Swala la uhakiki kama fasili ya fasihi ni swala ambalo limeendelea na kukua sana kihistoria. Ni swala pana sana na ni swala lenye utata mwingi. Uhakiki ni swala lililoendelea kwa sababu kila kuchapo panatokea nadharia au maelezo mapya kulihusu.
Kwa mfano, hapo jadi palikuwa na uhakiki uliohusu umithilishi, uasilia, na urasmi. Lakini baadaye pakaingia uhalisia, uhalisia wa kijamii, na ulimbwende. Baadaye pia pakaja umuundo, ufeministi, uhakiki-saikolojia na uhakiki- mamboleo [post-modernism]. Hii ni mifano tu, kwani kila mara panatokea nadharia mpya ya kuhakiki kazi za fasihi na hata zile za awali kuboreshwa.
Vile vile, swala la uhakiki ni pana kwa sababu pana nadharia na mitizamo kemkemu ya uhakiki. Kwa mfano, katika nadharia ya uhalisia peke yake, twapata uhalisia wa kijamii na uhalisia wa ujamaa. Swala la uhakiki halikadhalika ni lenye utata kwa sababu mpaka leo hakuna nadharia hata moja inayoweza kuchukuliwa kama inayoweza kueleza kikamilifu uhakiki ni nini na unapaswa kuzingatia nini. Yaani kila nadharia ina upungufu wake pamoja na ubora wake. Isitoshe, hapana njia yoyote halisi ya kuihakiki kazi ya fasihi. La muhimu ni kuzingatia mhakiki analenga kudhihirisha nini na anatumia vigezogani.
Licha ya mambo haya yote swala la uhakiki hutokea kuwa muhimu sana katika kila sura ambapo fasihi huingizwa. Na hatuwezi kutenganisha fasihi na uhakiki kamwe. Ndiposa katika utangulizi wao wa toleo la pili la Modern Literary Theory, wahariri wanakiri kwamba hapo awali uhakiki wa fasihi ulichukuliwa kama uwanja duni mbele ya fasihi lakini kwa hivi sasa, ni uwanja muhimu sana katika fasihi.
Nia yetu katika sehemu hii ni kujaribu kueleza uhakiki ni nini huku tukitoa kwa muhtasari mifano ya baadhi ya nadharia zinazotumiwa katika uhakiki wa fasihi. Kwanza pana maswali matatu ambayo twapaswa kuzingatia katika jukumu hili letu:
Uhakiki ninini?
Ni vigezo vipi huzingatiwa katikauhakiki?
Je, pana njia halisi yakuhakiki?
UHAKIKI NININI?
Uhakiki sawa na fasihi ni dhana ambayo imeelezwa kwa njia tofauti na wataalamu mbali mbali. Hata hivyo, wote wameeleza dhana ya uhakiki kwa kuihusisha na fasihi. Tutaanza kwa kunukuu maoni ya wataalum mbali mbali kisha tuyaunganishe pamoja ili kutoa fasili moja itakayotuongoza katika kuelewa dhana hii ya uhakiki. Peck na Coyle (1984) wanasema;
Uhakiki huchukuliwa kama utathimini, ufasili na uainishi wa kazi za fasihi. Haimaanishi 'kuitafutia makosa' kazi hiyo. Uhakiki kama kitendo cha kiakedemia humaanisha maoni ya msomaji kuhusu kinachotendeka kitabuni [tafsiri yetu].
Hapo twaona kwamba uhakiki unahusu tathimini na tafsili ya mambo yanayopatikana katika kazi anayoizingatia mhakiki. Lakini pia twaona maoni yao finyu yanayoiona kazi kama ya kiakademia na pia kuihusisha na fasihi-andishi.
Naye Hough (1966:5) anasema kwamba;
Uhakiki kuhusu kazi nyingi, ikiwemo haja ya kuuliza, kutathimini, kuweka katika mpangilio sawa na kulinganisha. [tafsiri yetu]
Coombes (1953:7) amezingatia zaidi kazi ya mhakiki huku akionyesha kazi ya mhakiki bora anaposema kwamba;
Kwa jumla twaweza kusema kuwa mhakiki bora awapo katika shughuli yake huwa anazingatia mambo mawili, au moja ya hayo mawili; hutupatia maoni yake kamili na yaliyo wazi kuhusu mtunzi, tamthilia, riwaya, shairi au tungo ili kutuwezesha tufurahie kazi ile pamoja na kuelewa tajiriba iliyomo katika utunzi pamoja na ile inayozingira utunzi huo. Au kwa kutathimini kazi ile kwa makini, hudhihirisha vipembe vinavyoipa thamani. [tafsiri yetu]
Coombes hakomei hapa bali anaendelea kusema kwamba:
Uhakiki wa kifasihi si chengine zaidi ya mguso aupatao mhakiki katika kazi ya fasihi anayoizingatia. [tafsiri yetu]
Kulingana na Coombes, kazi ya kuhakiki haiongozwi na hoja za kisayansi bali hujikita katika hisia. Kwa hivyo twapaswa kuihakiki kazi yoyote ile ya sanaa kwa misingi ya athari inayotoa kwa hisia zetu halisi.
Naye Abrams (1981) anasema kwamba
Uhakiki ni somo linalohusika na kueleza, kuainisha, kutathimini na kupima kazi za fasihi. [tafsiri yetu]
Kwa hivyo uhakiki ni somo; na ni somo linalolenga kueleza na kuchungua kwa makini kazi ya fasihi.
Linalodhihirika tunapochunguza maelezo ya wataalamu hawa kuhusu swala la uhakiki ni kwamba pana kauli kuu wanazozitoa. Wanaelekea kukubaliana kwamba uhakiki ni:
Kuthamini nakueleza
Kuainishana
Kutoamaoni
Kwa kuzingatia maoni haya yao tutajaribu kutoa fasili moja ya uhakiki tutakayoizingatia katika kazi yetu. Uhakiki kwa maoni yetu utakuwa ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Tumeingiza hoja ya kaida hapa kwa sababu twafahamu kuwa uhakiki hautokei katika ombwe tupu bali huongozwa na kaida na masharti maalum yaliyopo. Fasili hii yaweza kutumiwa kulenga kitendo cha hadhira inayohakiki shairi lilokaririwa na mwenzoa bila kuandikwa au kitendo cha kiakademia kinachofundishwa shuleni au chuoni.
Hapa tutatoa mifano zaidi inayoelemea kuhakiki katika kiwango cha kiakedemia ambapo pana somo halisi la uhakiki. Hata hivyo pana kiwango chengine cha uhakiki ambacho twaweza kukiita cha kimsingi ambacho huzingatiwa na wasomaji wengi wa jumla. Uhakiki ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu. Hata tusomapo magazeti kwa mfano, huwa panatendeka kiwango fulani cha uhakiki. Ndiposa Hough (1966:7) akasema kwamba
Yoyote anayelinganisha kile akipatacho katika kitabu na maudhui ya tajiriba yake maishani, yeyote anayelinganisha kitabu kimoja na chengine, kuwa amaeanza kuwa mhakiki [tafsiri yetu].
Bila shaka kitendo asilia anachokifanya ni kuisoma ile kazi ya fasihi. Hicho ni kitendo cha kawaida kabisa kwa mtu aliye na uwezo wa kusoma. Ni katika kitendo cha kutua na kujaribu kuielewa na kujibu maswali kama vile kwa nini, nani, na vipi ambapo uhakiki huanza. Kwa hivyo uhakiki ni shughuli iliyozingatiwa kwa makini sana hasa kiakedemia. Tumeamua kuzingatia kiwango hiki cha uhakiki kwa sababu katika uhakiki kama somo kinyume na uhakiki wa kujumla, pana kaida maalum zinazomwongoza mhakiki afanyapo kazi yake.
NI VIGEZO VIPI HUZINGATIWA KATIKAUHAKIKI?
Kazi ya uhakiki haifanyiki kisadfa bali huwa imepangwa kutokea. Ifahamike kwamba kile anachokisema mhakiki kuhusu kazi yoyote ya fasihi hutegemea kwa kiwango kikubwa mtizamo wa kihakiki anaoufuata. Hivi ni kumaanisha kwamba uhakiki
huanza kwa maoni ya msomaji (mhakiki) kuhusu kazi anayoizingatia na hivyo basi huenda akatoa uhakiki wa kimvuto au kimguso.
Kwa jumla, uhakiki unapaswa uzingatie tathimini halisi huku mbinu zilizotumiwa katika kazi ya fasihi pamoja na maudhui yake zikijadiliwa. Uhakiki bora hivyo basi hujishughulisha na uteuzi wa maudhui muhimu ya kazi husika na kisha kuona jinsi kazi yenyewe inavyoyatoa na kuyaendeleza maudhui hayo. Ni muhimu kushikilia kwamba tajiriba halisi au matukio yanayozingatiwa katika kazi ya fasihi ni kielelezo cha tajiriba za kijumla za binadamu. Kwa hivyo inatokea kwamba mhakiki anahitajika kuipitia kazi anayoizingatia ili kuona ni aina gani ya tajiriba za kawaida, hisia au shida zinazozingatiwa pale.
Halafu baada ya hapo, ili kuzungumzia matini yenyewe, lazima kuonyesha jinsi mambo aliyoyateua mtunzi - kwa mfano, maelezo au fafanuzi alizozitoa au maneno aliyoyatumia-husaidia kufafanua, kuendeleza au kutoa mwelemeo mpya kuhusu yanayochukuliwa kama mambo muhimu. Tahakiki hupata uzito zaidi iwapo mbinu alizotumia mtunzi katika kukabiliana na maswala yake hudhihirishwa. Hapo ndipo tahakiki hutofautiana na muhtasari wa kazi nzima.
Ikumbukwe kwamba kati ya majukumu yatekelezwayo na uhakiki, lile muhimu zaidi ni kuifasiri kazi ya fasihi. Kabla kazi yoyote ya fasihi kuhakikiwa au hata kuhusishwa na vitendo vingine vya kibinadamu, ni lazima kazi hiyo ieleweke ipasavyo. Tafsiri na maelezo ni dhana zinazojenga kitendo cha kuhakiki.
Dhana ya kuifasiri kazi ya fasihi yaweza kuelezwa kwa njia mbili; kwanza, ni kudhihirisha kusudio la mtunzi kwa kuondoa vikwazo vyovyote ambavyo vyaweza kutatiza uelewaji: yaani kueleza msamiati, misemo na mpangilio wa maneno, ili kuwezesha kuweka wazi maana iliyokusudiwa. Pili, ni kwenda zaidi ya hatua hiyo ya kwanza na kuiona kazi ile kama fumbo ambalo halieleweki hata baada ya kutoa maana ya maneno na misemo. Hivyo basi mhakiki analo jikumu la kupambanua fumbo au mafumbo katika kazi hiyo. Mafumbo hayo wakati mwingine hutokea bila mtunzi kukusudia vile.
Kwa muhtasari basi twaweza kusema kwamba vigezo vya kuhakiki vyaweza kuainishwa kulingana na wajibu unaohitajika kutelekelezwa na kazi ile. Hata hivyo vigezo vifuatavyo ni baadhi ya vigezo ambavyo vimezingatiwa na wahakiki wengi;
Kuhalalisha kazi za fasihi au kuifafanua ili kueleweka kwa hadhirahusika.
Kufasiri kazi za fasihi kwa wasomaji ambao huenda wasiieleweipasavyo.
Kuratibu kazi za fasihi kwa kutumia vigezo sanifu vyatathimini.
Kugundua na kutumia kanuni zinazoeleza nguzo za sanaabora.
Hata hivyo ni wazi kwamba kazi yoyote ya uhakiki huwa imejengeka katika misingi ya kujaribu kuunda kundi la istilahi, kanuni na vigezo vya kutumiwa katika kufasiri kazi za fasihi, pamoja na kutoa viwango na maadili ambayo kwayo kazi hizi na watunzi wake huratibiwa.
JE, KUNA NJIA HALISI YA KUHAKIKI?
Kiini cha swali hili ni je, pana nadharia ya fasihi inayoweza kuchukuliwa kama iliyo mwafaka zaidi ya zote? Ukweli ni kwamba hakuna! Hii ndiyo sababu inayofanya somo la uhakiki kuwa gumu hali kadhalika la kusisimua. Kazi ya fasihi imekuwa chanzo cha maoni na mijadala isiyoisha huku wahakiki wakijaribu kutoa njia zenye uzito zaidi za uhakiki lakini hakuna ile iliyo kamili.
Kwa maoni ya Hough(1966:7)
Hakuna kazi ya uhakiki iliyo kamili. Uhakiki haufanyiki mara moja na kukamilika kwani huwa inategemea mkondo wa kihistoria na hali ya maendeleo ya kijamii. Kila patokeapo mabadiliko kihistoria, fasihi ya awali huhitaji kuelezwa upya [tafsiri yetu].”
Kwa hivyo kazi ya uhakiki ni fululizi hivi kwamba haina kikomo na hakuna uhakiki unaojisimamia kivyake. Kila siku kazi mpya za fasihi huingizwa katika jamii ili kuchukuana na maisha ya jamii ya wakati wake. Na kazi hiyo huhitaji kutathiminiwa kwa misingi inayochukuana na hali hiyo. Tunachokisema ni kwamba hata ingawa kimsingi kazi ya uhakiki huweza kuchukuliwa kama kazi nafsia (kwamba kila mahakiki huona kazi ile kivyake), mtizamo wa kila mhakiki huathiriwa na mazingara ya kijamii pamoja na utamaduni ambamo kazi ile inatokea. Kama wanavyosema Peck na Coyle(1984:150)
Hadi kufikia karne ya kumi na nane, mtizamo mkuu wa fasihi ulikuwa ni kuichukulia kama "funzo la kuvutia", na hivyo basi uhakiki ulihusishwa na jinsi kazi hiyo ilivyofanikiwa kutoa funzo kwa msomaji. Katika kipindi cha ulimbwende, hali hii ilibadilika. Walibwende walisisitiza umuhimu wa ubinafsi, na hivyo basi uhakiki wa kilimbwende uliegemea upande wa thamani ya alichokisema mtunzi kama mtu binafsi [tafsiriyetu].”
Kwa hivyo kila uhakiki huchukuana na kipindi cha kihistoria cha wakati wake, na hivyo tahakiki hubadilika kadri jamii husika inavyobadilika. Pana hata wengi wanaopinga kabisa kitendo cha kuhakiki huku wakidai kwamba uhakiki ni kitendo cha kuishushia fasihi hadhi yake halisia. Okot P'Bitek (1973:22) ni mmoja anayeona hapana haja ya kuwa na uhakiki na hata kuendelea kudai kwamba hapana haja ya kuzingatia fasihi kama somo. Anasema;
Fasihi kamwe haiwezi kuwa somo la kutahiniwa kwa sababu hisia ndizo hujenga maelezo na sio elimu katika maelezo hayo. Waombolezaji katika mazishi hawalii ili kupata cheti. Swali sio "unajua nini kuhusu muundo wa wimbo?" bali ni " "umeufurahikia kwa kiasi gani? Umekugusa Kivipi?" [tafsiri yetu]
Linalodhihirika katika kauli hii ya P'Bitek ni kwamba fasihi hulenga hisi za hadhira. Jambo ambalo halizingatii ni ukweli kwamba sio kila mwanajamii anaweza kuwa mtunzi bora wa kazi ya fasihi lakini wanaofaidika kwa kazi hiyo ni wengi. Vile vile fasihi hulenga mambo mengi zaidi ya hisia; yaani ina majukumu mengi kwa jamii yake. Pia sio kila kazi inayotokea katika jamii huweza kuratibiwa kama fasihi au sanaa. Kwa nini pasiwe na kanuni za kuzingatiwa ili kuhakikisha mambo hayo na mengine mengi yamelainishwa?
Bila kutukuza wala kupinga kauli ya P'Bitek ningependa kutaja kwamba fasihi yaweza kushughulikiwa kwa kuzingatia njia mbali mbali na uhakiki ni mojawapo wa njia hizo. Vile vile kuhisi na kuathiriwa na kazi ya fasihi ni njia nyengine ya kuizingatia
fasihi; hivyo basi yategemea jukumu la anayehusika. Ama kwa hakika, katika kila kitendo kinachohusu fasihi uhakiki hufanyika, iwe ni kumkumbusha msanii majina ya wahusika, iwe ni kumhimiza anapotoa hadithi na kadhalika; yaani hapana utunzi bila kuhakiki hata wa kibinafsi. Kutambua kwamba waombolezaji wanalia kwa sababu ya kuguswa na kinachoendelea pale katika maombolezo ni kitendo cha kuhakiki kwani kinahusisha tokeo na sababu.
Naye McGilhrist, I(1982:21) anasema;
Uhakiki unazingatia zaidi maoni ya wengine kuliko fasihi
yenyewe. Tunawaona watunzi wetu kupitia nadharia za fasihi ambazo hutukuza maoni yetu kuliko kile tunachodhamiria kugundua.
[tafsiri yetu]
Maoni ya mtaalamu huyu ni kwamba uhakiki kwa msingi wake huwa na kaida na masharti ya kuuongoza, na kile anachofanya mhakiki ni kutizama kama kazi anayoizingatia inatimiza kaida hizo. Yaani, kwanza mhakiki haioni wala kuichunguza kazi ile kwa misingi yake [japo ni vigumu kutenga ubinafsia wa mhakiki na kazi anayofanya] bali hujaribu kuzingatia kaida maalum. Ndiposa McGilhrist(1982:38) anaendelea kusema “lazima uhakiki uheshimu ubinafsi wa kazi ya sanaa pamoja na ‘maana’ ya mtunzi[tafsiri yetu].”
Na kama ambavyo pana maana ya mtunzi huenda pia pakawa na maana ya mhakiki ambayo anaiona katika kazi ya fasihi anayoipitia. Ukweli ni kwamba huenda mhakiki, kwa kuongozwa na kaida za uhakiki wake, akazua mambo ambayo hakuyataja mtunzi asilia wa kazi ile. Yaani wakati mwingine mhakiki huzua mambo fulani ambayo mtunzi asilia hakuyafahamu au kuyatilia maanani katika kazi yake. Kauli hii yatuongoza katika hoja kwamba maoni yote ya binadamu hujikita katika tajiriba mbalimbali ambazo huzua fasihi mbalimbali na hivyo basi kutoa hitimisho tofauti. Hapana njia yoyote maalum ya kuhakiki au kuelewa kazi ya fasihi kwani yote huadhiriwa na mambo mbali mbali ambayo tumejaribu kudhihirisha katika kazi hii. Hali hii yapendekeza tujiulize ukweli ni upi kama upo?
0 Comments