CHANGAMOTO ZILIZOMO KATIKA KUHAKIKI FASIHI YA
KISWAHILI KIHISTORIA KWA KUREJELEA TAMTHILIA YA MASHETANI.
Ebrahim Hussein alizaliwa mnamo mwaka wa
1943. Aliandika tamthilia yake ya kwanza,Kinjeketile
(1969), Jogoo Kijijini (1976),
Mashetani (1971) na Arusi (1980). Tamthilia ya Mashetani iliandikwa 1971 takriban miaka kumi baada ya
Tanzania kujinyakulia uhuru. Harakati za waafrika kupigania uhuru, maono na
azma yao ya utawala bora wa Mwafrika ndio yalimchochea mwandishi huyu kuandika
tamthilia hii.
Nchi ya Tanganyika ilipata uhuru tarehe
1/5/1961 ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, na
kisha kuungana na serikali ya Zanzibar na kuwa Tanzania mwaka wa 1964 chini ya
uongozi wa
Abeid Amaan Karume.Waafrika waliokuwa na elimu ya juu wakachukua nyadhifa
mbalimbali za
uongozi. Kinyume na matarajio ya wananchi wa kawaida, viongozi hawa wakawa
‘Wazungu
Weusi'. Hii inamaanisha kuwa walichukua mienendo yote na kasumba zote za
wakoloni. Visa
vya ufisadi, ukabila, ubinafsi na tamaa ya kujilimbikizia mali ikawa hali ya
kawaida.
Isitoshe, serikali ya Zanzibar iliamua
kutaifisha mashamba yaliyokuwa yamenyakuliwa na viongozi
waliokuwepo katika enzi za utawala wa wakoloni na kugawia viongozi hawa wapya.
Hali hii
ikazua utabaka kwani, jamii ambazo zilikuwa tajiri hapo awali zikaanza kutamba
katika
mazingira ya uchochole. Waliokuwa maskini awali lakini wenye kisomo cha
kimagharibi
wakaanza kupanda ngazi ya ufanisi kiuchumi kwa haraka zaidi kama wasemavyo,
"kulala
maskini na kuamka tajiri".
Haya
ndio mazingira aliyokulia ndani mwandishi Ebrahim Hussein. Rais Nyerere
alipotanabahi udhaifu huu katika serikali yake, akaamua kubuni sera mpya ambayo
aliona kuwa ingeondoa utabaka na kuleta usawa wa kiuchumi katika jamii.
Akazindua Azmio la Arusha mnamo mwaka wa 1967. Hii ni sera ya serikali
iliyonuia kuunda mfumo wa Ujamaa.
Mfumo huu ulikusudia kuondoa pengo la utabaka na kufanya jamii ya Watanzania
kuishi kwa undugu. Mwanzoni, mfumo huu ulivuma sana kwa kuinua kiwango cha
elimu, afya na kupunguza utabaka. Hii ni kwa sababu alitaifisha sekta zote za
uchumi na kuanzisha mfumo wa kilimo kupitia kwa mashamba yaliyokuwa
yametaifishwa vijijini. Kiwango cha uzalishaji mali kikaongezeka kufikia hali
ya Tanzania kuanza kujitegemea.
Sera
hii haikudumu kwa sababu mfumo huu ulianza kukumbwa na changamoto za aina
mbalimbali. Kwanza, wawekezaji wa kibinafsi walianza kupungua kwa sababu sekta
nyingi za uchumi zilikuwa zimetaifishwa. Bidhaa zilizozalika kuanzia mazao ya
mashamabani hadi bidhaa za viwandani zikakosa soko la kimataifa kwa sababu ya
mfumko wa bei ulimwenguni. Mfumko huu ukaathiri pia taifa kuu la Tanzania hadi
kuifanya serikali kushindwa kutekeleza huduma muhimu.
Watu
wengi wakatamaushwa kwa sababu ya matatizo mengi ya kiuchumi. Kina cha matukio
haya ya kihistoria ndio yaliyomchochea Ebrahim Hussein kuandika tamthilia ya Mashetani.
CHANGAMOTO ZA KUHAKIKI FASIHI YA KISWAHILI KIHISTORIA.
Kimani
na Chimera(1999), wanaeleza kuwa kupitia kwa maigizo katika Mashetani,
msomaji,msikilizaji au mtazamaji huanza kufahamu mahusiano kati ya viongozi na
waongozwa, uhuru na ukoloni mamboleo, ukoloni mkongwe, na unyanyasaji wa
Waafrika na Wakoloni wazungu. Vile vile mtafaruku kati ya mabwana waliokuwa na
madaraka mbeleni na wale wanaochukuwa nyadhifa za uongozi baada ya uhuru
unaangaziwa. Matukio hayo japo ni ya mwandishi yanaafiki vilivyo historia ya
Tanzania. Mulokozi, M.M alidokeza vigezo vinne vikuu vya kuzingatia iwapo
utalinganisha fasihi na historia. Navyo ni matukio, wahusika na mbinu au mtindo wa
uandishi. Kwanza, matukio jinsi yalivyotukia katika Historia huwa
tofauti zaidi kuliko jinsi yanavyotukia katika mawanda ya fasihi. Baadhi ya
sehemu za matukio katika hadithi za fasihi zaweza kutokea kama zisizo za kweli,
licha ya kuwa hadithi yaweza kuwa ya kuvutia au yenye ubunifu mkubwa.
Matukio katika fasihi hurejelea wahusika wa kihistoria
ambao huundwa upya kisanaa. Historia huangazia matukio ya wahusika jinsi
wanavyojitokeza katika hali halisia. Historia ya Tanzania iliangazia wahusika
halisi waliochangia katika kuchipuka kwa mapinduzi kisiwani Zanzibar kama vile
Abedi Karume na Sultani. Wahusika hawa kihistoria walifafanuliwa kihistoria kwa
kueleza sifa na tabia zao asilia. Lakini fasihi, inawajenga wahusika wapya wa
kubuni kama vile jamii ya Juma na Kitaru, wanaoafiki viongozi hawa.
Katika
Historia mkazo huwekwa kwa matukio muhimu ambayo yana mchango mkuu katika
mkondo wa matendo yatakayoathiri maisha ya binadamu.Tukio kuu katika Historia
ya Tanzania ni mapinduzi ya Sultani wa Zanzibar na kujinyakulia uhuru kwa
Waafrika. Kwa upande mwingine, matukio makuu ya historia hutumiwa kama muktadha
wa matendo ya hadithi ambayo huweza kuwa ya ukweli au ya kubuni. Katika
tamthilia ya Mashetani, tukio la Shetani kumpa Binadamu kisu (uk 8), inaashiria
jinsi mzungu alivyopanga na kumpa Mwafrika uhuru kwa hiari yake bila
kushinikizwa. Tukio hili huenda likawa si la kweli bali ni ubunifu tu wa
mwandishi kwa sababu kuna vikosi vya wapiganaji ambao walimwaga damu kwa ajili
ya kujikomboa.
Fasihi
husistiza jinsi wahusika wa matukio madogo madogo ambayo huchopeka katika matukio
makuu ya kihistoria hujitokeza.Kwa mfano, fasihi yaweza kutoa msisitizo kwa
wahusika shujaa ambao labda katika hali halisia hawakuwahi ishi kamwe. Jamii ya
Kitaru na Juma ni ya kubuni tu, huenda jamii kama hizi hazikuwahi kuishi kama
jirani mjini Dar es salaam kama anavyodai mwandishi.Mwanafunzi ambaye angependa
kuelewa zaidi historia ya matukio haya, huenda hatanufaika zaidi akiegemea
matukio ya wahusika hawa.
Kwenye
fasihi, migogoro ya taifa au jamii hufasiriwa katika hisia na matendo ya watu
binafsi. Mgogoro kati ya Juma na Kitaru unaafiki migogoro iliyojitokeza kati ya
makabaila na mabwenyenye kihistoria:
Juma: Hatuonani tena.
Kitaru: Kwa nini?
Juma: Sababu nyingi.
Kitaru: Mojawapo?
Juma: Mpanda ngazi na mshuka ngazi hawawezi kushikana mikono. (Uk.55-56)
Katika kifungu hiki taswira ya utabaka inasawiriwa kupitia kwa mtafaruku
wa uhusiano uliopo kati ya Juma na Kitaru. Kama ingekuwa historia, ingeangazia
sifa halisi za tabaka hizi mbili bila kujikita kwa wahusika wawili tu katika
jamii.
Fasihi
inayofanikiwa sana ni ile inayojikita zaidi katika migogoro mikali zaidi ya
kihistoria. Fasihi ambayo haitaangazia migogoro mikali ya kijamii ya kufa na
kupona kama vita, utabaka au mapinduzi hupuuziliwa mbali.Tamthilia ya Mashetani ilivuma na kubobea zaidi kifasihi kuliko tamthilia
zingine za wakati huo kwa sababu iliafiki mapinduzi na kuzuka kwa utabaka
miongoni mwa Waafrika wenyewe, kinyume cha matarajio. Mwanafasihi ambaye
angependa kufurahia kusoma matukio hayo madogo huenda asipate makala ya
kutosha.
Historia
hueleza ukweli jinsi ulivyotokea. Kwa mfano Azimio la
Arusha la mwaka wa 1967, limeelezwa kwa undani zaidi
kupitia taaluma ya historia. Mipangilio, sera na mikakati yote ya utekelezaji
wake yalielezwa kinagaubaga katika taaluma ya historia.Watendaji wa matukio
katika historia hawapewi sifa au tabia kinyume cha jinsi walivyokuwa kihalisia.
Lakini baadhi ya matini ya fasihi huwapa wahusika wao majukumu mapya kinyume
cha hali ilivyokuwa kihistoria. Katika Mashetani, mwandishi
hakuzama zaidi kueleza suluhu la tatizo la mgogoro wa kitabaka kama
inavyobainika katika historia kwa kuanzishwa kwa ujamaa.
Wahusika wa Historia ni watu waliopata kuishi. Lakini katika
fasihi ni wahusika wa kubuni. Msomaji wa fasihi huona matukio ya kihistoria
kupitia kwa wahusika wa matini. Kisa cha Binadamu kumwua Shetani kwa kumdunga
kisu katika tamthilia ya Mashetani kinadhihirisha tukio la historia la Tanzania
kujinyakulia uhuru mnamo mwaka wa 1964 kutoka kwa Wazungu. Changamoto
zinazomkumba msomaji wa makala haya ni kwamba hataweza kusawiri hali halisi ya
kihistoria jinsi matukio hayo yalitukia. Kabla ya kuuawa, Shetani anapendekeza
kusherehekea kifo chake, kisha anakubali kumpa binadamu kisu ili amuue. Kila
pigo la kisu kwa shetani linazua kicheko.
Baada
ya mauaji Binadamu anashindwa kujitambua kama kweli alimuua Shetani au la.
Kadhia hii ilinuia kumfahamisha msomaji namna na jinsi Mwafrika alivyonyakua
mamlaka kutoka kwa mkoloni.Kwamba mzungu aliamua tu kumpa uhuru kwa hiari yake
bila kushinikizwa, na baadaye athari za kuendelea kuwepo kwa ukoloni mamboleo
ukaendelea kudhihirika kupitia kwa kicheko. Kimsingi ni kuwa fasihi hueleza
matukio yake kwa ubunifu mkubwa kuliko huistoria. Ubunifu huu huenda ukamshinda
msomaji wa kawaida kuelewa namna matukio hayo yalivyotukia kihistoria. Ni kweli
kihistoria kuwa wapiganiaji uhuru walikufa na wengine kujeruhiwa, kinyume na
inavyosawiriwa tamthilia kuwa Waafrika walipewa uhuru moja kwa moja kwa njia ya
mzaha.
Tabia za wahusika
wa fasihi wakati mwingine hupewa sifa za chuku. Mhusika Shetani ana uwezo wa
kurukia kwenye tawi, aweza kuamua kuuawa na namna ya kuuawa kwake. Vile vile,
anapodungwa kisu haonyeshi huzuni wala kilio bali anaonyesha furaha kupitia
kicheko. Wahusika wa historia wanadhihirisha tabia zao asilia. Historia
inapozungumzia mapinduzi ya Abedi Karume ya Zanzibar, husimulia tabia halisi ya
wanaharakati wa mapinduzi. Jambo hili huwanyima wanafasihi uhondo wa kuelewa
sifa halisi za wahusika wao.
Wahusika wa Historia ni watu waliopata kuishi. Lakini katika
fasihi ni wahusika wa kubuni. Msomaji wa fasihi huona matukio ya
kihistoria kupitia kwa wahusika wa matini. Kisa cha Binadamu kumwua Shetani kwa
kumdunga kisu katika tamthilia ya Mashetani kinadhihirisha tukio la historia la
Tanzania kujinyakulia uhuru mnamo mwaka wa 1964 kutoka kwa Wazungu. Changamoto
zinazomkumba msomaji wa makala haya ni kwamba hataweza kusawiri hali halisi ya
kihistoria jinsi matukio hayo yalitukia. Kabla ya kuuawa, Shetani anapendekeza
kusherehekea kifo chake, kisha anakubali kumpa binadamu kisu ili amuue. Kila
pigo la kisu kwa shetani linazua kicheko. Baada ya mauaji Binadamu anashindwa
kujitambua kama kweli alimuua Shetani au la. Kadhia hii ilinuia kumfahamisha
msomaji namna na jinsi Mwafrika alivyonyakua mamlaka kutoka kwa mkoloni.Kwamba
mzungu aliamua tu kumpa uhuru kwa hiari yake bila kushinikizwa, na baadaye
athari za kuendelea kuwepo kwa ukoloni mamboleo ukaendelea kudhihirika kupitia
kwa kicheko. Kimsingi ni kuwa fasihi hueleza matukio yake kwa ubunifu mkubwa
kuliko huistoria. Ubunifu huu huenda ukamshinda msomaji wa kawaida kuelewa
namna matukio hayo yalivyotukia kihistoria. Ni kweli kihistoria kuwa
wapiganiaji uhuru walikufa na wengine kujeruhiwa, kinyume na inavyosawiriwa
tamthilia kuwa Waafrika walipewa uhuru moja kwa moja kwa njia ya mzaha. Tabia za
wahusika wa fasihi wakati mwingine hupewa sifa za chuku. Mhusika Shetani ana
uwezo wa kurukia kwenye tawi, aweza kuamua kuuawa na namna ya kuuawa kwake.
Vile vile, anapodungwa kisu haonyeshi huzuni wala kilio bali anaonyesha furaha
kupitia kicheko. Wahusika wa historia wanadhihirisha tabia zao asilia. Historia
inapozungumzia mapinduzi ya Abedi Karume ya Zanzibar, husimulia tabia halisi ya
wanaharakati wa mapinduzi. Jambo hili huwanyima wanafasihi uhondo wa kuelewa
sifa halisi za wahusika wao.
Mtindo wa lugha ni kigezo kingine ambacho huzua changamoto katika
kuhakiki kazi ya fasihi kihisoria. Mbinu za lugha, mbinu za uandishi na mitindo
aliyotumia msanii wa fasihi huzua changamoto kwa wanahistoria.Historia hueleza
matukio yake kwa njia wazi na yenye muala kiusababishaji. Aidha, tukio la
kwanza kihistoria huwa mwanzoni kutokea na la mwisho huwa mwisho. Mwandishi wa
fasihi huvuruga kanuni hii kwa kutumia vipengele kama mbinu rejeshi au msuko usio muala. Katika Tamthilia ya Mashetani
tukio la Baba Kitaru kurudi nyumbani akiwa na furaha tele linaenda sambamba na
lile la Juma kuwa kwao nyumbani kwa kibanda akizungumza na Bibi. Matukio haya
yakiwekwa katika muktadha wa mtiririko wa kihistoria huzua changamoto tele. Kwa
mfano, katika historia huwezi kuzungumzia athari za vita kabla ya kuangaza
chanzo chake. Lugha ya Historia huwa rahisi na wazi ilhali lugha ya fasihi huwa
changamano na yenye mafumbo mengi.
Matumizi
ya jazanda na taswira humtatiza mwanahistoria anayechanganua matini ya fasihi.
Kimani na Chimera (1999), wanatoa mifano ya taswira iliyotumiwa na mwandishi
kusawiri matukio mengine tofauti. Shetani awakilisha mkoloni, Binadamu ni
Mwafrika mtawaliwa, chewa ni mfumo wa kibepari na ndoto ya Kitaru ni ufunuo wa
migogoro ya kitabaka iliyozuka baada ya kutaifisha mashamba. Kadhalika, joka la
vichwa saba linaashiria nchi saba za kibepari, manyoya aliyomea Kitaru
yanaashiria utajiri au mali.Haitawezekana maudhui kama vile: mahali pa
utamaduni halisi wa kiafrika, athari za ukoloni mkongwe, ubwanyenye,na ukoloni
mamboleo kueleweka ipasavyo ikiwa mwanahistoria hataainisha na kuelewa lugha
hii ya taswira, jazanda na ishara.
HITIMISHO
Jinsi ilivyojadiliwa katika makala hii, ni ukweli usiopingika kuwa kuna
uhusiano mkubwa zaidi kati ya fasihi na historia. Lakini kufasiri vilivyo kazi
ya fasihi kwa kuegemea taaluma ya historia huzua changamoto nyingi katika
ugunduzi na uelewekaji wa matini ya fasihi. Kwa hivyo, ili mwanahistoria aweze
kufurahia uhondo wa fasihi, lazima awe makini kuelewa na kubainisha mbinu za
kafasihi. Kutokuwa na maarifa na ujuzi wa kiuchanganuzi wa fasihi, kutamfanya
mwanahistoria kushindwa kuelewa vilivyo sanaa ya fasihi.
Marejeleo.
Kimani
N. Na Chimera, R. (1999).Ufundishaji wa fasihi, nadharia na mbinu.Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
Rajmund
Ohly, (2005). Historical Approach to Swahili Literature.An
Open Question.
Kiswahili
Juzuu la 68. Dar es Salaam:TUKI
Wafula
R. M. na Kimani, M (2007). Nadharia za uhakiki wa Fasihi.Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
Hussein Ebrahim, (1971). Mashetani. Nairobi: O.U.P.
0 Comments