Swali hili limegawanyika katika sehemu tatu, ambazo
ni utangulizi, kiini na hitimisho. Katika utangulizi ufafanuzi wa dhana ya
riwaya pamoja na historia fupi ya Riwaya ya Kiswahili imetolewa, katika kiini
kuna ufafanuzi wa mikondo ya riwaya ya Kiswahili na mwisho ni hitimisho la
swali.
1.0 Utangulizi
1.1 Fasili Mbalimbali
Msokile (1992), riwaya ni kazi ya sanaa ya kubuni,
ni maandishi ya nathari yanayosimulia hadithi ambayo kwa kawaida ina uzito,
upana, urefu wa kutosha, ina wahusika mbalimbali wenye tabia za aina nyingi;
ina migogoro mingi mikubwa na midogo. Fasili hii imetolewa kwa kuzingatia sifa
za riwaya.
Mulokozi (1996) wanaeleza kuwa, riwaya ya Kiswahili
ni masimulizi marefu yakinathari yaliyochangamana kiasi, yenye kuzungumzia
tajriba ya maisha ya binadamu kwa ubunifu. Fasili hii imejikita katika kigezo
cha urefu, lakini haielezi urefu huo unapaswa kuwa kiasi gani.
Kwa ujumla riwaya ni masimulizi ya kubuni ya
kinathari yenye msuko au mpangilio fulani wa matukio au ploti inayofungamana na
wakati au kusawili wakati na yenye visa vingi vivavyotendeka katika wakati
fulani na yenye mawanda mapana yenye mchangamano wa dhamira, visa na wahusika.
1.2 Historia ya Riwaya ya Kiswahili Tanzania
Utanzu wa riwaya umechelewa sana si Tanzania tu bali
katika Afrika na nchi zinazoendelea karibu zote. Nathari bunifu simulizi kama
vile hekaya na ngano iliyosimuliwa kwa mdomo ndizo zilitawala miongoni mwa
jamii. Kwa upande wa fasihi andishi maandiko ya kishairi hususani tendi za
Kiswahili katika hati za Kiarabu ndizo zilizotawala katika upwa wa Afrika
mashariki. Wazungu walipofika maeneo haya ya Afrika mashaiki wakiwa na
teknolojia yao mpya ya uandishi bado kulikuwa na utengano katiyao na waarabu hivyo pakawa na majilio ya
taratibu ya maandiko ya kinathari. Nathari ya kwanza kuandikwa ilikuwa ni ya Sheikh Ali bin Hamed ya Habari za Mrima
(1880) na kuchapishwa rasmi (1935) vilevile Habari za Wakilindi ya mwaka
(1895).
Kipindi cha waingereza kuliibuka kazi nyingi za
nathari za kibunifu ambazo kutokana na elimu ya waingereza walielekeza juhudi
za kupata kwa kuandia na kutafsiri ndiyo maana kuna tafsiri nyingi wakati huo
mfano. Hadithi za Esopo, Safari ya Msafiri, Kisiwa chenye Hazina, Safari ya
Gulliver. Kisiwa Chenye Hazina na vingine vingi. Waandishi wengine walianza
kuandika kazi zao kwa mfuatano wa kimkondo. Mikondo hiyo imeelezwa kama
ifuatavyo:
2.0 Kiini cha Swali
2.1 Mkondo wa kisafari na kimaadili.
Mkondo huu unajumuisha riwaya za mwanzo kabisa za
Kiswahili, zilizokuwa zikihusisha safari na maadili. Kazi ya kibunifu ya kwanza
ilikuwa ni Uhuru wa Watumwa (1934) iliyoandikwa na James Mbotela kisha
zikafuatiwa na riwaya za Shaban Robert ambazo ni kusadikika (1951),
Kufikirika (1952) na Adili na Nduguze (1952). Kazi hizi zilihusu
kufundisha maadili na mwenendo mwema katika maisha. Maranyingi riwaya hizi
huchukua muundo wa kisafari, vilevile muundo huwa katika kaida fulani za
kifasihi ambazo ni mwendelezo wa mazungumzo au dayalojia, matumizi ya muda au
wakati sifa za kiujumla na utumizi wa mubalagha.
2.2 Mkondo wa Kiethografia
Mkondo huu pia unaweza kuitwa mkondo wa kinyaraka,
hii ni kutokana na sifa yake kubwa ya kuhifadhi maswala muhimu ya kijamii na
kiutamaduni. mathalani, mila na desturi na historia ya jamii. Mifano ya riwaya
zinazopatikana katika mkondo huu ni riwaya ya Bwana Myombokere na Bibi
Bugonoka iliyoandikwa na Anicenti Kitereza (1945) na kuchapishwa baadaye
(1981). Riwaya hii imesimulia historia na tamaduni za Wakerewe ikiwemo mila na
desturi na maisha yao kiujumla pamoja na kipindi cha ujio wa wageni. Vilevile
riwaya ya Kurwa na Dotto (1951) iliyoandikwa na Salehe Farsy, riwaya hii
inasawiri mila na destiri za watu wa unguja pia mwaka (1971) riwaya nyingine za
kiethnografia iliyoibuka ni Mzishi wa Baba Anaradhi iliyoandikwa na
Felician Nkwera ambayo ilielezea maisha ya wapangwa ambao ni watu wa mwambao wa
ziwa nyasa.
2.3 Mkondo wa Kihalifu au Kipelelezi
Mkondo huu wa uhalifu au kipelelezi ulijitokeza
katika fasihi ya Kiswahili mwishoni mwa muongo wa 50 wa karne ya ishirini.
Riwaya ya kwanza kuibuka katika mkondo huu ni riwaya ya Mzimu wa Watu Wakale
(1957- 1958) iliyoandikwa na Mohamed Said Abdulla. Riwaya hii ilikuwa ni
matokeo ya mashindano ya uandishi wa hadithi za kubuni kwa lugha ya Kiswahili
kama ilivyoandaliwa na kamati ya lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki. baadaye
miaka ya 60 Faraji Katalambulla alienda riwaya katika mkondo huu iliyoitwa Simu
ya Kifo (1966). Mwandishi M.S. Abdulla alifanikiwa kupata mfuasi mzuri
mwishoni mwa miaka ya sabini ambaye ni Elistabulus Musiba aliandika hadithi
zake za kiualifu, kipelelezi na kimapenzi. Musiba aliandika riwaya ya kikosi
cha kisasi (1979) akiwa na muelekeo uleule wa Abdulla.
2.4 Mkondo wa kijamaa (kinostalgia na kiprognosia)
Mkondo huu katika riwaya ya Kiswahili umetokana na
mabadiliko ya hali ya kisiasa nchini Tanzania kupitia Azimio la Arusha la mwaka
(1967), hivyo hali hiyo iliathiri vikubwa muktadha wa Fasihi ya Kiswahili,
ushairi na tamthiliya ni tanzu za mwanzo katika kusawiri mabadiliko hayo.
Lakini riwaya ilichelewa kuyapokea mabadiliko hayo, kazi za fasihi zilisawiri
mabadiliko hayo kwa namna mbili tofauti kwani kuna waandishi waliona ujamaa
katika jicho la namna wahenga wetu walivyoishi pamoja na hivyo na jamiii yetu
irejee kulenyuma, pia kuna waandishi walioona kuwa matarajio kwamba kuna ujenzi
wa jamii mpya itakayoishi vyema kuliko hii ya sasa, kundi hili liliandika kwa
kusawiri ndoto zao kwa wakati ujao. Riwaya ya kwanza katika mkondo huu ilikuwa
ni ya "Njozi ya Usiku" (1972) iliyoandikwa na W. Seme ambayo
nayo inashadadia maisha ya wahenga kwa kusisitiza ushirikiano. Mifano za
Kiprognosia ni kama vile Ndoto ya Ndaria (1975) iliyoandikwa na J.
Ngomoi.
2.5 Mkondo wa Uhalisia – Teti (wakihakiki)
Mkondo huu wa uhalisia ulijitokeza mwishoni mwa
miaka ya (1970 - 1980). Katika kipindi hiki hali ya uchumi ilianza kudidimia.
Hali hii ya kudidimia kwa uchumi ilisababisha kuibuka kwa kazi za kinathari
ambazo zilielekeza kidole cha mashtaka kwa viongozi wa serikali kwa uroho wao,
usaliti na rushwa, viongozi ambao hawakutaka kuwasaidia viongozi wadogo ambao
bado walikuwa na imani katika ujenzi wa jamii mpya. Mifano ya riwaya hizo ni
Nyota ya Huzuni (1978) iliyoandikwa na Liwenga na Njozi Iliyopotea (1979)
ya Mung'ong'o pia riwaya zingine ni kama Kichwa Maji (1974) na Gamba
la Nyoka (1975) zilizoandikwa na Kezilahabi, Kabwela (1978) na Harusi
(1984) za Abdallah. J. Safari
2.6 Mkondo wa Kitafakuri ( mkondo wa kimajaribio)
Mkondo huu uliibuka miaka ya (1970-1980) ambapo
wasomi walituliza vichwa vyao na kuanza kutumia maarifa yao kueleza na
kuchambua maisha ya kijamii. Miongoni mwa waandishi walioibuka katika mkondo
huu ni Euphrase Kazilahabi aloyeandika Rosa Mistika (1971) kama nathari
bunilizi iliyoeleza kwa uwazi ukweli wa maisha na baadaye na wanamaadili wa
kimagharibi kwa kukiuka maadili ya kijamii. Pia aliandika baadaye kazi nyingine
za kidhanaishi mfano wa kazi hizo ni kama Dunia Uwanja wa Fujo (1976), Nagona
(1987) na Mzingile (1990). Baada ya kazi hizo waandishi wengine
waliathiriwa na mtindo wa kezilahabi na kuanza kuandika kazi zao kwa mtindo huo
ni kama; Willium Mkufya na kazi yake ya Ziraili na Zirani, Said Ahmed
Mohamed na bunilizi la Babu Alipokufa
(2001). Hivyo mkondo huu umeingiza namna mpya ya uandishi katika nathari
bunilizi.
2.7 Mkondo wa ufungwa.
Mkondo huu ni mgeni katika nathari bunulizi za
kiswahili. Haya ni maandiko ambayo yanaweza kuwa ni ya kitawasifu au kiwasifu
yakisawiri matukio ya gerezani au magereza. Maandiko haya yamekuweko katika
nchi nyingine kama vile nathari ya Nelson Mandela, long walk to freedom
(1995) aliyoiandika kuhusu maisha yake ya ufungwa huko Afrika ya kusini. Kenya
mwandishi wa nathari ya ufungwa ni ya Ngugi wa Thiong'o ambaye yameathiriwa
sana na kufungwa kwake kutokana na
harakati zake za kuushambulia ubepari unaoletwa na ukoloni mamboleo. Baadhi ya
vitabu vyake vimmetafsiriwa katika kiswahili kwa mfano Ntaoa Nikipenda
na Shetani Msalabani. Nigeria yuko Wole Soyinka na Malawi yupo Jack
Mapanje na katika Tanzania mwandishi wa nathari ya ufungwa hadi hivi sasa ni
Maulid Haji aliyejitokeza katika miaka ya 90 na kuandika Umleavyo (1990)
hadithi ambayo inasawiri maisha ya rumande na msimulizi wa kazi hiyo akiwa yeye
mwenyewe.
3.0 Hitimisho
Kwa kuhitimisha. Mikondo ya riwaya ya Kiswahili inaweza kugawanyika katika vipindi
tofauti tofauti vya miaka. Kwani katika kipindi fulani cha miaka kuna uwezekano
wa kuibuka kwa mikondo mbalimbali ya
riwaya ya Kiswahili inayojitokeza. Mathalani (1960 -1970) kulikuwa na mkondo wa
uhalisia, mkondo wa kijamaa, mkondo wa kitafakuri na mkondo wa kijamaa.
MAREJELEO
Madumulla, J. S (2009) Riwaya ya Kiswahili:
Nadharia, Historia na Misingi ya Uchambuzi.
Mture
Educational Publishers Limited; Dar es Salaam
Msokile, M.(1992) Misingi ya Hadithi Fupi. Dar
es Salaam Universty Press:
Dar es
Salaam
Mulokozi, M. M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili; Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili,
Dar es salaam.

0 Comments