anayeegemea uhakiki wa Ki-marx huwa anafahamu kwa hakika anachokizingatia kwani kazi yake itaongozwa na falsafa fulani zilizopo. Kazi yake itaongozwa na mtizamo wa Ki-marx kuhusu historia, ambapo mikinzano ya kitabaka huwa jambo muhimu na vile vile uhusiano kati ya fasihi na muundo wa Kiuchumi katika jamii husika lazima udhihirishwe.
Kwa jumla, twaweza kusema kwamba mhakiki wa Ki-marx hukita nadharia yake kwenye itikadi za Karl Marx na Fredrick Engels, na hasa kwenye madai ya hao wawili kuwa, katika tathimini ya mwisho kabisa maendeleo ya historia ya binadamu pamoja na taasisi zake, yatakuwa ni tokeo la mabadiliko katika njia za kimsingi za uzalishaji mali. Kwamba mabadiliko kama hayo husababisha mageuko katika muundo wa matabaka ya kijamii ambayo katika kila kipindi huendeleza kung'anga'aniwa kwa uwezo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii; na kwamba dini, fikra na utamaduni wa jumuiya yoyote (zikiwemo sanaa na fasihi kwa kiwango fulani) huwa ni `itikadi' na miundo maalum ya `kitabaka' ambayo ni zao la miundo na matabaka ya kijamii yaliyomo wakati huo.
Umarx huchukua kwamba jamii zote za kitabaka huzalisha mkururo wa miundo ya urazini inayokinzana na kushindana. Katika jamii ya kikapitolisti, kwa mfano, aina tofauti za mitizamo kuhusu maisha huwakilisha haja tofauti za kitabaka ambazo hutegemea hasa mikinzano kati ya mapato na nguvu za kutenda kazi. Kwa hivyo Umarx huhusisha itikadi na uzalishaji mali na jukumu lake katika mivutano ya kisiasa katika jamii. Jinsi watu binafsi wanavyoelewa msingi wa maisha yao hutokea kuwa kamba ya
mvutano ambapo wanaweza ama kubadilika au kuendelezwa. Kwa mfano, chini ya mfumo wa kikapitolisti, wafanyakazi wanashurutishwa kuuza uwezo wao wa kufanya kazi kwa wale wanaotawala mazao pamoja na huduma. Katika mpangilio huu, wanaotawala nguzo za uzalishaji mali hunufaika kupitia kwa dhamani ya ziada iliyozalishwa na wafanyakazi. Hii ni kati ya mali inayobakia baada ya kuondoa matumizi ya malighafi, mashine, na nguvukazi. Aidha faida hupatikana kwa kuwalipa wafanyakazi malipo ya chini kuliko dhamani ya kazi waliyofanya.
Uhakiki wa ki-marx hujishughulisha na tabaka la kiuchumi na sababu za kiitikadi zinazotawala jinsi mtunzi hufikiria na kuandika, lakini hasa huzingatia uhusiano wa kazi ya fasihi na uhalisi wa kijami uliopo wakati huo. Kama tokeo basi uhakiki wa Ki-marx hudai kwamba watunzi wanapaswa kumithilisha hali halisi ya maisha ya jamii wanazotungia. Wazo hili lilipingwa hata na wafuasi wa Marx. Mmoja kati yao ni mtaalam kutoka Hungary, George Lukac aliyekuwa na maoni kuwa badala ya fasihi kuimithilisha hali ya maisha, fasihi na sanaa zapaswa kuwa `picha ya uhalisi'. Ambapo picha hiyo inakiuka misingi ya kuiga moja kwa moja uhalisi.
Mhakiki wa Ki-marx, hivyo basi, tayari ametolewa picha halisi ya maisha. Shida aliyo nayo ni jinsi ya kuikabili na kuihakiki fasihi. Wahakiki wa ki-marx aghalabu wameiona fasihi kama iliyo halisi, hivi kwamba mtunzi wake huwa anajitenga na kuonyesha makosa katika jamii. Mbinu inayotumiwa na wahakiki wa jadi wa ki-marx ni kuunda tena mtizamo kuhusu yaliyopita kutokana na ithibati za kihistoria kisha wakadhihirisha uhalisi wa kazi fulani kama kielelezo cha jamii na kama njia ya kuelewa uhalisi wa kijamii.
Kwa jumla uhakiki wa ki-marx huhusisha kazi ya fasihi na mtazamo wa uhalisia wa kijamii wa wakati kazi hiyo ilitungwa. Vile vile uhakiki huu zaidi huzingatia maudhui katika fasihi huku pakitolewa uhakiki wa maadili, na njia za kuyaboresha maisha zilizoshughulikiwa. Ni muhimu kutaja kwamba pana aina mbali mbali za nadharia za uhakiki za ki-marx. Lakini licha ya wingi wa nadharia hizi, nadharia zote za ki-marx zina nguzo moja iliyo sawa; kwamba fasihi hueleweka tu katika msingi wa uhalisi wa kijamii hasa katika umilikaji mali. Wahakiki wa ki-marx hushikilia kwamba nadharia yoyote inayozingatia fasihi kwa kuitenga (kwa mfano kama kazi ya kimuundo au kama zao la mkondo wa fikra za kibinafsi za mtunzi) na kuiweka katika hali hiyohuku
ikitenganishwa na jamii na historia, huwa ni pungufu katika uwezo wake wa kueleza hasa fasihi ni nini.
Kwa wahakiki wa ki-marx uhalisi wa kijamii si chombo ovyo ambamo fasihi hujengeka na kutokea bali huchukuliwa kama ulio na umbo maalum, na umbo hili hupatikana katika historia ambayo kwa maoni yao ni mkururo wa mivutano kati ya matabaka yanayokinzana na njia za kiuchumi za kuzalisha mali ambazo zinazingatiwa katika jamii husika. Umbo hilo hupatikana pia katika hali yoyote ile ya jamii kwani mahusiano maalum ya kitabaka na hali halisi za kisiasa, kitamaduni na kijamii huchukuana na mfumo uliopo wa kuichumi kwa njia husishi.
Upungufu wa nadharia hizi hutokea katika kuchagua kiwango cha maisha kitakachozingatiwa kwani ni vigumu kwa kazi ya fasihi kuzingatia maisha ya jamii katika ujumla wake. Kwa mfano iwapo mtunzi atachagua kuonyesha starehe na buraha ya maisha ya tabaka tawala bila kuonyesha uchochole wa tabaka linalotawaliwa, atakuwa anakiuka misingi ya kutoa picha halisi ya maisha ya jamii? Ufinyu wa mtizamo wa ki- marx ni muweka jamii katika vikundi viwili kuu ambavyo yamkinika ni sawa. Yaani yaelekea kuwa wanatabaka la juu wote wamefanana kwa njia zote, na vivyo hivyo kwa wanatabaka la chini. Hapa ndipo ahakiki wa kifeministi wanaposema kwamba umarx unaepuka kuona kwamba hata katika maisha ya tabaka la juu wanawake hawakuwa na uhuru/nafasi sawa nawanaume.
Hata hivyo tutaje kwamba msisitizo wa nadharia za ki-marx kuhusu umuhimu wa mikinzano na migongano ya kitabaka umeathiri wahakiki wengi wa kijamii ambao hawazingatii itikadi zaki-marx.
NADHARIA YAUASILIA
Nguzo ya nadharia ya uasilia ni maisha kama yalivyokuwa - yaani maisha asilia. Kwa hivyo lengo la kimsingi la uhakiki huu ni kutoa picha ya maisha kama yalivyokuwa (kwa ukweli wake wote) ili kueleza misingi ya maisha yalivyo sasa. Wakati mwingine imesemekana kwamba uasilia hutoa picha halisi zaidi ya uhalisia. Nadharia ya uasilia huchagua maudhui maalum ya kuzingatia. Fauka ya hayo, nadharia hii ni aina ya ubunifu wa kifasihi ulioendelezwa na kundi la waandishi waliokuwa na tasnifu maalum ya kifalsafa. Tasnifu hii, iliyokuwa zao la maoni yaliyotokana na mtaalamu wa biolojia
Charles Darwin katikati ya karne ya kumi na tisa, ilishikilia kwamba binadamu alikuwa chini ya himaya ya maisha ya asilia na kamwe hakuwa na roho (soul) au uhusiano wowote wa kidini uliokiuka kaida za ulimwengu halisi. Hivyo basi binadamu alichukuliwa kama mnyama wa tabaka la juu ambaye tabia na maisha yake hutegemea uzawa wake na mazingira yake. Ni kwamba binadamu hurithi tabia zake za kibinafsi pamoja na haja zake za kiasilia na huwa anafuata, bila hiari, nguvu za kijamii na kiuchumi katika familia, tabaka na kundi alimozaliwa. Waandishi wanaufuata nadharia hii aghalabu huzingatia maswala asilia ya kisayansi katika maisha huku wakiwasawiri wahusika wao kama walio na nguvu na mivuto ya kinyama kama vile ulafi na hamu kubwa za kufanya mapenzi. Hatima au mwisho wa riwaya ya kiasilia aghalabu huwa ni tanzia.
Watunzi waliotunga kazi zao kwa kuzingatia nadharia hii wameshikilia ama mkondo wa kimaumbile, ambapo wamesisitiza hali ya kinyama aliyo nayo binadamu au mkondo wa uchumi wa kijamii ambapo binadamu anasawiriwa kama aliyeshiriki katika kujaribu kuishi katika ulimwengu asioulewa vilivyo. Kwa hivyo mara nyingi binadamu anaongozwa ni majaaliwa kwani hivyo ndivyo alivyopaswa kuwa.
Hivyo basi mhakiki anayezingatia nadharia hii hana budi kuona kama kweli visa vilivyo katika kazi anayoipitia vinaonyesha binadamu katika hali halisi ya kimaumbile na uasilia. Uasilia basi huwa ni kueleza chanzo cha maisha, hulka, mitazamo, na mipangilio ya maisha ya binadamu kama tuionavyo leo. Kwa mfano masomo mbali mbali yametumia mtizamo huu zikiwemo falsafa zilizoongoza ufemisnisti ambapo wengi walijaribu kuchunguza asili ya tofauti za kijamii kati ya mme na mke na kwa nini mme akatukuzwa huku mke akidunishwa. Huu ni mtizamo unaochukulia maisha ya binadamu kama fululizi yakiwa yanaanza na kiwango cha chini (cha kinyama) hadi cha juu (cha ustaarabu). Nyingi za hadithi na visa asili vya tamaduni zetu vyaweza kuchunguzwa kwa kuelemea mtizamohuu.
NADHARIA YAUMUUNDO
Katika miaka ya kwanza ya karne hii, mwanaisimu kwa jina Ferdinard De saussure alipendekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo
inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo. Alizua istilahi `parole' na
`langue' kueleza maoni yake: `Parole' au uzungumzi ni lugha katika matumizi na hiki ndicho walichokizingatia wanaisimu wa awali, lakini Saussure alivutiwa na mfumo wa kinadharia unaounda lugha zote au `Langue' - yaani masharti au kaida zinazoiwezesha lugha kuwepo na kuweza kufanya kazi.
Kazi hii ya Saussure ndiyo iliyozaa mkondo unaojulikana hivi sasa kama umuundo. Muundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi. Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao. Katika miaka ya 1950, mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii . Hasa alichotaka kuendeleza ni dhana ni kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na cha ndani (deep). Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Dhana hii ya uwili ilijitokeza katika nadharia nyingine za kijamii kama vile katika kazi ya Sigmund Freud ambaye aligawa mambo katika kiwango cha juu juu (manifest) ambacho chonekana na kila mmoja na kiwango cha ndani (latent) ambacho hupatikana kwa uchunguzi zaidi na ambacho ndicho hasa hueleza maana halisi; vile vile kazi ya Marx ilidhihiri uwili huu alipoeleza dhana ya juu juu ya ukengeushi (false consciousness) na hali halisi ya mambo ya unyonyaji(exploitation).
Kwa ujumla twaona usomi wa kuitizama jamii kwa uwili unaokinzana (binary opposition) ambao ulisambaa katika nyanja nyingi za usomi.
Awali ya hapo, anthropolijia ilizingatia makundi au makabila maalum ya watu ambayo yalizingatiwa kivyao, mifuma ambayo ilidhaniwa kwamba haibadiliki, lakini Levi-strauss alijishughulisha na mifumo inayohimili jamii zote. Strauss alidai kwamba pana muundo maalum ambao waweza kutumia kueleza jamii zote za ulimwengu, kama vile ilivyo na somo la hisabu au la uchumi ambapo pana njia (formula) ambayo yaweza kueleza maswala mengi katika somo hilio. Hapo ndipo dhana za umuundo zilipoingia
katika masomo mbali mbali hasa yale ya sayansi ya jamii na fasihi. Saussure alitoa maelezo ya nadharia changamano kuhusu lugha, na ni misingi ya nadharia zake inayotoa nguzo ya mbinu za umuundo. Ingawa huwa tunatumia lugha kuzungumza kuhusu maisha, Saussure hakulizingatia jambo hilo bali alisisitiza kwamba lugha ni kiungo kamili kinachojisimamia. Kwamba ni kiungo kilicho na masharti na sheria zake. Hivyo basi kuwepo kwa vitu duniani hakuathiri aina ya lugha iliyopo. Isitoshe, alidhamiria kudai kwamba lugha kwa kujisimamia haibadiliki wala vipande vyake haviadhiriwi na mabadiliko yoyote ya kijamii.
Katika mkabala huo, neno ni ishara huru inayoelezwa kwa kutofautishwa na nyengine. Lugha ni mfumo wa uhusiano kati ya viungo kadhaaa vinavyoijenga; ni muundo, sio kitu. Dhana hii yaweza kueleweka zaidi tukizingatia maneno ya Saussure ya
`kionyeshi' na `kinachoonyesha'. Neno katika lugha ndilo `kionyeshi' na dhana inayorejelewa ni neno hilo ndiyo `kinachoonyeshwa'. Vyote viwili haviwezi kutenganishwa, lakini umuundo hujishughulisha zaidi na uhusiano wa vionyeshi na jinsi vinavyofanya kazi kuliko kuangalia nje ya mfumo wa lugha, yaani kinachonyeshwa.
Kwa msingi kabisa, Saussure alizingatia zaidi mpangilio wa ndani wa lugha, ule muundo wake na sio mahusiano ya vipande vyake.
Wahakiki wanoegemea mkondo wa Saussure huzingatia kwamba matini husika ni mfumo unaojisimamia na hivyo basi huwa hamna haja ya kutumia mambo ya nje ili kuhakiki kazi ya fasihi. wahakiki huzingatia matini kama kiungo kamili kinachoweza kuhakikwa kivyake. Hivyo basi mhakiki wa umuundo hujaribu kuweka sarufi ya matini pamoja na sheria za jinsi matini hiyo hufanya kazi.
Mhakiki anayezingatia zaidi muundo wa lugha ya matini bila shaka hupuuza dhana ya jadi kuhusu kile matini hiyo huweza kutueleza kuhusu maisha; na hivyo basi hufanya mtindo wa kazi yenyewe kiini cha uhakiki wake. kwa hivyo wahakiki wanaotumia nadharia ya umuundo hujaribu kuzingatia matini peke yake huku wakiepuka kuifasiri kazi ile kulingana na kaida zilizowekwa kuhusu jinsi matini hufanyakazi.
Hata hivyo, huenda njia hii isiwe ya kufaa sana kwa sababu huwa inachukulia kwamba kila kitu kimeundwa katika mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine yaliyo nje yake. Ama kwa hakika, hata lugha yenyewe haiwezikabisa kufanya kazi bila kuathiriwa na mambo mengine kama vile mazingira yake.kama
tulivyotaja katika utangulizi wa sehemu hii hapana nadharia inayojitosheleza na isiyo na upungufu fulani. Upungufu wa nadharia hii ndiyo uliochochea kuzuka kwa Umuundo- mpya.
NADHARIA YAUMUUNDO-MPYA
Tunatumia neno Umuundo-mpya kuonyesha mtizamo wa kimuundo katika fasihi ambao ulitokea baada ya Umuundo. Japo dhana hii haiwezi kupewa maana moja maalum, imehusishwa na maendeleo kutoka au katika kazi za Derrida (1973, 1976), Lacan (1977), Kristeva (1981, 1984, 1986), Althusser (1971) na Foucault (1978, 1979a na b, 1981, 1986). Kazi hizi nazo zilichangiwa na kazi za Ferdinand de Saussure na Emile Benveniste (kuhusu isimu-jamii ya umuundo), kazi ya umarx hasa kupitia nadharia ya itikadi iliyoendelezwa na Louis Althusser, na kazi ya tathimini-nafsi ya Sigmund Freud na Jacques Lacan. Kazi hizi zimetoa athari mbali mbali kwa nadharia tofauti lakini zote zinazingatia makisio sawa kuhusu lugha, maana, na ubinafsia(subjectivity).
Lugha yachukuliwa kama nguzo maalum ya uainishi wa mpangilio wa jamii, maana za kijamii, nguvu na urazini wa kibinafsi. Hii ni kwa sababu ni katika lugha ambapo maana za mpangilio wa jamii na matokeo yake ya kisiasa na kijamii hujengwa na kupingwa. ni kupitia lugha ambapo hisia na maana yetu ya kibinafsi (ambayo inatufasili) hujengwa. Aidha, lugha haielezi ubinafsi wa kipekee wa mtu bali hujenga ubinafsia wa mtu kwa njia zilizojengeka katika miundo ya jamii yake. Katika Umuundo-mpya, ubinafsia sio hali yenye umoja au isiyobadilika, bali hubadilika kila mara ili kuchukuana na hali halisi ya kihistoria na kisiasa ili kudumisha nafasi ya mhusika katika jamii.
Umuundo-mpya, kama nadharia nyinginezo ina makisio fulani kuhusu lugha, ubinafsia, ufahamu, na ukweli. Nguzo zake, ambazo zatokana, kama tulivyotaja hapo juu, na mwanaisimu wa kiimuundo Ferninard de Saussure, ni kwamba lugha, badala ya kudhihirisha uhalisi wa kijamii uliopo, huwa yatujengea uhalisi huo wa kijamii. Kwa hivyo sio uhalisi wa kijamii wala ulimwengu asilia huwa na maana zinazodhihirishwa ni lugha. Lugha mbali mbali pamoja na matumizi mbali mbali ya lugha moja huugawa ulimwengu na kuupa maana kwa njia tofauti ambazo haziwezi kupatana ili kuunda kigezo kimoja kinachodhihirisha uhalisi wa jamii. Kwa mfano, maana ya tajiri hutofautiana katika lugha mbali mbali na hata kati ya miundo tofauti ya lugha moja, nahutegemea
matumizi na muktadha wa matumizi hayo. Ndiposa hapana maana moja ya neno au fungu la maneno.
Miundo yote ya umuundo-mpya huchukulia kwamba maana hujengwa katika lugha na huwa yule anayezungumza lugha hiyo hawezi kuhakikisha maana hiyo. Kwa hivyo tofauti na maoni ya Saussure, maana huzaliwa na kuundwa kwa njia mbali mbali. Hata hivyo nadharia hii hukubaliana na wazo lake kwamba lugha haimuliki maana; bali maana hukuzwa katika lugha na kwamba ishara hazina maana ya kivyake bali hupata maana katika mkururo wa lugha pamoja na tofauti yake na ishara nyingine. Dhana hii ni muhimu sana kwa sababu yadhihirisha lugha kama chombo cha kijamii ambacho chapingwa na kung'ang'aniwa.
Kulingana na nadharia hii basi, neno 'mama' kwa mfano, huwa halina maana ya kindani inayotokana na lugha husika bali huwa na maana za kijamii zilizotokana na lugha hiyo na ambazo zinakinzana na kubadilika kulingana na mazingira na kipindi cha kihistoria. Kwa hivyo kinyume na maoni ya wanamuundo kama vile Levi-Strauss walioshikilia kwamba maana ya kisa, kwa mfano, ipo katika matini na maana hiyo hiyo hutokea katika matini nyengine yoyote, nadharia hii yaeleza kuwa maana ya kisa ni amali ya msomaji/msikizi (hadhira) na kwamba pana fasili mbali mbali za kisa hicho kulingana na muktadha. Hivyo basi kwa umuundo-mpya twaweza kueleza kuwepo kwa wingi wa maana pamoja na mabadiliko yake kwa kuona maana sio kama iliyojengwa katika ishara zisizobadilika bali kama iliyo katika viashiria (signifiers) ambapo kiashiriwa (signified) hubadilikabadilika. Hapo ndipo alipojikita Derrida ambaye aliingiza dhana ya muktadha katika kueleza maana katika lugha na matini.
Umuundo-mpya ulimulika kazi ya Marx huku ukijaribu kuonyesha ufinya wa kuzingatia tu mahusiano yaliyopo kati ya wafanyakazi na walioshikilia nguvu za kuzalisha mali. Ni kwamba umarx haukudhihiri hali kwamba uhalisi wa kijamii huwa ni tofauti kwa wengi na katika miktadha mbali mbali. Isitoshe, uhalisi huo wapaswa kuzingatiwa kulingana na athari zake za kijamii ambazo hutoa maana tofauti kwa wanajamii tofauti. Umarx ulidunisha ubinafsi wa fikira, hisia, tajiriba, na mielekeo (ubinafsia) ya watu ambayo ni muhimu katika kueleza mahusiano ya kijamii. Ni katika kigezo hiki cha ubinafsia fikira na hisia za mtu binafsi, hali yake ya kipekee isiyofanana na mwengine, jinsi anavyojiona na kujielewa dhidi ya ulimwengu, huchukuliwa kama
nguzo kuu ya ummundo-mpya. Wahakiki wanaozingatia nadharia hii basi huongozwa na dhana ya kubadilika kwa maana katika miktadha mbali mbali na hivyo basi kuwashurutisha kuzingatia muktadha wa kazi hiyo kama nguzo ya kueleza kazi hiyo.
NADHARIA ZAUFEMINISTI
Aghalabu, uhakiki unaozuka miaka ya karibuni husisitiza umuhimu wa kuchunguza kazi yenyewe ya fasihi. Hata hivyo, yaelekea kwamba kila msomaji huwa na fikra za kiawali ambazo huziingiza katika kazi anayoipitia. Fikra hizi, kwa kawaida, huwa ni nuru ya maadili na imani muhimu za jamii husika wakati huo. Hali hii ndiyo iliyozaa Ufeministi ambao hujaribu kukiuka mitizamo ya kiume ambayo yaelekea imetumiwa sana katika jamii. Tukiangalia mifano ya nadharia tulizozitaja hapo awali, twaona kwamba waitifaki wake wote ni wanaume; na kama nadharia yaweza kuhusishwa na maoni ya mtunzi yaliyotokana na tajiriba yake ya kijamii basi ni wazi kwamba maoni ya wanawake hayapo pale. Hii ni kwa sababu wanaume na wanawake aghalabu huathiriwa na maisha ya kijamii kwa njia tofauti kwani misingi na kaida za kijamii zimejengwa ili kudhihiri na kuendeleza tofautihizo.
Nadharia hii hudhamiria kuonyesha kwamba uana na uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke ni mambo ya kati kabisa katika fasihi. Uhakiki huu pia hupiga hatua mbele na kuonyesha uhafifu wa hali ilivyo hasa katika nadharia nyingi zauhakiki.
Wahakiki wanaozingatia nadharia hii hudai kwamba tahakiki za kijadi zimekandamiza mjadala kuhusu uana jambo ambalo yaelekea ni kwa manufaa yao.
Kwa hivyo azma kuu ya Ufeministi ni `kusoma upya' kazi za fasihi ili kusisitiza umuhimu wa vipengele vilivyopuuzwa na wahakiki wengi au ambavyo hawangeviona kwa sababu walikuwa wanafanya kazi katika nadharia za kijadi zinazomtukuza mwanaume.
Ama kwa hakika Ufeministi ni siasa. Siasa kwa sababu mfumo huu wa uhakiki unaelekezwa katika kubadilisha uhusiano uliopo kati ya wanaume na wanawake uliopo sasa. Uhusiano huu, ambao umejaa mivutano, hughubika miundo yote ya maisha pakiwemo familia, elimu, kazi na siasa, utamaduni na hata mambo ya starehe na anasa. Hivyo basi, kwa kifupi ni kwamba uhusiano huu huongoza jinsi wanajamii wanavyoishi, wanachotenda, wanayemtendea, na jinsi watakavyokuwa siku za usoni.
Kama ilivyo na mitizamo mingine ya kijamii, Ufeministi una mizizi yake katika siasa ya ukombozi. Hasa, nadharia hii ilianguliwa katika muungano wa ukombozi wa wanawake uliopamba moto kunako miaka ya sitini (hasa Marekani). Baadhi ya mambo yaliyozingatiwa na muungano huu ni kuunda upya uhalisi wa mwanamke kwa kupangua na kudhihirisha miundo ya kijadi ambayo inamtukuza mwanamme na kumkandamiza mwanamke.
Kutokana na muungano huu, palizuka nyanja tatu kuu za Ufeministi; Ufeministi huru (liberal feminism), Ufeministi wa kijamii (socialist-feminism), na Ufeministi mapinduzi (radical feminism). Japo nyanja zote tatu zimegusia muundo wa jamii na tofauti za kimaumbile kati ya mwanamme na mwanamke, kila moja inahimiza mkondo fulani wa maoni. Wafeministi huru huchukua kwamba maisha ya jamii na uamuzi wa kupata watoto unategemea wahusika wenyewe; na kusisitiza uhuru wa wanawake kama watu binafsi wanaopaswa kuwa na uchaguzi ambao haufungwi na tofauti za kiuana. Kwa hivyo nia ya mtizamo huu ni kuona kwamba mwanamke anapata nafasi ya kujichagulia mkondo wa maisha anaotaka kuuchukua. Aidha, mtizamo huu hupendekeza pawe na usawa katika ulezi wa watoto na iwe ni kazi yenye malipo kama kazi nyinginezo. Kama hili litatimizwa, basi atakayehusika katika kazi hiyo, awe amechagua mwenyewe sio kwa kushurutishwa ni sababu za kijamii au kimaumbile.
Katika Ufeministi mapinduzi hamna nafasi ya jamii kama ilivyo hivi sasa kwa sababu mtizamo huu unasisitiza kwamba ukandamizaji wa wanawake umehusishwa na tofauti za kimaumbile. Hususa, jamii yachukuliwa kama chombo kikuu kinachoendeleza ukandamizaji wa wanawake na suluhisho ni kutenganisha wanawake na wanaume ili wanawake waweze kutawala miili na maisha yao bila kuongozwa na wanaume.
Ufeministi wa kijamii ni mtizamo unaochukua baadhi ya maoni yaliyoendelezwa na Karl Marx hasa kuhusiana na suala kwamba hali ya maisha ya mwanadamu ni zao la mahusiano ya kijamii ambayo huendelezwa na kubadilishwa na jamii husika. Kwa hivyo mtizamo huu hauchukulii mfumo wa kuumeni/upatriaki kama dhana moja bali kama muundo wa ukandamizaji unaobadilika kihistoria. Kwa hivyo masuala ya ubaguzi, ukapitolisti, na upatriaki ni namna za ukandamizaji zinazohusiana. Kwa mtizamo huu, wanaume wanapaswa kuhusishwa katika nyanja ya kulea watoto na kuwaacha wanawake wafanye uchaguzi wa maisha yao.
Mitizamo hii mitatu inapoingia katika fasihi huwa ni kama yachungua kazi za fasihi zinazoendeleza taasubi za kiume na hivyo kuzipinga na kuzipuuza. Aidha, inadhihirisha jinsi fasihi inavyotumiwa kuendeleza taasubi za kiume pamoja na kumkandamiza mwanamke. Vile vile mojawapo wa nguzo za Ufeministi ni kwamba hakuna nadharia yoyote ya fasihi inayotambuliwa vilivyo ambayo iliendelezwa na mwanamke. Hivyo basi, nadharia hii yaendelea, kwa vile mwanaume ameishi kujinufaisha kwanza, kila nadharia anayoiendeleza ni chombo kimoja cha kupalilia nafasi yake katika jamii na pia kuhimiza ukandamizwaji wa mwanamke.
Nadharia hii yaamini kwamba ujenzi wa maana anayodhamiriwa kupata msomaji ni zao la maana ambayo tayari ipo katika jamii. Na kwa vile waandishi wengi ni wanaume, mtizamo wa wanawake pamoja na tajiriba zao za maisha hazipo katika kazi nyingi za fasihi. Na hili ladhihirika katika usawiri na uwasilishi wa wanawake katika kazi za fasihi ambapo mtunzi, ambaye aghalabu ni mwanaume, humsawiri mwanamke kulingana na tajiriba ya kiume na kama anavyotarajia mwanamke kuwa. Ndiposa, Wafeministi walioanza kazi za uhakiki kunako miaka ya sabini, wanasisitiza zaidi kazi zilizoandikwa na wanawake na zinazoeleza tajiriba ya mwanamke kama aijuavyo na aionavyo. Na pia wanazingatia kazi zinazopinga taasubi za kiume. Kwa mifano ya kazi hizi za tahakiki angalia Showalter (1977), Gilbert na Gubar (1979) na Jacobus (1979).
Msingi wa ufeministi upo katika imana kwamba uana na tofauti zake ni tokeo la kijamii sio la kimaumbile; hivi kwamba hapana kilicho katika mwili wa mwanamke kinachomshurutisha kuwa mwuguzi na mwanamme kuwa daktari, mwanamke kuwa karani na mwanamme kuwa mkuu wa kampuni. Hulka, sifa, na amali walizonazo wanaume na wanawake ni zao la kijamii ambalo huzingatia kuwatayarisha ili kuchukua nafasi za kijamii walizotengewa. Ndiposa twaona hata kama hapana uhusiano wa moja kwa moja kati ya maumbile yetu kama wanaumme na wanawake na kazi za kijamii tunazozifanya pana uwiano usiotatanika kati ya kazi hizo na majukumu ya kijamii tunayolelewa kuyachukua. Hivyo basi kama hali zetu na tofauti zetu ni tokeo la kimakusudi la kijamii hali hiyo yaweza kubadilishwa. Huo ndio msukumo wa ufeministi.
Mhakiki anayezingatia nadharia hii huwa basi anaiangalia kazi ile ya fasihi kama iliyoumbwa kutokana na tajiriba za kiuana alizonazo mtunzi. jinsi alivyowasawiri wahusika wake na sifa anazowapa huweza kueleweka iwapo tunafahamu maana ya kuwa
mwanamke /mwanamme katika jamii hiyo na muktadha huo. Mara nyingi huenda maoni ya mtunzi kama yanavyojitokeza katika sifa na hulka za wahusika wake huwa ni maoni yake au msimamo wake kuhusu uana kama alivyofundishwa na jamii yake au kama anavyotarajia uwe. Mara nyingine huwa anasawiri wahusika waliokiuka misingi ya maana na matarajio ya sifa zao za kiuana kama njia ya kupendekeza mabadiliko katika hali halisi ya maisha.
Mara nyingi wengi wamechukulia Ufeministi kama nadharia inayopiga vita wanaume na hivyo basi kutoielewa ipasavyo. mtizamo huu aghalabu umetokana na jinsi dhana ya ufeministi ilivyosambazwa hasa nchi za kimagharibi ambapo wanaume walisawiriwa kama adui anayestahili kupigwa vita na wanawake. ukweli ni kwamba ufeministi husaidia kudhihirisha kwamba wanadamu wamelelwa ili kuchukua nafasi maalumu za kijamii ambazo zadhihirisha mahusiano kati ya wanawake na wanaume. Ni uhusiano huu ambao Wafeministi wengi wanaagiza uangaliwe upya ili kuwapa wanawake na wanaume nafasi sawa katika kumudu maisha na mazingira yao. Hivyo basi wanawake na wanaume hawakinzani bali wanasaidiana; lililo muhimu ni kwamba usaidizi huo uwe hauna masharti ya kuwakataza uhuru wa kuchagua jinsi na maana sawa aitakayo mhusika (awe mwanaume au mwanamke) katika kuyaendeleza maisha na kumudu mazingirayake.
NADHARIA YAUHALISIA
Nadharia hii katika upana wake, humaanisha uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi. Nadharia hii ilizuka katika karne ya kumi na tisa hususa kwa sababu za kupinga mkondo wa ulimbwende. Mhalisia huamini katika matokeo ya mambo na ukweli anaouzingatia ni ule unaoweza kuonekana na kuthibitishwa kwa tajiriba. Vile vile, wahalisia huiamini demokrasia kama hali ya maisha, na malighafi anayochagua kueleza maisha ni yale ya kawaida, ya kadiri na ya kila siku. Hivyo basi uhalisia hujikita katika mambo yaliyopo, tukio mahsusi na matokeo yanayowezakuthibitika.
Imani ya mhalisia ni kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuwaweka wanajamii husika katika ulimwengu wao wa kawaida, wa kweli, na halisi. Hivyo basi hata picha za ulimwengu atakazoumba msanii, zapaswa kudhihirisa hali hiyo. Kama tulivyotaja hapo juu, uhalisia ulizuka ili kupinga ulimbwende ambao ulizingatia mambo ya kihisia na
yasiyo halisi maishani. wahalisia wanaona kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuwa sahihi, iliyo wazi na inayozingatia maswala halisi moja kwa moja bila kupiga chuku. Maswala ya kati maishani huhusu maadili na hivyo basi msanii hana budi kuyazingatia kwa kiwango fulani cha uteuzi. Wahalisia wanashikilia kwamba msanii anapaswa kuteua lakini akiwa na nia ya kuendeleza maswala yake kama yanavyowahusu watu katika hali halisi za maisha. Mwelekeo huu wa uhalisi katika utunzi unamfanya mhalisia kumwona mhusika kama kiungo muhimu sana katika kazi ya fasihi (hususa riwaya). Hivyo basi anazingatia saikolojia ya wahusika katika hadithi.
Mhakiki anayezingatia nadharia hii ya uhalisia, hupembua namna mtunzi alivyodhihirisha uhalisi wa mambo kupitia maudhui aliyoyazingatia na wahusika aliowasawiri. Hivyo basi, mhakiki hutizama jinsi ukweli ulivyodhihirishwa katika juhudi za mtunzi za kuchora hali halisi ya mambo katika wakati maalum. Kwa muhtasari basi msanii anatarajiwa kusawiri wahusika, matukio na mandhari yanayokubalika na kuaminika katika jamii ya wakati wake. Ufahamu wa mazingira na maisha anayoyalenga mtunzi ni nguzo muhimu kwa mhakiki wa kihalisia. Shida inayoletwa na nadharia hii ni kuchukulia kwamba uhalisi na maana yake hauna utata wowote katika jamii yoyote, ni kwamba unachukulia kuwa watu wote katika jamii hiyo waona uhalisi mmoja na kuwa na fasili sawa kuhusu maisha yao.
NADHARIA YA UHALISIA-NAFSI(THATHMINI-SAIKOLOJIA)
Kiini cha nadharia hii ni tabia ya ndani ya mtunzi ambapo nia, azma, motisho na fikra za mtunzi ndizo huchukuliwa kama nguzo ya utunzi. Mwitifaki mkuu wa mkondo huu ni mtaalamu wa elimu ya nafsi Sigmund Freud ambaye mbali na kueleza vitendo vinavyozuliwa na nguvu za ndani za mtunzi alieleza kwanini vitendo hivyo hutokea.
Kimsingi, Freud alielemea maana ya kuwa utamaduni hutumiwa kufinya na kuondoa hisia na hamu zetu za kinyama tulizonazo ili kutustaarabisha na kutuwezesha kuisha na wengine. Lakini huwa hisia na hamu hizi hazitoweki bali hutokea katika sura mbali mbali za maisha yetu kama vile katika ndoto, matamanio, na michezo yetu. Wahakiki walioegemea mkondo huu waliingiza maoni ya Freud katika fasihi huku wakiiona kaziya mtunzi kama kielelezo cha hamu na hisiahizo.
Katika kueleza nguzo ya nadharia hii, Freud anamlinganisha mtunzi na mtoto anayecheza. Anasema kuwa kwa mtoto, jambo au kazi anayoipenda sana inayomridhisha, ni kucheza. Twaweza kusema kwamba mtoto awapo mchezoni, hufanana na mtunzi kwa ambavyo yeye (mtoto) huumba ulimwengu wake, au kwa maneno mengine yeye huvipanga upya vitu katika ulimwengu wake ili vimpendeze. Ni kosa kuchukulia kwamba mtoto huyu hatilii maanani huu ulimwengu wake; kinyume na hivyo, ni kwamba yeye huutilia maanani sana kiasi cha kwamba huhusisha kiwango kikubwa cha hisia zake. Ama kwa hakika, kinyume cha mchezo ni uhalisi. Ni katika ulimwengu huu wa mtoto ambapo anapata uhuru wa kutenda atakacho bila kukanywa na watu wazima. Hata ingawa kiwango kikubwa cha hisia zake huhusishwa katika huu ulimwengu wa mchezo, ifahamike kwamba huyo mtoto huubainisha ulimwengu wake wa mchezo na maisha halisi na hupenda kuvioanisha vitu vyake bunia na vile avipatavyo katika ulimwengu halisi. Ndoa hii ndiyo inayotofautisha kule kucheza na kuota (Phantasyzing).
Kulingana na nadharia hii, mtunzi hufanya kazi yake sawa na mtoto anayecheza. Yeye huumba ulimwengu wake bunia ambao anautilia maanani sana - yaani anahusisha kiasi kikubwa cha hisia zake pale - huku akiutengamisha na uhalisia. Jambo hili la kubuni hufaidi mtunzi kwa vile kazi yake huwa ya kuvutia kwa hadhira yake. Mara nyingi mtunzi hutumia visa halisi vya maisha na kuunda huu ulimwengu bunia wake ambapo mambo anayoyazingatia huwa ni yanayoweza kutokea.
Pana jambo lingine linalozingatiwa na nadharia hii. Baada ya mtoto kukua na kuacha kucheza na baada ya kupambana kwa miaka mingi kuhimili maisha katika uhalisia wake, huenda siku moja akajipata fikirani mwake amefikwa na ile hali ya kutenga mchezo na uhalisia. Jinsi watu wanavyokua ndivyo wanavyoacha kucheza na huonekana kana kwamba wamesahau raha waliokuwa wanapata mchezoni. Lakini yeyote anayemwelewa mwanadamu, hufahamu kwamba hakuna kitu kigumu kwake kama kusahau raha aliyowahi kupata. Ama kwa hakika hatuachi lolote, bali hulibadilisha na lingine, tukapata kitu chengine cha kuchukua nafasi ya shibe au utoshelezi uliyoletwa na mchezo. Yaani nafasi ya jambo moja huchukuliwa na lingine ili kuonekana kana kwamba la kwanza limetoweka. Hivyo basi wakati mtoto akuapo na kuacha kucheza, anachotengana nacho ni vifaa halisi, na badala ya kucheza yeye hushiriki ndoto.Hizi
ndoto, kulingana na nadharia hii, ndizo nguzo katika utunzi. Hii ni kwa sababu ni vigumu kuona ndoto za watu wazima ikilinganishwa na michezo ya watoto. Mtu mzima huona aibu kuwa na ndoto hizi kama amali za nafsi yake na kwa kawaida ataona ikiwa rahisi kukiri makosa yake kuliko kutoa kiini cha ndoto zake kwa yeyote.
Mchezo wa mtoto huongozwa na matamanio yake. Aghalabu yeye hucheza akiwa `mtu mzima' na katika michezo yake, yeye hushirikisha yale anayoyafahamu kuhusu watu wazima. Hana sababu yoyote ya kusetiri matamanio haya. Kwa upande ule mwingine, mtu mzima anafahamu kuwa hatarajiwi kuendelea kucheza au kuota, bali hupaswa kutenda mambo kihalisia, kiutu uzima; hivyo basi anongozwa na kufungwa na matarajio ya kijamii kwake. Isitoshe, baadhi ya matamanio yanayozua ndoto zake huwa ni yale yanayohitaji kusetiriwa yasijulikane kwa wengine kwani huwa ni kinyume na matarajio ya jamii. Hivyo basi hawezi kuyatoa hadharani lau yatachukuliwa kuwa ya kitoto na yasiyokubalika. Lakini ni lazima yatoke ili atue. Hapo ndipo anapata utulivu katika utunzi: anayatoa katika utunzi.
Kwa kawaida, chanzo na msukumo wa ndoto ni matamanio yasiyotimizwa, na kila ndoto hutokea kutimiza kila tamanio ili kuchukua nafasi ya uhalisia usioridhisha. Hivyo basi kazi ya fasihi, kulingana na mtizamo huo, huwa ni jaribio la kutimiza matamanio ya mtunzi ambayo hayakutimizwa katika ulimwengu halisi.
Uhusiano kati ya ndoto na wakati, kwa kawaida huwa muhimu sana na huchukuana na vipindi vitatu - - navyo ni vipindi vinavyohusika katika ujenzi wa dhana katika binadamu. Kazi ya fikra huanzishwa na jambo linalotokea wakati uliopo na linalosismua matamanio ya mhusika. Kutoka hapo linarejelea tajiriba ya awali ambapo tamaa hiyo ilitimizwa; kisha inajenga hali inayohusisha wakati ujao inayowakilisha kutimizwa kwa tamaa hiyo. Kile kinachotokea ni ndoto inayobeba chembe chembe za asili yake kutokana na hali iliyoizaa hiyo ndoto pamoja na ukumbufu (memory). Hivyo basi wakati uliopita, uliopo, na utakaokuja huunganishwa pamoja na uzi wa matamanio na kudhihirika katika utunzi.
Tunachokipata tangu michezo ya utotoni hadi ndoto na hadi kazi za sanaa ni kwamba Freud anataka kuonyesha jambo moja kuu; kwamba binadamu kwa kawaida huwa na hamu ya kubadili kilichopo na hasa kile kisichoridhisha au kisichotosha katika ulimwengu halisi. Kwa hivyo fikra zinaendelezwa katika kubuni hali ambapo matamanio
ambayo hayajaridhishwa hutimizwa. Hapo ndipo twaona kazi ya fasihi ikielezwa kama zao la ndoto na matamanio ya mtunzi anayehusika.
Mhakiki anayezingatia nadharia hii ataichukulia kazi ya fasihi kama kielezo cha matamanio ya mtunzi na juhudi zake za kuyatimiza katika ulimwengu wa sanaa. Hapo inahitajika wahakiki kwa kiwango fulani wazingatie maisha halisi ya mtunzi husika ili kuielewa kazi yake ipasavyo. Nadharia hii yaweza kutumiwa kueleza sanaa kama vile ya sinema, muziki, na drama ambazo maudhui yake huenda yakadhihiri mambo ambayo hayatendeki kwa ulimwengu halisi lakini ambayo yanasisimua na kuvutia hadhira kwa ambavyo yanatoa picha ya mambo ambayo yapaswa kutokea.
HITIMISHO
Ni kweli kwamba hizi ni baadhi tu ya nadharia za uhakiki zilizopo, hata hivyo tumejaribu kuonyesha kwamba kila nadharia ina kaida na kanuni zake ambazo huzitoa ili kuzingatiwa. Hamna nadharia yoyote ambayo yaweza kusemekana imejitosheleza katika uhakiki. Tutakariri tena kwamba nadharia anayoichagua mhakiki wa fasihi yapaswa kuongozwa na anachotaka kuthibitisha kwa kazi yake n.k.
Wakati mwingine mtunzi wa kazi ya fasihi huwa hazingatii nadharia yoyote katika utunzi wake na hivyo basi huenda nadharia yoyote ya uhakiki itumiwe kuihakiki kazi yake mradi tu pawe na ithibati za kutosha katika kazi hiyo kuchukuana na maoni ya nadharia hiyo. Kwa upande mwingine huwa inadhihirika kwamba mtunzi alizingatia nadharia maalum katika kutunga kazi yake na hivyo basi nadharia hiyo hiyo itakuwa mwafaka zaidi katika kuihahiki kazi hiyo. Kwa mfano kitabu cha S.A Mohammed, Dunia Mti Mkavu hudhihirisha uzingatifu wa nadharia ya Umarx na tahakiki yoyote inayofanyiwa kitabu hicho huenda ikajikita katika misingi ya nadharia za ki-marx. Hali kadhalika kitabu cha E. Kezilahabi, Rosa Mistika kimezingatia nadharia ya utamaushi (Extistentialism) na tahakiki zake mara nyingi huzingatia nadhariahiyo.
Pana nyakati ambapo kitabu kimoja au kazi moja ya fasihi huenda ikazingatiwa kwa nadharia zaidi ya moja kulingana na azma ya mhakiki. Hivyo basi hatuwezi kubana kazi yoyote ya fasihi kwa nadharia moja maalum. Kama tulivyotangulia kutaja, hakuna kazi ya uhakiki ilyo kamili na kila kuchapo, panazuka nadharia mpya ya uhakiki. Lililo dhahiri katika kazi nyingi za uhakiki ni kwamba zinachukuana na maelezo kuhusu
maisha ya wanadamu na mikondo na mikinzano inayoyakumba. Jinsi wanadamu wanavyojaribu kuuelewa ulimwengu wao ndivyo wanavyozua nadharia mbali mbali za kueleza maisha na tabia za wanajamii.
Kwa jumla tumeona kwamba uhakiki ni kitendo kinachoongozwa na kaida maalum zilizopo. Hivyo basi mhakiki huwa na nafasi ya kuzizingatia huku zikimwongoza katika kazi yake.
SURA YA TATU
MAENDELEO YAFASIHI-ANDISHI
Kwa vile tunazingatia kwa kijumla kazi za fasihi-andishi katika kazi hii yetu, ni muhimu tuchukue nafasi ndogo tueleze jinsi kazi hizi zilivyoanza na kuendelea.
Tutazingatia katika sehemu hii maendeleo ya tanzu tatu kuu za fasihi andishi - Tamthilia, Riwaya na Ushairi - ambazo aghalabu huchukua vigezo sawa katika kuhakikiwa.
Kwa jumla, maendeleo ya tanzu hizi tatu za fasihi yamepitia vipindi mbalimbali katika historia na kila kipindi kimekuwa na athari kwa tanzu hizo, yaani mabadiliko ya kijamii kihistoria, yamedhihirika katika tanzu hizi za fasihi hususa katika fani na maudhui.
Jambo hili litadhihirika zaidi wakati tutakapokuwa twazingatia utanzu mmoja mmoja.
TAMTHILIA
UTANGULIZI:
Tamthilia ni utanzu wa fasihi- andishi ambao twaweza kusema ni zao la mabadiliko ya fasihi kama kipengee cha utamaduni wa jamii. Jina tamthilia limetokana na kitendo `mithilisha' ambacho maana yake ni kufananisha au kumithilisha hali ya maisha fulani kwa vitendo. Tamthilia basi ni maigizo ya matukio au visa fulani kwa uhalisi wake kwa ajili ya kuyasawiri maudhui au maelezo fulani.
Dhana ya tamthilia imekuwepo tangu asili na jadi hata katika jamii zetu za kiafrika kabla ya athari za kinagharibi kupitia ukoloni, kwa vile pamekuwepo sanaa mbali mbali za maonyesho ambazo humithilishwa na tamthilia. Ama kwa hakika ugeni au tofauti ya tamthilia ya fasihi - andishi na sanaa za maonyesho za hapo awali, ni katika kugawanya mchezo katika vijisehemu - matendo na maonyesho na kumpa kila mhusika sehemu maalum ya kushiriki. Mtindo huu bila shaka ni zao la mabadiliko ya kijamii. Kabla ya tamthilia tuipatayo siku hizi, maigizo kwa jumla yalihimiza ushirikishaji wa hisia kama
zinavyovutia bila shuruti. Hata wahusika walizingatia mambo papo hapo bila kupanga vile au kakariri yaliyohifadhiwa pahali fulani; yaani hapakuwa na nafasi ya kupanga na kuandika maigizo hapo awali kama ilivyo katika tamthilia ya siku hizi.
Ama kwa hakika, mtindo tunaoupata katika tamthilia ya siku hizi umekopwa kutoka kwa ule wa fasihi ya kimagharibi ambao ulitufikia kupitia kwa elimu ya kikoloni. Mfano mzuri wa kazi zilizotoa athari hii ni zile za Shakespeare anayefahamika sana kwa utunzi wa tamthilia za kiingereza. Tamthilia ya aina hii hugawika katika matendo, na kila tendo huwa na maonyesho kadha. Kila onyesho huwa na waigizaji, kila mmoja wao akiwa na sehemu yake maalum ya kuigiza ambayo ametayarishiwa namtunzi.
Tamthilia hutofautiana na tanzu nyengine za fasihi kwa kuwashirikisha wahusika wake katika mazungumzo au vitendo ambavyo hubainisha hali ilivyo mbele ya hadhira. Tamthilia huihusisha sio tu lugha ya mdomo bali pia lugha bubu inayotokana na ishara za mwili wa mhusika. Kila mtunzi wa tamthilia huwaza jinsi kazi yake ingebainishwa jukwaani na ndiposa baadhi yao husisitiza mpangilio maalum wa mapambo

0 Comments