Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Leksografia: USAYANSI NA USANAA KATIKA UTUNZI WA KAMUSI



1.0  UTANGULIZI

Katika kazi hii tutajikita katika uchunguzi wa vipengele vya Kisayansi na Kisanaa katika utunzi wa kamusi. Ili kufikia lengo la kazi hii, sehemu kuu tatu zimezingatiwa ambazo ni fasili za dhana za msingi, kiini na hitimisho.

1.1  FASILI ZA DHANA ZA MSINGI

Wiegand (1984) akinukuliwa na Mdee ( 2010), utunzi wa kamusi ni sayansi ya kutunga kamusi. Anaendelea kusema kuwa, utungaji wa kamusi hujumuisha uorodheshaji wa msamiati wa lugha inayotungiwa kamusi pamoja na maelezo yenye kufafanua kila neno lililoorodheshwa kadri ya mahitaji ya mtumiaji aliyelengwa. Fasili hii ikichunguzwa kwa makini inabainika kuwa, mtaalamu huyu amezingatia usayansi na kupuuza vipengele vya sanaa ambavyo ama kwa hakika hutumika kukamilisha kamusi.

TUKI (2014) Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu katika maandishi, michoro, maigizo, nyimbo au uchongaji ni zao linalotokana na ufundi huo. Kwa ujumla Sanaa ni ubunifu alionao mtu katika kufanya au kutekeleza jambo fulani.

TUKI (2014) Sayansi ni elimu inayotokana na uchunguzi, majaribio, vipimo na kuthibitisha kwa muda uliopo. Hii ni kueleza kuwa sayansi ni maarifa yanayotokana na uvumbuzi, tafiti, uchunguzi na uchambuzi wa jambo fulani.

2.0 USAYANSI  NA USANAA WA KAMUSI

Ni kweli  kwamba kazi za utunzi wa kamusi ni ya kisayansi na kisanaa, ambapo michakato hiyo ndiyo hukamilisha nyenzo hii muhimu ya lugha. Kwakuanza kuuabiri usayansi ulipo katika kamusi ambapo hutokana na uzingativu wa kanuni na hatua mbalimbali katika kukamilisha utengenezaji wa kamusi.

2.1. USAYANSI WA KAMUSI

 Kwa kuegemea mawazo ya Mdee (2010, huu ndio usayansi uliopo katika utengenezaj wa kamusi.

2.1.1 Upangaji wa mradi wa kamusi,

Hii ni hatua ya mwanzo ambapo mtunga kamusi, hupangilia michakato mizima ya utoaji wa kamusi. Katika hatua hii mtunga kamusi huzingatia maamuzi ya aina ya kamusi itakayotungwa, ukubwa wa kamusi hiyo, idadi ya wataalamu watakao husika katika mradi ( wataalamu hawa huteuliwa kulingana na mahitaji ya kamusi), pamoja na kupanga bajeti nzima ya mradi. Usayansi katika hatua hii hutokana na kumhitaji mtunga kamusi kufanya tafiti pamoja na kupitia kamusi zilizo Keisha kuchapishwa, na  utumiaji wa elimu ya hisabati katika kupangilia bajeti nzima ya mradi.

2.1.2 Uandikaji wa kamusi,

Katika hatua hii huhusisha michakato mitatu ya kisayansi ambayo ni,

  2.1.2.1 Ukusanyaji wa data.

 Katika kipengele hiki humhitaji mtunga kamusi kukusanya data kulingana na aina ya kamusi anayotaka kutengeneza kama vile ukusanyaji wa leksimu kutoka katika jamii, au kutoka katika matini mbalimbali zinazo husiana na ugha ambao mtunga kamusi ameamua kutungia kamusi yake. Kwamfano kama mtunga kamusi anataka kutunga kamusi ya kichagga-kiswahili hana budi kwenya kukusanya data kutoka katika jamii ya wachagga au matini mbalimbali zilihusuzo jamii hiyo.

2.1.2.2 Uchambuzi wa data au leksimu.

 Kwa mujibu wa Mdee (2010), wataalam hutumia taaluma yao katika kufanyia  tafiti leksimu zilizo kusanywa na kuteua zile zilizokidhi vigezo vya aina ya kamusi inayoandikwa.

2.1.2.3 Uteuzi wa data,

Baada ya uchambuzi wa kisayansi wa data zilizo kusanywa watunga kamusi huamua ni data (leksimu) zipi zitumiwe kutokana na kukidhi haja ya mtunga kamusi, hii nikutokana kuwa zipo leksimu nyingi sana katika lugha na mtunga kamusi huchukua jukumu lakuteua leksimu zile tuu zilizo kidhi vigezo kutokana na aina ya kamusi aliyokusudia, malengo ya kamusi, na walengwa wa kamusi. Baada ya uchambuzi zileleksimu zilizo kidhi vigezo huingizwa katika kamusi kama taarifa kwa kuanza na kidahizo, tahajia, matamshi, etimolojia, mofolojia, maana na mwisho mifano na matumizi ya leksimu.



2.1.3 Uchapaji wa kamusi,

Hii ni hatua ya kuchapisha kamusi ambapo kwa kawaida hutumia hadi asilimia 10 ya muda wa utayarishaji wa kamusi kukamilika. Katika hatua hii kamusi hutolewa katika maandishi makubwa ili kubaini makosa na kuingizwa katika nakala tepe na baada ya urekebishaji hutolewa kama kazi kamili. Katika michakato hii huhusisha vifaa vya kiteknolojia kama vile tarakilishi na machine za uchapaji.



2.1.4 Uhariri na upitiaji wa kamusi,

Hii ni hatua nyingine inayo dhihirisha usayansi katika utengenezaji wa kamusi ambapo hii ndio hatu ya mwisho katika mchakato wa utengenezaji wa kamusi, na umuhitaji mtunga kamusi kuipiti kamusi yake, na kuihariri ili kubaini makosa na mapungufu mbalimbali yanayo jidhihirisha katika kamusi hiyo.



2.2 USANAA WA KAMUSI

Baada ya kuangalia vipengele hivyo vya kisayansi sasa tutalii usanaa uliopo katika kazi ya utungaji wa kamusi.

 2.2.1 Matumizi ya vielelezo,

 picha na michoro. Katika utungaji wa kamusi mtunga kamusi hulazimika kubuni picha, michoro na vielelezo ili kurahisisha uelewekaji wa vidahizo. Mtunga kamusi hutumia ufundi wake kubuni picha na vielelezo hivi na kuhakikisha vitaashriria dhana aliyo kusudia kwa msomaji wa kamusi. Mfano TUKI(2014) mtungaji katumia michoro katika kufafanua dhana mbalimbali kuanzia ukurasa wa kwanza hadi mwisho wa kamusi.

 2.2.2 Mpangilio wa vidahizo katika kamusi;

  Kwa mujibu wa Mdee (2010) maneno yanayoorodheshwa katika kamusi huweza kupangwa kwa kuzingatia mpangilio wa alfabeti au mpangilio wa leksimu ambapo katika mpangilio huo huelezea maneno yenye kuanza na herufi ya alfabeti ya aina moja ambazo hupangwa pamoja. Kwa mfano katika kamusi ya Kiswahili sanifu (imeshatajwa) imepangilia vidahizo kialfabeti.

Katika mpango wa leksimu huelezea maneno yenye uhusiano wa kimaana. Mpango huu wa kuorodhesha maneno kwa kufuata utaratibu wa maana ulitumiwa na Peter Marck Robert 1852 alipotunga Thesaurusi. Hivyo  mchakato huu unaonesha usanaa kwakuwa watunzi wa kamusi ndio wenye jukumu lakuamua namna ya kupangilia maneno katika kamusi yake.

2.2.3 Umbo la kamusi;

Katika utungaji wa kamusi mtunga kamusi huamua umbo la kamusi yake kulingana na vidahizo alivyo amua kuviingiza katika kamusi yake. Ikiwa mtunga kamusi atateua vidahizo vingi basi kamusi hiyo huwa kubwa sana na ikiwa ataingiza vidahizo vichache bass kamusi hiyo huwa ndogo au ya wastani mfano wa kamusi ya wastani/ndogo ni kamusi  ya Biolojia, Fizikia, na Kemia (2004). Hivyo umbo la kamusi hutokana na mapenzi na ufundi wa  mtunga kamusi.

2.2.4 Matumizi ya rangi katika kamusi.

Mtungaji  wa kamusi huweza kuamua kutumia rangi mbalimbali katika kamusi yake, kama vile kutumia rangi katika kuandika vidahizo katika kamusi au kutumia mkolezo katika kuonesha dhana za msingi katika kamusi yake. Mtunga kamusi hutumia sanaa hii ya rangi kwa lengo lakuifanya kamusi yake kuwa na mvuto au kuainisha dhana za msingi. Mfano katika kamusi ya Kiswahili- Kingereza(2014),  ametumia rangi ya bluu katika kuandika vidahizo.

 2.2.5 Matumizi ya vifupisho katika kamusi;

 Utungaji wa kamusi hutumia vifupisho katika baadhi ya maneno. Kwa mfano: TUKI (2004) kunavifupisho vya aina kuu mbili katika kamusi, vifupisho vya kawaida , yani vile vilivyo vya jumla na vifupisho mahususi, vifupisho vya jumla nikama adj, (adjective) n, Nomino, K.m kwamfano . Matumizi haya ya vifupisho huamuliwa kutumiwa na mtunga kamusi katika kuwakilisha dhana mbalimbali katika kamusi

 Mfano katika kamusi TUKI (201:99) imetumia vifupisho kama ifuatavyo ,

elewek.a kt be well known,  bee understood...

Pia, elem.a kt <ele> 1 be a burden to. Hata hivyo wakati wa kutumia sanaa hii ya vifupisho nilazima mtunga kamusi atoe ufafanuzi wa vifupisho alivyo vitumia katika kamusi yake.

3.0 HITIMISHO

Kwaujumla,  Katika utungaji wa kamusi matumizi ya vipengele vya kisayansi na kisanaa kwa pamoja ndivyo huweza kuikamilisha kamusi na kuifanya kamusi kuwa bora na yenye mvuto.



















































                           MAREJELEO

Mdaee  J.S(2010), Nadharia na Historia ya Leksikografia, TUKI: Dar es salaam.

TUKI (2004) Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia, na Kemia. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili:   Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

TUKI (2014), Kamusi ya Kiswahili-Kingereza, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili: Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

TUKI(2014), Kamusi ya kiswahili Sanifu.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es salaam.














Post a Comment

0 Comments