Header Ads Widget

Responsive Advertisement

utata katika ufundishaji wa sarufi yakiswahili

 

FAFANUA VIPENGELE MBALIMBALI AMBAVYO VINA UTATA KATIKA UFUNDISHAJI WA SARUFI YA KISWAHILI KISHA UPENDEKEZE JINSI UTATA HUO UNAVYOWEZA KUONDOLEWA.

Matatizo ya kufundisha sarufi

1.0: Utangulizi

Lugha ya Kiswahili imejikuta katika njia panda hasa kwa kurejelea vipengee mbalimbali ambavyo vinatia utata katika uelewa wa lugha hii. Baadhi ya vikwazo hivi ni fundishaji wa sarufi. Kwa kweli sarufi ndio mhimili katika lugha yoyote ile. Hata hivyo ufundishaji wa sarufi ya Kiswahili una vikwazo chungunzima. Vikwazo hivi ni pamoja na:-

1.1:Wanafunzi kukabiliana na sarufi ya Kiswahili kwakutumia lugha yao ya mama.

Hali kama hii huwafanya wanafunzi kufikiria na kukabiliana na Kiswahili kwakutumia lugha zao za kwanza. Hili huwa tatizo kubwa sana kiasi kwamba sarufi za lugha za mama haziingiliani na sarufi ya Kiswahili.

 

 

 

 

 

Kwa mfano katika nafsi za Kiswahili tunapata viwakilishinafsi vifuatavyo:

 

NAFSI

UMOJA

WINGI

1

NI

TU

2

U

M

3

A

WA

 

Zipo baadhi ya lugha mama hasa za kinailoti ambazo huvitumia au kuhamisha  viambishi nafsi vya lugha yao hadi Kiswahilipasi kufahamu madhara wanayoyaleta kwenye sarufi ya Kiswahili.

Kwa mfano katika lugha ya Waluo, utagundua kwamba wao hutumiwa kiwakilishinafsi A kurejelea nafsi ya kwanza hali ya umoja ambapo katika Kiswahili huwa nafsi ya tatu umoja.

Utawaskia wakisema :

a.      Abiro-Ninakuja

b.      Adwaro-Ninataka

Katika mtindo huo, wapo wale ambao huhamisha nafsi hii namna ilivyo hadi kwenye Kiswahili. Utawaskia wakisema:

a.       Mimi anaenda shuleni. Badala ya :Mimi ninaenda shuleni.

b.      Mimi  anaandika polepole.Badala ya:Mimi ninaandika polepole.

c.       Mimi  anasoma haraka. Badala ya:Mimi ninasoma haraka.

Kwa kufuata mifano ya hapo juu itaonekana wazi kuwa wanafunzi kutoka maeneo hayo ambao huitumia lugha yao ya kwanza kama kioo wanaposoma sarufi basi wana kazi ya ziada.

Hivyo basi wanafunzi hawa hustahili kuiacha kando lugha yao ya mama wanapoikabili sarufi ya Kiswahili la sivyo hali itawaendea mrama.

Waaidha zipo lafundhi za lugha hizi za kwanza ambazo huathiri san sarufi ya Kiswahili katika lugha ya Kikamba wengi wao hutamka konsonanti J kama Y. Utagundua kwamba asilimia kubwa ya Wakamba wanapozungumza mahali palipo na J watatamka Y.

Kwa mfano:

KISWAHILI

KIKAMBA

Jua

Yua

Juu

Yuu

Juni

Yuni

 

Waaidha palipo na  sauti G wao hupachika NG

Kwa mfano:

KISWAHILI

KIKAMBA

Goli

Ngoli

Gareji

Ngaleji

Goti

Ngoti

 

 

Palipo  na R wanaweka L.

KISWAHILI

KIKAMBA

Rudi

Ludi

Rarua

Lalua

Rinda

Linda

Mrembo

Mlembo

 

Mfano mwanafunzi hataeleweka iwapo ataambiwa aisome sentensi kama hizi;

a.      “Linda ana rinda refu lililoraruka vibaya.”

b.      “Mimi ni fundi wa kupaka rangi”

Utamsikia mwanafunzi akitamka:

a.      “Linda ana linda lebu lililolaluka bimbaya.”

b.      “Mimi ni bundi wa kubaka langi.”

Katika hili kama hii sarufi hufanywa chapwa mno.

Katika mfumo huo, jamii ya Waluhyia haijasazwa nje. Katika jamii hii utagundua kuwa lafudhi yao wakati mwingine huwatia mashakani katika uchambuzi na usomi wa Kiswahili.

Wengi wao badala ya sauti B hutia P, Sauti Z hutia S, D hutia T

Kwa mfano:-

Matamshi bora ya Kiswahili

Matamshi bandia ya Kiluhyia.

1

Baba

Papa

2

Bora

Pora

3

Bata

Pata

4

Bure

Pure

5

Bei

Pei

6

Birika

Pirika

7

Bila

Pila

 

 

Sauti Z na S

Matamshi bora ya Kiswahili

Matamshi bandia ya Kiluhyia.

1

Mzuri

Msuri

2

Mzee

Msee

3

Mzinga

Msinga

4

Muziki

Musiki

5

Mkizi

Mkisi

6

Zambarau

Sambarau

7

Mzigo

Msiko

 

Sauti D na T

Matamshi bora ya Kiswahili

Matamshi bandia ya Kiluhyia.

1

Dada

Tata

2

Daktari

Taktari

3

Dadisi

Tatisi

4

Dereva

Tereva

5

Darasa

Tarasa

6

Domo

Tomo

7

Daka

Taka

 

Kwa kuangaziwa athari za hapo juu ni dhihirisho tosha kuwa kufundisha sarufi katika mazingira hayo huwa kugumu sana. Tatizo kubwa ni kupata kuwa mwalimu na wanafunzi wote wana shida moja ingawa hawajagundua shida kama hiyo miongoni mwao.

Hivyo basi, ni muhimu kwa msomi au mwelekezi ambaye kwa njia moja au nyingine ana tatizo kama hili basi ni muhimu kuzingatia sauti za Kiswahili pamoja na konsonanti zote hukuakitilia maanani matamshi bora ambayo hayataathiriwa na lugha zao za kwanza.

Kwa hivyo athari kama hizi vile vile ni kuangaziwa kwa somo linalohusu konsonanti na sauti katika Kiswahili ili kujenga msingi imara katika matamshi ambayo huathiri sana sarufi ya Kiswahili.

Ikiwa hili halitapata tiba mapema litakuwapo tatizo kubwa hasa wanafunzi waathiriwa wanapoangazia somo kuhusu sentensi zenye utata vitatamshi.

1.2:Athari za Kiingereza kwa Kiswahili kisarufi

Matatizo katika sarufi ya Kiswahili huchangiwa vile vile sarufi katika somola Kiingereza.

Hapo hujitokeza sana kwa wasomi ambao wamemudi sana lugha ya Kiingereza hivyo basi kuwa na dhana potofu kuwa sarufi ya Kiswahili ni sawa na Kiingereza pasipo Kujua kuwa hizi ni lugha mbili tofauti na zilizo na miundo tofauti ya sentensi.

Kwa mfano katika Kiingereza utagungua kuwa kivumishi(adjective) hutangulia nomino kwenye sentensi. Kwa mfano:

Two boys were punished(Neno two ni kivumishi kinachotoa sifa zaidi kuhusu neno boys)

Iwapo sentensi hii itahamishwa kimuundo hadi Kiswahili, itakuwa:

Wawili wavulana waliadhibiwa(V+N+T). Hapa sentensi hii itakuwa imevunja kanuni za sarufi ya Kiswahili ambapo huwa na mfumo huu N+V bali sio V+N. Hivyo sentensi hii inafaa kuwa:

Wavulana wawili waliadhibiwa.(N+V+T)

A good meal was eaten.(Neno good ni kivumishi kinachotoa sifa kuhusu neno meal)

Sawasawa na mfano tangulizi sentensi ii hii Vilevile itakuwa na utata wa kisarufi kwani itasoma: Kizuri chakula kililiwa (V+N+T) badala ya Chakula kizuri kimeliwa.(N+V+T)

Waaidha utagundua kuwa katika nafsi za Kiingereza huwa nafsi ya pili(you)  hujitokeza kabla ya nafsi ya kwanza hasa unaporejelea swala fulani kwa mfano:

You and I were punished yesterday. Bali katika Kiswahili hutangulia na nafsi ya kwanza ndipo ya pili ikafuata.Hivyo  basi sentensi ii hii itasoma: Mimi na wewe tuliadhibiwa jana bali sio Wewe na mimi tuliadhibiwa jana.

Vile vile katika ukanushi wa vitenzi katika Kiingereza wakati mwingine Ufupisho hukubalika bali katika Kiswahili Ufupisho ukitumika mantiki na ufasaha lengwa utakosekana.

Mfano: If you force me to go to school, I won’t.  katika sentensi hii iwapo neno I wont litabakishwa jinsi lilivyo bado litaeleweka. Iwapo sentensi ii hii italazimishwa kimuundo katika Kiswahili kwakufupisha kitenzi katika hali yakutoa dhana ya Ufupisho sentensi hii itasoma hivi:

Ukinilazimisha kuenda shuleni,sita. Sasa hapa neno sita halijakamilika. Lina kikanushi(si) na kiwakilishi wakati (ta) bila kitenzi. Kwa hivyo sentensi haitakuwa na maana. Ingefaa iwe: Ukinilazimisha kuenda shuleni,sitaenda.

Kwa hivyo si bora kutumia muundo wa sarufi ya Kiingereza katika kujifunza au kufundisha sarufi ya Kiswahili.kwa hivyo ni muhimu kila mmoja kukita tu katika miundo ya sarufi ya Kiswahili pasi kuchanganya na ile ya Kiingereza.

Wakati mwingine utakuta kuwa mwalimu amesombwa na kasumba ya Kiingereza wakati wa Kiswahili kiasi kwamba anatumia lugha zote wakati mmoja katika kufundisha.unapomsikiliza mwalimu kama huyu utashindwa kuelewa iwapo anafunza Kiingereza au Kiswahili kwenye kipindi kimoja.

Inastahili masomo hayo yapewe heshima sawa na kukubalika na utawala ima uwe wa shule, taassisi au chuo chochote. Wanafunzi waweze kupewa siku zaidi ya moja kwajuma kuwasiliana kwa Kiswahili na pia ingekuwa bora walimu wa masomo mengine kutumia siotu Kiingereza wanapofundisha masomo yao bali vile vile watumie Kiswahili ili kiweze kukwea na kumea mizizi.

1.3:Kiswahili kuchukuliwa kama lugha duni.

LICHA ya hadhi na umaarufu wa Kiswahili ndani na nje ya nchi, bado lugha hii inakumbana na matatizo makubwa ya dhana na matumizi sahihi. Kuna baadhi ya watu wanaonasibisha Kiswahili na dini ya Kiislamu na hili limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa watumiaji wake. Hapa utagundua kuwa ile kasumba iwapo itamwingia msomi kwa misingi hiyo basi hawezi kuwa na umakinifu wa kuizingatia ifaavyo. Na pasipo mtu kuwa na msukumo katika kile afanyacho basi hawezi kutia bidii na juhudi hata kidogo.

Hii hata hudhihirika wazi wakati unapotembelea mwuza-magazeti kisha uagizie gazeti la Kiswahili mfanoTaifa Leo, mwuza-magazeti yuyo huyo ndiye atakayekuwa wa kwanza kuanza kushuku kuwango chako cha elimu na uelewa wako wa mambo. Sababu ni kuwa umenunua gazeti la Kiswahili. Kwa hivyo iwapo jamii kwa jumla haitabadili mafikiro haya basi mwalimu atazidi kuwa na ugumu katika kuifunza sarufi katika lugha ya Kiswahili kwa kuwa wanafunzi wameathirika na msimamo wa jamii.

 Pia kunao upinzani mkubwa kutoka katika lugha ambazo zimekwisha kujitanua kimatumizi kote duniani kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kijerumani, Kichina, Kireno na Kiarabu. Watumizi au watu wenye asili ya lugha hizo wanakipiga vita Kiswahili wakihofia kuwa wasipofanya hivyo kitazimeza lugha zao katika siku za usoni.

 

Hali kama hii huathiri sana mwalimu wa Kiswahili. Kwa mfano iwapo mwalimu atajikuta katika shule ya Kimataifa ambapo lugha ya lazima ni Kiingereza bali Kiswahili kiwe mwongoni mwa masomo ya kuteua, basi wanafunzi wengi wataangukia lugha nyingine kama kifaransa, kijerumani, au Kiarabu  ma kuachilia mbali Kiswahili.

 

Kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha nyinginezo za kigeni kwamba ndizo pekee zinazofaa kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa zina hadhi ni changamoto kubwa.

 

Papo hapo utagundua kuwa hata teknolojia inaweka nguvu sana katika masomo ya kisayansi huku lugha hasa Kiswahili zikiteketea kwani kila mtu kwa sasa anaimba wimbo wa kunawiri kisayansi pasipokujua kuwa huyo mwanasayansi huenda akahitajika kutekeleza wajibu wake katika maeneo yanayotumia Kiswahili tu! Hali hii vile vile ya jamii kuzipa kipaumbele taaluma nyingine hasa za uhandisi huku maswali ya kukuza lugha kama Kiswahili yakitupiliwa mbali

 

 

1.4:Kutoweka kwa Kiswahili katika matumizi.

.kuwa na mazoezi katika kila ufanyacho huwa nyenzo muhimu na Mihimili katika udhibiti wa kila ufanyacho. Katika mtazamo huo itakubalika kuwa wasomi wengi hawana mazoea katika kuendeleza kile wanachokisoma nje ya darasa. Utagundua kuwa kila wanachokisoma hubakia langoni pa darasa hadi wakati mwingine wa kipindi.

 

Hata iwapo mwalimu ataangazia mada ambayo wasomi wanahitaji kuifanyia mazoezi ya maongezi hawajatilii maanani kabisa. Wapo wasomi wngine ambao hata wakipewa kaziya ziada, kuifanya ni mtihani au ngoma. Kwa  hivyo ifahamike kuwa msomi yeyote ni wa kujituma na huku kujituma kuna mambo mengi ya kujitolea mhanga. Itakumbukwa kuwa apatacho msomi kutoka kwamwekekezi wake ni asilimia ndigo sana bali mzigo mkubwa unatoka kwake msomi mwenyewe.

 

Isije ikwa haliya kusema ati “Bora nimewasiliana si lazima kanuni”La hasha! Ndio maana vazi si vazi tu bali huwa vazi linapovaliwa sehemu ifaayo tu! Katika hali hiyo utagundua kuwa wasomi wetu hawajakuwa na hamu na tama ya kutaka kusoma mara kwa mara. Wamekuwa wavivu sana hasa kwa kutaka kutabaradi bila kufanya cha mno kuhusu mustakabaliwao.

 

 Sarufi kama somo lolote huhitaji kutengewa muda wa ziada na binafsi.hii ni kwa mwanafunzi husoma vyema hasa anapojigundulia mambo mbalimbali. Msomi  Kama huyu hupata balaa na beluwa hasa anapokuwa na nia ya kukwea ngazi kielimu kufikia uzamili au uzamifu. Hapo ni kuwa mwandani wa kusoma kwa kupanua na kujifunza ujuzi mpya.

 

 Hali hii imewafanya baadhi ya wasomi kutopata hata wasaa wa kufunua Kamusi ya Kiswahili. Wapo wasiojua kuwa kila neno katika Kamusi huelezwa ni aina gani ya neno(Nomino, kitenzi, kivumishi n.k).Hivyo basi bila kuwa mpenzi wa Kamusi basi kutakuwa na ugumu sana katika kubaini na kuichanganua maneno yanayotumiwa katika kukisoma Kiswahili.

Kwa hivyo wasomi watengewe muda wa kutosha wakusoma huku wakielekezwa ifaavyo. Ni bora wanafunzi wawe na aghalabu kipindi kimoja kwa wiki  cha maktaba ambapo watapata fursa ya kujisomea huku wengine wakielezwa. Kuhusu matumizi ya kamusini bora iwapo wasomi watazoeshwa mapema namna ya kuitumia Kamusi wakiwa katika madarasa ya awali.

1.5: Athari za vitandazi na mitandao ya kijamii.

Ieleweke kuwa Kiswahili kimeingia mtandaoni hivi karibuni baada ya lugha nyingine nyingi kunawiri kwenye mtandao. Hata vile vile kimeingiakama kwenye ukumbi wa Google transalate ikumbukwe kuwa huo ni ukumbi tu wa kutafsiri tena tafsiri sisisi ambapo hazikupi maana ya neno namna linavyostahili kuwa.

Tukiwa bado kwenye mtandao, kuwa vitandazi kama face book, tweeter, whatsup, histogram n.k

Vitandazi hivi vimeteka jamii bakunja kwamatumizi ya mikato ya maneno. Vifupisho hivi huathiri sarufi moja kwa moja.Waaidha utapata kuwavitandazi hivi vimezidisha uzembe katika usomi na kufanya mazoezi ya uandishi kwa kukosa kujuamaendelezo sahihi ya neno.

Hapo hapo kwenye mtandao utagundua kuwa nguvu za msongarika(peer pressure) zimewatanda wasomi kiasi kwamba wanahimizana kutozingatia wakifanyacho wakiwa nje ya darasa. Hii hi kwa kuwa wamebadili lengo lao la mawasiliano na kuwa ukumbi wa kujadilitu maswali mengine ya kijamii pasi Kujua kuwa jamii haikamiliki pasi usarufi wa lugha na mawazo. Kwa hivyo hili huwapelekea wasomi wengi kutumia lugha chapwa isiyojua kuwa zipo kanuni zinazifaa kufuatwa ima katika uandishi au uzungumzi.

1.6: Kiswahili kukosa udugu au ujirani na masomo mengine shuleni.

Katika shule zote, Taasisi hata vyuo vyote nchini Kiswahili ndiyo lugha ya pekee ambayo ni yatima katika kuifundisha. Mfano   tu ni kuwa katika shule za msingi wanafunzi huyasoma masomo haya:Sayansi,Hisabati, Kiingereza,Somo la Jamii Kiswahili, Stadi-ishi(life skills) Tarakilishi n.k.Ni ukweli mtupu kuwa masomo hayo mengine isipokuwa Kiswahili huingiliana.

Walimu  wa masomo hayo yote wanapoingia darasani kwa njia moja au nyingine hufundisha sarufiya Kiingereza.Hii ni kwa kuwa masomo hayo yote hufunzwa katika Kiingereza na mtihani vile vile kuandaliwa katika lugha ya Kiingereza.kwa hivyo kwanjia moja au nyingine lugha hizi hukipiga msasa Kiingereza huku Kiswahili kikibaki yatima kwani hubakitu pekee katika lughayake pekee. Atokapo mwalimu darasani hadi atakaporudi ndipo lugha hiyo labda isikike kinywani mwa mwalimu.

Kuongeza msumari moto kwenye kidonda ni kuwa katika shule nyingi nchini wanafunzi hupewa siku moja tu ya kuwasiliana katika Kiswahili huku Kiingereza kikibaki na siku nyingine zote. Hii inakinyima Kiswahili fursa ya kunawiri. Kwanza heri siku moja. Zipo shule nyingine ambazo kuwasiliana kwa Kiswahili nje ya somo la Kiswahili  ni hatia kubwa ambapo adhabu yake haitamaniki.

Ikiwa hata sheria za shule hazimruhusu mwalimu wa Kiswahili kuwasiliana na wasomiwake kwa Kiswahili atikwa kuhofia kupigwa kalamu basi huko ni kudidimiza ari ya kukua kwa lugha hii.

1.7: Uzalizaji na utumiaji wa msamiati bila mpangilio

Ikumbukwe kuwa kukua kwa msamiati ni kukua kwa lugha yoyote ile. Hata hivyo hili haliangaziwi na baadhi ya watumizi wa lugha hii.wengi wao wamekuwa na kasumba ya kuibuaibua msamiati bila kuelewa mbinu zifaazo kuzingatiwa. Ukasuku kama huu hauleti Ladha kabisa kiasi kwamba wasomi huchanganyikiwa kabisa.

Vile vile ni muhimu kugundua kuwa ukasuku katika uumizi wa lugha ya Kiswahili una athari zake. Ikumbukwe kuwa kabla ya kulitumia neno ni muhimu kulifanyia neno hilo utafiti  ndipo ulifahamu fika asili na matumizi yake barabara.

Kwa hivyo ni muhimu kufanya utafiti ufaao kwa kila neno ukutanalo nalo kabla ya kuanza kulitumia.

1.8: Athari za vyombo vya habari

Sarufi ni utaratibu maalumu wa lugha husika. Utaratibu huu ni kanuni, sheria au kaida nyingine zinazotawala mfumo mzima wa lugha ili iweze kukubalika na kueleweka katika matumizi ya lugha hiyo kwa wanajamii. Hivyo tunapoongea sarufi ya lugha moja kwa moja tunalenga utaratibu maalumu wa lugha Fulani. Kama zilivyo lugha nyingine, Kiswahili kina utaratibu wake pia, yaani sarufi ya Kiswahili, ambayo inafanya lugha hii kuwa katika utaarabu wake. 

Katika matumizi ya lugha, wadau wengi wa habari hasa waandishi, wa habari, watangazajia, na wahariri wa habari, wamekuwa wakifanya makosa ya kisarufi ya mara kwa mara katika habari wanazoandika na kuzichapisha kama zilivyo. Habari za magazetini, kwenye mitandao, runinga, hata zile zinazosikika redioni, hujaaa makosa mengi ya kisarufi. Makosa hayo ni kama kuchanganya au kuhazima sarufi ya lugha za kigeni kama kiingereza na kuitumia katika Kiswahili; mathali, mtangazaji katika kujitambulisha anaweza kusema "yangu majina" badala ya jina langu; "yangu matumaini" badala ya matumaini yangu. "Yangu Majina" ni sarufi ya kiingereza sio ya Kiswahili, alafu katika Kiswahili hatuna dhana ya;majina' kwa mtu mmoja, bali tuna jina. 

Katika utaratibu sahihi wa Kiswahili, jina/nomino hutangulia kivumishi na kivumishi hufuata kwani kivumishi hufanya kazi ya kutoa sifa kwa jina, ila kwa kiingerza utaratibu ni tofauti kwani kivumishi huweza kutangulia nomimo; mfano: my name (jina langu), beautiful lady    ( binti mrembo), strong man (mtu shupavu) n.k. Katika mifano hii, tungo za Kiswahili kwenye mabano ndio muundo sahihi kisarufi wa Kiswahili lakini kiingereza ni tofauti kwani katika kiingerza kivumishi hutangulia nomino katika mazungumzo au maandishi.

 Vilevile kutofuata kanuni za lugha ya Kiswahili imekuwa ni jambo la kawaida kwa wanahabari. Imekuwepo kasumba kwa baadhi ya watangazaji na waandishi wa habari hapa nchini kusema au kuandika neno "jumbe" wakiwa na dhana ya wingi wa;ujumbe'. Hakika katika taaluma ya sarufi ya Kiswahili hatuna wingi "jumbe" kwa maana ya ujumbe.

Katika vyombo hivi Vilevile tumekuwa na hali ya kubuni maneno ambayo hayana ithibati ya matumizi na kuyatumia katika lugha pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya maneno katika lugha.

Kosa hili limeshika kasi sana katika maisha ya sasa ya vijana na uga mzima wa habari. Katika mitandao ya kijamii, redio, runinga na magazetini yamekuwepo matumizi ya maneno ya kubuni na yamezoeleka ni ya kawaida kumbe sio. Pamoja na hayo yapo matumizi ya maneno ambayo sio sahihi kwa maana yake halisi. Mfano kuna maneno kama "tiririka au funguka" ; hutumika kumaanisha mtu kujieleza au kutoa ya moyoni( kwa matumizi ya sasa); matumizi ya maneno hayo sio sahihi katika mantiki yake ya msingi maneno haya kwa Kiswahili. Pia kuna "ngoma" kwa maana ya wimbo/muziki n.k.

Wanahabari wawa hawa vile vile wamekuwa na kosa la kuchanganya lugha mbili au zaidi(Kiswahili na KiingerezaLugha ya Kiswahili imekumbwa na wimbi hili zito la baadhi ya watu wengi kuchanganya lugha ya Kiswahili na lugha za kigeni.

Katika uga wa habari jambo hili siku hizi ni la kawaida. Ipo misemo, maneno ya kiingereza na lugha nyingine, ambayo hutumika kama maneno ya Kiswahili. Magazeti mengi na makala huandika habari kwa kuchanganya maneno ya lugha mbili tofauti. Mfano, "wikiendi/wikendi (mwisho wa wiki); wachezaji walikuwa kambini wakifanya training ya viungo; habari zilizotufikia katika newsroom (chumba cha habari), reporter wetu (mtoa habari wetu); time imekata(muda umeisha) n.k". Kwa mfano kule Tanzania katika gazeti la mwana sporti namba 1217 la tarehe 3 hadi 6, mwaka 2012, ukurasa wa 18, kuna kichwa cha habari kimeandikwa hivi,;First Eleven ya waliofunga mabao mengi'. Hivyo basi kuchanganya lugha sio taratibu sahihi katika kuhimarisha lugha. Ikumbukwe kuwa kazi ii hiiya uanahabari huzagaa haraka sana na ikiwa ina athari hasi basi sarufi ya Kiswahili hupata pigo kubwa.

Lugha ya Kiswahili ni lugha yenye sifa zote na inayokidhi mawasiliano miongoni mwa watumiaji wake kama zilivyo lugha nyinginezao hapa ulimwenguni, hivyo inapaswa iheshimike na ithaminiwe sawa kama lugha nyingine. Na kufanya hivyo, upendo katika lugha hii utakuwepo na kuitangaza lugha hii kimataifa. Sanjali na hili, ni jukumu letu sisi sote wapenzi wazalendo  kuifuatilia na kuisoma lugha hii kwa undani ili tuweze kuwa wamaizi kwa undani wake na kupunguza makosa madogo madogo madogo yanayosababisha lugha hii kutoendelea.


Tasnia ya habari, ni sehemu muhimu katika kuleta mchango na maendeleo makubwa katika jamii, na hivyo basi kupitia dhamana hii, vilevile wanahabari wanayo nafasi kubwa kuithamini, kuipenda, kuisoma na kuiendeleza lugha ya Kiswahili katika kutoa taarifa na babari katika jamii husika. Hii itaenda sambamba endapo wanahabari watafunguka macho na kuona umuhimu wa kusoma Kiswahili kama taaluma ya kumwezesha mtu kupata cheti kama mwanatabari. Makosa ya kisarufi, kuchanganya lugha, na mengineneyo hayataonekana katika matini mbalimbali za habari huku wahariri wakitakiwa kuwa ni wenye ujuzi wa lugha hii.

Wakati mwingine utamsikia mwanahabari mtangazaji akisema kuwa: “Majangili wawili waliivamia benki moja katika mji wa   ……………………………………….” Iwapo magangili watawageuza watu kuwawanyamapori kisha wawavamie basi hapo ni hatari kabisa, Majangili kwakawaida hawani wawindaji haramu wa wanyamapori, sasa itakuwa je sasa hawa majangili wamegeuza benki zetu kuwa hifadhi za wanyamapori? Wapo wengine ambao husema “ Gari waimokuwa wakisafiria lilipata ajali na kuwaua watu watatu papo hapo”. Huku ni kuitia kitanzi sarufi ya  Kiswahili moja kwa moja.

Hapa ni kuwa mtangazaji huyu hafahamu chochote kuhusu ngli ya mahali (PAKUMU) wala matumizi yake ni usiku wa giza. Angefaa kusema “Gari walilokuwa wakisafiria lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu watatu”.Ukasuku huu haufai katu na ndio unadidimiza juhudi za kuikuza sarufi ya Kiswahili.

Kupitia juhudi hizi, hakika, watumizi wa Kiswahili wote tukishirikiana tunaweza kuiendeleza lugha yetu murua ya Kiswahili na kuitangaza kimataifa

 

1.9: Ngeli za Kiswahili na athari zake.

Ngeli zimewachanganya wengi sana. Hasa kwa kukosa kufahamu namna ya kuvitumia viambishingeli kwenye mafungu tenzi hasa wakati nomino mbalimbali zinapotumika.

Kwa mfano ukitazama ngeli ya A-WA maelezo yake huwa ni ngeli inayorejelea ya majina ya viumbe wenye uhai k.v watu, wanyama, ndege,samaki, wadudu, miungu, malaika n.k Majina mengi katika ngeli ya A-WA huanza kwa sauti M- kwa umoja na sauti WA- kwa wingi. 

Katika ufafanuzi huu wa nomino wakati mwingine utangundua kuwa ufafanuzi huu una dosari kiwango fulani wakati msomi anapoanza kuangaziwa nomino zizo hizo lakini katika hali ya ukubwa. Mfano jitu,janadume,gombe n.k. kwa vile wanafunzi huenda wasitambue wenyewe kuwa nomino katika ngeli hii huihama hasa zinapukuzwa, huwa vigumu sana kumenyana nazo kisafufi.Mfano mzuri ni mazoea ya kutumia neno JIBWA kwa wengi wetu kurejelea Mnyama huyu katika hali yake ya Kawaida. Kasumba kama hii huwa hatari sana kiasi kwamba kumrekebisha huyu msomi ni mtihani.

Inastahili maelekezo kuzihusu ngeli yawekwe wazi kwa kutalii hali zozote ambazo huenda zikabashiriwa kuwa zinaweza kuleta utata katika kuzichanganua.

Katika usanjari huo zipo sentensi ambazo zinaweza kulazimishiwa katika wingi ingawa mantiki yakakosekana. Baadhi ya sentensi hizi ni zile ambazo zinarejelea nomino za pekee hasa majina ya watu.

Mfano wa sentensi kama hizi ni:

a.       Maria aliliruka shimo

b.      Daktari Jactone Onyango aliwasili darasani mapema.

c.       Bwana Omukabe ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika chuo kikuu cha Kenyatta.

Katika mifano hii ya hapa juu ni kuwa iwapo katika sarufi wasomi watalazimishiwa kuzibadili katika wingi huku wakirejelea sifa za ngeli ya A-WA , huenda umaantiki ukakosekana kabisa.

Zipo nomino nyingine ambazo haziwezi kujikuta katika ngeli zozote labda paibuke ngeli nyingine ya A-WA. Nomino hizini zile ambazo hurejelea majina ya vitu vya kufikirika na majina halisi ya watu. Mfano wa nomino hizi ni:-

a.       Mungu

b.      Yesu

c.       Mtume Muhammed

d.      Omukabe

e.       Onyango n,k

Itabidi utafiti wakina ufanywe ili kuziorodhesha nomino hizi ifaavyo. Wapo wanaonadi kuwa zipo katika ngeli ya A-WA huku wengine wakilonga kuwa ngeli yake ni A-A.Wakati wa kuichanganua swala hili huleta utata sana miongoni mwa wasomi.

Katika hali iyo hiyo ipo nomino ambayo hadi sasa hapajaibuka maelezo yafaayo kuihusu. Nomino yenyewe ni MAITI. Wapo wanaosema kuwa hii ni nomino katika ngeli ya A-WA huku wengine wakisema kuwa ngeli yake ni I-ZI.

Kwa hivyo ni bora sana iwapo wahusika watatoa mwelekeo ufaao kuhusu swala hili la ngeli ili kila mmoja aweze kunufaika.

Waaidha katika karne hii, teknolojia imeshika kasi sana kiasi kwamba, msamiati unazalika kucha kutwa. Kwa hivyo ni bora zaidi iwapo washika dau wote kushika kasi katika swala lauainishaji wa msamiati huu ili ngeli zake zieleweke barabara.

Kwa kutokosa namna ya kuziainisha nomino hizi katika ngeli, wengi wamejikita wakizilazimishia katika ngeli ya I-ZI.

 

Ili kuondoa utata huu. Ambaokwamba umekithiri na kuisonga Sarufi ya Kiswahili, ni muhimu sana kwa wahusika kuweka mikakati kabambe ambayo itaondoa utata huu. Iwapo hili litafanywa basi jamii haitakuwana ugumu wowote katika usomi wa sarufi ya Kiswahili. Sera borazaKiswahili ziwekwe na kuheshimika iwe shuleni au popote ambapo usomi wa Kiswahili upo.

Jamii vile vile inafaa iondoke katika fikra potovu za kupitwa na wakati ati Kiswahili nilugha ya watu duni wasioelimika. Hili litasaidia sana kuikuza lugha hii katika vizazivya sasa na vijavyo.

 

1.10: Ufinyu wa Vitabu vya utafiti wa sarufi ya Kiswahili

Kwa hakika hili ni swala zito mno ambalo linakandamiza sarufi ya Kiswahili katika viwango vyote ingawa viwango vya juu ndivyo vinavyoathirika pakubwa. Ukiingia katika maktaba yawe ya umma au ya Taasisi yoyote ile ni muhali kuvikuta Vitabu vya Kiswahili. Kutia msumari moto kwenye kidonda ni pale ambapo mwanafunzi wa kozi ya uzalimi au uzamifu katika vyuo vyetu vikuu anapopewa mwongozo wa kozi utagundua kuwa kupatika na kwa kitabu cha Marejeleo cha Kiswahili ni usiku wa giza.

Wingi wa Vitabu hivi ni vya Kiingereza. Katika hali hii mwanafunzi anastahili awe na ustadi wa lugha hizi mbili ili aweze kutafsiri anachokitalii katika Kiingereza huku akikitasiri katika Kiswahili. Kitendawili hapa ni kuwa, wakati msomi huyu anapofanya hivi basi moja kwa moja anachangia katika maendelezi ya sarufi ya Kiingereza huku ya Kiswahili ikizidi kuporomoka.

Kwa hivyo ni bora iwapo Vitabu vya Marejeleo viwe vile vimeandikwa katika lugha ya Kiswahili tu basi sio Kiingereza. Cha kushangaza ni kuwa wafanyao kozi za juu katika Kiingereza hawavitumii Vitabu vya Kiswahili kama vyombovya Marejeleo.


                                                MAREJELEO

1)      Massamba, D.P.B. (2011). Maendeleo Katika Nadharia ya Fonolojia. Taasisi ya Taaluma za  Kiswahili chuo Kikuu cha Dar es salaam. Dar es salaam: TUKI.

2)      Massamba, D.P.B. (2004). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu (FOKISA), Sekondari na Vyuo.
Dar es salaam. TUKI

3)      Matinde, R.S. (2012) Dafina ya lugha, Isimu na Nadharia Sekondari Vyuo vya kati na vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publisher (T) Ltd.

 

4)      Chomvisky, NN.& Halle,M.(1968)The sound pattern of English New York: Harper & Row

 

5)      Massamba, D.P.B(2012)Misingi ya Fonolojia. Dar es Salaam: TATAKI.

 

6)      Massamba, D.P.B(2011) Maendeleo katika Nadharia ya Fonojia .Dar es Salaam:TATAKI

 

7)      Massamba, D.P.B(2004)Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha.Dar es Salaam: TUKI.

 

8)      Jensen, J.T.(2004) Principles of Generative Phonology:An Introduction . Amsterdam: John Benjamins Publishing House.

 

9)      Kenstowicz, M(2006) “Generative Phonology”. Katika Brown, K na wenziwe, (wah)

 

10)  Encyclopedia of Language and Linguistics(2nd ed.) uk. 3276-3286.Elsevier Ltd

 

11)  Kiparsky, P. (1968) ‘How abstract is Phonology?’Bloomington, India: Indiana University Linguistics Club.

 

12)  Lass, R.(1984) Phonology: An Introduction to basic concepts.. Cambridge University Press.

 

13)  Chiduo, E.( 2002),”Syno nymy: A Defining Method in the Standard Swahili Dictionary: Its Strength and Weakness”, Kiswahili juzuu 65: 43-58.

14)  Bicrwisch., M (1970). Semantics.Katika j.Lyons( Mh.) New Horizons in Linguistics.Penguis book. 166-184.

15)  Kahigi, K. (1995). Lugha Katika Vitabu vya Watoto. Kioo cha Lugha (mfululizo mpya) juzuu 1:21-35.

16)  Lakoff, G. (1987) Women, Fire and Dangerous Things, What categories Reveal About the mind. Chicago; University of Chicago Press.

17)  Lyons, J. (1977). Semantics.Cambridge .Cambredge University press.

18)  Mkude, D. (1995).Towards a Semantic Typology of the Swahili Language. Institute for the study of Languages and Cultures of Asia and Africa (ILCAA).

19)  Goddarf C. (1998) Semantic Analysis: A practical Introduction.Oxford: Oxford University Press.

20)  Lakoff, G. (1987) na M.Johnson, (1980) Metaphors We Live By. Chicago; University of Chicago Press.

21)  Khamis, S A (1991), “Supperstration and Polysemy in Swahili; A Tentative Study in Lexical Semantics”, Kiswahili . juzuu 58: 25-33.

22)  Barwani Sheikh, Sauda. 1995. Masomo ya bidii: a Swahili intensive course. Hamburg: Helmut Buske.

23)  Bearth, Thomas. 1995. Wortstellung, Topik und Fokus. Katika Swahili-Handbuch, wahariri G. Miehe na W. J. G. Möhlig, k. 173-205. Cologne: Rüdiger Koppe.

24)  Dryer, Matthew S. 1986. Primary objects, secondary objects and antidative. Language 62:808- 845.

25)  Sacleux, Charles. 1939. Dictionnaire swahili-français. (Travaux et mémoires de l'Institut de 'l'Ethnologie, 36-37.) Paris: Musée de l'Homme.

26)  Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. 1990. Kämusi sanifu ya isimu na lugha. Dar es Salaam: Educational Publishers and Distributors kwa niaba ya TUKI

27)  Habwe, J. na Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, phoenix publishers LTD, Nairobi.

28)  Holm, P. and Karlgrey, K. (1995) The Theory of meaning and Different perspective on information System, Stockholm University, Marburg.

29)  Lyons, J. (1981) Language; Meaning and Context, Fontana Paperbacks.

30)  Matinde, R. S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu Serengeti Education publishers (T) LTD, Mwanza.

31)  Mdee, S. J. na wenzake (2011) Kamusi ya Karne ya 21: Kamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi Katika Karne Hii, Longhorn publishers LTD, Nairobi. 

32)  Sengo, T. S. Y.M (2009) Fasihi za Kinchi, The Regestered Trustees of Al Amin Education and Research Academy, Dar es Salaam.

33)  Wamitila, K. W, (2003) Kamusi: Istilahi na Nadharia, Kenya Focus Publications LTD, Nairobi

Post a Comment

0 Comments