Header Ads Widget

Responsive Advertisement

kiswahili na viswahili pamoja na athari zake

 

 

ATHARI ZA VISWAHILI KWA KISWAHILI SANIFU.

Utangulizi:

v  Kiswahili sanifu:
Kiswahili sanifu ni mtindo wa kusema na hasa wa kuandika lugha ya Kiswahili  kwa mujibu wa dhima fulani ambazo zinachukuliwa kuwa ni muhimu katika jamii.

Waaidha Kiswahili sanifu ni Kiswahili ambacho mara nyingi kimefanyiwa marekebisho fulani ambayo yanakiwezesha kukubalika na kutumiwa kwa upana zaidi.

 

Kiisimu, Kiswahili sanifu kimesukwa na kufanywa kijipambanue kutokana na ‘Viswahili’ vingine kutokana na sifa kadhaa za kimuundo.

 

Pamoja na kuainisha na kufafanua taratibu za ufasaha wake, ni lazima pia kuonyesha namna zitakazokiwezesha Kiswahili sanifu kijirekebishe kwa kadiri utamaduni wa jumuia unavyobadilika. Usukaji huu ni pamoja na kuweka taratibu ambazo zitatawala jinsi ya kukiandika.

 

Waaidha unaweza kusema kuwa Kiswahili sanifu ni lugha isiyokuwa na makosa ya kisarufi kwa kuwa huzingatia kanuni zote za lugha ya Kiswahili kama mofolojia, fonolojia, fonetiki na nyingine nyingi.

v  Viswahili:

Hivi ni vijilugha vilivyo na ujirani na lugha ya Kiswahili sanifu ingawa havijafanikiwa kujitosheleza kimofolojia, kifonolojia, kifonetiki na kileksia.

Kwa yakini viswahili vivi hivi vimekuwa na athari sufufu kwa Kiswahili sanifu. Athari zizi hizi zinajitokeza katika makumbo mbalimbali kama yafuatayo:-

§  Lahaja

§  Sheng

§  athari za lugha ya kwanza(mama)

§  Rejesta mbalimbali.

 

A)    Lahaja

Lahaja ni vilugha vidogovidogo vya lugha moja ambavyo hubainishwa na jamii au jiografia. Lahaja za lugha moja zinatofautiana katika matamshi, miundo ya sarufi na msamiati.

Dhana hii ya lahaja imechanganuliwa na wanaisimu mbalimbali. Massamba (2002) anasema kuwa lahaja ni lugha mbalimbali za pwani zilizokuwa na uhusianao wa karibu sana. Lugha hizo ni kama vile ci-mbalazi, ki-amu, ki-mvita, ki-jomvu, ki-mtang’ata, ki-makunduchi, ki-tumbatu, ki-mgao na ki-unguja. Wakati wengine wanaziita lahaja mfano, Polome (1967), Bryan (1959) pamoja na Temu (1980).

Msanjila (2009:124) anasema lahaja ni lugha mojawapo kati ya lugha ambazo kimsingi kuhesabiwa kuwa lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au muundo kutokana na eneo lugha hiyo inazungumzwa.

Lahaja za Kiswahili hutofautishwa kulingana na maeneo yake  kama Kiunguja  (kisiwani Zanzibar)  ambacho kimekuwa msingi wa  Kiswahili Sanifu  Kimvita (eneo la "Mvita" au Mombasa mjini, Kenya) , ambacho zamani kilikuwa lahaja  kubwa ya pili pamoja na Kiunguja, Kiamu (kisiwani Lamu, Kenya) na kadhalika.

Mifano mingine ya lahaja za Kiswahili ni pamoja na:

·         Kimrima: eneo la Pangani, Vanga, Dar es Salaam, Rufiji na Mafia kisiwani (Tanzania)

·         Kimgao: eneo la Kilwa (Tanzania)

·         Kingwana: Kiswahili cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

·         Shikomoro: Kiswahili cha Komoro

·         Shimaore: Shikomor cha Mayotte (Mahore)

·         Shindzuani: Shikomor cha Anjouan (Komoro)

·         Shingadzija: Shikomor cha Komoro Kuu

·         Kimwani: kaskazini mwa Msumbiji na visiwa vya Kerimba

·         Chimwiini: eneo la Barawa, kusini mwa Somalia

 

Kwa kuzingatia lahaja hizi utagundua kuwa lahaja hizi kwa njia moja au nyingine zinakilemaza Kiswahili Sanifu. Hali hii hujitokeza kwa wale watumizi wa lugha hii kwa wingi pasi kujali kuwa si rasmi wala sanifu kutumia. Kile ambacho wazungumzi hawa hawagundui ni kuwa ni lahaja moja tu ambayo iliinuliwa hadhi na kukubalika kama Kiswahili Sanifu ingawa ao hao bado katika usingizi wa pono huku wakizipigia debe lahaja zao.

Hebu tutazame mifano ya maumbo ya maneno katika lahaja mbalimbali ambayo huboronga Kiswahili Sanifu.

ü  Lahaja ya Kimtang’ata : Hii ni lahaja inayozungumzwa maeneo ya Tanga. Mfano ya misamiati yake ni ;

Msamiati katika lahaja ya Kimtang’ata

Kiswahili Sanifu

 

a

Tombo

Ziwa

b

Kifugutu

Kisu(ki)butu

 

c

Mbeko

Akiba ya nafaka

 

d

Uwanda

Tambarare

 

 

 

Lahaja ya Kitumbatu: Hii ni lahaja inayozungumziwa katuka kisiwa cha Tumbatu kaskazini mwa Unguja. Mfano wa misamiati ya lahaja hii ni;

Msamiati katika lahaja ya Kitumbatu

Kiswahili Sanifu

Ulanda

Kisu kikali

Kifuto

Kisu kibutu

Angulia

Piga bao(ramli)

chuchu

ziwa

Yula

Yule

 

Lahaja ya Kihadimu; hii nilahaja inayozungumzwa kisiwani Unguja. Mifano ya msamiati wa lahaja hii ni:-

Msamiati katika lahaja ya Kihadimu

Kiswahili Sanifu

Kule

Mbali

Rikacha

Pikicha

vacha

pacha

 

Lahaja ya Kimvita; hii nilahaja inayozungumzwa “Mvita” au Mombasa mjini. Mifano ya msamiati wa lahaja hii ni:-

Msamiati katika lahaja ya Kimvita

Kiswahili Sanifu

 

a

Mthezo

Mchezo

b

Mthuzi

Mchuzi

 

c

Thungu

Chungu

 

d

Thai

Chai

 

 

 

 

Mbali na lahaja ambazo zimeangaziwa hapajuu ambazo ni za kijiografia zile za kijamii vile vile zina uwezo mkubwa wa kuboronga Kiswahili Sanifu.Mifano mwafaka ni kama ifuatayo:-

·         katika kigezo cha kijinsia wanawake hutumia neno shosti na wanaume hutumia neno msela, wote wakiwa na maana ya rafiki katika Kiswahili sanifu

·         Pia kuna kigezo cha kiumri ambapo tunapata msamiati wa lahaja za kijamii kama vile; demu kwa vijana na binti kwa wazee ambapo wote wakiwa na maana ya msichana katika Kiswahili sanifu.

Kwa hivyo itafahamika kuwa lahaja huwa na athari kubwa sana kwa Kiswahili sanifu kwa kuwa wale wanaoizungumza lahaja teule huku wakaiona kuwa inafaa kabisa basi hutatiza Kiswahili sanifu huku wenyewe wakijitatiza kwa kukosa kuelewana kikamilifu na wale waliozamia Kiswahili Sanifu.

Ø  Ikumbukwe kuwa lahaja hutotautiana kimatamshi hali ambayo huathiri Kiswahili sanifu. Mfano wahaya kutoka mkoa wa Kagera katika matamshi yao hawana kitamkwa ng’ kwa hiyo wanapotamka maneno kama vile ng’ombe wao hutamka ngombe, neno ng’ang’ania hutamka ngangania, neno ung’amuzi wao hulitamka kama ungamuzi. Vile vile watu kutoka mkoa wa Mara ambao ni wakurya hutumia kitamkwa r badala ya l kwa mfano neno kula wao hulitamka kura, neno kulala hulitamka kurara, kulalamika wao hulitamka kuraramika.

Ø  Pia wazungumzaji kutoka mikoa ya kusini mfano kutoka mkoa wa Mtwara na Lindi ambao ni Wamakonde wao hutumia kitamkwa n badala ya m kwa mfano mtoto hutamka kama ntoto, msichana hutamka kama nsichana, mchana hutamka nchana. Vile vile wazungumzaji kutoka mkoa wa mbeya ambao ni wanyakyusa wao hutamka  badala ya v kwa mfano neno viatu vyangu hutamka kama fiatu fyangu, uvivu hutamka ufifu, viazi hutamka fiasi. Wazungumzaji wa kutoka mikoa ya kaskazini mfano wapare kutoka mkoa wa moshi hutumia kitakmwa th badala ya s kwa mfano badala ya kusema sisi sote ni wasichana wao hutamka thithi thote ni wathichana. Kwa hiyo tofauti hizo za kimatamshi zinatokana na athari za lahaja za mikoa waliyotoka.

Ø  Miundo ya sentensi vile vile huathirika. kwa mfano wazungumzaji wa mkoa wa Tabora hutumia wingi mahala pa nomino ya umoja wakiashiria heshima. Kwa mfano husema baba wanakuja badala ya kusema baba anakuja, mmefika salama? Badala ya kusema umefika salama?. Kwa hiyo mtu wa heshima kwao hutumia nomino ya wingi na hii yote ni kutokana na kuathiriwa na lahaja za mikoa watokayo.

Ø  Lahaja nyingine hizi vile vile huathiri mkazo katika maneno hali ambayo hutatiza mawasiliano.Mkazo ile ni hali ya neno au silabi katika neno kusikika kuwa na nguvu zaidi kuliko silabi au maneno mengine. Kwa hiyo ulahajia huweza kuelezea utofauti wa mkazo uliopo katika baadhi ya wazungumzaji wa lugha moja. Kwa mfano kabila la Wasukuma kutoka mkoa wa Mwanza huweka msisitizo katika mazungumzo, kwa mfano “baba anakujaa”, pia wanaongeza vitamkwa ambavyo si vya msingi katika maneno yanayojitosheleaza. kwa mfano neno amekuja wao huongezea kitamkwa ga, = amekujaga, neno ameenda + ga, = ameendaga, hakuna + ga.=hakunaga.

 

B)    Sheng

Yapo madai kuwa Sheng iliibuka katika mitaa ya Mashariki ya Nairobi mnamo miaka ya sabini (Osinde1986; Shitemi 2001). Kufuatia kupatikana kwa uhuru 1963, idadi ya wakazi wa Nairobi ilipanda kwa haraka sana kutokana na kumiminika kwa watu kutoka mashambani wakitafuta ajira katika mitaa ya viwanda humo jijini. Wananchi hao maskini waliishia kuishi katika mitaa ya makazi duni ya viwandani Mashariki ya Nairobi ambayo ni kitovu cha maendeleo ya viwanda.

Ijapokuwa wafanyakazi hawa pamoja na jamii zao walilazimika kutumia Kiswahili kwa mawasiliano baina yao, wengi walikichukia Kiswahili kwa vile kilikuwa kimedunishwa sana na sera ya ukoloni kama lugha ya mashambani, lugha ya vibarua au “maboi” wa kuwatumikia Wazungu. Hata hivyo, watoto wa wafanyikazi hao hawakupendelea kuendelea kukitumia Kiswahili kama wazazi wao kwa sababu kadhaa. Kinyume na wazazi wao, watoto walilazimika kuishi katika hali ya jamii ya utatu-lugha: 'lugha za kinyumbani’, Kiswahili na Kiingereza. Pia, walitambua kuwa ingawa walilazimika kutumia lugha nyingi, ni Kiingereza pekee ambacho kilipewa hadhi kama lugha ya utawala, mamlaka, heshima na uwezo mkubwa wa kiuchumi.

Ili kuepuka matatizo ya kimawasiliano na kama njia ya kusuluhisha utata wa hali hiyo iliyowakabili, vijana hao waligundua msimbo wa mawasiliano kati yao ambao, ingawa ulifuata sarufi ya Kiswahili, uliazima msamiati kutokana na lugha za kiasili na kuunda baadhi ya maneno yake. Msimbo huo ndio uliotokea kuwa Sheng hapo baadaye.

Sheng ama lugha simo ni lugha inayotumiwa na watu wa kundi maalum kwa ajili ya kutaka waelewane wao kwa wao na pengine kuwatenga watu wengine. Katika mukhtadha huo ni sawa kusema kuwa ni lugha isiyokuwa na mfumo wa rasmi wa sarufi kwani watu hubuni majina wanavyofikiria.


Majina yanaweza kubuniwa kutoka kwa vipande vya lugha tofauti, kubadilisha maneo kwa mfano kutoka nyuma ukirudi mwanzo na kadhalika. Kwa mfano neno bata unaweza kuwasikia vijana wakenya wakisema taba na kuoga wanasema kugao.


Kutokana  na maelezo hayo inaonyesha namna lugha hiyo inayotajwa kuwa ya kihuni na baadhi ya wasomi wa Kiswahili inatofautiana kutokana na mtu anachosema na mahali anaposemea. Hata hivyo kwa wataalamu wa isimu jamii ( social linguists) watakupiga mawe ukikashifu matumizi ya sheng. Wengine hata wamefanyia utafiti kipengee hicho.


Ingawa kuna mvutano mkubwa kuhusu matumizi ya sheng ama lugha simo, ni muhimu kutaja kuwa kuna baadhi ya maneno yaliyoanza kama sheng na yakaswahilishwa. Kwa mfano nchini Kenya, Matatu ni magari ya uchukuzi wa umma ama matwana kwa Kiswahili sanifu. Vivyo hivyo, Tanzania chombo hicho kinaitwa daladala ambalo si jina la Kiswahili sanifu lakini limetiwa katika matumizi.


Hata hivyo kuna hasara kubwa ya kutumia baadhi ya majina ya sheng ambayo yanapotosha maana halisi ya maneno hayo ya Kiswahili. Kwa mfano nchini Rwanda mtu akiwa hajakamilika kwa namna moja au nyingine watu wanamuita kasorobo. Kwa hakika kasorobo ni neno la Kiswahili kumaanisha kuna upungufu wa robo ya kitu kujalizia mahali fulani kama vile dakika kumi na tano za saa na kadhalika.


Hivyo inapotumika katika mazungumzo inawakanganya waswahili. Si hayo tu, Burundi ndio kuna mambo, eti muasi kwa lugha simo ya huko ni msichana mrembo.Kwa Kiswahili sanifu muasi ni mwanamgambo ama mtu msumbufu tu asiyeambilika wala kusemezeka.


Kenya na Tanzania ni nchi ambazo zinajulikana pia kuibuka na misimo mbalimbali na inayopotosha maana halisi ya maneno ya Kiswahili. Nchini Tanzania wengine huita msichana mrembo Mkwaju. Tunavyojua katika Kiswahili mkwaju ni namna moja ya kiboko cha kumchapa mtu. Je sasa twabadilisha jina la mrembo kuwa kiboko? Mambo mawili kando kabisa. Tanzania mtu atakwambia anasikia ubao kumaanisha kuwa anaona njaa. Inavyoeleweka ni kuwa ubao ni sehemu ya mti ama mbao katika Kiswahili sanifu. Na huko Tanzania mtu anapokwambia patachimbika ana maana ya kuwa pameharibika jambo. Utata unaojitokeza hapa ni kuwa patachimbika ni kitenzi cha Kiswahili kumaanisha hali ya pengine kufanya shimo mahali ama kutoboa kitu ilhali kuharibika ni kusambatarika kwa hali ama kitu fulani. Hizo ni dhana mbili tofauti kabisa kama mbingu na ardhi.

 


Nchini Kenya pia mambo ya sheng yanapigiwa upatu sana hususan na vijana. Hata hivyo ni muhimu kutaja kuwa matumizi ya maneno fulani huvuruga Kiswahili Kabisa. Kwa mfano katika lugha simo Kuro ni kahaba lakini ukweli ni kuwa katika Kiswahili kuro ni mnyama wa porini wa jamii ya paa anyefanana na kulungu. Yaani hapa kosa la kwanza ni kumlinganisha binadamu na mnyama. Pili neno mbuyu Kenya lina maana ya baba lakini katika Kiswahili ni mti unaozaa mibuyu na ikiwekwa semi na iwe "kuzunguka mbuyu" basi inamaanisha kutoa hongo.


Kadhalika neno demu ambalo linatumika Tanzania, Kenya na Jamhuri ya demokrasia ya Congo lina maana ya msichana lakini katika Kiswahili sanifu ni kitambaa kinachofunika mwanamke maziwa anapolima ama tambara hivi. Je unapomwita msichana demu hujui kwa Kiswahili unamlinganisha msichana huyo na tambara labda? Je huo ni uungwana? Kenya watu wanasema masa ni mama katika lugha simo lakini katika Kiswahili sanifu masa ni matendo mabaya yanayofanywa na mtu.

Athari nyingine ya lugha simo ni kuwa inaweza kuwafanya watu waache kuyatumia maneno mengine ya Kiswahili wakidhania ni Sheng. Baadhi ya maneno hayo ni kama vile manzi ambalo ni neno la Kiswahili sanifu kumaanisha msichana ila wengi hulitumia kama sheng. Ashara kumaanisha idadi kumi ni sawa kwa Kiswahili lakini Kenya watu wandhania hiyo ni sheng. Mifano zaidi ya msamiati wa Sheng:-

                   Sheng

        Kiswahili sanifu

 

a

Mnati, ras

Rasta

b

Babi, barbie

Mtu asiyeweza kuzungumza sheng

 

c

Bonga (bong-gah)

Zungumza/ongea/sema

 

d

Dungia (doong-gi-ah), gawia, chapia, vutia

Pigia mtu simu

 

e

Ocha, moshatha

Sehemu za mashambani

 

f

Njeve

baridi

 

g

Ngodha

chupi

 

h

Fegi, mozo, ngale, fuaka

Sigara

 

i

Kanjo

Askari wa mabaraza ya miji.

 

j

 Mboch.

mjakazi

 

k

Keja, hao, mbanyu, base, diggs

Nyumba/nyumbani

 

l

Magondi

Hofu/uwoga

 

m

Karau/kerea

polisi

 

C)    Athari za sajili kwa Kiswahili sanifu

Sajili ni mukhtadha/rejista mbalimbali au mitindo maalum ya lugha katika mazingira/hali mbalimbali. Itakubalika kuwa zipo rejista ambazo zinaathiri moja kwa moja Kiswahili  sanifu. Hivyo ni kuwa iwapo rejista hizi zitatumiwa kwa kiasi kwamba zinakuwa katika hali ya Kawaida ya mawasiliano basi Kiswahili Sanifu kitazidi kupata pigo.

Baadhi ya sajili ambazo hukandamiza Kiswahilisanifu nikama zifuatazo.

ü  Sajili ya Biashara

Lugha ya biashara huzungumzwa na wauzaji na wanunuzi katika sehemu za kibiashara. Inapaswa ikumbukwe kwamba lugha hii inaweza kubadilika kidogo kulingana na mazingira. Kwa mfano, katika mikutano ya kibiashara, lugha rasmi hutumiwa ilihali katika soko, lugha ya mitaani inaweza kutumika.

Sifa za Lugha ya Biashara

1.  Hutumia msamiati wa kibiashara kama vile:

      Fedha

      Faida

      Hasara

      Bei

      Bidhaa

2.  Hutumia misimu ili kuwavutia wanunuzi

3.  Ni lugha yenye malumbano hasa watu wanapojadiliana kuhusu bei

4.  Ni lugha legevu - haizingatii kanuni za lugha.

5.  Huchanganya ndimi kwa kuingiza maneno ya lugha za kigeni

6.  Ni yenye heshima na unyenyekevu kwa wanunuaji

7.  Msamiati katika lugha ya Kibiashara

Mfano wa Sajili ya Biashara

MtuX:

        Tatu kwa mia! Tatu kwa mia! Leo ni bei ya hasara!

MtuY:

        Unauza hii briefcase kwa pesa ngapi?

MtuX:

         Hiyo ni seventy bob mtu wangu

MtuY:

          Huwezi kunipunguzia. Niuzie hamsini hivi.

MtuX:

       Haiwezekani mtu wangu. NItapata hasara nikiuza hivyo. Ongeza    mkwaja, mama.

MtuY:

Basi hamsini na tano.

MtuX:

Tafadhali ongeza kitu kidogo. Unataka nikule hasara leo? Fikisha sitini na tano.

MtuY:

Basi sitanunua hii. Sina pesa hizo zote. Unajua uchumi ni mbaya siku hizi.

MtuX:

Tafadhali mtu wangu. Huu mkoba ni mzuri sana. Umetoka Germany. Angalia. Unaweka pesa hapa, kitambulisho hapa halafu unafunga hivi. Hauwezi kupoteza chochote ukiwa na mkoba huu. Angalia wewe mwenyewe. Hakuna mahali pengine utaweza kununua mkoba huu kwa bei ghali kama hii.

MtuY:

Nimekwambia sina hizo pesa. Nitanunua baadaye ukipunguza bei.

MtuX:

Lete sixty bob. Lakini utakuwa umeniumiza. Nakufanyia hivyo kwa kuwa wewe ni customer poa.

MtuY:

Sawa basi nitanunua. Shika sixty bob.

MtuX:

Asante Customer. Mungu akubariki. (akimfungia) Hey! Tatu kwa mia. Bei ya hasara! Tatu kwa mia!

ü  Sajili ya Bungeni

Hii ni lugha inayozungumzwa wakati wa kikao cha bunge. Sajili hii ni tofauti na na sajili ya siasa, ambayo huhusisha wanasiasa wakipiga kampeni.

Sifa za Lugha ya Bungeni

1.  Ni lugha yenye ushawishi – wabunge hutumia vishawishi ili kuwahimiza wenzao waunge ama kupinga msalaba

2.  Ni lugha ya mjadala yenye waungao na wapingao.

3.  Ni lugha yenye heshima na nidhamu. Maneno ya heshima kama mheshimiwa, tafadhali na samahani hutumika sana.

4.  Hutumia maneno maalum yanayopatikana katika mazingira ya bunge kama vile kikao, mswaada, kuunga mkono, kujadili, kupitisha, n.k.

5.  Lugha ya bungeni ni rasmi na sanifu.

6.  Hulenga maswala mbalimbali ya kisiasa na maendeleo katika taifa.

7.  Huwa na maelezo kamilifu

8.  Ni lugha yenye maswali na majibu miongoni mwa wabunge.

 

ü  Mfano wa sajili ya Bungeni

Spika:

Waheshimiwa, muda unayoyoma. Nawaomba mfanye mazungumzo yenu sauti ya chini tumsikize huyu. Endelea mheshimiwa.

Mbunge 1:

Asante Bwana spika. Hii siyo mara ya kwanza ya kuuwasilisha mswaada huu hapa. Kila mbunge anayethamini raia wa taifa hili ni lazima auunge mkono mswada huu. Katika kikao kilichotangulia, mliupinga mkidai kwamba hauna heshima kwa rais. Leo tumefanya ukarabati wote mliotaka. Hamna budi kuuunga mkono. Bwana spika….

Spika:

Muda wako umekwisha tafadhali keti. Wabunge wataamua hatima ya mswada huu ikiwa utapitishwa kama sheria. Lakini kumbukeni uamuzi wa mwisho ni wa rais

ü  Sajili ya Kidini

Katika sajili ya kidini tunaangazia lugha inayozungumzwa na waumini/washiriki wa imani fulani wakati wa ibada, sala, katika nyumba takatifu au mahali popote pale ambapo wanazungumzia mambo yanayorejelea imani au Mwenyezi Mungu.

Sifa za Lugha ya Kidini

1.  Hutumia msamiati wa kidini kama vile

      Bibilia

      maombi

      mbinguni

      jehanamu

      Madhabahu

      Paradiso

      Mbinguni

      Mwenyezi Mungu

      Mwokozi

2.  Ni lugha inayonukuu sana hasa wazungumzaji wanaporejelea Kitabu kitakatifu

3.  Lugha yenye heshima, upole na unyenyekevu

4.  Lugha sanifu

5.  Ni lugha iliyojaa ahadi nyingi kwa wanaoandamana na mafunzo ya kidini na vitisho kwa wanaoenda kinyume na mafundisho

6.  Huwa imejaa matumaini

7.  Ni lugha yenye kutoa maneno ya sifa, kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu

Mfano wa Sajili ya Kidini

Boriti:

Bwana asifiwe Bi...

Bi Rangile:

Amina, mchungaji. Watoto wanaendeleaje?

Boriti:

Karita hana neno. Mwenyezi Mungu ametunyeshea rehema na neema zake. Je, wajukuu wako wa hali gani?

Bi Rangile:

Wanaendelea vizuri isipokuwa hawataendelea na masomo. Sijui nilimfanyia Mungu dhambi gani.

Boriti:

Nasikitika sana kusikia hivyo. Mungu atawalinda mayatima hao. Yeye ndiye baba wa mayatima. Mungu ni mwenye huruma.

Bi Rangile:

Sijui hayo, mchungaji. Hata sijui maana ya kuishi hapa duniani. Kila siku ni matatizo.

Boriti:

Usife moyo. Mungu anasema katika kitabu cha Yohana 14:18, "Sitawaacha nyinyi kama mayatima..." Kwa hivyo, ukiwa na imani, Mungu atakuonekania.

Bi Rangile:

Basi niombee mchungaji ili Saumu na Neema wapate karo ya kurudi shuleni.

Boriti:

Funga macho tusali. Ewe Rabuka uliyejaa neema na baraka tele. Tunakushukuru na kulitukuza Jina lako takatifu kwa baraka zako za ajabu. Tunajua kwamba wewe ndiye Mungu uliyewatoa wana wa Israeli kutoka Misri. Sisi wenye dhambi tunakuja mbele yako tukiomba ukafanya miujiza katika nyumba hii ya Bi Rangile......

Wote:

Amina.

Sajili ya Kisayansi

Sifa za Lugha katika sajili hii

1.  Hutumia msamiati wa kipekee unaoambatana na taaluma inayorejelewa.

2.  Huwa na maelezo kwa ukamilifu.

3.  Huwa na mpangilio maalum na maendelezo ya hoja na ujumbe.

4.  Huchanganya ndimi na kutumia maneno ya kisayansi au lugha mbalimbali.

5.  Hutumia lugha sanifu.

6.  Ni lugha yenye udadisi mwingi (wakati wa kufanya utafiti)

Kwa sababu zisizoweza kuepukika, kikundi chetu hakitamaliza utafiti ulioratibiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwezi ujao. Hii ni kwa sababu ya changamoto kadhaa ambazo tumekutana nazo. Kwanza, viluwiluwi, ambao ndio tunaotafiti wamekuwa haba sana wakati huu wa ukame. Pili, kutokana na kufungwa kwa maabara ya kisayansi katika taasisi hii, ni muhali kufanya majaribio yoyote ya kazi yetu. Tatu, kumekuwa na pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya wanakijiji kwamba kukusanya viluwiluwi kunawatia hofu. Aidha, tume yetu imepungukiwa na fedha baada ya serikali kusitisha kudhamini utafiti huu.

Baada ya kujadiliana kwa vikao tatu mfululizo, tume yetu inapendekeza haya: Muda wa kufanya utafiti uongezewe kwa kipindi cha miezi sita; serikali kupitia kwa taasisi hii ifadhili wachunguzi. Wananchi wahamasishwe kuhusu umuhimu wa kuwafanyia viwavi utafiti na maabara ya utafiti ikaraatiwe haraka iwezekanayo.

Sajili ya Mahakamani

Hii ni lugha inayozungumzwa na wanasheria, mahakimu, mawakili, washitakiwa na mashahidi katika mahakama.

Sifa za Lugha ya Mahakamani

1.  Hutumia msamiati wa kipekee unaorejelea sheria kama vile

      katiba

      sheria

      mashtaka

      Hakimu

      Ushahidi

      Wakili

      Jela

      Mshitakiwa

      Kiongozi wa mashtakiwa

2.  Huwa na maelezo marefu na ya kina ili kutafuta ushahidi wowote uliopo

3.  Ni lugha yenye kunukuu sana hasa vipengele katika vitabu vya sheria kama vile katiba

4.  Ni lugha rasmi na sanifu

5.  Ni lugha iliyojaa maswali na majibizano

6.  Ni lugha yenye heshima

 

Mfano wa Sajili ya Mahakamani

Kiongozi:

Musa Kasorogani, mwanaye Bi Safina na Mzee Mpotevu Kasorogani; umeshtakiwa kwa kosa la jaribio la mauaji mnamo tarehe 23/08 mwaka huu. Unaweza kukubali mashitaka, kukana au kunyamaza. Je, unakubali mashitaka.

Musa:

Naomba kukanusha mashtaka hayo, bwana mkubwa.

Kiongozi:

Je, kuna shahidi yeyote katika kesi hii?

Katili:

Hapa mkubwa. Siku hiyo ya tarehe 23/08, Musa alipatikana akiwa akijinyonga usiku wa maneno. Kijiji chote kilikusanyika hapo kwenye boma ya Kasorogani. Nilipoleta polisi, wakamkamata na kumpeleka hospitalini atibiwe kwanza. Ndiposa ameletwa hapa siku ya leo.

Kiongozi:

Je, mshitakiwa una tetesi lolote. Ama pia unaweza kuleta wakili wako azungumze kwa niaba yako.

Kisaka:

Bwana mkubwa, mimi ndiye wakili na shahidi wa Musa. Musa hakuua mtu. Alikuwa akijinyonga kutokana na mkasa uliomfika tarehe hiyo ya Agosti 23 baada ya bibi harusi wake kubadilika. Mimi na mamake, Bi Safina Kasorogani tulijaribu kumtuliza jioni hiyo. Asubuhi nilipoamka siku iliyofuatia, nikapata habari kwamba alikuwa amepelekwa hospitalini. Je, alipojaribu kujiua, alimwua mtu yeyote?

Kiongozi:

Kulingana na katiba ya nchi hii, kifungu cha 12.ab, kuua ni kutoa uhai wa binadamu yeyote. Haijalishi ikiwa ni yeye mwenyewe au ikiwa ni rafiki yake. Hivyo basi jaribio la kujiua ni hatia kulingana na kanuni za nchi hii. Una jingine la kuulizia?

Kisaka:

Je, sheria yetu inaruhusu mtu kuadhibiwa kwa kosa ambalo hakufanya?

Kiongozi:

La hasha.

Kisaka:

Basi tutakuwa tumekiuka kanuni za nchi yetu iwapo tutamhukumu Musa kwa kujiua ilhali hakujiua bado. Tunawezaje kutambua kama angekufa?

Katili:

Inafaa ahukumiwe kinyonga au kifungo cha maisha gerezani. Hata alivunja simu yangu...

Kiongozi:

Order! Lazima kutii mpangilio wa mahakama. Katili hauruhusiwi kuongea bila ruhusa ya hakimu au kiongozi wa mashitaka. Polisi, mpelekeni nje.

ü  Sajili ya Michezoni

Lugha ya michezoni hutumiwa wakati wa mashindano ya michezo kama vile kandanda, ukimbiaji n.k Hii inaweza kuwa lugha ya watangazaji/wasimulizi wa mchezo, watazamaji, mashabiki au wachezaji.

Sifa za Lugha ya Michezoni

1.  Hutumia msamiati wa kipekee unaohusu michezo kama vile mpira, goli, mchezaji

2.  Huchanganya ndimi na kuingiza maneno ya lugha nyingine kama vile Kiingereza. mfano 'goal!!!'

3.  Ni lugha ambayo hutumia vihisishi na mshangao kwa wingi

4.  Sentensi nyingi katika lugha hii huachwa bila kukamilika hasa hali inapobadilika uwanjani

5.  Husimuliwa kwa haraka haraka ili kuambatana na kasi ya mchezo

6.  Ni lugha yenye sifa na na chuku kwa mfano msimulizi anaposimulia sifa za mchezaji fulani

7.  Hutumia misimu kama vile 'wametoka sare'

8.  Hutumia kwa ya kulinganisha ili kuelezea matokeo ya mechi k.m 'walitoka mbili kwa nunge'

9.  Ni lugha yenye kukariri (kurudia rudia) hasa mchezaji anapoumiliki mpira kwa muda mrefu au mwanariadha fulani anapoelekea kushinda katika mbio.

10.   Huwa na sentensi fupi fupi

 

Mfano wa Sajili ya Michezoni

Nakwambia ndugu msikilizaji hapa mambo yamechacha kwelikweli. Hawa wachezaji wa Manyuu hawacheki na watu leo. Wameamua kuishambulia timu ya Cheusi bila huruma. Kumbuka kwamba hii ni mara yao ya... Lo! Anauchukua mpira pale, mchezaji nambari tisa... Matiksta. Matiksta, Matiksta na mpira. Anaucharazacharaza pale. Anamwangalia mwenzake. Anaupiga mpira kwa kichwa pale! Lo! Mwenzake anaukosa. Akiushika mpira pale ni mchezaji wa timu ya Cheusi, Romana. Romana, Romana anaelekeza mpira kwenye lango la Manyuu. Anaupiga mpira kwa nguvu! Lo! Hatari sana. Hatari sana katika lango la Manyuu. Hatari! hatari! Goooooooooo ooooh! Wameukosa! Goal keeper ameudaka mpira huo. Pole sana wachezaji wa ... Mlinda lango anaupiga mpira huo kwa hasira. Juu kabisa. Anauchukua pale nambari saba, Saruta. Huyu ni mchezaji machahari sana. Mwaka uliopita, alipewa tuzo la mchezaji bora wa mwaka. Ananyang'anywa na mchezaji mwingine hapa. Wanakabiliana kidogo. Huyu mchezaji anaupiga mpira kwa mguu wa kushoto. Lo! Mpira umekuwa mwingi na ukatoka nje.

 

Mashabiki wa timu hizi mbili wanasubiri kwa hamu na ghamu kutambua ni nani atakayeibuka mshindi. Katika mechi zilizotangulia, timu hizi zimekuwa zikitoka sare. Lakini leo lazima mshindi atapatikana. Hawa ni fahali wawili. Kumbuka kwamba unapata matangazo haya moja kwa moja kupitia idhaa yako uipendayo, redio nambari moja kote nchini... Mpira unarudishwa uwanjani. Akienda kuurusha pale ni...

ü  Sajili ya Mitaani

Lugha ya mitaani ni lugha inayozungumzwa na vijana mtaani.

Sifa za Lugha ya Mtaani

1.  Ni lugha legevu isiyozingatia kanuni za kisarufi

2.  Huchanganya ndimi

3.  Hutumia misimu kwa wingi

4.  Hukosa mada maalum

 

Mfano wa Sajili ya Mtaani

Chali:

Hey, niaje msupaa?

Katosha:

Poa. So, mathee yako alikushow naweza kuja?

Chali:

Ha! Masa hana noma. Si unajua nita...

Katosha:

Chali! Unataka aniletee problem?

Chali:

Mimi ni boy wa maplans. Ngoja nifikirie venye tutamshow

Katosha:

Na by the way, kwani umejipaka mafuta ya manzi. Ama ulikuwa na msichana mgani?

Chali:

Oh! Niliscoop mafuta ya Anita. Si unajua nataka kunukia hmmmm...

Katosha:

Ok. So, umefikiria tumshow nini masa yako? Ama nikona idea poa.

Chali:

Nishow hiyo plot, na by the way, nataka unisaidie kuhusu ile deal yangu na Kaunda. Ile ya siz yangu.

Katosha:

Kwanza tutaplan na huyo siz yako, niwe ndiye nimekuja kuvisit. Mamako atakubali

Chali:

Wow! Idea poa. Utakuwa umekuja kufanya homework. Halafu masa akiishia kwa bed. Homework tutaitupa mbali.

Katosha:

So, utamshow Anita nakuja tufanye homework...

D)     Athari za lugha ya kwanza (mama)

Kiswahili sanifu vile vile huathirika kwa kiwango kikubwa na lugha za kwanza(mama) za wanaokizungumza. Lugha hizi huathiri pakubwa silabi pamoja na lafudhi ambapo wanazungumza lugha hizi, wengi wao wameathirika kiasi kwamba wanazihamisha silabi zao asilia hadi kwa Kiswahili huku wakiwa na dhana kuwa wanakijenga kumbe wanakibomoa Kiswahili Sanifu.

 

. Hili huwa tatizo kubwa sana kiasi kwamba sarufi za lugha za mama haziingiliani na sarufi ya Kiswahili sanifu.

Kwa mfano katika nafsi za Kiswahili Sanifu  tunapata viwakilishinafsi vifuatavyo:

NAFSI

UMOJA

WINGI

1

NI

TU

2

U

M

3

A

WA

 

Zipo baadhi ya lugha mama hasa za kinailoti ambazo huvitumia au kuhamisha  viambishi nafsi vya lugha yao hadi Kiswahilipasi kufahamu madhara wanayoyaleta kwenye sarufi ya Kiswahili.

Kwa mfano katika lugha ya Waluo, utagundua kwamba wao hutumiwa kiwakilishinafsi A kurejelea nafsi ya kwanza hali ya umoja ambapo katika Kiswahili huwa nafsi ya tatu umoja.

Utawaskia wakisema :

a.      Abiro-Ninakuja

b.      Adwaro-Ninataka

Katika mtindo huo, wapo wale ambao huhamisha nafsi hii namna ilivyo hadi kwenye Kiswahili. Utawaskia wakisema:

a.       Mimi anaenda shuleni. Badala ya :Mimi ninaenda shuleni.

b.      Mimi  anaandika polepole.Badala ya:Mimi ninaandika polepole.

c.       Mimi  anasoma haraka. Badala ya:Mimi ninasoma haraka.

Kwa kufuata mifano ya hapo juu itaonekana wazi kuwa wanaotoka  maeneo hayo ambao huitumia lugha yao ya kwanza kama kioo wanapozungumza Kiswahili  basi wana kazi ya ziada.

Hivyo basi wahusika hawa hustahili kuiacha kando lugha yao ya mama wanapoikabili sarufi ya Kiswahili la sivyo hali itawaendea mrama.

Waaidha zipo lafundhi za lugha hizi za kwanza ambazo huathiri sana sarufi ya Kiswahili katika lugha ya Kikamba wengi wao hutamka konsonanti J kama Y. Utagundua kwamba asilimia kubwa ya Wakamba wanapozungumza mahali palipo na J watatamka Y.

Kwa mfano:

KISWAHILI

KIKAMBA

Jua

Yua

Juu

Yuu

Juni

Yuni

 

Waaidha palipo na  sauti G wao hupachika NG

Kwa mfano:

KISWAHILI

KIKAMBA

Goli

Ngoli

Gareji

Ngaleji

Goti

Ngoti

 

Palipo  na R wanaweka L.

KISWAHILI

KIKAMBA

Rudi

Ludi

Rarua

Lalua

Rinda

Linda

Mrembo

Mlembo

 

Mfano mhusika hataeleweka iwapo ataambiwa aisome sentensi kama hizi;

a.      “Linda ana rinda refu lililoraruka vibaya.”

b.      “Mimi ni fundi wa kupaka rangi”

Utamsikia mhusika akitamka:

a.      “Linda ana linda lebu lililolaluka bimbaya.”

b.      “Mimi ni bundi wa kubaka langi.”

Katika hili kama hii sarufi Kiswahili sanifu hufanywa chapwa mno.

Katika mfumo huo, jamii ya Waluhyia haijasazwa nje. Katika jamii hii utagundua kuwa lafudhi yao wakati mwingine huwatia mashakani katika uchambuzi na usomi wa Kiswahili.

Wengi wao badala ya sauti B hutia P, Sauti Z hutia S, D hutia T

Kwa mfano:-

Matamshi bora ya Kiswahili

Matamshi bandia ya Kiluhyia.

1

Baba

Papa

2

Bora

Pora

3

Bata

Pata

4

Bure

Pure

5

Bei

Pei

6

Birika

Pirika

7

Bila

Pila

 

 

 

Sauti Z na S

Matamshi bora ya Kiswahili

Matamshi bandia ya Kiluhyia.

1

Mzuri

Msuri

2

Mzee

Msee

3

Mzinga

Msinga

4

Muziki

Musiki

5

Mkizi

Mkisi

6

Zambarau

Sambarau

7

Mzigo

Msiko

 

Sauti D na T

Matamshi bora ya Kiswahili

Matamshi bandia ya Kiluhyia.

1

Dada

Tata

2

Daktari

Taktari

3

Dadisi

Tatisi

4

Dereva

Tereva

5

Darasa

Tarasa

6

Domo

Tomo

7

Daka

Taka

 

Kwa kuangaziwa athari za hapo juu ni dhihirisho tosha kuwa kufundisha sarufi katika mazingira hayo huwa kugumu sana. Tatizo kubwa ni kupata kuwa kila mmoja ana  shida moja ingawa hakuna anayegungua  shida kama hiyo miongoni mwao.

Hivyo basi, ni muhimu kwa msomi au mwelekezi ambaye kwa njia moja au nyingine ana tatizo kama hili basi ni muhimu kuzingatia sauti za Kiswahili sanifu  pamoja na konsonanti zote hukuakitilia maanani matamshi bora ambayo hayataathiriwa na lugha zao za kwanza.

Kwa hivyo athari kama hizi vile vile ni kuangaziwa kwa somo linalohusu konsonanti na sauti katika Kiswahili ili kujenga msingi imara katika matamshi ambayo huathiri sana Kiswahili sanifu

Hitimisho.

Kwa yakini viswahili sanifu kina mapigo aina ainati ambayo yanakiathiri kucha kutwa.Baadhi ya mapigo haya hutokana moja kwa moja na watumizi wa Kiswahili wenyewe ambao kwamba hawakitumii kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa bali shaghalabaghala.Hivyo basi niwajibu wa kila mmoja kuona kuwa anapoitumia lugha hii ya Kiswahili, azingatie kanuni zote za kisarufi.

Waaidha yapo makosa yatokanayona mazingira ambayo kwa upande wake huwa na athari kubwa sana. Ni jambo la busara kwa yeyote kubaini kuwa usanifu wa Kiswahili ni swala nyeti la kuvaliwa njugabila simile.La sivyo hali hii ya mazigira huenda ikaleta utata mkubwa sana.

Ni wajibu piawa kila mmoja  kugungua kuwa baadhi ya lugha zetu za kwanza imaziwe za kibantu ama kinailoti, zina tofauti kubwa sana na Kiswahili sanifu. Hivyo basi ni jambo la msingi kwa kila mmoja kutofauti silabi za lugha zao za mama na silabi au sauti za Kiswahili hasa sanifu. Kwa wengi hufanya makosa pasipo hata wenyewe kufahamu kuwa wametenda makosa.

iwapo kila mmoja atakitumia Kiswahili kwa usanifu ufaao, basi kwa vyovyoteviwavyo lugha hii itakua na kuimarika na usanifu wake. Hivyo basi ni jukumu la kila mmoja kuitetea lugha hiikwa kuona kuwa usanifu wake unabaki na kutumika itakikanavyo.

MAREJELEO

a.       King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimujamii.Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Chuo kikuu cha Dar es salaam.  

b.      Mlacha, S.A.K. na Hurskainen, A. (1995). Lugha, Utamaduni Na Fasihi Simulizi ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Idara ya Taaluma za Asia na Afrika na Chuo Kikuu cha Helsinki. TUKI

c.       Msanjila, Y.P na wenzake. (2011). Isimujamii: Sekondari na Vyuo. TUKI. Dar es salaam.

d.      TUKI, (2004).Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).

e.       Crystal, D. (2002). The Cambridge of Encyclopedia of Language: Second edition. London. Cambridge University Press.

f.       Halliday, M.A.K. (1990). Spoken and Written Language. London. Oxford  University Press.

 

Post a Comment

0 Comments