Mjadala huu umegawanyika

katika sehemu kuu tatu, kwanza
utangulizi ambapo tumefasili dhana mbalimbali zilizojitokeza katika swali hili,
pili ni kiini cha swali ambapo tumeangalia lugha ya kifasihi kulingana na
mawazo ya Wamitila. Katika sehemu ya hitimisho, tumehitimisha kwa kutumia
mawazo yetu kulingana na namna swali linavyotaka.
Ufafanuzi wa Dhana Muhimu
Mulokozi (2017), Fasihi ni sanaa ya lugha yenye
ubunifu unaojaribu kusawiri vipengele vya maisha, mahusiano, mazingira na hisia
za watu katika muktadha fulani. Udhaifu wa fasili hii ni kuwa imesisitiza suala
la ubunifu na kuacha vipengele vya lugha.
Naye M’ngaruthi (2015) anafasili fasihi kuwa ni kazi
yoyote ya sanaa inayowasilishwa kupitia lugha ama iliyoandikwa au kutamkwa kwa
njia ya ubunifu. Udhaifu wa fasili hii ni kuwa haijabainishwa imemlenga haswa
nani.
Kwa ujumla, fasihi ni sanaa inayotumia lugha ili
kufikisha ujumbe kwa jamii au hadhira iliyokusudiwa.
Wamitila (2016) anafasili lugha kuwa ni mfumo mzima
wa sauti na maneno yanayotumiwa na watu kuwasiliana. Udhaifu wa fasili hii ni
kwamba imeangalia suala la sauti kwa ujumla na kusahau kuwepo kwa sauti za
nasibu.
Habwe na Karanja (2012) wanafasili lugha kuwa ni
mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii wenye utamaduni
unaofanana ili kuwasiliana.
Kwa ujumla, lugha ni mpangilio au utaratibu wa sauti
za nasibu zinazosemwa na watu wenye utamaduni mmoja ili kufikisha ujumbe kwa
jamii.
Wamitila (2008) anaeleza kuwa lugha ya kifasihi ni
lugha ambayo hutumiwa kwa njia ya kisanaa yanahusisha matumizi ya lugha ambayo
si ya kawaida.
Hivyo basi, lugha ya kifasihi ni ule ubunifu
unaotumiwa na mtunzi wa kazi ya fasihi ili kufikisha ujumbe kwa jamii
iliyokusudiwa.
Ni kweli kwamba hakuna lugha ya kifasihi bali kuna
matumizi ya lugha katika fasihi kwani rai hii imeshadadiwa na wataalamu mbalimbali
kama Njogu na Chimera (2011:8-9) wanashadadia rai hii kuwa hakuna lugha ya
kifasihi bali lugha ya lugha ya kifasihi huigeuza lugha ya kawaida kuwa lugha
ya kifasihi, hii ina maana kwamba kauli isemwayo kuwa kuna lugha ya kifasihi
iliyoteula, inapwaya. Lugha zote hutumia sitiari, jazanda, methali n.k. Hivyo
basi, tutafute kitu kingine cha kueleza
dhana ya fasihi mbali na matumizi ya lugha.
Hivyo basi, tunathibitisha rai hii kwa kutumia
mawazo ya Wamitila (2008:67-107) kama ifuatavyo:
Lugha na suala la uteuzi
Wamitila (2008:69) uteuzi wa maneno katika kazi ya
fasihi hutegemea malengo ya kimawasiliano na kisanii ya mtunzi, japo kuwa
ushairi huchukuliwa kama tokeo la matumizi ya lugha kwa njia maalumu hata hivyo
haina maana kuwa uteuzi wa namna hii haupatikani katika nathari hivyo basi,
ikiwa tuna lugha ya fasihi tunatarajia lugha hiyohiyo itumike katika kazi za
kifasihi kama riwaya, tamthiliya na ushairi lakini sivyo tunavyotarajia kwani
ushairi una namna ya uteuzi wake maalumu ambao ni tofauti na nathari zingine.
Mfano ushairi una mtindo wa udondoshaji wa maneno lakini kazi nyingine kama
riwaya zikitumia mtindo huo huonekana kama ni njia hasi ya kujibainisha.
Lugha na suala la lahaja na lafudhi;
Lahaja ni lugha ambayo ina sifa za kiisimu
zinazoitenga na vilugha vingine katika lugha fulani maalumu. Msingi wa kuwepo
kwa lahaja tofauti na wa kijiografia, uchumi na misingi mingine katika jamii
inayohusika. Lafudhi ni dhana inayorejelea sifa za kimatamshi katika matumizi
ya lugha ambazo zinahusisha na mtumiaji maalumu wa lugha. Lugha ya Kiswahili
ina lahaja nyingi za kijiografia kama vile Kimvita, Kipemba, Kimtang’ata n.k.
Uchunguzi wa fasihi ya Kiswahili unadhihirisha tofauti hizi katika matumizi ya
lugha ya kazi za waandishi kadha. Toafauti za lugha huweza kutokeza katika
kiwango cha lafudhi ya mzungumzaji maalumu anayehusika tofauti hizi zinatokana
na ukweli kwamba hakuna wazungumzaji wawili wa lugha wanaotumia au kuzungumza
kwa namna sawa kila binadamu ana sifa za kipekee za kiisimu na upekee wa
kimtindo ambao unamtambulisha. Sifa hizi zinajitokeza pia katika kazi za
kifasihi kwa kuchunguza kwa makini lugha wanazopewa wahusika wenyewe kwa mfano
katika kazi za S. A. Mohamedi, (Kiza katika Nuru, 31)
“Haya lete Besa yangu ya jamaa zima…..alianza
Ashura. He, Ashura naye kwa rakadha, hata sijatua ukumbini…..”
Naye J. Habwe, (Cheche za Moto, 27)
“Bw.
Mulee, iko mambo gani sikia?”
“Mambo yapi? Mulee alimuuliza huku amemlenga macho”
Lugha na Tanzu za Fasihi
Lugha inayotumiwa katika kazi za kifasihi huweza
kuwa tofauti kutegemeana na utanzu wa fasihi unaohusika. Ipo miundo ya lugha
ambayo inahusishwa zaidi na utanzu mmoja wa fasihi kuliko tanzu nyinginezo kwa
mfano utanzu wa ushairi unatumia msamiati wa kale ukilinganishwa na utanzu wa
riwaya na tamthiliya. Pili, utanzu huu wa ushairi umetumia msamiati maalumu
ambao unapatikana tu katika utanzu huo pia kama tunavyoona inawezekana kazi za
kifasihi zikayakiuka matarajio haya ya matumizi ya lugha na kuchanganya lugha
tofauti tofauti.
Lugha na Usimulizi.
Usimulizi wowote wa kazi za kifasihi hutegemea lugha
kwa kiasi kikubwa, lugha ndio nyenzo kuu ya sanaa ya fasihi. Kwa misingi hiyo
ubunifu na usimulizi ndio unaleta utofauti kila msimulizi ndio hutumia ubunifu
wake tofauti na wasimulizi wengine ili kuvutia hadhira yake
Lugha na Sajili.
Lugha hutofautiana kutegemeana na mazingira/muktadha
inakotumiwa huu ndio msingi wa kile kinachojulikana kama rejesta. Rejesta hizi
huwa na sifa kadha wa kadha ikiwemo uwanja au mandhari, lengo la mahusiano n.k.
Hakuna namna moja ya uwasilishaji wa kazi moja huweza kutofautiana kutokana na
dhamira, wahusika na tamathali za semi. Hivyo, lugha ni nyenzo kuu ya kukuza na
kuendeleza maudhui na sajili kama kipengele muhimu cha lugha hiyo ambacho
kinashirikiana katika kuvyanza dhamira ya kazi inayohusika na sajili
inayotawala. Katika kazi fulani huashiriwa na kuelekezwa na uteuzi wa msamiati,
tamathali za semi na motifu zinazoelekezwa. Vilevile, suala la sajali na
usawiri wa wahusika hutegemeana na matumizi ya lugha katika muktadha maalumu
hutambulisha sajili inayohusishwa na wahusika wanaopatikana katika mazingira
fulani kama ni wasomi, wakulima au wafugaji. Pia, sajili na uashiriaji na
tamathali za semi hapa tunaangalia mbinu za uashiriaji zinazotumiwa na mtunzi
pamoja na tamathali za semi zinazoteuliwa lazima pawepo na mwingiliano wa
muktadha na mazingira yanayohusika au sijali inayotumia mbinu za uashiriaji na
tamathali za usemi ni mbinu zinazotumiwa na msanii au mwandishi na zinapaswa
kutumiwa kwa njia ya kuendeleza hilo.
Utata na Usayakini wa lugha na maana katika fasihi.
Utata ni sifa ya kilugha, kiusemaji ambayo huweza
kuwa msingi wa kueleweka kwa neno, kirai au kauli kwa namna tofauti. Hata
hivyo, utata si tamathali au mbinu za
kifasihi ambayo huteuliwa na mtumiaji bali ni sifa ya kiuasilia ambayo
hufungamana na lugha yenyewe. Utata wa kifasihi huweza kutokea kutegemea sauti,
maana au miundo. Hivyo basi, utata wa kifasihi unatokana na matumizi ya tamathali
za semi kama tashbiha, sitiari na taashira. Utata haupatikani tu katika matini
za kazi za kifasihi bali hata katika mazungumzo ya lugha ya kila siku.
Lugha na suala la uteuzi,
Uteuzi wa lugha katika kazi ya fasihi unaofanywa na
mtunzi wa kazi husika na uteuzi huu unathibitiwa kwa kiasi kikubwa na malengo
ya kimasiliano ya kisanii ya mtunzi maalumu. Suala hili la uteuzi wa lugha
hujitokeza kwa uwazi katika ushairi, ushairi huchukuliwa kama tokeo la lugha
kwa njia maalumu hii aina maana haupatikani katika nathari zingine vilevile
zipo riwaya nyingi zinaakisi mtindo wa lugha inayohusishwa na ushairi kama vile
mtindo wa lugha inayohusishwa na ushairi kama vile mtindo wa udondoshaji. Sifa
hii pia inapatikana katika kazi za Shaaban Robert, S. A. Mohamedi.
Hivyo basi, kimsingi hakuna lugha ya fasihi bali
kuna matumizi ya lugha katika fasihi kwa mfano ukichunguza kwa undani zaidi
tutaona hakuna lugha au mtindo mmoja ambao unapatikana katika kazi zote za
kifasihi. Kila mtunzi ana namna yake ya ubunifu katika uandishi na usimulizi wa
kazi za kifasihi na sio namna moja ya kujibainisha.
MAREJELEO
Habwe, J. na Karanja, P. (2012) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi:
Phoenix Publishers Ltd.
M’ngaruthi (2015) Fasihi Simulizi na Utamaduni. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Mulokozi, M. M. (2017) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili, Kazi za
Fasihi Vyuoni na Vyuo Vikuu. Dar es Salaam: Moccony Printing Press.
Njogu, K na Chimerah, R. (2011) Ufundishaji wa Fasihi; Nadharia na Mbinu.
Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Njogu, K na Wafula, R. M. (2013) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi:
The Jomo Kenyatta Foundation.
Wamitila, K. W. (2008) Kanzi ya Fasihi Misingi ya Uchanganuzi wa
Fasihi. Nairobi: Vide~Muwa Publishers.
_____________ (2016) Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide~Muwa
Publishers.
0 Comments